Misaada ya Kujifunza
Tafsiri ya Joseph Smith (TJS)


Tafsiri ya Joseph Smith (TJS)

Marudio au tafsiri ya Toleo la Mfalme James la Biblia katika lugha ya Kiingereza, ambayo Joseph Smith Nabii alianza mwezi Juni 1830. Aliamriwa na Mungu kufanya tafsiri hiyo na alijichukulia kama sehemu ya wito wake kama nabii.

Ingawa Joseph alimaliza tafsiri hiyo ilipofika Julai 1833, aliendelea hadi kifo chake katika mwaka 1844 akifanya marekebisho wakati akitayarisha muswada kwa ajili ya kuchapisha. Ingawa alichapisha baadhi ya sehemu za tafsiri hiyo wakati wa uhai wake, inawezekana kwamba angelikuwa amefanya nyongeza ya mabadiliko kama angeliishi hadi kuchapisha kazi yote. Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho Lililoundwa Upya lilichapisha toleo la kwanza la tafsiri ya Joseph Smith ya kuongozwa na Mungu katika mwaka 1867. Wamechapisha matoleo kadha wa kadha tokea wakati huo.

Nabii alijifunza mambo mengi wakati wa shughuli ya kutafsiri. Sehemu kadhaa za Mafundisho na Maagano zilipokelewa kwa sababu ya kazi ya kutafsiri (kama vile M&M 76; 77; 91; na 132). Pia, Bwana alimpa Joseph maelekezo maalumu kwa ajili ya tafsiri hiyo, ambayo yameandikwa katika Mafundisho na Maagano (M&M 37:1; 45:60–61; 76:15–18; 90:13; 91; 94:10; 104:58; 124:89). Kitabu cha Musa na Joseph Smith—Mathayo, sasa kimejumuishwa katika Lulu ya Thamani Kuu, zilichukuliwa moja kwa moja kutoka kwa Tafsiri ya Joseph Smith.

Tafsiri ya Joseph Smith imerejesha baadhi ya mambo yaliyo wazi na yenye thamani ambayo yalikuwa yamepotea kutoka katika Biblia (1 Ne. 13). Ingawa siyo Biblia rasmi ya Kanisa, tafsiri hii inatoa utambuzi mwingi ulio mzuri na ni muhimu sana katika kuielewa Biblia. Pia ni ushahidi wa wito mtakatifu na huduma ya Joseph Smith Nabii.