Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 75


Sehemu ya 75

Ufunuo uliotolewa kupitia Joseph Smith Nabii, huko Amherst, Ohio, 25 Januari 1832. Sehemu hii ina mafunuo mawili tofauti (wa kwanza ni katika aya ya 1 hadi ya 22 na wa pili ni katika aya ya 23 hadi 36) yalitolewa siku hiyo hiyo, Tukio lilikuwa la mkutano ambapo Joseph Smith alikubaliwa na kutawazwa kuwa Rais wa Ukuhani Mkuu. Wazee kadhaa walitamani kujua zaidi juu ya kazi zao kwa wakati huo. Mafunuo haya yalifuata.

1–5, Wazee waaminifu ambao wanaihubiri injili watapata uzima wa milele; 6–12, Ombeni ili muweze kumpokea Mfariji, afundishaye mambo yote; 13–22, Wazee watawahukumu wale walioukataa ujumbe wao; 23–36, Familia za wamisionari zitapata msaada kutoka Kanisani.

1 Amini, amini, ninawaambia, Mimi nisemaye hata kwa sauti ya Roho wangu, Alfa na Omega, Bwana wenu na Mungu wenu—

2 Sikilizeni, Enyi mliotoa majina yenu kwenda kutangaza injili yangu, na kupogoa shamba langu la mizabibu.

3 Tazama, ninawaambia kuwa ni mapenzi yangu kuwa ninyi mwende na wala msibaki, wala msikae bure pasipo kazi bali fanyeni kazi kwa nguvu zenu—

4 Mkipaza sauti zenu kama tarumbeta, mkitangaza ukweli kulingana na mafunuo na amri ambazo nimewapa.

5 Na hivyo, endapo mtakuwa waaminifu mtabebeshwa miganda mingi, na kuvikwa heshima, na utukufu, na kutokufa, na uzima wa milele.

6 Kwa sababu hiyo, amini ninamwambia mtumishi wangu William E. McLellin, ninaifuta kazi niliyoitoa kwake ya kwenda nchi ya mashariki;

7 Na Mimi naitoa kwake kazi mpya na amri mpya, ambayo kwayo Mimi, Bwana, ninamrudi kwa sababu ya manungʼuniko ya moyoni mwake;

8 Na ametenda dhambi; hata hivyo, ninamsamehe na kumwambia tena, Nenda katika nchi za kusini.

9 Na mtumishi wangu Luke Johnson aende pamoja naye, na watangaze mambo ambayo nimewaamuru—

10 Wakililingana jina la Bwana, kwa Mfariji, ambaye atawafundisha mambo yote yaliyo muhimu kwao—

11 Wakisali daima ili wasikate tamaa; kadiri watakavyofanya haya, nitakuwa pamoja nao hata mwisho.

12 Tazama, haya ndiyo mapenzi ya Bwana Mungu wenu juu yenu. Hivyo ndivyo. Amina.

13 Na tena, amini hivyo ndivyo asemavyo Bwana, na mtumishi wangu Orson Hyde na mtumishi wangu Samuel H. Smith wafanye safari yao katika nchi za mashariki, na kutangaza mambo ambayo nimewaamuru; na ilimradi wao ni waaminifu, lo, Mimi nitakuwa pamoja nao, hata mwisho.

14 Na tena, amini ninamwambia mtumishi wangu Lyman Johnson, na mtumishi wangu Orson Pratt, watafanya safari yao pia katika nchi za mashariki; na tazama, na lo, Mimi niko pamoja nao pia, hata mwisho.

15 Na tena, nasema kwa mtumishi wangu Asa Dodds, na kwa mtumishi wangu Calves Wilson, kwamba nao pia wafunge safari yao kwenda nchi za magharibi, na kutangaza injili yangu, hata kama vile nilivyowaamuru wao.

16 Na yule aliye mwaminifu atashinda mambo yote, na atainuliwa juu siku ile ya mwisho.

17 Na tena, ninasema kwa watumishi wangu Major N. Ashley, na mtumishi wangu Burr Riggs, na wafunge safari yao pia kwenda katika nchi ya kusini.

18 Ndiyo, na wote wafunge safari zao, kama nilivyowaamuru, wakipita toka nyumba hadi nyumba, na kutoka kijiji hadi kijiji, na kutoka mji hadi mji.

19 Na nyumba yoyote mtakayoingia; na wakawakaribisha, iacheni baraka yenu juu ya nyumba hiyo.

20 Na katika nyumba yoyote mtakayoingia na wala hawakuwakaribisha, mtatoka upesi kutoka humo, na yakungʼuteni mavumbi ya miguu yenu kuwa ushuhuda juu yao.

21 Nanyi mtakuwa na shangwe na furaha; na fahamuni neno hili, kwamba katika siku ile ya hukumu ninyi mtakuwa mahakimu wa nyumba hiyo, na kuwahukumu;

22 Na itakuwa rahisi kuvumilika kwa mpagani katika siku ya hukumu, kuliko watu wa nyumba hiyo; kwa hiyo, vifungeni viuno vyenu na kuweni waaminifu, nanyi mtayashinda mambo yote, na mtainuliwa juu siku ile ya mwisho. Hivyo ndivyo. Amina.

23 Na tena, hivyo ndivyo asemavyo Bwana kwenu ninyi, Enyi wazee wa kanisa langu, ambao mmeyatoa majina yenu ili muweze kujua mapenzi yake juu yenu—

24 Tazama, ninawaambia, kuwa ni wajibu wa kanisa kusaidia katika kutunza familia za wale, na pia kutunza familia za wale walioitwa na wale watakaohitajika kutumwa ulimwenguni kuitangaza injili kwa ulimwengu.

25 Kwa hiyo, Mimi, Bwana, ninatoa amri hii kwenu, kwamba tafuteni mahali kwa familia zenu, ili mradi ndugu zenu wapo tayari kuifungua mioyo yao.

26 Na wale wote wanaoweza kupata mahali kwa ajili ya familia zao, na msaada wa kanisa kwa ajili yao, wasiache kwenda katika ulimwengu, iwe mashariki au magharibi, kaskazini au kusini.

27 Na waombe nao watapata, wabishe nao watafunguliwa, na watajulishwa kutoka juu, hata kwa Mfariji, mahali pa kwenda.

28 Na tena, amini ninawaambia, kwamba kila mtu anaye wajibika kuitunza familia yake mwenyewe, na aitunze, na kwa vyovyote vile hatapoteza taji lake; na afanye kazi katika kanisa.

29 Na kila mtu afanye bidii katika mambo yote. Na mzembe hatakuwa na nafasi katika kanisa, isipokuwa atubu na kurekebisha njia zake.

30 Kwa hiyo, mtumishi wangu Simeon Carter na mtumishi wangu Emer Harris waungane katika huduma;

31 Na pia mtumishi wangu Ezra Thayre na mtumishi wangu Thomas B. Marsh;

32 Pia mtumishi wangu Hyrum Smith na mtumishi wangu Reynolds Cahoon;

33 Na pia mtumishi wangu Daniel Stanton na mtumishi wangu Seymour Brunson;

34 Na pia mtumishi wangu Sylvester Smith na mtumishi wangu Gideon Carter;

35 Na pia mtumishi wangu Ruggles Eames na mtumishi wangu Stephen Burnett;

36 Na pia mtumishi wangu Micah B. Welton na pia mtumishi wangu Eden Smith. Hivyo ndivyo. Amina.

Chapisha