Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 20


Sehemu ya 20

Ufunuo juu ya mfumo na utawala wa Kanisa, uliotolewa kupitia Joseph Smith Nabii, huko au jirani na Fayette, New York. Sehemu ya ufunuo huu yawezekana kuwa ilikuwa imetolewa mapema zaidi katika kiangazi cha 1829. Ufunuo kamili, uliojulikana nyakati hizo kama Kanuni na Maagano, yawezekana yaliandikwa mara baada ya 6 Aprili 1830 (siku Kanisa lilipoanzishwa) Nabii aliandika, “Tulipata kutoka kwake Yeye [Yesu Kristo] yafuatayo, kwa roho wa unabii na ufunuo; ambayo siyo tu ilitupa sisi taarifa nyingi, lakini pia ilituonyesha siku sahihi ambayo, kulingana na mapenzi Yake na amri, ilitupasa kuendelea kuliunda Kanisa Lake mara nyingine hapa duniani.”

1–16, Kitabu cha Mormoni huthibitisha utakatifu wa kazi ya siku za mwisho; 17–28, Mafundisho ya uumbaji, anguko, upatanisho na ubatizo yanathibitishwa; 29–37, Sheria zinazotawala toba, kuhesabiwa haki, na kutakasa, na ubatizo zatolewa; 38–67, Kazi za wazee, makuhani, walimu, na mashemasi zatolewa kwa muhtasari; 68–74, Kazi ya waumini, baraka za watoto, na mtindo wa ubatizo unafunuliwa; 75–84, Sala za Sakramenti na kanuni zinazotawala waumini wa Kanisa zinatolewa.

1 Kuibuka kwa Kanisa la Kristo katika siku hizi za mwisho, ikiwa ni miaka elfu moja mia nane na thelathini toka kuja kwa Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo katika mwili, likiwa kama kawaida limeundwa na kuanzishwa kulingana na sheria za nchi yetu, kwa mapenzi na amri za Mungu, katika mwezi wa nne, na siku ya sita ya mwezi ambao unaitwa Aprili—

2 Amri ambazo alipewa Joseph Smith, Mdogo, ambaye aliitwa na Mungu, na kutawazwa kuwa mtume wa Yesu Kristo, kuwa mzee wa kwanza wa kanisa hili;

3 Na kwa Oliver Cowdery, ambaye pia aliitwa na Mungu, mtume wa Yesu Kristo, kuwa mzee wa pili wa kanisa hili, na kutawazwa chini ya mikono yake;

4 Na hii ni kulingana na neema ya Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo, utukufu wote na uwe kwake, sasa na hata milele. Amina.

5 Baada ya kuwa imefunuliwa kwake mzee huyu wa kwanza kwamba amepokea ondoleo la dhambi zake, alitatizwa tena na majivuno ya ulimwengu;

6 Lakini baada ya kutubu na kujinyenyekeza mwenyewe kwa moyo, kwa njia ya imani, Mungu alimhudumia kwa njia ya malaika mtakatifu, ambaye uso wake ilikuwa kama radi, na ambaye mavazi yake yalikuwa masafi na meupe kupita weupe wote;

7 Na akampa amri ambazo zilimvutia;

8 Na akampa uwezo kutoka juu, kwa njia ambayo iliandaliwa mapema, ya kutafsiri Kitabu cha Mormoni;

9 Ambacho kina kumbukumbu ya watu walioanguka, na utimilifu wa injili ya Yesu Kristo kwa Wayunani na kwa Wayahudi pia;

10 Ambayo ilitolewa kwa maongozi, na imethibitishwa kwa wengine kwa huduma za malaika, na kuhubiriwa kwa walimwengu na wao—

11 Kuthibitisha kwa ulimwengu kwamba maandiko matakatifu ni ya kweli, na kwamba Mungu huwaongoza watu na kuwaita kwenye kazi yake takatifu katika kipindi na kizazi hiki, kama vile katika vizazi vya kale;

12 Kwa hiyo akionyesha kwamba yeye ni Mungu yeye yule jana, leo, na milele. Amina.

13 Kwa sababu hii, wakiwa mashahidi wakuu, kwa hao ulimwengu utahukumiwa, hata kadiri wengi baadaye watakavyo kuja kujua kazi hii.

14 Na wale ambao wanaipokea katika imani, na wakatenda kwa haki, watapokea taji la uzima wa milele;

15 Lakini wale ambao huishupaza mioyo yao katika kutoamini, na kuikataa, itageuka kuwa laana kwao wenyewe—

16 Kwani Bwana Mungu amesema hivi; na sisi, wazee wa kanisa, tumesikia na kutoa ushahidi kwa maneno ya mtukufu Mfalme aliye juu, utukufu na uwe kwake milele na milele. Amina.

