Misaada ya Kujifunza
Wakolosai, Waraka kwa


Wakolosai, Waraka kwa

Kitabu katika Agano Jipya. Kwa asili ilikuwa ni barua ambayo Mtume Paulo aliiandika kwenda kwa Wakolosai baada ya kutembelewa na Epafra, mwinjilisti wa Kanisa katika Kolosai (Kol. 1:7–8). Epafra alimwambia Paulo ya kuwa Wakolosai wanaingia katika kosa lililo kubwa—walijidhania ya kuwa wao ni bora zaidi kuliko watu wengine kwa sababu wao walikuwa waangalifu sana juu ya ibada fulani za kimwili (Kol. 2:16), wakijizuia matakwa fulani ya kimwili, na wakiabudu malaika (Kol. 2:18). Matendo haya yaliwafanya Wakolosai wajisikie kuwa walikuwa wakitakaswa. Wao pia walidhani kuwa walikuwa wakielewa siri za ulimwengu vizuri zaidi kuliko waumini wengine wa Kanisa. Katika barua yake, Paulo aliwasahihisha kwa kuwafundisha kwamba ukombozi waja tu kupitia Kristo na ya kwamba tuwe na hekima na kumtumikia.

Mlango wa 1 ni salamu za Paulo kwa Wakolosai. Mlango wa 2–3 ni ya mafundisho na zina maelezo juu ya Kristo kama ndiye Mkombozi, hatari ya ibada za uongo, na umuhimu wa Ufufuko. Mlango wa 4 unafundisha kwamba Watakatifu wawe na hekima katika mambo yote.