Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 55


Sehemu ya 55

Ufunuo uliotolewa kupitia Joseph Smith Nabii kwa William W. Phelps, huko Kirtland, Ohio, 14 Juni 1831. William W. Phelps, mchapishaji, na familia yake walikuwa wamewasili hivi karibuni huko Kirtland, na Nabii alimwomba Bwana taarifa juu yake.

1–3, William W. Phelps ameitwa na kuteuliwa kubatizwa, kutawazwa kuwa mzee, na kuhubiri injili; 4, Pia ataandika vitabu vya watoto katika shule za Kanisa; 5–6, Yeye atasafiri kwenda Missouri, mahali ambako litakuwa eneo lake la kazi.

1 Tazama, hivyo ndivyo asemavyo Bwana kwako, mtumishi wangu William, ndiyo, hata Bwana wa dunia yote, wewe umeitwa na umeteuliwa; na baada ya kuwa umebatizwa kwa maji, kitu ambacho ukikifanya na jicho lako likiwa kwenye utukufu wangu pekee, utapata ondoleo la dhambi zako, na utampokea Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono;

2 Na halafu utatawazwa kwa mkono wa mtumishi wangu Joseph Smith, Mdogo, kuwa mzee katika kanisa hili, ili kuhubiri toba na ondoleo la dhambi kwa njia ya ubatizo katika jina la Yesu Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.

3 Na kwa wale wote utakaowawekea mikono yako, kama watajuta mbele zangu, utakuwa na uwezo wa kuwapa Roho Mtakatifu.

4 Na tena, utatawazwa kumsaidia mtumishi wangu Oliver Cowdery kufanya kazi ya kuchapa, na kuchagua na kuandika vitabu kwa ajili ya shule za kanisa hili, ili kwamba watoto wadogo nao waweze kupokea maelekezo mbele zangu kama inipendezavyo.

5 Na tena, amini ninakuambia, kwa sababu hii utafanya safari yako pamoja na watumishi wangu Joseph Smith, Mdogo, na Sidney Rigdon, ili uweze kuwekwa katika nchi ya urithi wako kwa kufanya kazi hii.

6 Na tena, na mtumishi wangu Joseph Coe pia ashike safari yake pamoja nao. Mabaki yatafunuliwa baadaye, kadiri nitakavyotaka. Amina.

Chapisha