Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 111


Sehemu ya 111

Ufunuo uliotolewa kupitia Joseph Smith Nabii, huko Salem, Massachusetts, 6 Agosti 1836. Wakati huu viongozi wa Kanisa walikuwa katika deni kubwa kutokana na kazi zao katika huduma. Kwa kuwa walisikia kwamba kiasi kikubwa cha fedha kitapatikana kwao huko Salem, Nabii, Sidney Rigdon, Hyrum Smith, na Oliver Cowdery walisafiri kwenda huko kutoka Kirtland, Ohio, ili kuchunguza dai hili, pamoja na kuhubiri injili. Ndugu hawa walitimiza shughuli kadhaa za Kanisa na kufanya mahubiri. Wakati ilipokuja kujulikana wazi kwamba hapakuwa na fedha yoyote itakayokuja, walirejea Kirtland. Sehemu muhimu kadhaa katika historia hii zimeelezwa katika maneno yaliyotumiwa katika ufunuo huu.

1–5, Bwana huangalia mahitaji ya kimwili ya watumishi Wake; 6–11, Kwa rehema, ataitendea Sayuni na kupanga mambo yote kwa faida ya watumishi Wake.

1 Mimi, Bwana Mungu wenu, siyo kwamba sijapendezwa na kuja kwenu katika safari hii, licha ya upuuzi wenu.

2 Ninayo hazina kubwa katika mji huu kwa ajili yenu, kwa faida ya Sayuni, na watu wengi katika mji huu, ambao nitawakusanya katika wakati wake kwa faida ya Sayuni, kwa kuwatumia ninyi.

3 Kwa hiyo, ninyi hamna budi kuzoeana na watu wa mji huu, kama vile mtakavyoongozwa, na kama vile mtakavyopewa.

4 Na itakuwa kwamba katika wakati wake nitautoa mji huu mikononi mwenu, kwamba mtakuwa na uwezo juu yake, kiasi kwamba wao hawatagundua siri zenu; na utajiri wake unaohusu dhahabu na fedha utakuwa wenu.

5 Msijisumbue juu ya madeni yenu, kwani nitawapa uwezo wa kuyalipa.

6 Msisumbuke kuhusu Sayuni, kwani nitamrehemu.

7 Kaeni mahali hapa, na katika maeneo ya karibu;

8 Na mahali ambapo nitapenda ninyi mkae, kwani sehemu kubwa, itaonyeshwa kwenu kwa amani na uwezo wa Roho yangu, ambayo itamiminika kwenu.

9 Sehemu hii mtaweza kuipata kwa kuikodi. Na ulizeni kwa bidii juu ya wakazi wa kale zaidi na waanzilishi wa mji huu;

10 Kwani ziko hazina nyingi zaidi ya moja kwa ajili yenu katika mji huu.

11 Basi, muwe na busara kama nyoka lakini pasipo kuwa na dhambi; nami nitayapanga mambo yote kwa faida yenu, haraka kadiri mtakavyoweza kuyapokea. Amina.

Chapisha