Misaada ya Kujifunza
Ukuhani wa Melkizedeki


Ukuhani wa Melkizedeki

Ukuhani wa Melkizedeki ni ukuhani wa juu zaidi au mkuu zaidi; Ukuhani wa Haruni ni ukuhani mdogo zaidi. Ukuhani wa Melkizedeki unajumuisha funguo za baraka za kiroho za Kanisa. Kwa njia ya ibada za ukuhani wa juu zaidi nguvu za uchamungu huonekana kwa wanadamu (M&M 84:18–25; 107:18–21).

Mungu kwanza aliufunua ukuhani huu mkuu zaidi kwa Adamu. Mapatriaki na manabii katika kila kipindi walikuwa na mamlaka haya (M&M 84:6–17). Mwanzoni uliitwa Ukuhani Mtakatifu, kwa Mfano wa Mwana wa Mungu. Baadaye ukajulikana kama Ukuhani wa Melkizedeki (M&M 107:2–4).

Wana wa Israeli waliposhindwa kuishi kulingana na heshima na maagano ya Ukuhani wa Melkizedeki, Bwana aliiondoa sheria hii ya juu zaidi na akawapa ukuhani mdogo zaidi na torati ndogo zaidi (M&M 84:23–26). Hizi ziliitwa Ukuhani wa Haruni na torati ya Musa. Yesu alipokuja duniani, Alirejesha Ukuhani wa Melkizedeki kwa Wayahudi na akaanza kulijenga Kanisa miongoni mwao. Hata hivyo, ukuhani na Kanisa ukapotea tena kwa njia ya ukengeufu. Ukarejeshwa tena baadaye kupitia Joseph Smith Mdogo (M&M 27:12–13; 128:20; JS—H 1:73).

Ndani ya Ukuhani wa Melkizedeki kuna ofisi za mzee, kuhani mkuu, patriaki, Sabini, na Mtume (M&M 107). Ukuhani wa Melkizedeki daima utakuwa ni sehemu ya ufalme wa Mungu duniani.

Rais wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ndiye rais wa Ukuhani mkuu au wa Melkizedeki, naye hushikilia funguo zote zihusuzo ufalme wa Mungu duniani. Wito wa Rais hushikiliwa na mwanamume mmoja tu kwa wakati mmoja, naye ndiye mtu pekee duniani aliye na mamlaka ya kutumia funguo zote za ukuhani (M&M 107:64–67; 132:7).