Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 63


Sehemu ya 63

Ufunuo uliotolewa kupitia Joseph Smith Nabii, huko Kirtland, Ohio, mwishoni mwa 30 Agosti 1831. Nabii, Sidney Rigdon, na Oliver Cowdery waliwasili Kirtland 27 Agosti kutoka safari yao ya Missouri. Historia ya Joseph Smith inauelezea ufunuo huu: “Katika siku hizi za uchanga wa Kanisa, palikuwa na shauku kubwa ya kupata neno la Bwana juu ya kila jambo ambalo kwa namna yoyote ile lililohusu wokovu wetu; na kwa vile nchi ya Sayuni ilikuwa ndicho kitu kilicho kuwa cha maana zaidi usoni, nilimwomba Bwana taarifa zaidi juu ya kukusanyika kwa Watakatifu, na ya ununuzi wa ardhi, na mambo mengineyo.”

1–6, Siku ya ghadhabu itafika juu ya waovu; 7–12, Ishara huja kwa imani; 13–19, Afanyaye uzinzi moyoni ataikana imani na atatupwa katika ziwa la moto; 20, Wale walio waaminifu watapokea wokovu juu ya dunia iliyobadilishwa; 21, Habari kamili ya matukio juu ya Mlima wa Kugeuka Sura bado hayajafunuliwa; 22–23, Watiifu hupokea siri za ufalme; 24–31, Urithi katika Sayuni utanunuliwa; 32–35, Bwana hutangaza vita, na waovu huwaua waovu; 36–48, Watakatifu watakusanyika Sayuni na watatoa fedha za kuijenga; 49–54, Waaminifu wamehakikishiwa baraka katika Ujio wa Pili, katika Ufufuko, na wakati wa Milenia; 55–58, Hii ni siku ya onyo; 59–66, Jina la Bwana latajwa bure na wale ambao hulitumia bila mamlaka.

1 Sikilizeni, Enyi watu, na funueni mioyo yenu na tegeni sikio kutoka mbali, na sikieni, ninyi mjiitao watu wa Bwana, na lisikizeni neno la Bwana na mapenzi yake juu yenu.

2 Ndiyo, amini, nawaambia, sikizeni neno lake yeye ambaye hasira yake inawaka dhidi ya waovu na waasi;

3 Yeye apendaye kuwachukuwa hata wale atakao kuwachukua, na kuwabakisha katika uhai wale apendao kuwabakisha;

4 Yeye ajengaye kwa mapenzi na ridhaa yake; na huharibu wakati atakao, na anaweza akaitupa nafsi jehanamu.

5 Tazama, Mimi, Bwana, naitoa sauti yangu, na mtaitii.

6 Kwa hiyo, amini ninasema, acha waovu wasikie, na waasi waogope na kutetemeka; acha wasioamini wafunge midomo yao, kwani siku ya ghadhabu itawafikia kama tufani, na wote wenye mwili watajua kuwa Mimi ndimi Mungu.

7 Na yule atafutaye ishara ataziona ishara, lakini siyo kwa wokovu.

8 Amini, ninawaambia, kuna watu miongoni mwenu ambao wanatafuta ishara, na wamekuwepo wa aina hiyo hata tangu mwanzo;

9 Lakini, tazama, imani haiji kwa ishara, bali ishara huwafuata wote wenye kuamini.

10 Ndiyo, ishara huja kwa imani, siyo kwa matakwa ya wanadamu, wala siyo kama wapendavyo, bali kwa mapenzi ya Mungu.

11 Ndiyo, ishara huja kwa imani, kwa matendo makuu, kwani pasipo imani hakuna mwanadamu awezaye kumpendeza Mungu; na kwa yule ambaye Mungu amemkasirikia hapendezwi naye; kwa hivyo, kwa watu wa aina hiyo haonyeshi ishara, isipokuwa katika ghadhabu kwa maangamizo yao.

12 Kwa hiyo, Mimi, Bwana, sijapendezwa na wale miongoni mwenu ambao walitafuta ishara na maajabu kwa ajili ya imani, na siyo kwa faida ya wanadamu kwa utukufu wangu.

13 Hata hivyo, nimetoa amri, na wengi wamegeuka kutoka kwenye amri zangu na hawakuzishika.

14 Palikuwa na wazinzi miongoni mwenu; baadhi yao wamegeuka, na wengine wamebaki pamoja nanyi, ambao baada ya hapa watajulikana.

