Misaada ya Kujifunza
Yerusalemu


Yerusalemu

Mji ulioko katika Israeli ya sasa. Ni mji maarufu sana katika historia ya Biblia. Baadhi ya maeneo matakatifu sana zaidi kwa Wakristo, Wayahudi na Waislamuu yako katika mji huu na hutembelewa mara kwa mara na waumini wengi walio waaminifu. Mara nyingi unaelezwa kama mji mtakatifu.

Wakati fulani ulijulikana kama Salemu (Mwa. 14:18; Zab. 76:2), Yerusalemu ulikuwa mji wa Myebusi hadi ulipotwaliwa na Daudi (Yos. 10:1; 15:8; 2 Sam. 5:6–7); ambaye aliufanya kuwa makao makuu yake. Hadi wakati huo ulikuwa ukitumika sana kama ngome ya milimani, iliyokuwa kiasi cha futi 2600 (mita 800) juu ya usawa wa bahari. Umezungukwa na mabonde marefu katika pande zake zote isipokuwa kaskazini.

Wakati wa utawala wa Mfalme Daudi katika Yerusalemu, yeye alikaa katika kasri ya mbao. Hata hivyo, wakati wa utawala wa Suleimani, watu walifanya mambo mengi ya kuuremba mji huu, ikiwa ni pamoja na kujenga ikulu ya mfalme na hekalu.

Baada ya falme za Israeli na Yuda kugawanyika, Yerusalemu ulibakia kuwa mji mkuu wa Yuda. Mara kwa mara ulikuwa ukishambuliwa na majeshi ya uvamizi. (1 Fal. 14:25; 2 Fal. 14:13; 16:5; 18–19; 24:10; 25). Chini ya Hezekia, Yerusalemu ikawa kituo cha kuabudu kidini, lakini sehemu ya mji huo iliangamizwa katika mwaka wa 320 K.K., 168 K.K., na 65 K.K., Herode alijenga upya kuta zake na hekalu, lakini katika mwaka 70 B.K. Warumi wakauangamiza kabisa.