Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 101


Sehemu ya 101

Ufunuo uliotolewa kwa Joseph Smith Nabii, huko Kirtland, Ohio, 16 na 17 Desemba 1833. Wakati huu Watakatifu waliokuwa wamekusanyika Missouri walikuwa wakiudhiwa kwa mateso makubwa. Makundi ya wahuni yaliwafukuza kutoka majumbani mwao katika Wilaya ya Jackson; na baadhi ya Watakatifu walijaribu kuanzisha makazi yao katika Wilaya za Van Buren, Lafayette, na Ray, lakini usumbufu uliwafuata. Kundi kubwa la Watakatifu kwa wakati huo lilikuwa katika Wilaya ya Clay, Missouri. Vitisho vya mauaji dhidi ya watu wa Kanisa vilikuwa vingi. Watakatifu huko Wilaya ya Jackson walikuwa wamepoteza samani za majumbani, nguo, mifugo, na mali nyingine binafsi; mengi ya mazao yao yalikuwa yameharibiwa.

1–8, Watakatifu wanarudiwa na kuteswa kwa sababu ya uvunjaji wao wa sheria; 9–15, Uchungu wa hasira ya Bwana utaanguka juu ya mataifa, lakini watu Wake atawakusanya na kuwafariji; 16–21, Sayuni na vigingi vyake vitaimarishwa; 22–31, Namna ya maisha wakati wa Milenia yaelezwa; 32–42, Watakatifu watabarikiwa na kuzawadiwa wakati huo; 43–62, Mfano juu ya watu maarufu na mizeituni inaelezea ya matatizo na hatimaye ukombozi wa Sayuni; 63–75, Watakatifu waendelee kukusanyika pamoja; 76–80, Bwana aliiweka Katiba ya Marekani; 81–101, Watakatifu lazima waombe kwa ajili ya kufidiwa kwa mambo yasiyo ya haki, kulingana na mfano wa mwanamke na mwamuzi asiye na haki.

1 Amini ninawaambia, juu ya ndugu zenu ambao wameumizwa, na kuteswa, na kufukuzwa kutoka kwenye nchi ya urithi wao—

2 Mimi, Bwana, nimeruhusu mateso yaje juu yao, ambayo kwayo wameteswa, kama matokeo ya uvunjaji wao wa sheria;

3 Hata hivyo nitawamiliki, nao watakuwa wangu katika siku ile wakati nitakapokuja kuwafanya kuwa hazina yangu.

4 Kwa hiyo, hawana budi kurudiwa na kujaribiwa, hata kama Ibrahimu, ambaye aliamriwa kumtoa mwanawe wa pekee.

5 Kwani wale wote ambao hawatastahimili kurudiwa, bali kunikana Mimi, hawawezi kutakaswa.

6 Tazama, ninawaambia, palikuwa na mafarakano, na mabishano, na wivu, na migongano, na ashiki na tamaa mbaya miongoni mwao; kwa hiyo kwa mambo haya waliuchafua urithi wao.

7 Walikuwa wazito wa kusikiliza sauti ya Bwana Mungu wao; kwa sababu hiyo, Bwana Mungu wao amekuwa mzito wa kusikiliza sala zao, kwa kuwajibu katika siku ya matatizo yao.

8 Katika siku ya amani yao huuchukulia kwa wepesi ushauri wangu; lakini, katika siku ya matatizo yao, wanaona umuhimu wa kunitafuta.

9 Amini ninawaambia, licha ya dhambi zao, moyo wangu umejaa huruma juu yao. Sitawafukuzilia mbali, na katika siku ya ghadhabu nitakumbuka huruma.

10 Nimeapa, na azimio limekwisha toka amri ya zamani ambayo nilitoa kwenu, ya kwamba ningeachia ushuke upanga wa uchungu wa hasira yangu kwa niaba ya watu wangu; na kama vile nilivyosema, itakuwa hivyo.

11 Uchungu wa hasira yangu karibu utamwagwa pasipo kipimo juu ya mataifa yote; na hili nitalifanya wakati kikombe cha uovu wao kitakapokuwa kimejaa.

12 Na katika siku ile wote watakaopatikana juu ya mnara wa doria, au kwa maneno mengine, Waisraeli wangu wote, wataokolewa.

