Sehemu ya 138
Ono, lililotolewa kwa Rais Joseph F. Smith katika Jiji la Salt Lake, Utah, mnamo tarehe 3 Oktoba 1918. Katika hotuba yake ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 89 wa Nusu Mwaka wa Kanisa, 4 Oktoba 1918, Rais Smith alitangaza kwamba alikuwa amepokea mawasiliano matakatifu kadhaa katika kipindi cha mwezi uliopita. Moja ya haya, ni juu ya Mwokozi kutembea ulimwengu wa wafu wakati mwili wake ulipokuwa kaburini, Rais Smith alikuwa amelipokea siku ya jana yake. Liliandikwa mara moja baada ya kufungwa kwa mkutano. Mnamo tarehe 31 Oktoba 1918, liliwakilishwa kwa washauri katika Urais wa Kwanza, Baraza la Mitume Kumi na Wawili, na Patriaki, nalo walilikubali kwa kauli moja.
1–10, Rais Joseph F. Smith atafakari juu ya maandiko ya Petro na matembezi ya Bwana wetu katika ulimwengu wa kiroho; 11–24, Rais Smith awaona wafu wenye haki wamekusanyika peponi na huduma ya Kristo miongoni mwao; 25–37, Anaona jinsi kuhubiriwa kwa injili kulivyoanzishwa miongoni mwa roho hizo; 38–52, Anamwona Adamu, Hawa, na wengi wa manabii watakatifu katika ulimwengu wa roho ambao waliitazama hali kabla ya ufufuko wao kama kifungoni; 53–60, Wafu wenye haki wa leo huendelea na kazi zao katika ulimwengu wa kiroho.
1 Siku ya tatu ya Oktoba, katika mwaka wa elfu moja mia tisa na kumi na nane, nilikaa chumbani mwangu nikitafakari juu ya maandiko;
2 Na nikitazama juu ya dhabihu kuu ya upatanisho ambao ulifanywa na Mwana wa Mungu, kwa ajili ya ukombozi wa ulimwengu;
3 Na upendo mkuu na wa ajabu ulioonyeshwa na Baba na Mwana katika kuja kwa Mkombozi ulimwenguni;
4 Ili kwa njia ya upatanisho wake, na kwa utii kwa kanuni za injili, mwanadamu apate kuokolewa.
5 Wakati nikiwa ninajishughulisha hivyo, akili yangu ilirejea kwenye maandiko ya mtume Petro, kwa watakatifu wa mwanzo waliosambaa sehemu za Ponto, Galatia, Kapadokia, na sehemu nyinginezo za Asia, ambako injili ilikuwa imehubiriwa baada ya kusulubiwa kwa Bwana.
6 Nilifungua Biblia na kusoma mlango wa tatu na wa nne ya waraka wa Petro, na nilivyokuwa nikisoma nilivutiwa sana, kuliko ilivyokuwa kabla yake, na sehemu hizi zifuatazo:
7 “Kwa maana Kristo naye ameteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio na haki, ili atulete kwa Mungu, mwili wake akauawa, bali akahuishwa na Roho:
8 “Ambayo kwa hiyo pia aliwaendea roho waliokaa kifungoni akawahubiria;
9 “Wakati mmoja walikuwa hawatii wakati uvumilivu wa Mungu ulipokuwa ukingoja katika siku za Nuhu, wakati safina ilipokuwa ikitengenezwa, ambamo ndani yake wachache, yaani, watu wanane waliokoka kwa maji.” (1 Petro 3:18–20.)
10 “Maana kwa ajili hii hata hao waliokufa pia walihubiriwa injili, ili wapate kuhukumiwa kulingana na wanadamu katika mwili, bali waishi kulingana na Mungu katika roho.” (1 Petro 4:6.)
11 Nilipokuwa nikitafakari juu ya mambo haya ambayo yameandikwa, macho yangu ya ufahamu yakafunguliwa, na Roho wa Bwana akatulia juu yangu, na nikaona jeshi la waliokufa wote, wadogo na wakubwa.
