Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 127


Sehemu ya 127

Waraka kutoka kwa Joseph Smith Nabii kwa Watakatifu wa Siku za Mwisho huko Nauvoo, Illinois, wenye maelekezo juu ya ubatizo kwa ajili ya wafu, ulioandikwa huko Nauvoo, 1 Septemba 1842.

1–4, Joseph Smith afurahi katika taabu na dhiki; 5–12, Kumbukumbu lazima zitunzwe juu ya ubatizo wa wafu.

1 Kwa kuwa Bwana amenifunulia kwamba maadui zangu, wote wa Missouri na wa Jimbo hili, walikuwa tena wakinisaka; na kwa vile wananisaka bila sababu, na wala hawana kivuli wala rangi ya kunitendea kisheria au haki kwa upande wao kuhusiana na kuniletea mashtaka yao dhidi yangu; na kwa vile visingizio vyao vyote vinatokana na uongo wa rangi nyeusi, nimefikiri ni muhimu na ni hekima kwangu kuondoka mahali hapa kwa muda mfupi, kwa usalama wangu mwenyewe na kwa usalama wa watu hawa. Ningelisema kwa wale wote wenye shughuli na mimi, kwamba nimeacha mambo yangu kwa mawakala na makarani ambao watashughulikia mambo yote mara moja na ipasavyo, nao wataona kwamba madeni yangu yote yanalipwa kwa wakati wake, kwa kuuza mali, au kwa njia nyingineyo, kadiri itakavyohitajika, au kadiri hali itavyoruhusu. Nitakapojua kwamba dhoruba imemalizika kabisa, ndipo nitarejea kwenu tena.

2 Na juu ya hatari ambazo nimeitwa kuzipitia, yaonekana kuwa jambo dogo kwangu, kama vile wivu na ghadhabu za mwanadamu zimekuwa jambo la kawaida siku zote za maisha yangu; na kwa sababu yake yaonekana kuwa miujiza, isipokuwa kama nilitawazwa kabla ya kuwekwa msingi wa ulimwengu kwa ajili ya madhumuni mema, au mabaya, kama mtakavyochagua kuita. Hukumuni ninyi wenyewe. Mungu anajua mambo haya yote, kama ni mazuri au mabaya. Lakini hata hivyo, maji ya kina kirefu nimezoea kuogelea ndani yake. Hii yote imekuwa kawaida ya pili kwangu; na ninajisikia, kama Paulo, kufurahia katika taabu; kwa sababu hadi siku hii Mungu wa baba zangu amenikomboa na haya yote, na atanikomboa kutoka sasa na kuendelea; kwani tazama, na lo, nitawashinda adui zangu wote, kwani Bwana Mungu amesema hayo.

3 Acha watakatifu wote na wafurahi, kwa sababu hiyo, na wawe na furaha tele; kwa kuwa Mungu wa Israeli ndiye Mungu wao, naye atawagawia malipo ya ujira wa haki juu ya vichwa vya watesi wao wote.

4 Na tena, amini hivyo ndivyo asemavyo Bwana: Acha kazi ya hekalu langu, na kazi zote ambazo nimewapangia, ziendelezwe na zisisimame; na jitihada zenu, na uvumilivu wenu, na ustahimilivu, na kazi zenu zizidishwe mara mbili, nanyi kwa vyovyote vile hamtakosa ujira wenu, asema Bwana wa Majeshi. Na kama wanavyowatesa ninyi, ndivyo walivyowatesa manabii na watu wenye haki waliokuwepo kabla yenu. Kwani kwa haya yote kuna thawabu mbinguni.

5 Na tena, ninatoa kwenu ninyi neno lihusulo ubatizo kwa ajili ya wafu wenu.

6 Amini, hivyo ndivyo asemavyo Bwana kwenu ninyi juu ya wafu wenu: Wakati mmoja wenu abatizwapo kwa ajili ya wafu wenu, acha awepo na mwandishi, naye awe shahidi wa macho wa ubatizo wenu; acha asikie kwa masikio yake, ili apate kuishuhudia kweli, asema Bwana;

7 Ili kumbukumbu zenu zote zipate kuandikwa mbinguni; lolote mtakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lolote mtakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni;

8 Kwani ni karibu kuyarejesha mambo mengi duniani, yahusuyo ukuhani, asema Bwana wa Majeshi.

9 Na tena, acha kumbukumbu zote zitunzwe kwa mpangilio, ili zipate kuwekwa kwenye nyaraka za hekalu langu takatifu, ili ziweze kutunzwa katika ukumbusho toka kizazi hadi kizazi, asema Bwana wa Majeshi.

10 Nitasema kwa watakatifu wote, kwamba nimetamani, kwa tamaa kubwa kupita kiasi, kuwahubiria kutoka jukwaani juu ya jambo la ubatizo kwa ajili ya wafu, siku ya Sabato ijayo. Lakini kwa vile hiyo iko nje ya uwezo wangu kufanya hivyo, nitawaandikia neno la Bwana mara kwa mara, juu ya jambo hilo, na kulituma kwenu kwa njia ya barua, vile vile mambo mengineyo.

11 Sasa ninaifunga barua yangu kwa wakati huu, kwa sababu ya uchache wa muda; kwani adui yuko tayari, na kama Mwokozi alivyosema, yuaja mtawala wa ulimwengu huu, lakini hana kitu kwangu.

12 Tazama, sala yangu kwa Mungu ni kwamba ninyi nyote mpate kuokolewa. Na ninatia saini mimi mwenyewe kama mtumishi wenu katika Bwana, nabii na mwonaji wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.

Joseph Smith.