13 Na wale waliotawanywa watakusanywa.

14 Na wale wote wenye huzuni watafarijika.

15 Na wale wote walioutoa uhai wao kwa ajili ya jina langu watatuzwa;

16 Kwa hiyo, mioyo yenu na ifarijike juu ya Sayuni; kwa kuwa wenye mwili wote wako mikononi mwangu; tulieni na jueni kuwa Mimi ni Mungu.

17 Sayuni haitaondoshwa kutoka mahali pake, licha ya kuwa watoto wake wametawanywa.

18 Wale wanaobaki, na wako safi moyoni, watarejea, na kuja kwenye urithi wao, wao na watoto wao, kwa nyimbo za shangwe isiyo na mwisho, kujenga mahali palipoharibiwa pa Sayuni—

19 Na haya yote yatakuwa ili unabii wa manabii utimizwe.

20 Na, tazama, hapana mahali pengine palipoteuliwa zaidi ya pale nilipopateua; wala hapatakuwa mahali pengine patakapoteuliwa zaidi ya pale nilipopateua, kwa ajili ya kazi ya kuwakusanya watakatifu wangu—

21 Hadi siku itakapofika wakati itakapoonekana hakuna nafasi zaidi kwa ajili yao; na halafu tena ninazo sehemu nyingine ambazo nitawateulia, nazo zitaitwa vigingi, kwa ajili ya mapazia au nguvu ya Sayuni.

22 Tazama, ni mapenzi yangu, kwamba wale wote walilinganao jina langu, na kuniabudu kulingana na injili yangu isiyo na mwisho, yawapasa kukusanyika pamoja, na kusimama mahali patakatifu;

23 Na kujitayarisha kwa ufunuo ujao, wakati pazia lifunikalo hekalu langu, katika hema takatifu yangu, ambayo huificha dunia, litakapoondolewa, na wote wenye mwili wataniona kwa pamoja.

24 Na kila kitu kilichoharibika, iwe mwanadamu, au mnyama wa mwituni, au ndege wa angani, au samaki wa baharini, vile viishivyo juu ya uso wote wa dunia vyote, vitateketezwa;

25 Na pia vile vitu vya asili vitayeyuka kwa joto kali; na vitu vyote vitakuwa vipya, ili ufahamu na utukufu wangu vipate kukaa juu ya dunia yote.

26 Na katika siku hiyo uadui wa mwanadamu, na uadui wa wanyama, ndiyo, uadui wa wote wenye mwili utakoma kutoka mbele ya uso wangu.

27 Na katika siku hiyo lolote ambalo mtu yeyote ataliomba, atapewa.

28 Na katika siku hiyo Shetani hatakuwa na uwezo wa kumjaribu mwanadamu yeyote.

29 Na hapatakuwa na huzuni kwa sababu hapatakuwa na mauti.

30 Katika siku hiyo mtoto mchanga hatakufa hadi amekuwa mzee; na uhai wake utakuwa kama umri wa mti;

31 Na wakati atakapokufa hatalala, kama tusemavyo duniani, bali atabadilishwa kwa dakika moja kufumba na kufumbua jicho, na kunyakuliwa, na pumziko lake litakuwa tukufu.

32 Ndiyo, amini ninawaambia, katika siku hiyo wakati Bwana atakapokuja, atayafunua mambo yote—

33 Mambo yaliyokwishapita, na mambo yaliyofichika ambayo hapana mwanadamu aliyejua, mambo ya dunia, ambayo kwayo iliumbwa, na madhumuni na mwisho wake—

34 Mambo yaliyo muhimu zaidi, mambo yaliyo juu, na mambo yaliyo chini, mambo yaliyo ndani ya dunia, na juu ya dunia, na mbinguni.

35 Na wale wote wasumbukao na mateso kwa ajili ya jina langu, na kustahimili katika imani, ingawa wameitwa kuutoa uhai wao kwa ajili yangu hata hivyo nao watashiriki utukufu huu wote.

36 Kwa hiyo, msiogope hata kwa mauti; kwani katika ulimwengu huu shangwe yenu siyo kamilifu, bali ndani yangu shangwe yenu ni kamilifu.