17 Kwa mambo haya sisi tunajua kwamba yuko Mungu mbinguni, ambaye hana mwisho na wa milele, tangu milele hata milele yule yule Mungu asiyebadilika, aliyezifanya mbingu na dunia, na vitu vyote vilivyomo ndani yake;

18 Na kwamba alimuumba mtu, mwanamume na mwanamke, kwa sura na kwa mfano wake, aliwaumba;

19 Na akawapa wao amri kwamba inawapasa kumpenda na kumtumikia yeye, pekee aliye hai na Mungu wa kweli, na kwamba yapasa awe pekee wanayepaswa kumwabudu.

20 Lakini kwa uvunjaji wa sheria hizi takatifu mwanadamu akawa mwenye tamaa na mwovu na akawa mwanadamu aliyeanguka.

21 Kwa hiyo, Mwenyezi Mungu akamtoa Mwanawe wa Pekee, kama ilivyoandikwa katika yale maandiko ambayo yametolewa naye.

22 Akakumbwa na majaribio lakini hakuyasikiliza;

23 Akasulubiwa, akafa, na akafufuka tena siku ya tatu;

24 Na akapaa mbinguni, kukaa mkono wa kuume wa Baba, kutawala kwa uwezo mkuu kulingana na mapenzi ya Baba;

25 Kwamba kadiri wengi watakavyo amini na kubatizwa katika jina lake takatifu, na kuvumilia katika imani hadi mwisho, wapate kuokolewa—

26 Siyo tu wale ambao waliamini baada ya kuja kwake wakati wa meridiani, katika mwili, bali wale wote toka mwanzo, hata wengi waliokuwepo kabla ya kuja kwake, ambao waliamini katika maneno ya manabii watakatifu, ambao walinena kama walivyoongozwa kwa kipawa cha Roho Mtakatifu, ambaye hakika alimshuhudia katika mambo yote, waweze kuwa na uzima wa milele,

27 Pia na wale ambao watakuja baadaye, ambao wataamini katika vipawa na miito ya Mungu kwa Roho Mtakatifu, ambao hutoa ushuhuda wa Baba na Mwana;

28 Ambao Baba, Mwana na Roho Mtakatifu ni Mungu mmoja, asiye na mwisho na wa milele, bila mwisho. Amina.

29 Na sisi tunajua kwamba watu wote lazima watubu na kuamini kwa jina la Yesu Kristo, na kumwabudu Baba katika jina lake, na kuvumilia katika imani kwa jina lake hadi mwisho, au hawawezi kuokolewa katika ufalme wa Mungu.

30 Na tunajua kwamba kuhesabiwa haki kwa njia ya neema ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo ni haki na kweli;

31 Na tunajua pia, kwamba utakaso kwa njia ya neema ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo ni haki na kweli, kwa wale wote ambao wanampenda na kumtumikia Mungu kwa uwezo, akili na nguvu zao zote.

32 Lakini upo uwezekano kwamba mwanadamu akaweza kuanguka kutoka katika hali ya neema, na kujitenga kutoka kwa Mungu aliye hai;

33 Kwa hiyo kanisa na lichukue tahadhari, na kusali daima, wasije wakaanguka majaribuni;

34 Ndiyo, na hata wale waliotakaswa wachukue tahadhari vile vile.

35 Na tunajua kwamba mambo haya ni ya kweli na kulingana na mafunuo ya Yohana, bila kuongeza wala kupunguza kutoka katika unabii wa kitabu chake, maandiko matakatifu, au mafunuo ya Mungu ambayo yatakuja hapo baadaye kwa kipawa na nguvu za Roho Mtakatifu, sauti ya Mungu, au huduma za malaika.

36 Na Bwana Mungu amesema hilo; na heshima, nguvu na utukufu, utolewe kwa jina lake takatifu, sasa na milele. Amina.

37 Na tena, kwa njia ya amri kwa kanisa kuhusiana na jinsi ya ubatizo—Wale wote wenye kunyenyekea wenyewe mbele za Mungu, na kutamani kubatizwa, na wakija na mioyo iliyovunjika na roho zilizopondeka, na kushuhudia mbele ya kanisa kwamba hakika wametubu dhambi zao zote, na wako radhi kujichukulia juu yao jina la Yesu Kristo, wakiwa na dhamira ya kumtumikia hadi mwisho, na hakika wakithibitisha kwa matendo yao kwamba wamempokea Roho wa Kristo kwa msamaha wa dhambi zao, na wapokelewe kwa ubatizo katika kanisa lake.

