Sehemu ya 45
Ufunuo uliotolewa kupitia Joseph Smith Nabii kwa Kanisa, huko Kirtland, Ohio, 7 Machi 1831. Kama utangulizi wa kumbu kumbu ya ufunuo huu, Historia ya Joseph Smith inaeleza kwamba “katika umri huu wa Kanisa … taarifa nyingi za uongo … na hadithi za kijinga, zilichapishwa … na kusambazwa, ili kuwazuia watu wasichunguze kazi, au kuikumbatia imani. … Lakini kwa shangwe ya Watakatifu, nilipokea yafuatayo.”
1–5, Kristo ni mtetezi wetu kwa Baba; 6–10, Injili ni ujumbe wa kuitengeneza njia mbele za Bwana; 11–15, Enoki na nduguze wamepokelewa kwa Bwana Mwenyewe; 16–23, Kristo alifunua ishara za ujio Wake kama zilivyotolewa kwenye Mlima wa Mizeituni; 24–38, Injili itarejeshwa, nyakati za Wayunani zitakapotimia, na maradhi ya ukiwa yatakapoifunika nchi; 39–47, Ishara, maajabu na Ufufuko zitaambatana na Ujio wa Pili; 48–53, Kristo atasimama juu ya Mlima wa Mizeituni, na Wayahudi wataona majeraha katika mikono Yake na miguu; 54–59, Bwana atatawala wakati wa Milenia; 60–62, Nabii anaelekezwa kuanza tafsiri ya Agano Jipya, kupitia hilo taarifa muhimu zitafanywa kujulikana; 63–75, Watakatifu wanaamriwa kukusanyika na kujenga Yerusalemu Mpya, ambamo watu kutoka mataifa yote watakuja.
1 Sikilizeni, Enyi watu wa kanisa langu, ambao kwenu ufalme umetolewa; sikilizeni na mtege sikio kwake yule aliyeweka msingi wa dunia, na aliyefanya mbingu na vyote vilivyomo, na ambaye kwake yeye vitu vyote vilifanyika vinavyoishi, na vinavyokwenda, na kuwa na uhai.
2 Na tena ninasema, sikilizeni sauti yangu, isije mauti ikawapata; katika saa msiyodhani wakati wa majira ya joto yamepita, na mavuno yamekwisha, na nafsi zenu hazijaokolewa.
3 Msikilizeni yeye aliye mtetezi kwa Baba, anayetetea mambo yetu mbele zake—
4 Akisema: Baba, tazama mateso na kifo chake yeye ambaye hakutenda dhambi, ambaye ulipendezwa naye; tazama damu ya mwanao iliyomwagika; damu yake yeye ambaye ulimtoa ili upate kutukuzwa;
5 Kwa hiyo, Baba, wasamehe hawa ndugu zangu ambao wanaamini juu ya neno langu, ili waweze kuja kwangu na kupata uzima usio na mwisho.
6 Sikilizeni, Enyi watu wa kanisa langu, nanyi wazee sikilizeni kwa pamoja, na isikilizeni sauti yangu wakati iitapo leo, na msiishupaze mioyo yenu;
7 Kwani amini ninawaambia kwamba Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, nuru na uzima wa ulimwengu—nuru ile ingʼaayo gizani na giza haiitambui.
8 Nilikuja kwa walio wangu, na walio wangu hawakunipokea; bali wote walionipokea niliwapa uwezo wa kufanya miujiza mingi, na kuwa wana wa Mungu; na hata kwa wale wote ambao waliamini juu ya jina langu niliwapa uwezo wa kupata uzima wa milele.
9 Na hata hivyo nimepeleka agano langu lisilo na mwisho ulimwenguni, liwe nuru ya ulimwengu, na itakuwa ishara kwa watu wangu, na kwa Wayunani waitafute, na kuwa ujumbe mbele ya uso wangu atakayeitengeneza njia mbele zangu.
10 Kwa hiyo, njooni, na pamoja naye yule ajaye nitahojiana naye kama vile watu katika siku za kale, na nitawaonyesha ninyi hoja zangu zenye nguvu.
