Sehemu ya 29
Ufunuo uliotolewa kupitia Joseph Smith Nabii, mbele ya wazee sita, huko Fayette, New York, Septemba 1830. Ufunuo huu ulitolewa siku kadhaa kabla ya mkutano, kuanzia 26Â Septemba 1830.
1–8, Kristo anawakusanya wateule Wake; 9–11, Ujio wake waonyesha kuanza kwa Milenia; 12–13, Mitume Kumi na Wawili watawahukumu wana wa Israeli wote; 14–21, Ishara, mabaa, na ukiwa utautangulia Ujio wa Pili; 22–28, Ufufuo wa mwisho na hukumu ya mwisho itafuatia Milenia; 29–35, Mambo yote kwa Bwana ni ya kiroho; 36–39, Ibilisi na Majeshi yake walifukuzwa kutoka mbinguni ili wawajaribu wanadamu; 40–45, Anguko na Upatanisho huleta wokovu; 46–50, Watoto wadogo wamekombolewa kupitia Upatanisho.
1 Sikilizeni sauti ya Yesu Kristo, Mkombozi wenu, Mimi Ndimi Mkuu, ambaye mkono wake wa rehema umefanya upatanisho kwa ajili ya dhambi zenu;
2 Ambaye atawakusanya watu wake kama kuku avikusanyavyo vifaranga vyake chini ya mabawa yake, hata wengi kadiri watakavyoifuata sauti yangu na kujinyenyekeza mbele zangu, na kunilingana kwa sala kuu.
3 Tazama, amini, amini, ninawaambia, kwamba kwa wakati huu dhambi zenu zimesamehewa, kwa sababu hiyo pokeeni mambo haya; lakini kumbukeni msitende dhambi tena, isije hatari kubwa ikaja juu yenu.
4 Amini, ninawaambia kwamba ninyi ni wateule toka ulimwenguni kwa kuitangaza injili yangu kwa shangwe, kama shangwe, kama sauti ya parapanda.
5 Inueni mioyo yenu na furahini, kwani Mimi niko katikati yenu, na ni mtetezi wenu kwa Baba; na ni mapenzi yake kuwapa ule ufalme.
6 Na, kama ilivyoandikwa—Lolote mtakaloomba katika imani, mkiwa mmeungana katika sala mkiamini kulingana na amri yangu, mtapokea.
7 Na ninyi mmeitwa kuwakusanya wateule wangu; kwani wateule wangu huisikia sauti yangu na wala hawaishupazi mioyo yao;
8 Kwa hiyo amri imetoka kwa Baba kwamba wakusanywe mahali pamoja juu ya uso wa nchi hii, ili kuitayarisha mioyo yao na kujitayarisha katika mambo yote dhidi ya siku ile wakati taabu na ukiwa vitakapokuja juu ya waovu.
9 Kwani saa i karibu na siku yaja haraka wakati dunia imekomaa; na wote wenye kiburi na wao ambao hufanya maovu watakuwa kama makapi; na nitawateketeza, asema Bwana wa Majeshi, kwamba uovu hautakuwepo duniani;
10 Kwani saa i karibu, na yale yaliyonenwa na mitume wangu lazima yatatimia; kwani kama vile walivyosema ndivyo itakavyokuwa;
11 Kwani nitajifunua mwenyewe kutoka mbinguni kwa uwezo na utukufu mkuu, pamoja na majeshi yote ya mbinguni, na kukaa katika haki pamoja na wanadamu duniani miaka elfu moja, na waovu hawatastahimili.
12 Na tena, amini, amini, ninawaambia, na imetolewa amri kali, kwa mapenzi yake Baba, kwamba mitume wangu, wale Kumi na Wawili ambao walikuwa nami katika huduma yangu kule Yerusalemu, watasimama mkono wangu wa kuume katika siku ile ya kuja kwangu katika nguzo ya moto, wakiwa wamevikwa joho ya haki, na mataji juu ya vichwa vyao, katika utukufu kama vile Mimi nilivyo, kuihukumu nyumba yote ya Israeli, kadiri ya wengi jinsi walivyonipenda Mimi na kushika amri zangu, na siyo wengineo.
13 Kwani parapanda italia kwa sauti yenye kuendelea na kwa sauti, kama vile juu ya Mlima wa Sinai, na dunia yote itatetemeka, nao watatoka—ndiyo, hata wafu waliokufa katika Mimi, ili kupokea taji la haki, na kuvishwa, kama Mimi, na kuwa pamoja nami, ili tuweze kuwa na umoja.
