Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 19


Sehemu ya 19

Ufunuo uliotolewa kupitia Joseph Smith, huko Manchester, New York, yawezekana kabisa ilikuwa katika kiangazi cha 1829. Katika historia yake, Nabii alitambulisha hii kama “amri ya Mungu na siyo ya mwanadamu, kwa Martin Harris, iliyotolewa na yeye aliye wa Milele.”

1–3, Kristo anao uwezo wote; 4–5, Watu wote lazima watubu au wateseke; 6–12, Adhabu ya milele ni adhabu ya Mungu; 13–20, Kristo aliteseka kwa ajili ya wote, kwamba wao wasiteseke kama watatubu; 21–28, Hubiri injili ya toba; 29–41, Tangaza habari njema.

1 Mimi ni Alfa na Omega, Kristo Bwana; ndiyo, Mimi ndiye, mwanzo na mwisho, Mkombozi wa ulimwengu.

2 Mimi, nikiwa nimefanikisha na kutimiza mapenzi yake yeye niliye wake, hata Baba, juu yangu—nikiwa nimefanya hili ili niweze kuvitiisha vitu vyote chini yangu—

3 Nikishikilia nguvu zote, hata ya kumwangamiza Shetani na kazi zake hapo mwisho wa dunia, na siku ile kuu ya hukumu, ambayo nitaipitisha juu ya wakazi wake, nikimhukumu kila mtu kulingana na kazi zake na matendo ambayo ameyafanya.

4 Na ni hakika kila mwanadamu ni lazima atubu au ateseke, kwani Mimi, Mungu, sina mwisho.

5 Kwa hiyo sijafuta hukumu ambayo nitaipitisha, lakini huzuni itajitokeza, kilio, kuomboleza na kusaga meno, ndiyo, kwa wale ambao watapatikana katika mkono wangu wa kushoto.

6 Hata hivyo, haikuandikwa kwamba hapatakuwa na mwisho wa mateso haya, bali imeandikwa mateso yasiyo na mwisho.

7 Tena, imeandikwa laana ya milele; kwa hiyo hii ni wazi zaidi kuliko maandiko mengine, ili liweze kufanya kazi katika mioyo ya wanadamu, kwa ajili ya utukufu wa jina langu.

8 Kwa hivyo, nitakuelezea wewe siri hii, kwani ni muhimu kwako kujua hata kama mitume wangu.

9 Ninasema kwenu ninyi ambao mmechaguliwa katika jambo hili, kama vile mmoja, ili kwamba muweze kuingia katika pumziko langu.

10 Kwani, tazama, siri ya uchamungu, ni kuu namna gani! Kwani, tazama, Mimi sina mwisho, na adhabu iliyotolewa kutoka mikononi mwangu ni adhabu isiyo na mwisho, kwani Bila mwisho ndilo jina langu. Kwa hiyo—

11 Adhabu ya milele ni adhabu ya Mungu.

12 Adhabu isiyo na mwisho ni adhabu ya Mungu.

13 Kwa hiyo, ninakuamuru wewe kutubu, na kuzishika amri ambazo umezipokea kwa mkono wa mtumishi wangu Joseph Smith, Mdogo, katika jina langu;

14 Na ni kwa uwezo wangu mkuu kwamba mmeyapata hayo;

15 Kwa sababu hii ninakuamuru wewe kutubu—tubu, nisije nikakupiga kwa fimbo ya kinywa changu, na ghadhabu yangu, na kwa hasira yangu, na mateso yako kuwa machungu—machungu namna gani hujui, makali namna gani hujui, ndiyo, namna gani magumu kuyavumilia hujui.

16 Kwani tazama, Mimi, Mungu nimeteseka mambo haya kwa ajili ya wote, ili kwamba wasipate kuteseka kama watatubu;

17 Lakini kama hawatatubu lazima wateseke hata kama Mimi;

18 Mateso ambayo yaliyosababisha Mimi mwenyewe, hata Mungu, mkuu kuliko yote, kutetemeka kwa sababu ya maumivu, na kutoka damu kwenye kila kinyweleo, na kuteseka mwili na roho—na kutamani nisinywe kikombe kichungu, na kusita—

19 Hata hivyo, utukufu na uwe kwa Baba, na Mimi nikachukua na kukamilisha maandalizi yangu kwa wanadamu.

20 Kwa hiyo, ninakuamuru tena kutubu, nisije nikakunyenyekeza wewe kwa uwezo wangu mkuu; na kwamba ukiri dhambi zako, usije ukateseka kwa adhabu hizi ambazo nimezisema, ambazo katika udogo wake, ndiyo, hata katika kiwango kidogo ulionja wakati ule Mimi nilipomwondoa Roho yangu.