37 Kwa hiyo, msiujali mwili, wala uzima wa mwili; bali zijalini nafsi, na uzima wa nafsi.

38 Na utafuteni uso wa Bwana daima, ili kwa subira mpate kuziponya nafsi zenu, nanyi mtapata uzima wa milele.

39 Wakati wanadamu wanapoitwa kwa injili yangu isiyo na mwisho, na kuahidi kwa agano lisilo na mwisho, wao huhesabika kama chumvi ya dunia na ladha ya wanadamu;

40 Wao huitwa kuwa ladha kwa wanadamu; kwa hiyo, ikiwa chumvi ya dunia itapoteza ladha yake, tazama, haifai tena kwa lolote ila kutupwa nje na kukanyagwa na miguu ya watu.

41 Tazama, hapa ndipo penye hekima kuhusu watoto wa Sayuni, hata wengi, bali siyo wote; walipatikana wavunjaji wa sheria, kwa hiyo hawana budi kurudiwa—

42 Yule ajikwezaye mwenyewe atadhiliwa, naye ajidhiliye mwenyewe atakwezwa.

43 Na sasa, nitawaonyesha mfano, ili mpate kujua mapenzi yangu kuhusu ukombozi wa Sayuni.

44 Mtu mmoja kabaila alikuwa na eneo la ardhi, zuri sana; na akawaambia watumishi wake: Enendeni katika shamba langu la mizabibu, hata juu ya sehemu hii ya kipande kilicho kizuri sana, na mpande miti kumi na miwili ya mizeituni;

45 Na wawekeni walinzi kuizunguka, na kujenga mnara, ili mmoja aweze kutazama kuzunguka shamba lote, ili awepo mlinzi juu ya mnara, ili mizeituni yangu isiweze kuvunjwa wakati adui atakapokuja kuiharibu na kujichukulia tunda la mizabibu wangu.

46 Sasa, watumishi wa yule kabaila walikwenda na kufanya kama bwana wao alivyowaamuru, na wakapanda ile mizeituni, na kujenga ua kuizunguka, nakuweka walinzi, na wakaanza kujenga mnara.

47 Na wakati wakiwa bado wanajenga msingi wake, wakaanza kusemezana wao kwa wao: Na bwana wangu anahaja gani na mnara huu?

48 Na wakasemezana kwa muda mrefu, wakisemezana miongoni mwao: Ni haja gani aliyo nayo bwana wangu kwa mnara huu, mbona huu ni wakati wa amani?

49 Fedha hii ingepaswa kuwekwa kwa watoao riba? Kwani hapana haja ya mambo haya.

50 Na wakati walipokuwa wakitofautiana mmoja na mwingine wakawa wavivu sana, na hawakutii ile amri ya bwana wao.

51 Na adui akaja usiku, na akavunja ua; na watumishi wa kabaila yule walipoamka na wakaogopa, na wakakimbia; na adui akaziharibu kazi zao, na kuivunja mizeituni.

52 Sasa, tazama, kabaila, bwana mwenye shamba la mizabibu, aliwaita watumishi wake, na akawaambia, Kwa nini! nini chanzo cha uovu huu mkubwa?

53 Ninyi hamkupaswa kufanya kama nilivyowaamuru, na—baada ya kuwa mmepanda shamba la mizabibu, na kujenga ua kulizunguka, na kuwaweka walinzi juu ya ukuta wake—mjenge mnara pia, na kumweka mlinzi juu ya mnara, na kulinda kwa ajili ya shamba langu la mizabibu, na siyo kulala, asije adui akaja juu yenu?

54 Na tazama, mlinzi juu ya mnara angelimwona adui wakati angali bado yuko mbali; na ndipo ninyi mngejitayarisha kuwa tayari na mngelimzuia adui asivunje ua wake, na hivyo kuokoa shamba langu la mizabibu kutoka mikononi mwa mharibifu.

55 Na bwana wa shamba la mizabibu akamwambia mmoja wa watumishi wake: Nenda na uwakusanye watumishi wangu waliobakia, na uchukue nguvu ya nyumba yangu yote, ambao ni wapiganaji wangu, vijana wangu, na wale ambao ni wa umri wa kati pia miongoni mwa watumishi wangu wote, ambao ndiyo nguvu ya nyumba yangu, isipokuwa wale tu ambao nimewateua kukaa;

56 Na nendeni moja kwa moja kwenye nchi ya shamba langu la mizabibu, na mlikomboe shamba langu la mizabibu; kwani ni langu; nimelinunua kwa fedha.