14 Lakini, tazama, ninawaambia kwamba kabla siku hii kuu haijaja jua litatiwa giza, na mwezi utageuzwa kuwa damu, na nyota zitaanguka kutoka mbinguni, na kutakuwa na ishara kuu katika mbingu juu na nchi chini;
15 Na kutakuwa na kulia na kuomboleza miongoni mwa umati wa watu;
16 Na kutakuwa tufani kuu itakayoletwa ili kuangamiza mazao ya ulimwengu.
17 Na itakuwa kwa sababu ya uovu wa ulimwengu, kwamba nitalipiza kisasi juu ya waovu, kwa kuwa hawatatubu; kwani kikombe cha uchungu wa hasira yangu kimejaa; kwani tazama, damu yangu haitawatakasa kama hawatanisikiliza.
18 Kwa hiyo, Mimi Bwana Mungu nitawaleta inzi juu ya uso wa dunia, ambao watawazidi wakazi wake, nao watakula nyama zao, na kusababisha funza kuingia ndani yao;
19 Na ndimi zao zitazuiliwa kwamba hazitanena dhidi yangu; na nyama ya miili yao itaanguka kutoka kwenye mifupa yao, na macho yao kutoka kwenye matundu yake;
20 Na itakuwa kwamba wanyama wa porini na ndege wa angani watawala.
21 Na kanisa lile kuu na la machukizo, ambalo ni kahaba wa ulimwengu wote, litaangamizwa kwa moto uteketezao, kama ilivyonenwa kwa kinywa cha Ezekieli nabii, ambaye alinena juu ya mambo haya, ambayo bado hayajatokea bali kwa hakika ni lazima, kama vile Mimi niishivyo, kwani machukizo hayawezi kutawala.
22 Na tena, amini, amini, ninawaambia kwamba na hiyo miaka elfu itakapokwisha, na wanadamu wakianza tena kumkataa Mungu wao, ndipo nitakapouachia ulimwengu lakini kwa muda mchache;
23 Na mwisho utakapokuja, na mbingu na dunia zitaangamizwa na kupita, na hapo patakuwa na mbingu mpya na dunia mpya.
24 Na ya kale yote yatapita, na yote yatakuwa mapya, hata mbingu na dunia, na vyote vilivyomo, watu na wanyama, ndege wa angani, na samaki wa baharini;
25 Na hapana hata unywele mmoja, wala chembe moja, itakayopotea, kwani hiyo ni kazi ya mikono yangu.
26 Lakini, tazama, amini ninawaambia, kabla dunia haijapita, Mikaeli, malaika wangu mkuu, atapiga parapanda yake, na ndipo wafu wote wataamka, kwani makaburi yao yatafunguka, nao watatoka—ndiyo, hata wote.
27 Na wenye haki watakusanywa mkono wangu wa kuume kwa uzima wa milele; na waovu mkono wangu wa kushoto ndiyo ambao nitaona aibu kuwamiliki mbele za Baba;
28 Kwa hiyo nitawaambia—Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto usio na mwisho, aliowekewa tayari ibilisi na malaika zake,
29 Na sasa, tazama, ninawaambia, kamwe wakati wowote sijawahi kueleza kutoka kinywani mwangu kwamba watarejea, kwani mahali nilipo hawawezi kufika, kwani hawana uwezo huo.
30 Lakini kumbukeni kwamba hukumu zangu zote hazijatolewa kwa wanadamu; na kama vile maneno yalivyotoka kinywani mwangu hivyo alivyo yatakayotimia, kwamba wa kwanza atakuwa wa mwisho na wa mwisho atakuwa wa kwanza katika mambo yote niliyoyaumba kwa amri ya uwezo wangu, ambao ni nguvu ya Roho wangu.
31 Kwani kwa nguvu ya Roho wangu niliviumba; ndiyo, vitu vyote vya kiroho na kimwili—
32 Kwanza kiroho, pili kimwili, ambao ndiyo mwanzo wa kazi yangu; na tena, kwanza kimwili, na pili kiroho, ambao ndiyo mwisho wa kazi yangu—
33 Nikizungumza nanyi ili mpate kuelewa kwa namna ya kawaida; lakini kwangu mimi mwenyewe kazi zangu hazina mwisho, wala mwanzo; lakini imetolewa kwenu ili mpate kuelewa, kwa sababu mmeniomba na kukubaliwa.