21 Na ninakuamuru wewe usihubiri chochote bali toba, na usiyaonyeshe mambo haya kwa ulimwengu mpaka itakapokuwa hekima kwangu.

22 Kwani hao hawaiwezi nyama sasa, bali maziwa lazima wapate; kwa sababu hiyo, wao ni lazima wasiyajue mambo haya, wasije wakaangamia.

23 Jifunze kwangu, na sikiliza maneno yangu; enenda katika unyenyekevu wa Roho yangu, na utapata amani kwangu.

24 Mimi ni Yesu Kristo; nilikuja kwa mapenzi ya Baba, na ninafanya mapenzi yake.

25 Na tena, ninakuamuru wewe, kwamba usitamani mke wa jirani yako; wala kutafuta maisha ya jirani yako.

26 Na tena, ninakuamuru kwamba usitamani mali yako mwenyewe, bali itoe bure kwa uchapishaji wa Kitabu cha Mormoni, ambacho kina ukweli wa neno la Mungu—

27 Ambacho ni neno langu kwa Myunani, kwamba karibu kitaweza kwenda kwa Myahudi, ambao kwao Walamani ni baki, ili waweze kuiamini injili, na wasitazamie kuja kwa Masiya ambaye tayari amekuja.

28 Na tena, ninakuamuru kwamba itakupasa kusali kwa sauti na pia katika moyo wako; ndiyo, mbele ya umati na vile vile sirini, katika hadhara na pia kibinafsi.

29 Na wewe utatangaza habari njema, ndiyo, uitangaze juu ya milima, na juu ya kila mwinuko, na miongoni mwa kila watu ambao utaruhusiwa kuwaona.

30 Na utafanya kwa unyenyekevu wote, ukiamini katika Mimi, usitukane dhidi ya wenye kutukana.

31 Na juu ya imani wewe usizungumzie, bali wewe utatangaza toba na imani juu ya Mwokozi, na ondoleo la dhambi kwa ubatizo, na kwa moto, ndivyo, hata Roho Mtakatifu.

32 Tazama, hii ni kuu na amri ya mwisho ambayo nitakupa wewe kuhusiana na jambo hili; kwani hili litatosha kwa matembezi yako ya kila siku, hata mwisho wa maisha yako.

33 Na mateso utapata kama utapuuza ushauri huu, ndiyo, hata maangamizo yako mwenyewe na mali yako.

34 Toa sehemu ya mali yako, ndiyo, hata sehemu ya ardhi yako, na yote isipokuwa ya kutegemeza familia yako.

35 Lipa deni ambalo ulikubaliana na mchapishaji. Jiondoe mwenyewe kutoka kwenye utumwa.

36 Ondoka nyumbani mwako, isipokuwa wakati wewe utakapotamani kuiona familia yako;

37 Na sema kwa uhuru na wote; ndiyo, hubiri, shawishi, tangaza ukweli, hata kwa sauti kubwa, na kwa sauti ya furaha, paza sauti—Hosana, hosana, libarikiwe jina la Bwana Mungu!

38 Omba daima, na Mimi nitakumwagia Roho yangu juu yako, na baraka kubwa itakuwa juu yako—ndiyo, hata zaidi kuliko kama ungelipata hazina za dunia na uozo uliomo ndani yake.

39 Tazama, unaweza wewe kusoma haya bila kufurahi na kuinua moyo wako kwa furaha?

40 Au waweza wewe kukimbia mwendo mrefu kama kiongozi kipofu?

41 Au waweza wewe kuwa mnyenyekevu na msikivu, na kujiendesha mwenyewe kwa hekima mbele zangu? Ndiyo, uje kwangu Mimi Mwokozi wako. Amina.

Chapisha