57 Kwa hiyo, nendeni haraka kwenye nchi yangu; bomoeni kuta za adui zangu; angusheni chini mnara wao, na watawanyeni walinzi wao.

58 Na kadiri watakavyo kusanyika pamoja dhidi yenu, nipatieni haki na adui wangu, ili haraka niweze kuja pamoja na mabaki ya nyumba yangu na kuimiliki nchi.

59 Na yule mtumishi akamwambia bwana wake: Mambo haya yatakuwa lini?

60 Naye akamwambia mtumishi wake: Wakati nitakapotaka; enenda zako haraka, na ukafanye mambo yote niliyokuamuru;

61 Na huu ndiyo utakuwa muhuri wangu na baraka juu yako—wakili mwaminifu na mwenye busara ndani ya nyumba yangu, mtawala katika ufalme wangu.

62 Na watumishi wake wakaenda upesi, na wakafanya mambo yote waliyoamriwa na Bwana wake; na baada ya siku nyingi mambo yote yalitimizwa.

63 Tena, amini ninawaambia, nitawaonyesha nionalo kuwa hekima juu ya makanisa yote, ilimradi wapo tayari kuongozwa katika njia ya haki na iliyo sahihi kwa wokovu wao—

64 Ili kazi ya kuwakusanya pamoja watakatifu wangu ipate kuendelea, ili niweze kuwajenga kwa jina langu juu ya mahali patakatifu; kwani wakati wa mavuno umewadia, na neno langu halina budi kutimizwa.

65 Kwa hiyo, ni lazima niwakusanye watu wangu pamoja, kulingana na mfano wa ngano na magugu, ili ngano ipate kuhifadhiwa ghalani ili kumiliki uzima wa milele, na kuvikwa taji la utukufu wa selestia, wakati nitakapokuja katika ufalme wa Baba yangu kumzawadia kila mtu kulingana na matendo yake yatakavyokuwa;

66 Wakati magugu yatafungwa mafungu mafungu, na kamba zake zitakuwa imara, ili yaweze kuchomwa kwa moto usiozimika.

67 Kwa hiyo, amri ninaitoa kwa makanisa yote, kwamba wataendelea kukusanyika pamoja mahali pale ambapo nimepateua.

68 Hata hivyo, kama vile nilivyowaambia ninyi katika amri ya awali, na kukusanyika kwenu kusiwe kwa haraka, wala kwa kuruka; bali acheni mambo yote yawe yameandaliwa kabla yenu.

69 Na ili mambo yote yawe yameandaliwa kabla yenu, zishikeni amri ambazo nimezitoa kwenu juu ya mambo haya—

70 Ambayo husema, au hufundisha, kununua ardhi yote kwa fedha, ile iwezekanayo kununuliwa kwa fedha, katika maeneo ya kando ya nchi ambayo nimeiteua kuwa nchi ya Sayuni, kwa ajili ya kuanzia kukusanya watakatifu wangu;

71 Ardhi yote ambayo inaweza kununuliwa katika wilaya ya Jackson, na wilaya za kando kando, na kuyaacha yaliyosalia mikononi mwangu.

72 Sasa, amini ninawaambia, makanisa yote na yakusanye pamoja fedha zao zote; mambo haya na yafanyike kwa wakati wake, lakini siyo kwa haraka; na kuangalia mambo yote yawe yameandaliwa mapema.

73 Na watu maarufu wateuliwe, hata watu wenye hekima, na watumwe kwenda kununua ardhi hiyo.

74 Na makanisa katika nchi za mashariki, wakati yatakapokuwa yamejengwa, ikiwa yatausikiliza ushauri huu yanaweza kununua ardhi na kukusanyika pamoja juu yake; na kwa njia hii yataweza kuanzisha Sayuni.

75 Imekwisha kuwa tayari ghalani ya kutosha, ndiyo, hata kwa wingi, kuikomboa Sayuni, na kupajenga mahali pake palipoharibiwa, pasitupwe chini tena, iwapo makanisa hayo, ambayo hujiita kwa jina langu, yangekuwa tayari kuisikiliza sauti yangu.