38 Kazi za wazee, makuhani, walimu, mashemasi, na waumini wa kanisa la KristoMtume ni mzee, na ni wito wake kubatiza;

39 Na kuwatawaza wazee wengine, makuhani, walimu, na mashemasi;

40 Na kuhudumia mkate na divai—ishara ya mwili na damu ya Kristo—

41 Na kuwathibitisha wale wanaobatizwa katika kanisa, kwa kuwawekea mikono kwa ajili ya ubatizo wa moto na Roho Mtakatifu, kulingana na maandiko;

42 Na kufundisha, kuelezea, kushawishi, kubatiza, na kusimamia kanisa;

43 Na kulithibitisha kanisa kwa kuwekea mikono yao, na kutunukia Roho Mtakatifu;

44 Na kuchukua uongozi wa mikutano yote.

45 Wazee wataendesha mikutano kadiri watakavyoongozwa na Roho Mtakatifu, kulingana na amri na mafunuo ya Mungu.

46 Kazi ya kuhani ni kuhubiri, kufundisha, kuelezea, kushawishi, na kubatiza, na kuhudumia sakramenti,

47 Na kutembelea nyumba ya kila muumini, na kuwashawishi kusali kwa sauti na kwa siri na kushiriki kazi zote za familia.

48 Na anaweza pia kuwatawaza makuhani wenzie, walimu, na mashemasi.

49 Na yeye atachukua uongozi wa mikutano endapo hakuna mzee katika mahali hapo;

50 Lakini akiwepo mzee, yeye ni wa kuhubiri tu, kufundisha, kuelezea, kushawishi na kubatiza,

51 Na kutembelea nyumba ya kila muumini, akihimiza kusali kwa sauti na sirini na kushiriki kwa kazi zote za familia.

52 Katika kazi hizi zote kuhani ni wa kumsaida mzee kama itahitajika.

53 Kazi ya mwalimu ni kuliangalia kanisa daima, na kuwa nalo, na kuwaimarisha;

54 Na kuona kwamba hakuna uovu katika kanisa, wala kuzozana baina yao, wala kudanganya, kusengenya, wala kusemana mabaya;

55 Na kuona kwamba kanisa linakutana pamoja mara kwa mara, na pia kuona kwamba waumini wote wanatimiza wajibu wao.

56 Na atachukua uongozi wa mikutano ikiwa mzee na kuhani hawapo—

57 Na atasaidiwa daima, katika kazi zake zote katika kanisa, na mashemasi, kama itahitajika.

58 Lakini, si walimu wala mashemasi walio na mamlaka ya kubatiza, kuhudumia Sakramenti, au kumwekelea mikono;

59 Wao, kwa hivyo ni wa kuwaonya, kuelezea, kushawishi, na kufundisha, na kuwakaribisha watu wote kuja kwa Kristo.

60 Kila mzee, kuhani, mwalimu, au shemasi apaswa kutawazwa kufuatana na vipawa na miito aliyopewa na Mungu; na atatawazwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, ambaye yu ndani ya yule mwenye kumtawaza.

61 Wazee kadha wanaounda hili kanisa la Kristo watakutana katika mkutano katika kila miezi mitatu, au mara kwa mara kama mikutano hiyo itakavyoelekeza au kuamuriwa;

62 Na mikutano hiyo iliyosemwa ni ya kufanya kazi yoyote ya kanisa iliyo muhimu kufanyika kwa wakati huo.

63 Wazee wanapaswa kupokea leseni zao kutoka kwa wazee wengine, kwa kura ya kanisa ambako wanatoka, au kutoka kwenye mikutano.

64 Kila kuhani, mwalimu, au shemasi, ambaye ametawazwa na kuhani, anaweza kuchukua hati kutoka kwake wakati huo, hati ambayo, ikitolewa kwa mzee, yaweza kumpa yeye haki ya kupewa leseni, ambayo itampa mamlaka yeye ya kufanya kazi za wito wake, au aweza kuipata kutoka mkutanoni;

65 Hakuna mtu atakayetawazwa katika ofisi yoyote katika kanisa hili, mahali ambapo hakuna tawi la kanisa lililoanzishwa kiutaratibu, bila ya kupigiwa kura na kanisa hilo;

66 Lakini wazee viongozi, maaskofu wanaosafiri, baraza kuu, makuhani wakuu, na wazee, wanaweza kuwa na haki ya kutawaza, mahali ambapo hakuna tawi la kanisa ambapo kura yaweza kuitishwa.

67 Kila rais wa ukuhani mkuu (au mzee kiongozi), askofu, mjumbe wa baraza kuu, na kuhani mkuu, anapaswa kutawazwa kwa maelekezo ya baraza kuu au mkutano mkuu.

