Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 6


Sehemu ya 6

Ufunuo uliotolewa kwa Joseph Smith Nabii na Oliver Cowdery, huko Harmony, Pennsylvania, Aprili 1829. Oliver Cowdery alianza kazi yake ya uandishi katika tafsiri ya Kitabu cha Mormoni, 7 Aprili 1829. Alikuwa tayari amekwisha pokea ufunuo mtakatifu wa ukweli wa ushuhuda wa Nabii kuhusiana na mabamba ambayo juu yake imechorwa kumbukumbu ya Kitabu cha Mormoni. Nabii alimwuliza Bwana kupitia Urimu na Thumimu naye akapata jibu hili.

1–6, Wafanyakazi katika shamba la Bwana hupata wokovu; 7–13, Hakuna zawadi iliyo kubwa zaidi kuliko zawadi ya wokovu; 14–27, Ushuhuda wa ukweli huja kwa uwezo wa Roho; 28–37, Mtegemee Kristo na tenda mema daima.

1 Kazi kubwa na ya ajabu i karibu kuja kwa wanadamu.

2 Tazama, Mimi ndimi Mungu; litiini neno langu, lililo hai na lenye nguvu, kali kuliko upanga wenye makali pande mbili, kwa kugawanya viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; hivyo basi yatiini maneno yangu.

3 Tazama, shamba ni jeupe tayari kwa mavuno; kwa hiyo, yeyote atakaye kuvuna, na aingize mundu yake kwa nguvu zake, na kuvuna wakati siku ingali, ili aweze kujiwekea akiba kwa ajili ya nafsi yake wokovu usio na mwisho katika ufalme wa Mungu.

4 Ndiyo, yeyote yule atakayeingiza mundu yake na kuvuna, yeye huyo ameitwa na Mungu.

5 Kwa hiyo, kama wewe utaniomba mimi utapata, kama utabisha utafunguliwa.

6 Sasa, kama ulivyoomba, tazama ninakuambia, shika amri zangu, na tafuta kuianzisha na kustawisha kusudi la Sayuni;

7 Usitafute utajiri bali hekima, na tazama, siri za Mungu zitafichuliwa kwako, na ndipo wewe utafanywa tajiri. Tazama, yeye aliye na uzima wa milele ndiye tajiri.

8 Amini, amini, nakuambia, kama unavyotaka kwangu na itakuwa hivyo kwako; na kama unataka, utakuwa chanzo cha kufanya mambo mema mengi katika kizazi hiki.

9 Usiseme lolote bali toba kwa kizazi hiki; shika amri zangu, na saidia kuitenda kazi yangu, kulingana na amri zangu, na wewe utabarikiwa.

10 Tazama nawe unacho kipawa, na umebarikiwa kwa sababu ya kipawa chako. Kumbuka ni kitakatifu na chatoka juu—

11 Na kama wewe utauliza, utapata kujua siri zilizo kubwa na za ajabu; hivyo basi wewe unapaswa kutumia kipawa chako, kwamba uweze kuzigundua siri, kwamba uweze kuwaleta wengi kwenye maarifa ya ukweli, ndiyo, kuwashawishi wao juu ya makosa ya njia zao.

12 Usifanye kipawa chako kijulikane kwa yeyote ila kwa wale tu wa imani yako. Usicheze na mambo matakatifu.

13 Kama wewe wataka kutenda mema, ndiyo, na endelea kwa uaminifu hadi mwisho, nawe utaokolewa katika ufalme wa Mungu, ambayo ndiyo zawadi kubwa kuliko zote kwa Mungu; kwani hakuna zawadi kubwa zaidi kuliko zawadi ya wokovu.

14 Amini, amini, nakuambia, umebarikiwa wewe, kwa kile ulichofanya; kwani wewe umeniuliza Mimi, na tazama, kama daima ulivyoniuliza, nawe umepata maelekezo ya Roho wangu. Kama isingelikuwa hivyo, wewe usingelifika mahali ulipo sasa.

15 Tazama, na wewe wajua kwamba uliniuliza Mimi na Mimi nikaiangaza akili yako; na sasa ninakuambia wewe mambo haya kwamba uweze kuelewa kwamba wewe uliangaziwa na Roho wa ukweli;

16 Ndiyo, ninakuambia, ili wewe upate kujua kwamba hapana yeyote ila Mungu ambaye hujua mawazo yako na dhamira ya moyo wako.

