Misaada ya Kujifunza
Mungu, Uungu


Mungu, Uungu

Kuna watu watatu tofauti katika Uungu; Mungu, Baba wa Milele; Mwanawe, Yesu Kristo, na Roho Mtakatifu. Tunaamini katika kila mmoja Wao (M ya I 1:1). Kutokana na ufunuo wa siku za mwisho tunajifunza kwamba Baba na Mwana wana miili yenye kushikika ya nyama na mifupa na kwamba Roho Mtakatifu ni mtu wa kiroho, pasipo nyama na mifupa (M&M 130:22–23). Watu hawa watatu ni wamoja katika umoja mkamilifu na wenye mapatano ya madhumuni na mafundisho (Yn. 17:21–23; 2 Ne. 31:21; 3 Ne. 11:27, 36).

Mungu Baba

Kwa ujumla ni Baba, au Elohimu, ambaye hutajwa kwa jina hili Mungu. Yeye anaitwa Baba kwa sababu Yeye ni baba wa roho zetu (Hes. 16:22; 27:16; Mal. 2:10; Mt. 6:9; Efe. 4:6; Ebr. 12:9). Mungu Baba ndiye mtawala mkuu wa ulimwengu. Yeye ni mweza yote (Mwa. 18:14; Alma 26:35; M&M 19:1–3), mjua yote (Mt. 6:8; 2 Ne. 2:24), na aliye mahali pote kwa njia ya Roho Wake (Zab. 139:7–12; M&M 88:7–13, 41). Mwanadamu anao uhusiano maalumu na Mungu ambao humtenga mwanadamu mbali na vitu vingine vyote vilivyoumbwa: wanaume na wanawake ni watoto wa kiroho wa Mungu (Zab. 82:6; 1 Yoh. 3:1–3; M&M 20:17–18).

Kuna matukio machache ya Mungu Baba kumtokea au kuongea na mwanadamu. Maandiko yanasema kwamba Alinena kwa Adamu na Hawa (Musa 4:14–31) na akamtambulisha Yesu Kristo katika matukio kadha wa kadha (Mt. 3:17; 17:5; Yn. 12:28–29; 3 Ne. 11:3–7). Alimtokea Stefano (Mdo. 7:55–56) na Joseph Smith (JS—H 1:17). Baadaye Aliwatokea wote Joseph Smith na Sidney Rigdon (M&M 76:20, 23). Kwa wale wenye kumpenda Mungu na kujitakasa wenyewe mbele Yake, Mungu wakati mwingine hutoa nafasi ya kumwona na kujua wao wenyewe kwamba Yeye ndiye Mungu (Mt. 5:8; 3 Ne. 12:8; M&M 76:116–118; 93:1).

Mungu Mwana

Mungu ajulikanaye kama Yehova ni Mwana, Yesu Kristo (Isa. 12:2; 43:11; 49:26; 1 Kor. 10:1–4; 1 Tim. 1:1; Ufu. 1:8; 2 Ne. 22:2). Yesu hutenda kazi chini ya maelekezo ya Baba na wako katika mapatano timilifu na Yeye. Wanadamu wote ni kaka na dada Zake, kwa kuwa Yeye ndiye mkubwa kuliko watoto wote wa kiroho wa Elohimu. Baadhi ya dondoo za maandiko humwita Yeye kwa neno la Mungu. Kwa mfano, andiko lasema kwamba “Mungu aliumba mbingu na dunia” (Mwa. 1:1), lakini ukweli ulikuwa kwamba Yesu ndiye alikuwa Muumba chini ya maelekezo ya Mungu Baba (Yn. 1:1–3, 10, 14; Ebr. 1:1–2).

Mungu Roho Mtakatifu

Roho Mtakatifu pia ni Mungu naye anaitwa Roho Mtakatifu, Roho, na Roho wa Mungu, miongoni mwa majina na vyeo vingine. Kwa msaada wa Roho Mtakatifu, mwanadamu anaweza kujua mapenzi ya Mungu Baba na kujua kwamba Yesu ndiye Kristo (1 Kor. 12:3).