34 Kwa hiyo, amini ninawaambia kwamba mambo haya yote kwangu mimi ni ya kiroho, na hata wakati wowote sijatoa sheria kwenu ambayo ni ya kimwili; wala mtu yeyote, wala wanadamu; wala si Adamu, baba yenu, ambaye nilimuumba.
35 Tazama, nilimpa yeye ili apate kujiamulia mwenyewe; na nikampa amri, lakini siyo amri ya kimwili nilimpa yeye, kwani amri zangu ni za kiroho; siyo za kiasili wala kimwili, si tamaa ya kimwili wala si ya kianasa.
36 Na ikawa kwamba Adamu, akijaribiwa na ibilisi—kwani, tazama, ibilisi alikuwako kabla ya Adamu, kwani yeye aliniasi mimi, akisema, Nipe mimi heshima yako, ambayo ndiyo uwezo wangu; na pia theluthi moja ya majeshi ya mbinguni aliyafanya yanigeuke kwa sababu ya haki yao ya kujiamulia;
37 Na wakatupwa chini, na hivyo ndivyo kuja kwa ibilisi na malaika zake;
38 Na, tazama, kuna mahali palipotayarishwa kwa ajili yao kutoka mwanzo, mahali hapo ni jehanamu.
39 Na hapana budi kwamba ibilisi lazima awajaribu wanadamu, vinginevyo hawangeweza kujiamulia wao wenyewe; kwani kama kamwe hawakuonja uchungu wasingeliweza kuijua utamu—
40 Kwa hiyo ikawa kwamba ibilisi akamjaribu Adamu, na yeye akala tunda lililokatazwa, na akaivunja amri, hivyo basi akajiingiza chini ya matakwa ya ibilisi, kwa sababu alikubali majaribu.
41 Kwa hiyo, Mimi, Bwana Mungu, nikamfukuza kutoka katika Bustani ya Edeni, kutoka machoni pangu, kwa sababu ya uvunjaji wake wa sheria, kwa ajili hiyo akawa mfu kiroho, ambacho ni kifo cha kwanza, ambacho ni sawa sawa na kifo cha mwisho, ambacho ni cha kiroho, ambacho kitahukumiwa kwao walio waovu nitakaposema: Ondokeni, ninyi mliolaaniwa.
42 Lakini, tazama, ninawaambia kwamba Mimi, Bwana Mungu, nilitoa kwa Adamu na uzao wake, kwamba wasife kwa kifo cha kimwili, hadi Mimi, Bwana Mungu, nitakapowatuma malaika kutangaza kwao toba na ukombozi, kwa njia ya imani juu ya jina la Mwana Pekee.
43 Na hivyo ndivyo nilivyofanya Mimi, Bwana Mungu, kumteua mtu kama siku zake za majaribio—kwamba kwa kifo chake cha kimwili aweza kuinuliwa katika mwili usiokufa hadi uzima wa milele, hata wengi kadiri watakavyoamini;
44 Na wale wasioamini juu ya laana ya milele; kwani hawawezi kukombolewa kutokana na anguko lao la kiroho, kwa sababu hawatubu;
45 Kwani wao hupenda zaidi giza kuliko nuru, na matendo yao ni maovu, na wao hupokea ujira wao kwa yeye wanayemtii.
46 Lakini tazama, ninawaambia, kuwa watoto wadogo wamekombolewa tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu kwa njia ya Mwanangu wa Pekee;
47 Kwa hiyo hawafanyi dhambi, kwani uwezo haujatolewa kwa Shetani wa kuwajaribu watoto wadogo, hadi wanapoanza kuwajibika mbele zangu;
48 Kwani imetolewa kwao hata kama vile nitakavyo Mimi, kulingana na mapenzi yangu, ili kwamba mambo muhimu yaweze kuhitajika kutoka kwenye mikono ya baba zao.
49 Na, tena, ninawaambia, kwamba yeyote aliye na maarifa, sijamuamuru kutubu?
50 Na yeye ambaye hana ufahamu, hubaki ndani yangu kufanya kama ilivyoandikwa. Na sasa sitasema zaidi kwenu kwa wakati huu. Amina.