76 Na tena ninawaambia, wale ambao wametawanywa na adui zao, ni mapenzi yangu kwamba yawapasa kuendelea kuililia haki na urejesho, na ukombozi, kwa mikono ya wale waliowekwa kama watawala na walio katika mamlaka juu yenu—

77 Kulingana na sheria na katiba ya watu, ambayo nimeiruhusu iwekwe, na kulindwa kwa ajili ya haki na ulinzi wa wote wenye mwili, kulingana na kanuni zilizo za haki na takatifu;

78 Ili kila mtu aweze kutenda kulingana na mafundisho na kanuni zihusuzo hali yake ya baadaye, kulingana na haki ya kujiamulia ambayo nimempa, ili kila mtu aweze kuwajibika kutokana na dhambi zake mwenyewe katika siku ya hukumu.

79 Kwa hiyo, siyo sahihi kwamba mtu yeyote awe mtumwa kwa mtu mwingine.

80 Na kwa dhumuni hili nimeiweka Katiba ya nchi hii, kwa mikono ya watu wenye hekima ambao niliwainua hasa kwa dhumuni hili, na kuikomboa nchi kwa kumwaga damu.

81 Sasa, tuwalinganishe na nini watoto wa Sayuni? Nitawalinganisha na mfano wa mwanamke na mwamuzi asiye na haki, kwani wanadamu imewapasa daima kuomba na pasipo kuchoka, ambao husema—

82 Palikuwako katika mji mwamuzi ambaye hakumwogopa Mungu, wala hakumjali mtu.

83 Na palikuwako na mwanamke mjane katika mji ule, naye alimwendea, akisema: Nipatie haki na adui yangu.

84 Naye kwa muda alikataa, lakini baadaye akasema moyoni mwake: Ijapokuwa simwogopi Mungu, wala sijali mtu, lakini kwa sababu mjane huyu ananisumbua nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima.

85 Hivyo ndivyo nitakavyo walinganisha watoto wa Sayuni.

86 Na walie chini ya miguu ya mwamuzi;

87 Na ikiwa hatawasikiliza, na walie chini ya miguu ya gavana;

88 Na ikiwa gavana hatawasikiliza, na walie chini ya miguu ya rais;

89 Na kama rais hatawasikiliza, ndipo Bwana atainuka na kutoka mahali pake alipojificha, na katika hasira yake kuu atalitesa taifa;

90 Na katika hasira yake, na katika ghadhabu yake, katika wakati wake, atawakatilia mbali wale waovu, wasio waaminifu, na watumishi wasio na haki, na kuwateulia nafasi yao miongoni mwa wanafiki, na wasioamini;

91 Hata nje gizani, ndiko kuna kilio, na kuomboleza, na kusaga meno.

92 Kwa hiyo, ombeni, kwamba masikio yao yapate kufunguliwa kwa vilio vyenu, ili niweze kuwahurumia, ili mambo haya yasiwafikie juu yao.

93 Niliyoyasema kwenu hayana budi kutukia, ili watu wote wasiwe na udhuru;

94 Ili watu wenye hekima na watawala wapate kusikia na kujua yale ambayo kamwe hawakuyafahamu;

95 Ili nilitimize tendo langu, tendo langu la ajabu, na kufanya kazi yangu, kazi yangu ya ajabu, ili watu wapate kupambanua kati ya wenye haki na waovu, asema Mungu wenu.

96 Na tena, ninawaambia, ni kinyume cha amri na mapenzi yangu kwamba mtumishi wangu Sidney Gilbert kuuza ghala yangu, ambayo nimeikabidhi kwa watu wangu, kuiuza mikononi mwa adui zangu.

97 Msiache kile nilichowakabidhi kichafuliwe kwa mikono ya adui zangu, kwa idhini ya wale wajiitao kwa jina langu;

98 Kwani hii ni dhambi mbaya na kubwa sana dhidi yangu, na dhidi ya watu wangu, kwa sababu ya mambo yale ambayo nimeyatangaza na ambayo karibu yatawaangukia mataifa.

99 Kwa hiyo, ni mapenzi yangu kwamba watu wangu wadai, na washikilie madai yao juu ya kile nilichowagawia, ingawa hawataruhusiwa kuishi juu yake.

100 Hata hivyo, sisemi kwamba hawataishi juu yake; kwani ilimradi wao watazaa matunda na kazi zinazostahili kwa ufalme wangu wataishi juu yake.

101 Watajenga, na mtu mwingine hatairithi; nao wapanda mizabibu, na kula matunda yake. Hivyo ndivyo. Amina.

Chapisha