Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 94


Sehemu ya 94

Ufunuo uliotolewa kupitia Joseph Smith Nabii, huko Kirtland, Ohio, 2 Agosti 1833. Hyrum Smith, Reynolds Cahoon, na Jared Carter wanateuliwa kama kamati ya Ujenzi wa Kanisa.

1–9, Bwana anatoa amri kuhusu ujenzi wa nyumba kwa ajili ya kazi ya Urais; 10–12, Nyumba ya kupiga chapa ijengwe; 13–17, Urithi kiasi fulani watolewa.

1 Na tena, amini ninawaambia, marafiki zangu, ninawapa amri, ya kuwa mtaanza kazi ya kuweka na kutayarisha mwanzo na msingi wa mji wa kigingi cha Sayuni, hapa katika ardhi ya Kirtland, kuanzia katika nyumba yangu,

2 Na tazama, ni lazima ifanywe kulingana na mpangilio ambao nimeutoa kwenu.

3 Na kiwanja cha kwanza upande wa kusini kiwekwe wakfu kwangu kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya urais, kwa ajili ya kazi ya urais, kwa ajili ya kupokelea mafunuo; na kwa ajili ya kazi ya huduma ya urais, katika mambo yote yahusuyo kanisa na ufalme.

4 Amini ninawaambia, kwamba itajengwa futi hamsini na tano kwa sitini na tano katika upana wake na katika urefu wake, katika ukumbi wa ndani.

5 Na patakuwapo na ukumbi wa chini na ukumbi wa juu, kulingana na mfano ambao utatolewa kwenu hapo baadaye.

6 Na iwekwe wakfu kwa Bwana kuanzia msingi wake, kulingana na mfano wa ukuhani, kulingana na utaratibu ambao utatolewa kwenu hapo baadaye.

7 Na yote itawekwa wakfu kwa Bwana kwa ajili ya kazi ya urais.

8 Na msiruhusu kitu chochote kichafu kuja ndani yake; na utukufu wangu utakuwa humo, na uwepo wangu utakuwa hapo.

9 Lakini kama kitakuja ndani yake kitu chochote kilicho kichafu, utukufu wangu hautakuwa humo; na uwepo wangu hautakuja ndani yake.

10 Na tena, amini ninawaambia, kiwanja cha pili upande wa kusini kitawekwa wakfu kwangu mimi kwa ajili ya ujenzi wa nyumba yangu, kwa ajili ya kazi ya kupiga chapa ya tafsiri ya maandiko yangu, na mambo yote nitakayo waamuru ninyi.

11 Nayo itakuwa futi hamsini na tano kwa sitini na tano katika upana wake na urefu wake, katika ukumbi wa ndani; na patakuwa na ukumbi wa chini na wa juu.

12 Na nyumba hii yote itawekwa wakfu kwa Bwana kutoka msingi wake, kwa ajili ya kazi ya upigaji chapa, katika mambo yote yale nitakayowaamuru, iwe takatifu, isiyochafuliwa, kulingana na mfano wake katika mambo yote, kama itakavyotolewa kwenu.

13 Na juu ya kiwanja cha tatu mtumishi wangu Hyrum Smith atapokea urithi wake.

14 Na juu ya kiwanja cha kwanza na cha pili upande wa kaskazini mtumishi wangu Reynolds Cahoon na Jared Carter watapata urithi wao—

15 Ili waweze kufanya kazi nilizowapangia, kuwa kamati ya kujenga nyumba zangu, kulingana na amri, ambazo Mimi, Bwana Mungu, nimezitoa kwenu.

16 Nyumba hizi mbili zisijengwe hadi nitakapowapa amri juu yake.

17 Na sasa sitatoa zaidi kwenu kwa wakati huu. Amina.