Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 1


Mafundisho na Maagano

Sehemu ya 1

Ufunuo uliotolewa kupitia Joseph Smith Nabii, 1 Novemba 1831, wakati wa mkutano maalumu wa wazee wa Kanisa, uliofanyika Hiram, Ohio. Mafunuo mengi yalikuwa yamekwisha pokelewa kutoka kwa Bwana kabla ya wakati huu, na ukusanyaji kwa ajili ya uchapishaji katika muundo wa kitabu ni moja ya mambo muhimu yaliyopitishwa katika mkutano huo. Sehemu hii inafanya utangulizi wa Bwana wa mafundisho, maagano, na amri alizozitoa katika kipindi hiki.

1–7, Sauti ya onyo ni kwa watu wote; 8–16, Ukengeufu na uovu utatangulia Ujio wa Pili; 17–23, Joseph Smith ameitwa kurejesha duniani ukweli na uwezo wa Bwana; 24–33, Kitabu cha Mormoni kinafichuliwa na Kanisa la kweli linaanzishwa; 34–36, Amani itaondolewa duniani; 37–39, Zichunguzeni amri hizi.

1 Sikilizeni, Enyi watu wa kanisa langu, yasema sauti ya yeye akaaye juu, na ambaye macho yake yako juu ya watu wote; ndiyo, amini ninawaambia: Sikilizeni enyi watu wa kutoka mbali; nanyi mlio juu ya visiwa vya bahari, sikilizeni kwa pamoja.

2 Kwani hakika sauti ya Bwana ni kwa watu wote, na hakuna atakayeepuka; na hakuna jicho ambalo halitaona, wala sikio ambalo halitasikia, wala moyo ambao hautapenywa.

3 Na waasi watachomwa kwa uchungu mwingi; kwani uovu wao utasemwa juu ya paa za nyumba, na matendo yao ya siri yatafichuliwa.

4 Na sauti ya onyo itakuwa kwa watu wote, kwa vinywa vya wanafunzi wangu, ambao nimewachagua katika siku hizi za mwisho.

5 Nao watasonga mbele wala hakuna wa kuwazuia, kwani Mimi Bwana nimewaamuru.

6 Tazama, hii ni mamlaka yangu, na ni mamlaka ya watumishi wangu, na ni utangulizi wa kitabu cha amri zangu, ambazo nimewapa wao kuchapisha kwa ajili yenu, Enyi wakazi wa dunia.

7 Hivyo basi, ogopeni na tetemekeni, Enyi watu, kwani Mimi Bwana niliyoagiza ndani yake yatakamilika.

8 Na amini ninawaambia ninyi, kwamba wao waendeleao mbele, wakitangaza habari hizi kwa wakazi wa dunia, kwao uwezo umetolewa wa kufunga kote duniani na mbinguni, wale wasioamini na waasi;

9 Ndiyo, amini, kuwafungia wao hadi siku ile wakati ghadhabu ya Mungu itakapomwagwa juu ya waovu pasipo kipimo—

10 Hadi siku ile wakati Bwana atakapokuja kumlipa kila mtu kulingana na matendo yake, na kumpimia kila mtu kulingana na kipimo alichowapimia wanadamu wenzake.

11 Kwa hiyo sauti ya Bwana ni hata miisho ya dunia, kwamba wale wote watakaosikia na wasikie:

12 Jitayarisheni, jitayarisheni kwa lile ambalo laja, kwani Bwana yu karibu;

13 Na hasira ya Bwana inawaka, na upanga wake unaoshwa mbinguni, nao utawashukia wakazi wa dunia.

14 Na mkono wa Bwana utafunuliwa; na siku yaja kwamba wale ambao hawataisikia sauti ya Bwana, wala sauti ya watumishi wake, wala kutii maneno ya manabii na mitume, watakatiliwa mbali kutoka miongoni mwa watu;

15 Kwani wamepotoka kutoka kwenye ibada zangu, na wamevunja agano langu lisilo na mwisho;

16 Hawamtakii Bwana kuendeleza haki zake, bali kila mtu huenenda katika njia zake mwenyewe, na akifuata mfano wa mungu wake mwenyewe, ambaye ni mfano wa kitu cha duniani, na wa sanamu ya kuchonga, ambayo mali ghafi yake huzeeka na kuangamia katika Babiloni, hata Babiloni ile kuu, ambayo itaanguka.

