Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 68


Sehemu ya 68

Ufunuo uliotolewa kupitia Joseph Smith Nabii, huko Hiram, Ohio, 1 Novemba 1831, katika jibu la maombi kwamba mapenzi ya Bwana yafahamike kuhusu Orson Hyde, Luke S. Johnson, Lyman E. Johnson, na William E. McLellin. Ingawa sehemu ya ufunuo huu ilielekezwa kwa watu hawa wanne, mengi ya yaliyomo yanalihusu Kanisa zima. Ufunuo huu ulipanuliwa kwa maelekezo ya Joseph Smith wakati ulipochapishwa katika toleo la mwaka 1835 la Mafundisho na Maagano.

1–5, Maneno ya wazee wakati wakiongozwa na Roho Mtakatifu ni maandiko; 6–12, Wazee watahubiri na kubatiza, na ishara zitawafuata waumini wa kweli; 13–24, Mzaliwa wa kwanza miongoni mwa wana wa Haruni aweza kutumika kama Askofu Kiongozi (hii maana yake, anashikilia funguo za urais kama askofu) chini ya maelekezo ya Urais wa Kwanza; 25–28, Wazazi wanaamriwa kuwafundisha injili watoto wao; 29–35, Watakatifu wataishika Sabato, watafanya kazi kwa bidii, na kuomba.

1 Mtumishi wangu, Orson Hyde, aliitwa kwa kutawazwa kwake kuitangaza injili isiyo na mwisho, kwa Roho wa Mungu aliye hai, kutoka taifa hadi taifa, na kutoka nchi hadi nchi, katika mikutano ya waovu, katika masinagogi yao, akisemezana nao na kuwaelezea maandiko yote.

2 Na, tazama, na lo, huu ni mfano kwa wale wote ambao wametawazwa katika ukuhani huu, wale ambao kazi imekwisha tolewa kwao kwenda—

3 Na huu ni mfano kwao, kwamba watasema kama vile walivyoongozwa na Roho Mtakatifu.

4 Na lolote watakalolisema wakati wanaongozwa na Roho Mtakatifu litakuwa andiko, litakuwa ni mapenzi ya Bwana, litakuwa ni nia ya Bwana, litakuwa ni neno la Bwana, itakuwa ni sauti ya Bwana, na ni uwezo wa Mungu kwa wokovu.

5 Tazama, hii ni ahadi ya Bwana kwenu, Enyi watumishi wangu.

6 Kwa hiyo, changamkeni, na msiogope, kwani Mimi Bwana nipo pamoja nanyi, na nitasimama karibu yenu; nanyi mtanishuhudia, hata Yesu Kristo, kuwa Mimi ndimi Mwana wa Mungu aliye hai, kwamba nilikuwepo, kwamba nipo, na kwamba nitakuja.

7 Hili ndilo neno la Bwana kwenu, mtumishi wangu Orson Hyde, na pia mtumishi wangu Luke Johnson, na kwa mtumishi wangu Lyman Johnson, na kwa mtumishi wangu William E. McLellin, na kwa wazee wote waaminifu wa kanisa langu—

8 Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri injili kwa kila kiumbe, mkitenda katika mamlaka ambayo nimewapa, mkibatiza katika jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu.

9 Na yule aaminiye na kubatizwa ataokolewa, na yule asiyeamini atalaaniwa.

10 Na yule aliyeamini atabarikiwa kwa ishara kumfuata, hata kama ilivyoandikwa.

11 Nanyi mtapewa kujua ishara za nyakati, na ishara za kuja kwa Mwana wa Mtu;

12 Na kuhusu wale wote kama vile Baba atakavyowashuhudia, ninyi mtapewa uwezo wa kuwafunga katika uzima wa milele. Amina.

13 Na sasa, kuhusu mambo ya nyongeza katika maangano na amri, nayo ni haya—

14 Yanayobaki baada ya hapa, katika wakati wa Bwana ufikapo, maaskofu wengine wateuliwe kwa ajili ya kanisa, kuhudumu hata kama wale wa kwanza;

15 Kwa hiyo, watakuwa makuhani wakuu wenye kustahili, na wateuliwe na Urais wa Kwanza wa Ukuhani wa Melkizedeki, isipokuwa wale walio wazaliwa wa ukoo wa Haruni.

