Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 104


Sehemu ya 104

Ufunuo uliotolewa kwa Joseph Smith Nabii, huko Kirtland, Ohio au jirani na hapo, 23 Aprili 1834, juu ya Kampuni ya Ushirika, (ona vichwa vya habari sehemu ya 78 na 82). Tukio yawezekana lilikuwa lile la mkutano wa wanachama wa Kampuni ya Ushirika, ambao ulijadili mahitaji ya kimwili yaliyokuwa yakilisumbua Kanisa. Mkutano wa awali wa kampuni hiyo uliofanyika 10 Aprili ulikuwa umeazimia kampuni hiyo ivunjwe. Ufunuo huu unaelekeza kwamba kampuni badala yake iundwe upya; na mali zake zigawanywe miongoni mwa wanachama wa kampuni hiyo kama wasimamizi. Chini ya maelekezo ya Joseph Smith, jina Kampuni ya Ushirika liliachwa na badala yake lilitumika “Mpango wa Ushirika” katika ufunuo huu.

1–10, Watakatifu wanaovunja sheria za mpango wa ushirika watalaaniwa; 11–16, Bwana hutimiza mahitaji ya Watakatifu Wake katika njia Yake mwenyewe; 17–18, Sheria ya injili hutawala uangalizi wa maskini; 19–46, Usimamizi na baraka za ndugu mbali mbali zaonyeshwa; 47–53, Mpango wa ushirika huko Kirtland na mpango wa Sayuni zitatenda kazi tofauti; 54–66, Hazina takatifu ya Bwana imewekwa kwa ajili ya kuchapisha maandiko; 67–77, Hazina kuu ya mpango wa ushirika itatenda kazi juu ya msingi wa makubaliano; 78–86, Wale waliomo katika mpango wa ushirika watalipa madeni yao yote, na Bwana atawakomboa kutoka katika utumwa wa kifedha.

1 Amini ninawaambia, marafiki zangu, ninawapa ushauri, na amri, kuhusu mali zote ambazo ni za mpango ambao nimeamuru uundwe na kuanzishwa, ili uwe mpango wa ushirika, na mpango usio na mwisho kwa faida ya kanisa langu, na kwa ajili ya wokovu wa wanadamu hadi nitakapokuja—

2 Kwa ahadi isiyogeuka na isiyoweza kubadilika, kwamba kadiri wale ambao niliwaamuru walivyokuwa waaminifu wabarikiwe kwa baraka nyingi;

3 Lakini kadiri walivyokuwa siyo waaminifu walikuwa wamekaribia kwenye laana.

4 Kwa hiyo, kwa vile baadhi ya watumishi wangu hawakuzishika amri, bali wamevunja agano kwa tamaa mbaya, na maneno ya kutunga, mimi nimewalaani kwa laana kali na chungu.

5 Kwani Mimi, Bwana, nimeazimia moyoni mwangu, kwamba kadiri mtu yeyote aliye wa mpango huu atakavyoonekana kuwa mvunjaji wa sheria, au, kwa maneno mengine, atavunja agano ambalo kwalo amefungwa, atalaaniwa maishani mwake, na kukanyagwa na yeyote nitakayemtaka;

6 Kwa kuwa Mimi, Bwana, sidhihakiwi katika mambo haya—

7 Na hii yote ili asiye na hatia miongoni mwenu asipate kuhukumiwa pamoja na wasio na haki; na ili mwenye hatia miongoni mwenu asiweze kukwepa; kwa sababu Mimi, Bwana, nimewaahidi taji la utukufu katika mkono wangu wa kulia.

8 Kwa hiyo, kadiri mlivyoonekana kuwa wenye kuvunja sheria, hamwezi kuepuka ghadhabu yangu katika maisha yenu.

9 Na kadiri mlivyokatiliwa mbali kwa ajili ya uvunjaji wenu wa sheria, hamwezi kuepuka mapigo ya Shetani hadi siku ya ukombozi.

10 Nami sasa ninawapa uwezo kutoka saa hii hii, kama kuna mtu yeyote miongoni mwenu, wa mpango huu, atakayepatikana kuwa mvunjaji wa sheria na wala hatubu uovu huo, kwamba mtoeni aende kwenye mapigo ya Shetani; naye hatakuwa na uwezo wa kuleta uovu juu yenu.