12 Nao walikusanywa pamoja katika mahali pamoja kundi kubwa lisilohesabika la roho za wenye haki, ambao wamekuwa waaminifu katika ushuhuda wa Yesu wakati walipoishi katika mwili wenye kufa;
13 Na ambao walikuwa wametoa dhabihu katika mfano wa dhabihu iliyo kuu ya Mwana wa Mungu, na wakapata taabu katika jina la Mkombozi wao.
14 Hawa wote wameondoka katika mwili wenye kufa, wakiwa imara katika tumaini la ufufuko mtukufu, kupitia neema ya Mungu Baba na Mwanawe wa Pekee, Yesu Kristo.
15 Niliona kwamba walijawa na shangwe na furaha, nao walikuwa wanafurahi kwa pamoja kwa sababu siku ya ukombozi wao ilikuwa imefika.
16 Walikusanyika kusubiri kuja kwa Mwana wa Mungu katika ulimwengu wa roho, kuwatangazia ukombozi wao kutokana na kamba za mauti.
17 Mavumbi yao yaliyolala yangerejeshwa kwenye umbile kamili, mfupa kwa mfupa mwenzie na mafuta na nyama juu yake, roho na mwili kuunganika kamwe isitengane tena, ili wapate kupokea utimilifu wa shangwe.
18 Wakati umati huu mkubwa ulipokuwa ukisubiri na kuongea, wakifurahia katika saa ya ukombozi wao kutokana na minyororo ya mauti, Mwana wa Mungu akatokea, akitangaza uhuru kwa wafungwa waliokuwa waaminifu;
19 Na hapo akawahubiria wao injili isiyo na mwisho, mafundisho ya ufufuko na ukombozi wa mwanadamu kutokana na anguko, na kutokana na dhambi za binafsi kwa masharti ya toba.
20 Lakini kwa waovu hakwenda, na miongoni mwa wasio mcha Mungu na wasiotubu ambao wamejichafua wenyewe wakati wakiwa katika mwili, sauti yake haikusikika;
21 Wala waasi ambao walikataa shuhuda na maonyo ya manabii wa kale hawakuona uwepo wake, wala kuutazama uso wake.
22 Pale walipokuwa hawa, giza lilitawala, lakini miongoni mwa wenye haki kulikuwa na amani;
23 Na watakatifu walifurahia katika ukombozi wao, nao walipiga magoti na kumshukuru Mwana wa Mungu kama Mkombozi na Mwokozi wao kutokana na mauti na minyororo ya jehanamu.
24 Nyuso zao zilingʼara, na nuru kutoka katika uwepo wa Bwana ilitulia juu yao, nao wakaimba nyimbo za sifa kwa jina lake takatifu.
25 Nilistaajabia, kwani nilitambua kwamba Mwokozi alitumia kiasi cha miaka mitatu katika huduma yake miongoni mwa Wayahudi na wale walio nyumba ya Israeli, akijitahidi kuwafundisha wao injili isiyo na mwisho na kuwaita kwenye toba;
26 Na bado, licha ya matendo yake makuu, na miujiza, na tangazo la ukweli, katika uwezo mkubwa na mamlaka, palikuwa na wachache tu walio isikiliza sauti yake, na kufurahia mbele zake, na kupokea wokovu kutoka kwake.
27 Lakini huduma yake miongoni mwa wale walio wafu ilikuwa fupi na ya muda mchache iliyokuwa katikati ya kusulubiwa na kufufuka kwake;
28 Na niliona ajabu kwa maneno ya Petro—ambamo anasema kwamba Mwana wa Mungu alizihubiria roho zilizokuwa kifungoni, ambao wakati fulani hawakuwa watiifu, wakati uvumilivu wa Mungu ulipokuwa ukingoja siku za Nuhu—na ni kwa jinsi gani iliwezekana kwake yeye kuhubiria roho zile na kufanya kazi muhimu miongoni mwao katika kipindi kifupi namna hiyo.
