Maandiko Matakatifu
Tamko Rasmi 1


Tamko Rasmi 1

Biblia na Kitabu cha Mormoni hufundisha kwamba ndoa kati ya mke au mme mmoja ndiyo kiwango cha ndoa kilichowekwa na Mungu isipokuwa pale Yeye anapotamka vinginevyo (ona 2 Samweli 12:7–8 na Yakobo [KM] 2:27, 30). Kufuatia ufunuo kwa Joseph Smith, kanuni ya ndoa ya wake wengi ilianzishwa miongoni mwa waumini wa Kanisa mapema katika miaka ya 1840 (ona sehemu ya 132). Kuanzia miaka ya 1860 hadi ile ya 1880, serikali ya Marekani ilipitisha sheria ya kuifanya desturi hii ya kidini kuwa kinyume cha sheria. Sheria hizi hatimaye ziliungwa mkono na Mahakama Kuu ya Marekani Baada ya kupokea ufunuo, Rais Wilford Woodruff alitoa Manifesto ifuatayo, ambayo ilikubalika na Kanisa kama mamlaka sahihi na ya kutiiwa mnamo 6 Oktoba 1890. Na hii ilisababisha kukoma kwa desturi ya ndoa za wake wengi katika Kanisa.

Kwa Yeyote Anayehusika:

Taarifa ya habari iliyotumwa kwa madhumuni ya kisiasa, kutoka Jiji la Salt Lake, ambayo imechapishwa sehemu nyingi, ikionyesha kwamba Tume ya Utah, katika taarifa yake ya hivi karibuni kwa Katibu wa Mambo ya Ndani, inadai kwamba ndoa za mitala bado zinafungishwa na kwamba ndoa arobaini au zaidi zimefungwa hapa Utah kutoka Juni iliyopita au wakati wa mwaka jana, pia kwamba katika mahubiri ya hadhara viongozi wa Kanisa wamefundisha, kuchochea na kuhimiza uendelezaji wa tabia ya mitala—

Kwa hiyo, mimi, kama Rais wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, kwa heshima na taadhima, ninatamka kwamba madai haya ni ya uongo. Sisi hatufundishi mitala au ndoa za wake wengi, au kumruhusu mtu yeyote kuingia katika kutenda hayo, na ninakana kwamba ndoa arobaini au idadi yoyote ya ndoa za wake wengi hazijawahi kufungishwa katika Mahekalu yetu kwa kipindi hicho au mahali pengine popote katika Eneo hili.

Jambo moja limearifiwa, ambalo wahusika wanadai kwamba ndoa ilifungwa katika Nyumba ya Endaomenti, katika Jiji la Salt Lake, wakati wa majira ya kuchipua ya 1889, lakini sijaweza kumjua aliyefungisha hiyo; lolote lililofanyika katika jambo hili lilikuwa pasipo kujua kwangu. Kama matokeo ya madai haya Nyumba ya Endaomenti, kwa maelekezo yangu, imebomolewa mara moja.

Kwa vile sheria zimekwishatungwa na Bunge zikikataza ndoa za wake wengi, sheria ambazo zimetangazwa kikatiba na mahakama iliyo kimbilio la mwisho, ninatangaza madhumuni yangu ya kuwa mtiifu kwa sheria hizo, na kutumia uwezo wangu juu ya waumini wa Kanisa ambao ninawaongoza kufanya hivyo hivyo.

Hakuna lolote katika mafundisho yangu kwa Kanisa au katika yale ya wenzangu, kwa kipindi hicho kilichotajwa, ambayo yanaweza kutafsiriwa kuwa yanafundishwa au kuhimiza mitala; na wakati Mzee yeyote wa Kanisa alipotumia lugha ambayo ilionekana kuelezea mafundisho yoyote ya aina hiyo, amekemewa mara moja. Na sasa ninatangaza hadharani kwamba ushauri wangu kwa Watakatifu wa Siku za Mwisho ni kuacha kufunga ndoa yoyote iliyokatazwa na sheria ya nchi.

Wilford Woodruff

Rais wa Kanisa la Yesu Kristo
la Watakatifu wa Siku za Mwisho.

Rais Lorenzo Snow alisema yafuatayo:

“Ninapendekeza, tukimtambua Wilford Woodruff kama Rais wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, na mtu pekee duniani kwa wakati huu ambaye anashikilia funguo za ibada za kuunganisha, tunatambua kwamba anayo mamlaka kamili kutokana na nafasi yake kutoa Manifesto ambayo imesomwa nasi tumeisikia, na ambayo imetolewa tarehe 24 Septemba 1890, na kwamba kama Kanisa katika Mkutano Mkuu tuliokusanyika, kwamba tunalikubali tamko lake juu ya ndoa ya mke mmoja kuwa ni rasmi na hatuna budi kulitii.”

Jiji la Salt Lake, Utah, 6 Oktoba 1890.

Dondoo kutoka Hotuba Tatu
za Rais Wilford Woodruff
Juu ya Manifesto

Bwana hataniruhusu mimi au mtu mwingine yoyote asimamaye kama Rais wa Kanisa kuwaongoza ninyi vibaya. Haipo katika mpangilio. Haipo katika mawazo ya Mungu. Kama ningejaribu hilo, Bwana angeniondoa katika nafasi yangu, na hivyo atamfanya mtu yeyote atakaye jaribu kuwaongoza wanadamu nje ya ufunuo wa Mungu na kutoka kwenye wajibu wao. (Mkutano Mkuu wa Nusu Mwaka Sitini na Moja wa Kanisa, Jumatatu, 6 Oktoba 1890, Jiji la Salt Lake, Utah. Ulioripotiwa na Deseret Evening News, 11 Oktoba 1890, uk. 2.)