11 Kwa hiyo, sikilizeni ninyi kwa pamoja na acheni niwaonyeshe hata hekima yangu—hekima yake huyo msemaye ni Mungu wa Henoko, na ndugu zake,
12 Waliotengwa kutoka duniani, na kupokelewa kwangu mwenyewe—mji uliohifadhiwa hadi siku ya haki itakapofika—siku ambayo ilitafutwa na watu wote watakatifu, na hawakuipata kwa sababu ya uovu na machukizo;
13 Na wakakiri kwamba walikuwa wageni na wasafiri juu ya dunia;
14 Lakini wakapata ahadi kwamba yawapasa kuitafuta na kuiona wakiwa katika miili yao.
15 Kwa hiyo, sikilizeni na mimi nitahojiana na nanyi, na nitasema kwenu na kutoa unabii, kama kwa watu katika siku za kale.
16 Nami nitaonyesha wazi kama nilivyoonyesha kwa wanafunzi wangu kama nilivyosimama mbele yao katika mwili, na kuwaambia wao, nikisema: Kama mlivyoomba kwangu juu ya ishara za kuja kwangu, katika siku nitakapokuja katika utukufu wangu katika mawingu ya mbinguni, ili kuzitimiza ahadi ambazo nilizifanya kwa babu zenu,
17 Kama mlivyoangalia kutoweka kwa muda mrefu kwa roho zenu kutoka katika miili yenu kuwa hali ya kufungwa, nitaonyesha kwenu jinsi siku ya ukombozi itakavyokuja, na pia urejesho wa Waisraeli waliotawanywa.
18 Na sasa mmeliona hili hekalu lililoko katika Yerusalemu, ambalo mnaliita nyumba ya Mungu, na maadui zenu wanasema kwamba nyumba hii kamwe haitaanguka.
19 Lakini, amini ninawaambia, kwamba ukiwa utakuja juu ya kizazi hiki kama vile mwizi ajavyo usiku, na watu hawa wataangamizwa na kutawanywa miongoni mwa mataifa yote.
20 Na hekalu hili ambalo mnaliona litatupwa chini kwamba halitasalia jiwe juu ya jiwe.
21 Na itakuwa, kwamba kizazi hiki cha Wayahudi hakitapita hadi kila ukiwa ambao nimewaambia juu yao utakapotokea.
22 Ninyi mnasema kwamba mnajua kwamba mwisho wa ulimwengu unakuja; mnasema pia mnajua kwamba mbingu na dunia zitapita;
23 Na katika hii ninyi mnasema kweli, kwani hivyo ndivyo; lakini mambo haya ambayo nimewaambia ninyi hayatapita hadi yote yatimie.
24 Na hili nimewaambia ninyi juu ya Yerusalemu; na wakati siku ile itakapokuja, baki litatawanywa miongoni mwa mataifa yote;
25 Lakini watakusanywa tena; isipokuwa watabakia hadi nyakati za Wayunani zitakapotimia.
26 Na katika siku ile kutasikika vita na minongʼono ya vita, na ulimwengu wote utakuwa katika ghasia, na watu watavunjika mioyo kwa hofu, na watasema kwamba Kristo anakawia kuja hadi mwisho wa dunia.
27 Na upendo wa wanadamu utapoa, na uovu utaongezeka.
28 Na wakati wa Wayunani ukifika, mwanga utazuka miongoni mwao wakaao gizani, nayo itakuwa utimilifu wa injili yangu;
29 Lakini hawaipokei; kwani hawaioni nuru hii, na wanaigeuza mioyo yao kutoka kwangu kwa sababu ya maagizo ya wanadamu.
30 Na katika kizazi hicho nyakati za Wayunani zitatimizwa.
31 Na kutakuwa na watu waliosimama katika kizazi kile, ambao hawatapita hadi waone pigo lifurikalo; kwani maradhi ya ukiwa yataifunika nchi.
32 Lakini wanafunzi wangu watasimama katika mahali pa takatifu, na wala hawataondoshwa; lakini miongoni mwa waovu, watu watapaza sauti zao na kumlaani Mungu na kufa.