11 Ni hekima kwangu; kwa hiyo, amri ninawapa ya kwamba mtajipanga wenyewe na kumgawia kila mtu usimamizi wake;

12 Ili kila mtu apate kutoa hesabu kwangu ya usimamizi wake aliogawiwa.

13 Kwani ni muhimu kwamba Mimi, Bwana, yanipasa kumfanya kila mtu awajibike, kama msimamizi juu ya baraka za kidunia, ambazo nimezifanya na kuzitayarisha kwa ajili ya viumbe vyangu.

14 Mimi, Bwana, nilizitandaza mbingu, na kuijenga dunia, kazi halisi ya mkono wangu; na vitu vyote vilivyomo ni mali yangu.

15 Na ni madhumuni yangu kuwa niwapatie mahitaji watakatifu wangu, kwani vitu vyote ni mali yangu.

16 Lakini haina budi kufanyika katika njia yangu mwenyewe; na tazama hii ndiyo njia ambayo Mimi, Bwana, nimeazimia kutoa mahitaji ya watakatifu wangu, ili maskini wapate kuinuliwa, na kwa njia hiyo matajiri hushushwa.

17 Kwani dunia imejaa, na viko vya kutosha na kubaki; ndiyo, nilitayarisha vitu vyote, na nikawapa wanadamu kuwa na uwezo wa kujiamulia wenyewe.

18 Kwa hiyo, kama mtu yeyote atajichukulia kutoka kwa hivyo vingi nilivyovitengeneza, na asiigawe hiyo sehemu yake, kulingana na sheria ya injili yangu, kwa maskini na wenye shida, yeye, pamoja na waovu, atainua macho yake e jehanamu, akiwa katika mateso.

19 Na sasa, amini ninawaambia, juu ya mali ya ushirika

20 Acha mtumishi wangu Sidney Rigdon apewe mahali ambapo anaishi sasa, na mahali pa kiwanja cha kiwanda cha ukaushaji wa ngozi kwa usimamizi wake, ili vimsaidie wakati akifanya kazi katika shamba langu la mizabibu, hata kama nitakavyotaka, wakati nitakapo mwamuru.

21 Na acha mambo yote yatendeke kulingana na maelezo ya ushirika, na ridhaa ya ushirika au sauti ya ushirika, ambao wanaishi katika nchi ya Kirtland.

22 Na usimamizi huu na baraka hii, Mimi, Bwana ninatoa juu ya mtumishi wangu Sidney Rigdon kama baraka juu yake, na uzao wake baada yake;

23 Nami nitazidisha baraka juu yake, kadiri yeye atakavyokuwa mnyenyekevu mbele zangu.

24 Na tena, acha mtumishi wangu Martin Harris akabidhiwe, kwa ajili ya usimamizi wake, kiwanja cha ardhi ambacho mtumishi wangu John Johnson alikipata kwa kubadilishana na urithi wake wa awali, kwa ajili yake na uzao wake baada yake;

25 Na ilimradi ni mwaminifu, nitamzidishia baraka juu yake na uzao wake baada yake.

26 Na acha mtumishi wangu Martin Harris atoe fedha zake kwa ajili ya kuyatangaza maneno yangu, kulingana na vile mtumishi wangu Joseph Smith, Mdogo, atakavyomwelekeza.

27 Na tena, acha mtumishi wangu Frederick G. Williams apate sehemu ambayo sasa anaishi.

28 Na acha mtumishi wangu Oliver Cowdery apate kiwanja ambacho kimejitenga lakini karibu na nyumba, ambayo itakuwa kwa ajili ya ofisi ya uchapishaji, ambacho ni kiwanja nambari moja, na pia kiwanja ambacho juu yake baba yake anakaa.

29 Na acha watumishi wangu Frederick G. Williams na Oliver Cowdery wapate ofisi ya uchapishaji na vitu vyote vihusikanavyo.