Si muhimu nani anaishi au nani anakufa, au nani anaitwa kuliongoza Kanisa hili, wanalazimika kuliongoza kwa mwongozo wa Mwenyezi Mungu. Kama hawafanyi kwa njia hiyo, hawawezi kufanya kwa njia nyingine yoyote. …

Nimepata mafunuo kadhaa hivi karibuni, na ya muhimu sana kwangu, nayo nitawaambia kile Bwana alichoniambia. Wacha niyarejeshe mawazo yenu katika hiki kitu kinachoitwa Manifesto. …

Bwana ameniambia niwaulize Watakatifu wa Siku za Mwisho swali, pia akaniambia kama watasikiliza kile nilichowaambia na kujibu swali lililoulizwa kwao, kwa Roho na kwa uwezo wa Mungu, wote watajibu sawa sawa, na wote wataamini sawa sawa juu ya jambo hili.

Swali ni hili: Njia ipi iliyo ya busara zaidi kwa Watakatifu wa Siku za Mwisho kuifuata—kuendelea kujaribu kufunga ndoa za wake wengi, licha ya sheria za taifa dhidi yake na upinzani wa watu milioni sitini, na kwa gharama ya utaifishaji na upotevu wa Mahekalu yote, na kusimamishwa kwa ibada zake zote, za wote walio hai na wafu, na kufungwa gerezani kwa Urais wa Kwanza na Mitume Kumi na Wawili na viongozi wa familia katika Kanisa, na kutaifishwa kwa mali za watu binafsi (hivi vyote peke yake vinaweza kusimamisha tabia hiyo); au, baada ya kufanya na kuteseka haya tuliyoteseka kupitia kujitoa kwetu kwa kanuni hii kuacha kanuni hii na kutii sheria, na kwa kufanya hivyo tutawaacha Manabii, Mitume na akina baba majumbani, ili waweze kuwafundisha watu na kutimiza wajibu wao kwa Kanisa, na kuyaacha Mahekalu mikononi mwa Watakatifu, ili waweze kutekeleza ibada za injili, wote kwa ajili ya walio hai na wafu?

Bwana alinionyesha kwa ono na ufunuo hasa yatakayotokea kama hatungekomesha desturi hii. Kama hatungeikomesha msingeliweza kuwatumia … mtu yeyote katika hekalu hili la Logan; kwani ibada zote zingelikoma nchi yote ya Sayuni. Vurugu ingetawala nchi yote ya Israeli, na watu wengi wangefanywa kuwa wafungwa. Taabu hii ingekuja juu ya Kanisa lote, na tungelilazimika kukomesha desturi hii. Sasa, swali ni hili, je, ikomeshwe kwa jinsi hii, au katika njia ambayo Bwana ameionyesha kwetu, na kuwaacha Manabii wetu na Mitume na akina baba kuwa huru, na mahekalu kuwa mikononi mwa watu, ili wafu wapate kukombolewa. Idadi kubwa tayari imekwisha kukombolewa kutoka kifungoni katika ulimwengu wa roho na watu hawa, na kazi iendelee au isimame? Hili ndilo swali ninaloliweka mbele ya Watakatifu wa Siku za Mwisho. Yawapasa kuamua ninyi wenyewe. Ninakutakeni mjibu wenyewe. Mimi sitajibu; lakini ninakuambieni kwamba hii ndiyo hali halisi ambayo sisi watu tungelikuwa nayo kama tusingechukua hatua tulizochukua.

… Nimeona hasa kile ambacho kitakuja kuwa kama pasingefanyika chochote. Nimekuwa na roho hii juu yangu kwa muda mrefu. Lakini nataka kusema hili: Ningeweza kuyaachia mahekalu yote kutoka mikononi mwetu; ningelikwenda gerezani mimi mwenyewe, na kumwacha kila mwanaume kwenda huko, kama Mungu wa mbinguni asingeliniamuru kufanya haya niliyoyafanya; na wakati saa ilipofika ambayo niliamriwa kufanya hilo, yote ilikuwa wazi kwangu. Nilikwenda mbele za Bwana, na nikaandika kile Bwana alichoniambia kuandika. …

Ninawaachia hili, kwa ajili ya kulitazama na kutafakari. Bwana yupo kazini pamoja nasi. (Mkutano wa Kigingi cha Cache, Logan, Utah, Jumapili ya 1 Novemba 1891. Iliandikwa katika Deseret Weekly, 14 Novemba 1891.)

Sasa nitawaambia kilichofunuliwa kwangu na kile Mwana wa Mungu alichokifanya, katika jambo hili. … Mambo haya yote yangelitokea, kama vile Mungu Mwenyezi aishivyo, kama Manifesto ile isingelitolewa. Kwa hiyo, Mwana wa Mungu alielekeza mambo haya yatolewe kwa kanisa na kwa ulimwengu kwa madhumuni yaliyoko akilini mwake. Bwana ameazimia kuistawisha Sayuni. Ameazimia kumalizika kwa hekalu hili. Ameazimia kwamba wokovu wa walio hai na wafu lazima utolewe katika mabonde haya ya milima. Na Mwenyezi Mungu alitangaza kwamba Ibilisi hataizuia. Kama mnaweza kuelewa hilo, huo ndiyo ufunguo wake. (Kutoka katika mafundisho ya kipindi cha sita cha ibada ya kuwekwa Wakfu kwa Hekalu la Salt Lake, Aprili 1893. Muswada uliopigwa chapa wa Ibada ya kuweka Wakfu. Hifadhi ya Nyaraka, Idara ya Historia ya Kanisa, katika Mji Salt Lake, Utah.)