Misaada ya Kujifunza
Kitabu cha Mormoni


Kitabu cha Mormoni

Moja ya vitabu vinne vya maandiko yanayokubalika na Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Ni ufupisho uliofanywa na nabii wa kale aliyeitwa Mormoni juu ya kumbukumbu ya wakazi wa kale wa bara la Marekani. Kiliandikwa ili kushuhudia ya kuwa Yesu ndiye Kristo. Kuhusu kitabu hiki, Joseph Smith Nabii, ambaye alikitafsiri kwa kipawa na uwezo wa Mungu, alisema: “Niliwaambia ndugu zangu kwamba Kitabu cha Mormoni kilikuwa kitabu kilicho sahihi kuliko kingine chochote duniani, na ni jiwe la tao la dini yetu, na mtu angelikuwa karibu zaidi na Mungu kwa kuishi kulingana na maagizo yake, kuliko kitabu kingine chochote” (ona dibaji mwanzoni mwa Kitabu cha Mormoni).

Kitabu cha Mormoni ni kumbukumbu ya kidini ya makundi matatu ya watu ambao walihamia kutoka Ulimwengu wa Zamani kwenda mabara ya Marekani. Makundi haya yaliongozwa na manabii ambao waliandika historia zao za kidini na kijamii kwenye mabamba ya chuma. Kitabu cha Mormoni kinaelezea juu ya Yesu Kristo kuwatembelea watu katika Marekani baada ya Ufufuko Wake. Kipindi cha miaka mia mbili ya amani kilifuatia matembezi haya ya Kristo.

Moroni, nabii Mnefi na mwanahistoria wa mwisho, alizifunga kumbukumbu hizi zilizofanyiwa ufupisho za watu hawa na kuzificha karibu mwaka 421 B.K. Katika mwaka 1823, Moroni mfufuka alimtokea Joseph Smith na baadaye akampatia kumbukumbu hizi zilizo takatifu na za kale ili azitafsiri na kuzitoa ulimwenguni kama ushuhuda mwingine wa Yesu Kristo.