30 Na huu utakuwa usimamizi wao watakaokabidhiwa.

31 Na kadiri watakavyokuwa waaminifu, tazama nitawabariki, na kuzidisha baraka juu yao.

32 Na huu ndiyo mwanzo wa usimamizi niliowakabidhi wao, kwa ajili yao na uzao wao baada yao.

33 Na, kadiri watakavyokuwa waaminifu, nitazidisha baraka juu yao na uzao wao baada yao, hata wingi wa baraka.

34 Na tena, acha mtumishi wangu John Johnson achukue nyumba ambayo sasa anaishi, na kwa urithi, na kila kitu isipokuwa ardhi iliyotengwa kwa ujenzi wa nyumba zangu, ambayo ni sehemu ya urithi huo, na viwanja vile ambavyo viliwekwa kwa ajili ya mtumishi wangu Oliver Cowdery.

35 Na kadiri atakavyokuwa mwaminifu, nitazidisha baraka juu yake.

36 Na ni mapenzi yangu kwamba auze viwanja vile vilivyopimwa na kutengwa kwa ajili ya ujenzi wa mji wa watakatifu wangu, kadiri itakavyojulishwa kwake kwa sauti ya Roho, na kulingana na maelekezo ya ushirika, na kwa sauti ya ushirika.

37 Na huu ndiyo mwanzo wa usimamizi ambao nimemkabidhi, kwa ajili ya baraka kwake na uzao wake baada yake.

38 Na kadiri atakavyokuwa mwaminifu, nitazidisha wingi wa baraka juu yake.

39 Na tena, acheni mtumishi wangu Newel K. Whitney akabidhiwe nyumba na kiwanja ambamo sasa anaishi, na kiwanja na jengo ambamo ndani yake biashara hufanyika, na pia kiwanja kilichoko kwenye kona ya kusini mwa stoo ya biashara, na pia kiwanja ambacho kipo kiwanda cha majivu.

40 Na hii yote nimeikabidhi kwa mtumishi wangu Newel K. Whitney kwa ajili ya usimamizi wake, kama baraka juu yake na uzao wake baada yake, kwa manufaa ya biashara za ushirika wangu ambao nimeuanzisha kwa ajili ya kigingi changu katika nchi ya Kirtland.

41 Ndiyo, amini, huu ndiyo usimamizi nilioukabidhi kwa mtumishi wangu N. K. Whitney, hata hii biashara yote, yeye na wakala wake, na uzao wake baada yake.

42 Na kadiri atakavyokuwa mwaminifu katika kushika amri zangu, ambazo nimezitoa kwake, nitazidisha baraka juu yake na uzao wake baada yake, hata wingi wa baraka.

43 Na tena, acha mtumishi wangu Joseph Smith, Mdogo, nimemkabidhi kiwanja ambacho kimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba yangu, ambacho ni karibu mita mia mbili urefu na sitini upana, na pia urithi ambao juu yake baba yake anaishi sasa;

44 Na huu ndiyo mwanzo wa usimamizi ambao nimemkabidhi, kama baraka juu yake, na juu ya baba yake.

45 Tazama, nimeutunza urithi kwa ajili ya baba yake, kwa ajili ya kumsaidia; kwa hiyo atatambulika katika nyumba ya mtumishi wangu Joseph Smith, Mdogo.

46 Nami nitazidisha baraka juu ya nyumba hiyo ya mtumishi wangu Joseph Smith, Mdogo, kadiri atakavyokuwa mwaminifu, hata wingi wa baraka.

47 Na sasa, amri ninatoa kwenu juu ya Sayuni, kwamba ninyi hamtafungwa kuanzia sasa kama ushirika na ndugu zenu wa Sayuni, isipokuwa tu katika hekima hii—

48 Baada ya kuwa mmejipanga, mtakuwa mkiitwa Mpango wa Ushirika wa Kigingi cha Sayuni, katika Mji wa Kirtland. Na ndugu zenu, baada ya kuwa wamejipanga, watakuwa wakiitwa Mpango wa Ushirika wa Mji wa Sayuni.