16 Na kama watakuwa wazaliwa halisi wa ukoo wa Haruni wao wanayo haki kisheria ya uaskofu, kama ni wazaliwa wa kwanza miongoni mwa wana wa Haruni;

17 Kwani mzaliwa wa kwanza anashikilia haki ya urais wa Ukuhani huu, na funguo au mamlaka yake.

18 Hakuna mtu aliye na haki kisheria kwenye ofisi hii, kushikilia funguo za ukuhani huu, isipokuwa yule aliye mzaliwa halisi wa ukoo na ni mzaliwa wa kwanza wa Haruni.

19 Lakini, kama kuhani mkuu wa Ukuhani wa Melkizedeki anayo mamlaka ya kutenda katika ofisi zile ndogo anazoweza kuzitenda kazi katika ofisi ya askofu ikiwa hakuna mzaliwa halisi wa ukoo wa Haruni anayeweza kupatikana, ili mradi ameitwa na kutengwa na kutawazwa katika mamlaka haya, chini ya mikono ya Urais wa Kwanza wa Ukuhani wa Melkizedeki.

20 Na mzaliwa halisi wa ukoo wa Haruni, pia, lazima ateuliwe na Urais huu, na aonekane mwenye kustahili, na kupakwa mafuta, na kutawazwa chini ya mikono ya Urais huu, vinginevyo hawajaruhusiwa kisheria kutenda kazi katika ukuhani wao.

21 Lakini, kwa sababu ya kupitia azimio kuhusu haki yao ya ukuhani kutoka kwa baba hadi kwa mwana, wanaweza kudai haki ya kupakwa kwao mafuta kama wakati wowote wanaweza kuthibitisha safu ya mfuatano wa kuzaliwa, au itafanywa kwa kuhakikisha kwa ufunuo kutoka kwa Bwana chini ya mikono ya Urais uliotajwa hapo juu.

22 Na tena, hakuna askofu au kuhani mkuu ambaye atasimikwa kwa ajili ya huduma hii ambaye atashtakiwa au kuhukumiwa kwa jinai yoyote, isipokuwa mbele ya Urais wa Kwanza wa kanisa;

23 Na kadiri atapatikana na hatia mbele ya Urais huu, kwa ushuhuda ambao hauwezi kutuhumiwa, atahukumiwa;

24 Na kama atatubu atasamehewa, kulingana na maagano na amri za kanisa.

25 Na tena, ili mradi wazazi wanao watoto katika Sayuni, au katika kigingi chake chochote ambacho kimeundwa, ambao hawawafundishi wao kuelewa mafundisho ya toba, imani katika Kristo Mwana wa Mungu aliye hai, na ubatizo na kipawa cha Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono, wafikapo miaka minane, dhambi zao zitakuwa juu ya vichwa vya wazazi.

26 Kwani hii itakuwa sheria kwa wakazi wa Sayuni, au katika kila kigingi chake kilichoundwa.

27 Na watoto wao wabatizwe kwa ajili ya ondoleo la dhambi zao wafikishapo umri wa miaka minane na kupokea kuwekwa mikono.

28 Na pia wawafundishe watoto wao kuomba, na kusimama wima mbele za Bwana.

29 Na wakazi wa Sayuni pia waikumbuke siku ya Sabato kuishika kitakatifu.

30 Na wakazi wa Sayuni pia wazikumbuke kazi zao, ili mradi wameteuliwa kufanya kazi, kwa uaminifu wote; kwani mvivu atakumbukwa mbele za Bwana.

31 Sasa, Mimi, Bwana sipendezwi na wakazi wa Sayuni, kwani kuna wavivu miongoni mwao; na watoto wao pia wanakua katika uovu; pia hawatafuti kwa dhati utajiri wa milele, bali macho yao yamejaa tamaa.

32 Mambo haya hayafai kuwa hivyo, na lazima yakomeshwe kutoka miongoni mwao; kwa hiyo, acha mtumishi wangu Oliver Cowdery ayapeleke maneno haya kwenye nchi ya Sayuni.

33 Na amri ninatoa kwao—kwamba yule asiyefanya sala zake mbele za Bwana katika wakati unaostahili, acha akumbukwe mbele za mwamuzi wa watu wangu.

34 Na misemo hii ni ya kweli na ya kuaminika; kwa hiyo, msiivunje, wala kuondoa lolote ndani yake.

35 Tazama, Mimi ni Alfa na Omega, na naja haraka. Amina.

Chapisha