17 Hivyo basi, Mimi Bwana, nikijua majanga yajayo juu ya wakazi wa dunia, nimemwita mtumishi wangu Joseph Smith, Mdogo, na kusema naye kutoka mbinguni, na nikampa yeye amri;

18 Na pia nikawapa amri wengine, kwamba yawalazimu kuyatangaza mambo haya duniani; na haya yote kwamba yapate kukamilika yale yaliyoandikwa na manabii—

19 Mambo dhaifu ya dunia yatakuja kuyavunja yale yaliyo makubwa na yenye nguvu, kwamba mwanadamu asimshauri mwanadamu mwenzake, wala asiutegemee mkono wa mwanadamu—

20 Bali kwamba kila mwanadamu aweze kuongea katika jina la Mungu Bwana, hata Mwokozi wa ulimwengu;

21 Kwamba imani pia ipate kuongezeka katika dunia;

22 Kwamba agano langu lisilo na mwisho liweze kuanzishwa;

23 Kwamba utimilifu wa injili yangu uweze kutangazwa na watu walio dhaifu na wa kawaida hata mwisho wa dunia, na mbele ya wafalme na watawala.

24 Tazama, Mimi ni Mungu; na nimeyasema haya; amri hizi ni zangu, na zilitolewa kwa watumishi wangu katika udhaifu wao, kwa namna ya lugha yao, kwamba wapate kuelewa.

25 Na hata wakikosea iweze kujulikana;

26 Na kadiri watakavyoitafuta hekima waweze kuelekezwa;

27 Na kadiri walivyotenda dhambi waweze kukemewa, ili waweze kutubu;

28 Na kadiri walivyokuwa wanyenyekevu waweze kufanywa imara, na kubarikiwa kutoka juu na kupokea maarifa mara kwa mara.

29 Baada ya kupokea kumbukumbu ya Wanefi, ndiyo, hata, mtumishi wangu Joseph Smith, Mdogo, kupata uwezo wa kutafsiri, Kitabu cha Mormoni, kwa rehema ya Mungu, na kwa uwezo wa Mungu, Kitabu cha Mormoni.

30 Na pia kwa wale ambao amri hizi zimetolewa, waweze kupata uwezo wa kuweka msingi wa kanisa hili, na kulitoa kutoka lisikoonekana na kutoka gizani, kanisa pekee la kweli na lililo hai katika uso wa dunia yote, ambalo Mimi, Bwana, napendezwa nalo, nikizungumza na kanisa kwa ujumla na siyo mmoja mmoja—

31 Kwani Mimi Bwana siwezi kuiangalia dhambi na kuivumilia hata kidogo;

32 Hata hivyo, yeye anayetubu na kutimiza amri za Bwana huyo atasamehewa;

33 Na yeye ambaye hatubu, kutoka kwake itachukuliwa hata ile nuru aliyoipokea; kwani Roho yangu haitashindana daima na mwanadamu, asema Bwana wa Majeshi.

34 Na tena, amini ninawaambia, Enyi wakazi wa dunia: Mimi Bwana ni radhi kufanya mambo haya yajulikane kwa watu wote;

35 Kwani siwapendelei watu, na ninataka watu wote wajue kwamba siku ile yaja haraka; saa ingali, lakini i karibu, wakati amani itakapoondolewa duniani, na ibilisi atakuwa na uwezo juu ya utawala wake mwenyewe.

36 Na pia Bwana atakuwa na uwezo juu ya watakatifu wake, naye atatawala katikati yao, na atashuka chini kwa hukumu juu ya Idumaya, au ulimwengu.

37 Zichunguzeni amri hizi, kwani ni za kweli na za kuaminika, na unabii na ahadi zilizomo ndani yake zote zitatimilizwa.

38 Kile ambacho Mimi Bwana nimesema, nimekisema, na wala sijutii, na ingawa mbingu na dunia zitapita, neno langu halitapita kamwe, bali litatimia, iwe kwa sauti yangu mwenyewe au kwa sauti ya watumishi wangu, yote ni sawa.

39 Kwani tazama, na lo, Bwana ni Mungu, na Roho hushuhudia, na ushuhuda wake ni wa kweli, na ukweli hudumu milele na milele. Amina.

Chapisha