Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 122


Sehemu ya 122

Neno la Bwana kwa Joseph Smith Nabii, wakati akiwa mfungwa gerezani huko Liberty, Missouri. Sehemu hii ni dondoo kutoka katika waraka kwa Kanisa ulioandikwa 20 Machi 1839 (ona kichwa cha habari kwa sehemu ya 121).

1–4, Miisho ya dunia italiulizia jina la Joseph Smith; 5–7, Hatari na mateso yake yote vitampa uzoefu na yatakuwa kwa faida yake; 8–9, Mwana wa Mtu amejishusha chini yao wote.

1 Miisho ya dunia italiulizia jina lako, na wapumbavu watakudhihaki, na jehanamu itapigana nawe kwa hasira;

2 Wakati walio safi moyoni, na wenye hekima, na walio maarufu, na walio wema, watautafuta ushauri, na mamlaka, na baraka kutoka chini ya mkono wako daima.

3 Na watu wako kamwe hawatakugeuka kwa ushuhuda wa wasaliti.

4 Na ingawa uwezo wao utakutupa katika matatizo, na gerezani, wewe utaheshimika; na lakini kwa muda mfupi na sauti yako itakuwa ya kutisha sana katikati ya adui zako kuliko simba mkali, kwa sababu ya uadilifu wako; na Mungu wako atakusimamia milele na milele.

5 Kama wewe umeitwa kupita kwenye taabu, kama wewe uko katika hatari miongoni mwa ndugu wa uongo; kama wewe uko katika hatari kati ya wezi; kama wewe ukiwa katika hatari nchi kavu au baharini;

6 Kama wewe utashtakiwa kwa namna zote za shutuma za uongo; kama adui zako wataanguka juu yako; kama watakuondoa wewe kutoka kwenye jumuia ya baba yako na mama na kaka na dada zako; na kama kwa upanga uliotolewa alani mwake adui zako watakuondoa kutoka kifuani mwa mke wako, na kwa wazao wako, na kwa mwana wako wa kwanza, ingawa ni wa umri wa miaka sita tu, atangʼangʼania kwenye mavazi yako, naye atasema, Baba yangu, baba yangu, kwa nini huwezi kukaa na sisi? Ee, baba yangu watu hawa wanakwenda kukufanya nini? na kama hivyo watamwondoa kwako kwa upanga, nawe utaburuzwa kwenda gerezani, na adui zako watakuzungukazunguka kama mbwa mwitu wakitafuta damu ya mwanakondoo;

7 Na kama utatupwa ndani ya shimo, au katika mikono ya wauaji, na hukumu ya kifo ikapitishwa juu yako; kama utatupwa kilindini; kama mawimbi makali yatakula njama dhidi yako; kama upepo mkali utakuja kuwa adui yako; kama mbingu zitakusanya giza, na vitu vyote vya asili vikiungana ili kuzingira njia yako; na juu ya yote, kama mataya yale ya jehanamu yataachama kinywa wazi kwa ajili yako, fahamu wewe, mwanangu, kwamba mambo haya yote yatakupa wewe uzoefu, na yatakuwa kwa faida yako.

8 Mwana wa Mtu amejishusha chini yao wote. Je, wewe u mkuu kuliko yeye?

9 Kwa hiyo, shikilia njia yako, na ukuhani utabakia nawe; kwa kuwa mipaka yao imewekwa, hawawezi kuivuka. Siku zako zinafahamika, na miaka yako haitahesabika kuwa michache; kwa hiyo, usiogope mwanadamu awezacho kukutenda, kwani Mungu atakuwa pamoja nawe milele na milele.

Chapisha