49 Na watakuwa wamejipanga katika majina yao wenyewe, na katika majina yao wenyewe; nao watakuwa wakifanya shughuli zao katika jina lao wenyewe, na katika majina yao wenyewe;

50 Nanyi mtafanya shughuli zenu katika jina lenu wenyewe, na katika majina yenu wenyewe.

51 Na hii nimeamuru lifanyike kwa ajili ya wokovu wenu, na pia kwa ajili ya wokovu wao, kama matokeo ya kufukuzwa kwao na lile linalokuja.

52 Kuvunjwa kwa maagano kwa njia ya uvunjaji wa sheria, kwa tamaa mbaya na maneno ya kutunga—

53 Kwa hiyo, mmevunjwa kama mpango wa ushirika pamoja na ndugu zenu, kwamba hamjafungwa nao hadi hivi sasa tu, ni katika njia hii tu, kama nilivyosema, kwa mkopo kama itakavyokubalika na ushirika huu katika baraza, kama hali yenu itakavyoruhusu na sauti ya baraza itakavyoelekeza.

54 Na tena, amri ninaitoa kwenu juu ya usimamizi ambao nimewachagulia.

55 Tazama, mali hizo zote ni mali yangu, au vinginevyo imani yenu ni bure, nanyi mtaonekana kuwa ni wanafiki, na maagano mliyoyafanya kwangu yamevunjika;

56 Na kama mali hizo ni zangu, hivyo basi ninyi ni wasimamizi; vinginevyo ninyi si wasimamizi.

57 Lakini, amini ninawaambia, nimewateua ninyi kuwa wasimamizi juu ya nyumba yangu, hata wasimamizi wa kweli.

58 Na kwa dhumuni hili nimewaamuru kujipanga wenyewe, hata kwa kuchapa maneno yangu, utimilifu wa maandiko yangu, mafunuo ambayo nimeyatoa kwenu ninyi, na ambayo nitayatoa, baadaye, kwa nyakati tofauti nitayatoa kwenu—

59 Kwa dhumuni la kulijenga kanisa na ufalme wangu juu ya dunia, na kuwaandaa watu wangu kwa ajili ya wakati nitakapokuja kukaa pamoja nao, wakati ambao u karibu.

60 Na mtajitayarishia wenyewe mahali kwa ajili ya hazina, na kupaweka wakfu kwa jina langu.

61 Na mtateua mmoja miongoni mwenu kuitunza hazina hiyo, naye atawazwe kwa baraka hii.

62 Na pawepo lakiri juu ya hazina, na vitu vyote vitakatifu vitawekwa katika hazina; na hakuna mtu miongoni mwenu atakayeiita mali yake mwenyewe, au sehemu yoyote ya hazina hiyo, kwa kuwa itakuwa ni mali yenu ninyi nyote kwa pamoja.

63 Na ninaitoa kwenu ninyi kutoka hivi sasa; na sasa angalieni, kwamba mnaenda na kufanya matumizi ya usimamizi wenu ambao nimewachagulia, isipokuwa kwa mambo matakatifu, kwa ajili ya dhumuni la uchapishaji wa mambo haya matakatifu kama nilivyosema.

64 Na mapato yatokanayo na mambo haya matakatifu yawekwe katika hazina, na lakiri iwe juu yake; na haitatumika au kutolewa nje ya hazina na yeyote, wala lakiri yake itakayowekwa juu yake isilegezwe, isipokuwa tu kwa sauti ya ushirika, au kwa amri.

65 Na hivyo ndivyo mtavyotunza mapato ya mambo matakatifu katika hazina, kwa ajili ya madhumuni yaliyo matakatifu.

66 Na hii itaitwa hazina takatifu ya Bwana; na lakiri itawekwa juu yake ili iweze kuwa takatifu na kuwekwa wakfu kwa Bwana.

67 Na tena, itatayarishwa hazina nyingine, na mtunza hazina ateuliwe wa kutunza hazina, na lakiri itawekwa juu yake;

68 Na fedha zote ambazo mnazipokea katika usimamizi wenu, kwa kuboresha mali ambazo nimewakabidhi, katika majumba, au katika ardhi, au katika ngʼombe, au katika vitu vyote isipokuwa katika maandiko matakatifu na yaliyo ya Mungu, ambayo nimeyaacha kwangu mimi mwenyewe kwa ajili ya madhumuni yaliyo matakatifu, zitawekwa ndani ya hazina haraka mara upokeapo fedha hizo, kwa mamia, au kwa hamsini hamsini, au kwa ishirini ishirini, au kwa makumi, au kwa tano tano.