68 Kazi ya waumini baada ya kupokelewa kwa ubatizo—Wazee au makuhani wanapaswa kuwa na muda wa kutosha wa kuelezea mambo yote kuhusu kanisa la Kristo kwa ufahamu wao, kabla ya kupokea kwao sakramenti na kuwa wamethibitishwa kwa kuwekewa mikono ya wazee, ili kwamba mambo yote yaweze kufanyika katika utaratibu.

69 Na waumini wataonyesha mbele ya kanisa, na pia mbele za wazee, kwa mwenendo wa kiucha mungu na katika mazungumzo, kwamba wanastahili, ili paweze kuwa na kazi na imani inayokubaliana na maandiko matakatifu—wakienenda katika utakatifu mbele za Bwana.

70 Kila muumini wa kanisa la Kristo mwenye watoto anapaswa kuwaleta kwa wazee mbele za kanisa, ambao wataweka mikono juu yao katika jina la Yesu Kristo, na kuwabariki katika jina lake.

71 Hakuna yeyote anayeweza kupokelewa katika kanisa la Kristo isipokuwa amefikia katika umri wa uwajibikaji mbele za Mungu, na mwenye uwezo wa toba.

72 Ubatizo yapaswa kufanyika katika njia ifuatayo kwa wale wote wanaotubu—

73 Mtu aliyeitwa na Mungu na mwenye mamlaka kutoka kwa Yesu Kristo ya kubatiza, ataingia katika maji pamoja na mtu aliyejileta mwenyewe kwa ajili ya ubatizo, naye atasema, akimwita kwa jina lake: Kwa mamlaka niliyopewa na Yesu Kristo, ninakubatiza katika jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu. Amina.

74 Ndipo atamzamisha kabisa mtu huyo katika maji, na kumwinua kutoka majini.

75 Yafaa kwamba kanisa likutane pamoja mara kwa mara kupokea mkate na divai katika ukumbusho wake Bwana Yesu;

76 Na mzee au kuhani atahudumu; na kwa njia hii atafanya—atapiga magoti pamoja na kanisa na kulingana Baba katika sala ya dhati, akisema:

77 Ee Mungu, Baba wa Milele, tunakuomba katika jina la Mwanao, Yesu Kristo, ubariki na utakase mkate huu kwa roho za wale wote watakaoula, ili waweze kuula kwa ukumbusho wa mwili wa Mwanao, na wakushuhudie, Ee Mungu, Baba wa Milele, kwamba wako radhi kujichukulia juu yao jina la Mwanao, na daima kumkumbuka, na kushika amri zake ambazo amewapa; ili daima Roho wake apate kuwa pamoja nao. Amina.

78 Namna ya kuhudumia divai—atachukua kikombe pia, na atasema:

79 Ee Mungu, Baba wa Milele, tunakuomba katika jina la Mwanao, Yesu Kristo, ubariki na utakase divai hii kwa roho za wale wote watakaoinywa, ili waweze kufanya hivi kwa ukumbusho wa damu ya Mwanao, ambayo ilimwagwa kwa ajili yao; kwamba washuhudie kwako, Ee Mungu, Baba wa Milele, kwamba daima wamkumbuke, ili Roho wake apate kuwa pamoja nao. Amina.

80 Muumini yeyote katika kanisa la Yesu Kristo anayevunja, au kughafilika katika kosa, ashughulikiwe kulingana na maelekezo ya maandiko.

81 Utakuwa wajibu wa makanisa kadhaa, yanayounda kanisa la Kristo, kumpeleka mwalimu mmoja au zaidi kuhudhuria mikutano kadha wa kadha inayohudhuriwa na wazee wa kanisa,

82 Pamoja na orodha ya majina ya waumini kadhaa wakijiunga pamoja na kanisa toka mkutano uliopita; au kupeleka kwa mikono ya kuhani; ili kwamba orodha ya kudumu ya majina yote ya kanisa zima iweze kutunzwa katika kitabu na mmoja wa wazee, yeyote yule ambaye wazee wengine watamchagua kila wakati;

83 Na pia, kama yeyote ameondolewa kutoka katika kanisa, ili kwamba majina yao yaweze kufutwa kwenye kumbukumbu ya majina ya kanisa.

84 Waumini wote wakihama kutoka katika kanisa mahali wanapoishi, na kwenda kwenye kanisa mahali wasipojulikana, wanaweza kuchukua barua ikithibitisha kwamba wao ni waumini na kwamba ni waaminifu, hati ambayo inaweza kusainiwa na mzee yeyote au kuhani kama muumini atakayepokea barua hiyo anafahamiana na mzee au kuhani, au yaweza kusainiwa na walimu au mashemasi wa kanisa.

Chapisha