Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 97


Sehemu ya 97

Ufunuo uliotolewa kupitia Joseph Smith Nabii, huko Kirtland, Ohio, 2 Agosti 1833. Ufunuo huu unashughulika hususani na mambo ya Watakatifu katika Sayuni, Wilaya ya Jackson, Missouri, katika jibu la maombi ya Nabii kwa Bwana juu ya taarifa. Waumini wa Kanisa huko Missouri kwa wakati huu walikuwa chini ya mateso makali na, mnamo tarehe 23 Julai 1833, walikuwa wamelazimishwa kuweka saini makubaliano ya kuhama Wilaya ya Jackson.

1–2, Watakatifu wengi katika Sayuni (Wilaya ya Jackson, Missouri) wanabarikiwa kwa ajili ya uaminifu wao; 3–5, Parley P. Pratt anapongezwa kwa kazi yake ya shule katika Sayuni; 6–9, Wale wanaotunza maagano yao wanakubaliwa na Bwana; 10–17, Nyumba na ijengwe katika Sayuni ambamo ndani yake wale walio safi moyoni watamwona Mungu; 18–21, Sayuni ni walio safi moyoni; 22–28, Sayuni ataepuka adhabu ya Bwana kama atakuwa mwaminifu.

1 Amini ninawaambia marafiki zangu, ninasema nanyi kwa sauti yangu, hata sauti ya Roho yangu, ili niweze kuonyesha kwenu mapenzi yangu juu ya ndugu zenu katika nchi ya Sayuni, wengi wao ni wanyenyekevu wa kweli na wanatafuta kwa bidii kujifunza hekima na kupata ukweli.

2 Amini, amini ninawaambia, heri hao, kwani watapata; kwa kuwa Mimi, Bwana, huonyesha huruma kwa wote walio wapole, na juu ya wale wote nitakao, ili niweze kuhukumu kwa haki wakati niwaletapo wao kwenye hukumu.

3 Tazama, ninawaambia, juu ya shule katika Sayuni, Mimi, Bwana, ninapendezwa kuwa pawepo shule katika Sayuni, na pia pamoja na mtumishi wangu Parley P. Pratt, kwa kuwa yeye hukaa ndani yangu.

4 Na kadiri yeye atakavyoendelea kukaa ndani yangu ataendelea kuisimamia shule katika nchi ya Sayuni hadi nitakapotoa kwake amri nyingine.

5 Nami nitambariki yeye kwa baraka nyingi zaidi, katika kuyaeleza maandiko na siri zote kwa kuijenga shule, na kanisa katika Sayuni.

6 Na kwa mabaki ya shule, Mimi, Bwana, niko radhi kuonyesha huruma; hata hivyo, kuna wale ambao ni lazima kuwarudi, na matendo yao yatafanywa yajulikane.

7 Na shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni. Mimi, Bwana, nimesema.

8 Amini ninawaambia, wote miongoni mwao wale ambao wanajua kuwa mioyo yao ni ya uaminifu, na imevunjika, na roho zao zimepondeka, na wako radhi kuyatunza maagano yao kwa dhabihu—ndiyo, kila dhabihu ambayo Mimi, Bwana, nitaamuru—wanakubaliwa kwangu.

9 Kwani, Mimi, Bwana, nitawafanya wazae kama mti uzaao matunda ambao umepandwa katika ardhi nzuri, kando kando ya vijito vya maji, uzaao matunda yaliyo mazuri sana.

10 Amini ninawaambia, kwamba ni mapenzi yangu kuwa nyumba ijengwe kwa ajili yangu katika nchi ya Sayuni, kulingana na vipimo ambavyo nimewapa.

11 Ndiyo, na ijengwe haraka, kwa zaka ya watu wangu.

12 Tazama, hii ndiyo zaka na dhabihu ambayo Mimi, Bwana, nayataka kutoka kwao, ili paweze kujengwa nyumba kwa ajili ya wokovu wa Sayuni—

13 Mahali pa shukrani kwa watakatifu wote, na mahali pa mafundisho kwa wale wote walioitwa kufanya kazi ya huduma katika miito na ofisi zao zote mbalimbali;

14 Ili waweze kukamilishwa katika ufahamu wa huduma zao, katika nadharia, katika kanuni, na katika mafundisho, katika mambo yote yahusuyo ufalme wa Mungu juu ya dunia, ufalme ambao funguo zake zimewekwa juu yenu.

15 Na ilimradi watu wangu wakinijengea nyumba katika jina la Bwana, na ikiwa hawataruhusu kitu chochote kichafu kuingia ndani yake, ili isichafuliwe, utukufu wangu utatulia juu yake;

16 Ndiyo, na uwepo wangu utakuwa ndani yake, kwa kuwa nitakuja ndani yake, na wote walio safi moyoni ambao watakuja ndani yake watamwona Mungu.

17 Lakini kama itachafuliwa sitakuja ndani yake, na utukufu wangu hautakuwa humo; kwa kuwa sitakuja ndani ya mahekalu yasiyo matakatifu.

18 Na, sasa, tazama, kama Sayuni itafanya mambo haya itastawi, na kujipanua na kuwa tukufu sana, kuu sana, na ya kutisha sana.

19 Na mataifa ya dunia yatamheshimu, na yatasema: Hakika Sayuni ni mji wa Mungu wetu, na hakika Sayuni haiwezi kuanguka, wala kuondolewa katika mahali pake, kwa kuwa Mungu yuko pale na mkono wa Bwana uko pale;

20 Na ameapa kwa uwezo wa nguvu zake kuwa wokovu wake na mnara wake mrefu.

21 Kwa hiyo, amini, hivyo ndivyo asemavyo Bwana, Sayuni na ifurahi, kwani hii ndiyo Sayuniwalio safi moyoni; kwa hiyo, Sayuni na ifurahi, wakati waovu wote wataomboleza.

22 Kwani tazama, na lo, kisasi chaja upesi juu ya wasiomcha Mungu kama kimbunga; na ni nani atakayekiepuka?

23 Adhabu ya Bwana itapita usiku na mchana, na habari yake itawaudhi watu wote; ndiyo, haitazuiliwa hadi ajapo Bwana;

24 Kwani uchungu wa Bwana unawaka dhidi ya machukizo yao na matendo yao yote ya uovu.

25 Hata hivyo, Sayuni ataepuka kama atajitahidi kutenda mambo yote niliyomwamuru yeye.

26 Lakini kama hatajitahidi kufanya chochote nilichomwamuru, nitamtembelea yeye kulingana na matendo yake, kwa mateso makali, kwa tauni, kwa baa, kwa upanga, kwa kisasi, kwa moto uangamizao.

27 Hata hivyo, na isomwe mara hii ya kwanza masikioni mwake, kwamba Mimi, Bwana, nimeyakubali matoleo yake; na kama hatatenda dhambi tena hakuna jambo lolote katika haya litakalo mpata;

28 Na nitambariki kwa baraka, na kuongeza wingi wa baraka juu yake, na juu ya vizazi vyake milele na milele, asema Bwana Mungu wenu. Amina.