Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 115


Sehemu ya 115

Ufunuo uliotolewa kupitia Joseph Smith Nabii, huko Far West, Missouri, 26 Aprili 1838, ukijulisha mapenzi ya Mungu juu ya ujenzi wa mahali pale na wa nyumba ya Bwana. Ufunuo huu unaelekezwa kwa maofisa viongozi na waumini wa Kanisa.

1–4, Bwana analiita kanisa Lake Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho; 5–6, Sayuni na vigingi vyake ni mahali pa ngome na makimbilio kwa Watakatifu; 7–16, Watakatifu wanaamriwa kujenga nyumba ya Bwana huko Far West; 17–19, Joseph Smith anashikilia funguo za ufalme wa Mungu duniani.

1 Amini hivyo ndivyo asemavyo Bwana kwako, mtumishi wangu Joseph Smith, Mdogo, na pia mtumishi wangu Sidney Rigdon, na pia mtumishi wangu Hyrum Smith, na washauri wenu waliopo na watakaoteuliwa hapo baadaye;

2 Na pia kwako wewe, mtumishi wangu Edward Partridge, na washauri wake;

3 Na pia kwa watumishi wangu waaminifu ambao ni wa baraza kuu la kanisa langu katika Sayuni, kwani hivyo ndivyo litakavyoitwa, na kwa wazee wote na watu wa Kanisa langu la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, waliotawanyika ulimwenguni kote;

4 Kwani hivyo ndivyo kanisa langu litakavyoitwa katika siku za mwisho, hata Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.

5 Amini ninawaambia ninyi nyote: Inukeni na mngʼare, ili nuru yenu ipate kuwa bendera kwa ajili ya mataifa;

6 Na ili kukusanyika pamoja juu ya nchi ya Sayuni, na juu ya vigingi vyake, kupata kuwa ngome, na makimbilio wakati wa tufani, na ghadhabu wakati itakapomwagwa pasipo kuchanganywa juu ya dunia yote.

7 Acha mji wa Far West, uwe mji mtakatifu na uliowekwa wakfu kwangu; nao utaitwa mtakatifu sana, kwani ardhi ambayo juu yake umesimama ni takatifu.

8 Kwa hiyo, nakuamuruni kunijengea nyumba, kwa ajili ya kukusanyika pamoja watakatifu wangu, ili wapate kuniabudu.

9 Na acha uwepo mwanzo wa kazi hii, na msingi, na kazi ya maandalizi ya kiangazi hiki kijacho;

10 Na acha mwanzo ufanyike siku ya nne ya Julai ijayo; na tangu wakati ule na kuendelea acha watu wangu wafanye kazi kwa bidii kuijenga nyumba katika jina langu;

11 Na katika mwaka mmoja kutoka siku hii acha waanze kuweka msingi wa nyumba yangu.

12 Hivyo acha kuanzia tangu wakati ule na kuendelea wafanye kazi kwa bidii hadi itakapomalizika, kutoka jiwe lake la kona hadi juu yake, hadi pasiwepo na kitu chochote kitakachobakia bila kumalizika.

13 Amini ninawaambia, msiache mtumishi wangu, Joseph, wala mtumishi wangu Sidney, wala mtumishi wangu Hyrum, waingie tena katika deni kwa ajili ya ujenzi wa nyumba katika jina langu;

14 Bali acha nyumba ijengwe kwa jina langu kulingana na utaratibu ambao nitauonyesha kwao.

15 Na kama watu wangu hawatajenga kulingana na utaratibu ambao nitauonyesha kwa urais wao, sitaipokea kutoka kutoka kwao.

16 Lakini ikiwa watu wangu wataijenga kulingana na utaratibu ambao nitauonyesha kwa urais wao, hata mtumishi wangu Joseph na washauri wake, ndipo nitaipokea kutoka mikononi mwa watu wangu.

17 Na tena, amini ninawaambia, ni mapenzi yangu kwamba mji wa Far West lazima ujengwe haraka kwa kukusanyika kwa watakatifu wangu;

18 Na pia kwamba mahali pengine pateuliwe kwa ajili ya vigingi katika maeneo ya jirani, kama vile yatakavyofunuliwa kwa mtumishi wangu Joseph, mara kwa mara.

19 Kwani tazama, Mimi nitakuwa pamoja naye, nami nitamtakasa mbele ya hawa watu; kwani yeye nimempa funguo za ufalme huu na huduma hii. Hivyo ndivyo. Amina.

Chapisha