29 Na nilipokuwa nikistaajabu, macho yangu yakafunguliwa, na ufahamu wangu ukahuishwa, nami nikatambua kwamba Bwana hakwenda kifungoni miongoni mwa waovu na wasiokuwa watiifu ambao waliukataa ukweli, kuwafundisha wao;
30 Bali tazama, kutoka miongoni mwa wenye haki, aliunda jeshi lake na akawateua wajumbe, waliovikwa uwezo na mamlaka, na akawapa mamlaka ya kwenda na kupeleka nuru ya injili kwa wao ambao walikuwa gizani, hata kwa roho zote za wanadamu; na hivyo ndivyo injili ilivyohubiriwa kwa wafu.
31 Na wajumbe waliochaguliwa walikwenda kuitangaza siku iliyokubaliwa ya Bwana na kutangaza uhuru kwa wafungwa ambao walifungwa, hata kwa wote ambao wangetubu dhambi zao na kuipokea injili.
32 Hivyo ndivyo injili ilivyo hubiriwa kwa wale ambao walikufa katika dhambi zao, pasipo ufahamu wa ukweli, au katika uvunjaji wa sheria, wakiwa wamewakataa manabii.
33 Hawa walifundishwa imani kwa Mungu, toba ya dhambi, ubatizo ufanywa kwa niaba ya wafu kwa ajili ya ondoleo la dhambi, kipawa cha Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono;
34 Na kanuni nyingine zote za injili ambazo zilikuwa muhimu kwao kuzijua ili kujithibitishia wenyewe kwamba waweze kuhukumiwa kulingana na wanadamu katika mwili, lakini waishi kulingana na Mungu katika roho.
35 Na hivyo ilijulikana miongoni mwa wafu, wote wadogo na wakubwa, wasio na haki vile vile waaminifu, kwamba ukombozi ulitimizwa kwa njia ya dhabihu ya Mwana wa Mungu juu ya msalaba.
36 Hivyo ndivyo ilivyojulikana kwamba Mkombozi wetu aliutumia muda wake wakati wa kuishi kwake katika ulimwengu wa roho, akifundisha na kuziandaa roho za manabii waaminifu ambao walimshuhudia yeye katika mwili;
37 Ili wao wapate kuupeleka ujumbe wa ukombozi kwa wafu wote, ambao hakuweza kuwaendea yeye mwenyewe, kwa sababu ya uasi wao na uvunjaji wao wa sheria, ili wao kwa njia ya huduma ya watumishi wake wapate pia kuyasikia maneno yake.
38 Miongoni mwa wakuu na wenye nguvu waliokuwa wamekusanyika katika mkutano huu mkuu wa wenye haki walikuwa Baba Adamu, Mzee wa Siku nyingi na baba wa wote,
39 Na mtukufu Mama yetu Hawa, pamoja na mabinti zake wengi waaminifu ambao wameishi katika karne na wakimwabudu Mungu wa kweli na aliye hai.
40 Habili, wa kwanza aliyeuawa kiushahidi wa dini, alikuwepo, na kaka yake Sethi, mmoja kati ya wenye nguvu, ambaye alikuwa katika mfano wa baba yake, Adamu.
41 Nuhu, aliyetoa tahadhari ya gharika; Shemu, kuhani aliye mkuu; Ibrahimu, baba wa walio waaminifu; Isaka, Yakobo, na Musa mtoa-sheria mkuu wa Israeli;
42 Na Isaya, ambaye alitangaza kwa unabii kwamba Mkombozi alipakwa mafuta ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa kufunguliwa kwao, pia walikuwepo hapo.