33 Na kutakuwa na matetemeko ya ardhi pia mahali mbali mbali, na ukiwa mwingi; bado watu wataishupaza mioyo yao dhidi yangu, na watashika upanga, mmoja dhidi ya mwingine, na watauana wao kwa wao.
34 Na sasa, wakati Mimi Bwana nilipoyasema maneno haya kwa wanafunzi wangu, walifadhaika.
35 Nami nikawaambia: Msifadhaike, kwani haya yote yatakapokuja kutukia, ili ninyi muweze kujua kwamba ahadi ambazo zimefanywa kwenu zitatimizwa.
36 Na wakati nuru itakapoanza kuzuka, itakuwa kwao kama mfano ambao nitawaonyesha—
37 Angalieni na tazameni mtini, nanyi mnaiona kwa macho yenu, na mnasema wakati inapoanza kuchipua, na majani yake yakiwa bado laini, kwamba kiangazi sasa ki karibu;
38 Vivyo hivyo itakuwa katika siku ile watakapoona mambo haya yote, ndipo watakapojua kwamba saa i karibu.
39 Na itakuja kutokea kwamba yule ambaye ananiogopa mimi atakuwa akiitazamia siku ile kuu ya Bwana itakapokuja, hata kwa ishara za kuja kwa Mwana wa Mtu.
40 Nao wataona ishara na maajabu, kwani zitaonyeshwa mbinguni juu, na chini ya dunia.
41 Na wataona damu, na moto, na mvuke wa moshi.
42 Na kabla ya kuja kwa siku ya Bwana, jua litatiwa giza, na mwezi utageuka kuwa damu, na nyota zitaanguka kutoka mbinguni.
43 Na baki litakusanywa mahali hapa;
44 Na ndipo watanitafuta, na, tazama, nitakuja; na wataniona katika mawingu ya mbinguni, nimevikwa nguvu na utukufu mkuu; pamoja na malaika wote watakatifu; na yule asiyenitazamia mimi ataondolewa.
45 Lakini kabla mkono wa Bwana haujashuka, malaika atapiga parapanda yake, na watakatifu waliolala watakuja kunilaki mawinguni.
46 Kwa hivyo, kama umelala katika imani umebarikiwa; kwani kama sasa unionavyo na kujua kwamba Mimi ndimi, hata hivyo ndipo utakuja kwangu na roho yako itaishi, na ukombozi wako utakamilishwa; na watakatifu watakuja kutoka pande nne za dunia.
47 Ndipo mkono wa Bwana utashuka juu ya mataifa.
48 Na halafu Bwana atakanyaga mguu wake juu ya mlima huu, nao utapasuka katika pande mbili, na dunia itatetemeka, na kuyumba mbele na nyuma, na mbingu pia zitatetemeka.
49 Na Bwana atatoa sauti yake, na miisho yote ya dunia itaisikia; na mataifa ya ulimwengu yataomboleza, na wale waliocheka wataona makosa yao.
50 Na majanga yatamfunika mwenye kudhihaki, na mwenye dharau atakoma; na wote watazamiao uovu watakatiliwa mbali na kutupwa katika moto.
51 Na ndipo Wayahudi watanitazama mimi na kusema: Je, haya majeraha katika mikono yako na katika miguu yako ni nini?
52 Ndipo watakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana; kwani nitawaambia: Majeraha haya ni majeraha niliyotiwa katika nyumba ya marafiki zangu. Mimi ndiye yule aliyeinuliwa. Mimi ni Yesu ambaye alisulubiwa. Mimi ni Mwana wa Mungu.
53 Na ndipo watakapolia kwa sababu ya uovu wao; ndipo watakapoomboleza kwa sababu walimtesa mfalme wao.
54 Na ndipo mataifa ya wapagani yatakombolewa, na wale ambao hawakuijua sheria watakapokuwa na sehemu katika ufufuo wa kwanza; na hali yao itastahimiliwa.
