Misaada ya Kujifunza
Daudi


Daudi

Mfalme wa kale wa Israeli katika Agano la Kale.

Daudi alikuwa mwana wa Yese wa kabila la Yuda. Alikuwa kijana jasiri aliyemwua simba, dubu, na jitu kubwa la Kifilisti Goliathi (1 Sam. 17). Daudi alichaguliwa na kupakwa mafuta kuwa mfalme wa Israeli. Kama Sauli, katika utu uzima wake alikuwa na hatia ya kufanya makosa makubwa ya jinai, lakini, tofauti na Sauli, yeye alikuwa na uwezo wa kuonyesha majuto ya kweli. Hivyo basi aliweza kupata msamaha, isipokuwa katika mauaji ya Uria (M&M 132:39). Maisha yake yanaweza kugawanywa katika sehemu nne: (1) huko Bethlehemu, ambako alikuwa mchungaji wa kondoo (1 Sam. 16–17); (2) katika baraza la Mfalme Sauli (1 Sam. 18:1–19:18); (3) kama mtoro (1 Sam. 19:18–31:13; 2 Sam. 1); (4) kama mfalme juu ya Yuda huko Hebroni (2 Sam. 2–4) na mwishowe kama mfalme juu ya Israeli yote (2 Sam. 5–24; 1 Fal. 1:1–2:11).

Dhambi ya uzinzi ya Daudi na Bath-sheba ilifuatiwa na mfuatano wa mabalaa ambayo yaliiharibu miaka ishirini ya mwisho ya uhai wake. Taifa kwa ujumla lilistawi wakati wa utawala wake, lakini Daudi mwenyewe aliteseka kutokana na matokeo ya dhambi zake. Daima kulikuwepo na ugomvi mkubwa wa kifamilia, ambao, katika shauri la Absalomu na Adonia, uliishia katika uasi wa wazi. Matukio haya ni utimilifu wa laana iliyotamkwa na Nathani nabii juu ya Daudi kwa sababu ya dhambi yake (2 Sam. 12:7–13).

Ingawa kulikuwa na mabalaa haya, utawala wa Daudi ulikuwa utawala ulio mzuri kuliko wowote katika historia ya Israeli, kwa sababu (1) aliyaunganisha makabila kuwa katika taifa moja, (2) alipata milki ya nchi pasipo mabishano, (3) aliiweka serikali juu ya misingi ya dini ya kweli kiasi kwamba mapenzi ya Mungu yakawa ndiyo sheria ya Israeli. Kwa sababu hizi, utawala wa Daudi mwishowe uliheshimiwa kama enzi ya dhahabu ya taifa na iliyo kuwa mfano wa enzi tukufu zaidi wakati Masiya atakapokuja (Isa. 16:5; Yer. 23:5; Eze. 37:24–28).

Maisha ya Daudi hutufundisha umuhimu kwa watu wote kustahmili hadi mwisho. Alipokuwa kijana, alisemekana kuwa mtu aliye mfano wa “moyo wa Bwana mwenyewe” (1 Sam. 13:14); kama mwanadamu, alinena kwa Roho naye alikuwa na mafunuo mengi. Lakini alilipa gharama nzito kwa ajili ya utovu wake wa utiifu kwa amri za Mungu (M&M 132:39).