43 Zaidi ya hao, Ezekieli, ambaye alionyeshwa ndotoni bonde kuu la mifupa mikavu, ambayo ilikuwa ivikwe mwili, ili kuja tena katika ufufuko wa wafu, kama nafsi hai;
44 Danieli, ambaye aliona na kutabiri juu ya kuanzishwa kwa ufalme wa Mungu katika siku za mwisho, ambao kamwe hautaharibiwa wala kutolewa kwa watu wengine;
45 Elia, aliyekuwa pamoja na Musa juu ya Mlima wa Kugeuka sura;
46 Na Malaki, nabii aliyeshuhudia juu ya kuja kwa Eliya—ambaye pia Moroni alimsema kwa Nabii Joseph Smith, akisema kwamba yeye lazima atakuja kabla ya kuja kwa siku ile iliyo kuu na ya kutisha ya Bwana—pia walikuwepo pale.
47 Nabii Eliya alikuwa apande katika mioyo ya watoto ahadi zilizofanywa kwa baba zao.
48 Ikionyeshwa dalili ya kazi kuu itakayofanyika katika mahekalu ya Bwana katika kipindi cha utimilifu wa nyakati, kwa ajili ya ukombozi wa wafu, na kuwafunga watoto kwa wazazi wao, isije dunia yote ikapigwa kwa laana na kuharibiwa kabisa wakati wa kuja kwake.
49 Wote hawa na wengine zaidi, hata manabii walioishi miongoni mwa Wanefi na wakashuhudia juu ya kuja kwa Mwana wa Mungu, walichanganyika katika kusanyiko hili kuu na wakimsubiri kwa ajili ya ukombozi wao,
50 Kwani wafu waliotazamiwa kwa muda mrefu kutokuwepo kwa roho zao kutoka kwenye miili yao kama ni utumwa.
51 Hizi Bwana alizifundisha, na kuzipa uwezo wa kutoka, baada ya ufufuko wake kutoka kwa wafu, ili kuingia katika ufalme wa Baba yake; ili kuvikwa kutokufa na uzima wa milele.
52 Na kuendelea kutoka saa hiyo kufanya kazi zao kama ilivyoahidiwa na Bwana, na kuwa washiriki wa baraka zote ambazo zilishikiliwa kwa akiba kwa ajili yao waliompenda yeye.
53 Nabii Joseph Smith, na baba yangu, Hyrum Smith, Brigham Young, John Taylor, Wilford Woodruff, na roho wengine wateule ambao walihifadhiwa ili kuja katika kipindi cha utimilifu wa nyakati kushiriki katika kuweka misingi ya kazi kuu ya siku za mwisho,
54 Pamoja na ujenzi wa mahekalu na utekelezaji wa ibada zake kwa ajili ya ukombozi wa wafu, walikuwa pia katika ulimwengu wa roho.
55 Niligundua kwamba walikuwako pia miongoni mwa wakuu na watu maarufu waliochaguliwa mwanzoni kuwa watawala katika Kanisa la Mungu.
56 Hata kabla hawajazaliwa, hao, pamoja na wengine wengi, walipokea somo lao la kwanza katika ulimwengu wa roho na waliandaliwa kuja katika wakati ufaao wa Bwana kufanya kazi katika shamba lake la mizabibu kwa ajili ya wokovu wa roho za wanadamu.
57 Niliona kwamba wazee waaminifu wa kipindi hiki, wakati wakiondoka kutoka maisha katika mwili wenye kufa, huendelea na kazi zao katika kuhubiri injili ya toba na ukombozi, kupitia dhabihu ya Mwana Pekee wa Mungu, miongoni mwa wale walio gizani, na chini ya utumwa wa dhambi katika ulimwengu mkuu wa roho za wafu.
58 Wafu wanaotubu watakombolewa, kwa njia ya utii kwa ibada za nyumba ya Mungu.
59 Na baada ya kulipia adhabu ya uvunjaji wao wa sheria, na kuoshwa safi, watapokea thawabu kulingana na matendo yao, kwa kuwa wao ni warithi wa wokovu.
60 Hivyo ndivyo lilivyokuwa ono la ukombozi wa wafu lililofunuliwa kwangu, na ninashuhudia, na ninajua kwamba ushuhuda huu ni wa kweli, kwa njia ya baraka ya Bwana wetu na Mwokozi, Yesu Kristo, hivyo ndivyo. Amina.