17 Ninakuambia mambo haya kama ushahidi kwako—kwamba maneno au kazi ambayo wewe umekuwa ukiandika ni ya kweli.

18 Kwa hivyo fanya bidii; simama pamoja na mtumishi wangu Joseph, kiuaminifu, katika hali yoyote iwayo ngumu atakayoweza kuwa kwa sababu ya neno.

19 Muonye katika makosa yake na pia pokea maonyo yake. Kuwa mvumilivu; mtulivu; mwenye kiasi, uwe na subira, imani, tumaini na hisani.

20 Tazama, wewe ndiwe Oliver, na nimesema nawe kwa sababu ya matakwa yako; kwa hiyo yatunze maneno haya katika moyo wako. Uwe mwaminifu na mwenye juhudi katika kushika amri za Mungu, na mimi nitakuzungushia mikono ya upendo wangu.

21 Tazama, Mimi ndimi Yesu Kristo, Mwana wa Mungu. Mimi ni yule yule ambaye nilikuja kwa walio wangu, na walio wangu hawakunipokea. Mimi ni nuru inayongʼaa gizani, nalo giza halikuiweza.

22 Amini, amini, ninakuambia, kama wataka ushahidi zaidi, rejesha mawazo yako juu ya usiku ule uliponililia katika moyo wako, kwamba uweze kujua ukweli wa mambo haya.

23 Sikusema amani akilini mwako kuhusiana na jambo hili? Ni ushahidi gani mkubwa zaidi unaoweza kupata kuliko kutoka kwa Mungu?

24 Na sasa, tazama, umepata ushahidi; kwani kama mimi nimekuambia mambo ambayo hakuna mtu ajuaye, je hujapata ushahidi?

25 Na, tazama, ninakupa kipawa, kama wataka kutoka kwangu, cha kutafsiri, hata kama mtumishi wangu Joseph.

26 Amini, amini, ninakuambia, kwamba zipo kumbukumbu ambazo zimechukua kiasi kikubwa cha injili yangu, ambayo ilizuiliwa kwa sababu ya uovu wa watu;

27 Na sasa ninakuamuru, kwamba kama unayo tamaa njema—tamaa ya kujiwekea hazina yako mbinguni—ndipo utasaidia katika kuzileta kwenye nuru, kwa kipawa chako, sehemu zile za maandiko yangu matakatifu ambayo yamefichwa kwa sababu ya uovu.

28 Na sasa, tazama, ninakupa wewe pamoja na mtumishi wangu Joseph funguo za kipawa hiki, ambacho kitaileta nuruni huduma hii; na katika vinywa vya mashahidi wawili au watatu kila neno lithibitike.

29 Amini, amini, ninawaambia, kama wao wanakataa maneno yangu, na sehemu hii ya injili yangu na huduma, mmebarikiwa ninyi, kwani wao hawatafanya zaidi kwenu kuliko walivyonifanyia mimi.

30 Na hata kama watawafanyia ninyi kama walivyonifanyia Mimi, mmebarikiwa ninyi, kwani mtaishi pamoja na mimi katika utukufu.

31 Lakini kama hawatayakataa maneno yangu, ambayo yataanzishwa kwa ushuhuda ambao utatolewa, wamebarikiwa wao, na ndipo ninyi mtapata shangwe ya matunda ya kazi yenu.

32 Amini, amini, ninawaambia, kama nilivyosema kwa wanafunzi wangu, walipo wawili au watatu waliokusanyika pamoja katika jina langu, wakigusia jambo moja, tazama, mimi nitakuwa katikati yao—hata sasa nipo katikati yenu.

33 Msiogope kufanya mema, wana wangu, kwani chochote unachopanda, ndicho pia wewe utakachokivuna; kwa hiyo kama utapanda mema pia utavuna mema kwa thawabu zenu.

34 Kwa sababu hiyo, msiogope, enyi kundi dogo; tendeni mema; acha dunia na jehanamu ziungane dhidi yenu, kwani kama mmejengwa juu ya mwamba wangu, haziwezi kuwashinda.

35 Tazama, siwahukumu ninyi; nendeni zenu na msitende dhambi tena; fanyeni kwa utaratibu kazi ambayo nimewaamuru.

36 Nitegemeeni katika kila wazo; msitie shaka, msiogope.

37 Tazama majeraha yaliyoko yaliotobolewa ubavuni mwangu, na pia alama za misumari katika mikono na miguu yangu; kuweni waaminifu, zishikeni amri zangu, na mtaurithi ufalme wa mbinguni. Amina.

Chapisha