Msaada wa Masomo
Amini, Imani


Amini, Imani

Kuwa na imani au kutumaini katika mtu fulani au kukikubali kitu fulani kuwa ni kweli. Kama itumikavyo mara kwa mara katika maandiko, imani ni matumaini na mategemeo katika Yesu Kristo ambayo humwongoza mtu katika kumtii yeye, ili apate kuolekewa katika uflame wa Mungu (M&M 20:29). Imani lazima ilenge katika Yesu Kristo ili iweze kumwongoza mtu kwenye wokovu. Watakatifu wa siku za mwisho pia wanayo imani katika Mungu Baba, Roho Mtakatifu, uwezo wa ukuhani, na vipengele vingine muhimu vya injili ya urejesho.

Imani ni pamoja na matumaini juu ya vitu visivyoonekana, lakini ni vya kweli (Ebr. 11:1; Alma 32:21; Eth. 12:6). Imani huwashwa kwa kusikia injili ifundishwayo na wahudumu walio na mamlaka waliotumwa na Mungu (Rum. 10:14–17). Miujiza haizai imani, bali imani iliyo imara huendelezwa na utiifu kwa injili ya Yesu Kristo. Kwa maneno mengine, imani huja kwa maisha ya haki (Alma 32:40–43; Eth. 12:4, 6, 12; M&M 63:9–12).

Imani ya kweli huleta miujiza, maono, ndoto, uponyaji, na vipawa vyote vya Mungu vile ambavyo Yeye huvitoa kwa Watakatifu Wake. Kwa imani mtu hupata ondoleo la dhambi na mwishowe huweza kukaa mbele za Mungu. Ukosefu wa imani humpelekea mtu katika kukata tamaa, ambako huja kwa sababu ya dhambi (Moro. 10:22).