69 Au katika maneno mengine, kama mtu yeyote miongoni mwenu anapata dola tano na acheni aziweke katika hazina, au kama akipata dola kumi, au ishirini, au hamsini, au mia moja, acha afanye vivyo hivyo;

70 Na acheni pasiwe na yeyote miongoni mwenu atakayesema kwamba ni yake mwenyewe; kwa kuwa haitaitwa yake, wala hata sehemu yake.

71 Na isitumiwe sehemu yake yoyote, au kuchukuliwa kutoka kwenye hazina, isipokuwa tu kwa sauti na ridhaa ya ushirika.

72 Na hii itakuwa sauti na ridhaa ya ushirika—kwamba mtu yeyote miongoni mwenu atamwambia mtunza hazina: Nina shida ya kitu hiki ili kunisaidia katika usimamizi wangu—

73 Kama itakuwa dola tano, au kama itakuwa dola kumi, au ishirini, au hamsini, au mia, mtunza hazina atampa yeye kiasi ambacho anakihitaji ili kumsaidia katika usimamizi wake—

74 Hadi atakapopatikana kuwa mvunja sheria, na kudhihirika mbele ya baraza la ushirika kwa uwazi kwamba siyo mwaminifu na mtumishi asiye na hekima.

75 Lakini ilimradi yeye yu katika ushirika mkamilifu, na ni mwaminifu na mwenye hekima katika usimamizi wake, hii ndiyo itakuwa ishara yake kwa mtunza hazina ili mtunza hazina asimnyime.

76 Lakini katika hali ya uvunjaji wa sheria, mtunza hazina atawajibika kwa baraza na sauti ya ushirika.

77 Na ikiwa mtunza hazina ataonekana si mwaminifu na si mtumishi mwenye hekima, atawajibika kwa baraza na sauti ya ushirika, naye ataondolewa kutoka nafasi yake, na mwingine atateuliwa badala yake.

78 Na tena, amini ninawaambia, juu ya madeni yenu—tazama, ni mapenzi yangu kuwa mlipe madeni yenu yote.

79 Na ni mapenzi yangu kuwa mtajinyenyekeza wenyewe mbele zangu, na kupata baraka hii kwa juhudi yenu na unyenyekevu na sala ya imani.

80 Na kadiri mtakavyokuwa wenye bidii na wanyenyekevu, na kutumia sala ya imani, tazama, nitailainisha mioyo ya wale wadeni wenu, hadi nitakapowaletea njia kwa ajili ya ukombozi wenu.

81 Kwa hiyo andika haraka kwa New York na andika kulingana na kile Roho atachosema; nami nitailainisha mioyo ya wale wanaowadai, ili iweze kuondolewa kutoka akilini mwao mawazo ya kuleta mateso juu yenu.

82 Na kadiri mtakavyokuwa wanyenyekevu na waaminifu na kulilingana jina langu, tazama, nitawapatia ushindi.

83 Ninatoa kwenu ahadi, kwamba mtakombolewa mara moja hii kutoka utumwani mwenu.

84 Kadiri utakavyopata nafasi ya kukopa fedha kwa mamia, au maelfu, hata hadi utakopa mkopo wa kutosha kujikomboa mwenyewe kutoka utumwani, ni nafasi yako.

85 Na kuweka rehani mali ambazo nimeziweka mikononi mwako, mara hii moja, kwa kutoa majina yenu kwa ridhaa ya wote au vinginevyo, kama itakavyoonekana kuwa vyema kwenu ninyi.

86 Ninatoa kwenu nafasi hii, mara hii moja; na tazama, kama utaenda kufanya mambo ambayo nimeyaweka mbele yenu, kulingana na amri zangu, vitu hivi vyote ni vyangu, nanyi ni watumishi wangu, na bwana hatakubali nyumba yake ivunjwe. Hivyo ndivyo. Amina.