Misaada ya Kujifunza
Nyaraka za Paulo


Nyaraka za Paulo

Vitabu kumi na vinne katika Agano Jipya ambavyo awali vilikuwa ni barua zilizoandikwa na mtume Paulo kwa waumini wa Kanisa. Vinaweza kugawanywa katika makundi kama ifuatavyo:

1 na 2 Wathesalonike (50–51 B.K.)

Paulo aliandika nyaraka hizi kwa Wathesalonike kutoka Korintho wakati wa safari yake ya pili ya kimisionari. Kazi yake katika Thesalonike imeelekezwa katika Matendo 17. Alitaka kurudi tena Thesalonike, lakini hakuweza kufanya hivyo (1 The. 2:18). Kwa hiyo alimtuma Timotheo ili kuwachangamsha waongofu na ili amletee taarifa juu ya namna wanavyoendelea. Waraka wa kwanza ni matokeo ya shukrani zake juu ya kurudi kwa Timotheo. Waraka wa pili uliandikwa muda mfupi baadaye.

1 na 2 Wakorintho, Wagalatia, Warumi (55–57 B.K.)

Paulo aliandika nyaraka hizi kwa Wakorintho wakati wa safari yake ya tatu ya kimisionari ili kujibu maswali na kusahihisha machafuko miongoni mwa Watakatifu katika Korintho.

Waraka kwa Wagalatia yawezekana kuwa uliandikwa kwa vikundi vingi vya Kanisa katika Galatia. Baadhi ya waumini wa Kanisa walikuwa wakiacha injili kwa sababu ya sheria za Kiyahudi. Katika barua hii, Paulo alielezea madhumuni ya torati ya Musa na maana ya dini ya kiroho.

Paulo aliandika waraka kwa Warumi kutoka Korintho, kwa upande mmoja ili kuwatayarisha Watakatifu wa Rumi kwa ajili ya ziara aliyotumaini kuifanya kwao. Barua hii pia inasisitiza usahihi wa mafundisho ambayo yalikuwa yakipingwa na baadhi ya Wayahudi ambao wameongolewa katika Ukristo.

Wafilipi, Wakolosai, Waefeso, Filemoni, Waebrania (60–62 B.K.)

Paulo aliandika nyaraka hizi wakati alipokuwa gerezani kwa mara ya kwanza katika Roma.

Paulo aliandika waraka kwa Wafilipi kwa madhumuni ya kueleza shukrani yake na upendo wake kwa Watakatifu wa Filipi na kuwatia furaha kutokana na kukata kwao tamaa kwa sababu ya kifungo chake cha muda mrefu gerezani.

Paulo aliandika waraka kwa Wakolosai kama matokeo ya taarifa ya kwamba Watakatifu wa Kolosai walikuwa wakianguka katika makosa makubwa. Waliamini kwamba ukamilifu huja kwa kushika, kwa uangalifu, ibada za kimwili pekee yake kuliko kukuza tabia kama za Kristo.

Waraka kwa Waefeso ni wa umuhimu mkubwa, kwani una mafundisho ya Paulo juu ya Kanisa la Kristo.

Waraka kwa Filemoni ni barua ya siri juu ya Onesmo, mtumwa aliyemwibia bwana wake, Filemoni, na akakimbilia Roma. Paulo alimrudisha Onesmo kwa bwana wake pamoja na barua akiomba Onesmo asamehewa.

Paulo aliandika waraka kwa Waebrania waumini wa Kanisa wa Kiyahudi akiwashawishi kwamba torati ya Musa imetimilika katika Kristo na kwamba sheria ya injili ya Kristo imechukua nafasi yake.

1 na 2 Timotheo, Tito (64–65 B.K.)

Paulo aliandika nyaraka hizi baada ya kuachiliwa huru kutoka gerezani katika Roma kwa mara ya kwanza.

Paulo alisafiri kwenda Efeso, ambako alimwacha Timotheo kukomesha ukuaji wa aina fulani ya mafundisho yasiyo ya uhakika, akidhamiria kurudi tena baadaye. Aliandika waraka wake wa kwanza kwa Timotheo, pengine kutoka Makedonia, ili kumshauri na kumtia moyo katika kutimiza wajibu wake.

Paulo aliandika waraka kwa Tito wakati alipokuwa huru kutoka gerezani. Yawezekana alikuwa ametembelea Krete mahali ambapo Tito alikuwa akitumika. Barua hii hususani inashughulika na maisha ya uadilifu na nidhamu ndani ya Kanisa.

Paulo aliandika waraka wake wa pili kwa Timotheo wakati akiwa gerezani kwa mara ya pili, muda mfupi kabla ya kifo cha kishahidi cha Paulo. Waraka huu una maneno ya mwisho ya Paulo na huonyesha ujasiri na matumaini ya ajabu ambayo kwayo alikabili mauti.