55 Na Shetani atafungwa, kwamba hatakuwa na sehemu katika mioyo ya wanadamu.
56 Na siku ile, wakati nitakapokuja katika utukufu wangu, ndipo mfano utakapotimia ambalo nilisema juu ya wanawali kumi.
57 Kwani wale walio na hekima na kupokea ukweli, na kumchukua Roho Mtakatifu kuwa kiongozi wao, na hawajadanganyika—amini ninawaambia, hawatakatiliwa chini na kutupwa katika moto, bali watastahimili siku ile.
58 Na dunia itatolewa kwao kwa urithi; nao wataongezeka na kuwa na nguvu, na watoto wao watakua pasipo dhambi hadi kwenye wokovu.
59 Kwa kuwa Bwana atakuwa katikati yao, na utukufu wake utakuwa juu yao, naye atakuwa mfalme wao na mtoa sheria wao.
60 Na sasa, tazama, ninawaambia, haitatolewa kwenu kujua zaidi juu ya mlango huu, hadi Agano Jipya litakapokuwa limetafsiriwa, na humo mambo haya yote yatafanywa yajulikane;
61 Kwa hivyo ninaitoa kwenu ili ninyi muweze sasa kutafsiri, ili muweze kujitayarisha kwa ajili ya mambo yajayo.
62 Kwani amini ninawaambia, kwamba mambo makubwa yanawasubiri;
63 Mnasikia juu ya vita katika nchi za ngʼambo; lakini, tazameni, ninawaambia, i karibu, milangoni mwenu, na siyo miaka mingi kutoka sasa mtasikia vita katika nchi yenu wenyewe.
64 Kwa hivyo Mimi, Bwana, nimesema, kusanyikeni kutoka nchi za mashariki, jikusanyeni pamoja ninyi wazee wa kanisa langu; enendeni katika nchi za magharibi, watangazieni wakazi wake watubu, na kadiri watakavyotubu, yajengeni makanisa kwa ajili yangu.
65 Na kwa moyo mmoja na nia moja, kusanyeni mali yenu ili muweze kununua urithi ambao baadaye utatolewa kwenu.
66 Nayo itaitwa Yerusalemu Mpya, nchi ya amani, mji wa kimbilio, mahali pa usalama kwa watakatifu wa Mungu Aliye Juu Sana;
67 Na utukufu wa Bwana utakuwa hapo, na hofu ya Bwana pia itakuwa hapo, kiasi kwamba waovu hawataufikia, na utaitwa Sayuni.
68 Na itakuwa miongoni mwa waovu, kwamba kila mtu ambaye hatauchukua upanga wake dhidi ya jirani yake itamlazimu kukimbilia Sayuni kwa usalama.
69 Na hapo watakusanyika kutoka kila taifa chini ya mbingu; na watakuwa watu pekee ambao hawatakuwa vitani mmoja dhidi ya mwingine.
70 Na itasemwa miongoni mwa waovu: Na tusiende kupigana na Sayuni, kwani wakazi wa Sayuni ni wa kuogopwa; kwa sababu hiyo hatuwezi kusimama.
71 Na itakuwa kwamba wenye haki watakusanywa kutoka miongoni mwa mataifa yote, nao watakuja Sayuni, wakiimba nyimbo za shangwe isiyo na mwisho.
72 Na sasa ninawaambia, yashikilieni mambo haya yasiende ngʼambo kwa walimwengu hadi itakapokuwa vyema kwangu, ili muweze kukamilisha kazi hii machoni pa watu, na machoni pa adui zenu, ili wao wasiweze kujua kazi zenu hadi mtakapomaliza jambo ambalo nimewaamuru;
73 Ili wakati watakapojua, waweze kuyafikiria mambo haya.
74 Kwani wakati ambao Bwana atajitokeza atakuwa mwenye kuogofya kwao, kwamba hofu yaweza kuwakamata, na wao watasimama mbali na wakitetemeka.
75 Na mataifa yote yataogopa kwa sababu ya hofu ya Bwana, na nguvu zake nyingi. Hivyo ndivyo. Amina.