15 Wa aina hiyo wajihadhari na watubu upesi, hukumu isije ikawajia kama mtego, na upumbavu wao utafanywa dhahiri, na kazi za mikono yao zitawafuata machoni pa watu.

16 Na amini ninawaaambia, kama nilivyosema hapo awali, mtu amtazamaye mwanamke kwa kumtamani, au kama wale watakaofanya uzinzi mioyoni mwao, hawatakuwa na Roho, bali wataikana imani na wataogopa.

17 Kwa hiyo, Mimi, Bwana, nimesema kuwa waoga, na wasioamini, na waongo wote, na yeyote apendaye uongo na kuufanya, na wazinzi, na wachawi, watakuwa na sehemu yao katika ziwa lile liwakalo moto na kiberiti ambacho ni kifo cha pili.

18 Amini ninasena, kwamba hawatakuwa na sehemu katika ufufuko wa kwanza.

19 Na sasa tazama, Mimi, Bwana, ninawaambia kwamba hamjahesabiwa haki, kwani mambo haya yapo miongoni mwenu.

20 Hata hivyo, yule astahimiliye katika imani na kutimiza mapenzi yangu, huyo atashinda, na kupokea urithi juu ya dunia wakati siku ya kugeuka sura itakapofika;

21 Wakati dunia itakapogeuzwa sura, hata sawasawa na utaratibu ulioonyeshwa kwa mitume wangu juu ya mlima; habari ambazo utimilifu wake hamjapokea.

22 Na sasa, amini ninawaambia, kama nilivyosema kuwa nitawajulisha matakwa yangu, tazama nitawajulisha, siyo kwa njia ya amri, kwa kuwa wapo wengi wasiojali kuzishika amri zangu.

23 Lakini kwake yeye ashikaye amri zangu nitampa siri za ufalme wangu, na ndani yake patakuwa na chemchemi ya maji ya uzima, yakibubujikia kwenye uzima usio na mwisho.

24 Na sasa, tazama, haya ndiyo mapenzi ya Bwana Mungu wenu kuhusu watakatifu wake, kwamba wanapaswa kujikusanya pamoja katika nchi ya Sayuni, siyo katika haraka, pasije kuwa na mchafuko, uletao mateso.

25 Tazama, nchi ya Sayuni—Mimi, Bwana, ninaishika katika mikono yangu;

26 Hata hivyo, Mimi, Bwana, hutoa kwa Kaisari vitu vilivyo vya Kaisari.

27 Kwa hivyo, Mimi, Bwana, ninataka kuwa mnunue ardhi, ili muweze kuyashinda ya ulimwengu, ili muweze kuwa na haki kwa walimwengu, ili wasichochewe kwa hasira.

28 Kwani Shetani huiweka katika mioyo yao ili wakasirike dhidi yenu, kiasi cha umwagaji damu.

29 Kwa hivyo, nchi ya Sayuni haitapatikana ila kwa kununua au kwa damu, vinginevyo hakuna urithi wowote kwa ajili yenu.

30 Na kama ni kwa kununua, tazama mmebarikiwa;

31 Na kama ni kwa damu, ninyi mmezuiliwa kumwaga damu, lo, adui zenu wapo juu yenu, na mtafukuzwa kutoka mji hadi mji, na kutoka sinagogi hadi sinagogi, na ni wachache tu watakaosimama na kupokea urithi.

32 Mimi, Bwana, ninakasirishwa na waovu; ninaizuia Roho yangu kwa wakazi wa dunia.

33 Nimeapa katika ghadhabu yangu, na kutangaza vita juu ya uso wa dunia, na waovu watachinja waovu, na woga utakuja juu ya kila mwanadamu;

34 Na watakatifu pia kwa shida wataepuka; hata hivyo, Mimi, Bwana, niko pamoja nao, nami nitashuka kutoka mbinguni kwenye uwepo wa Baba yangu na kuwaangamiza waovu kwa moto usiozimika.

35 Na tazama, hili bado, lakini li karibu.

36 Kwa hiyo, kwa kuona hivyo, Mimi, Bwana, nikatangaza mambo haya yote juu ya uso wa dunia, ninataka kwamba watakatifu wangu wakusanyike katika nchi ya Sayuni;

37 Na kwamba kila mtu ajichukulie haki katika mikono yake na uaminifu viunoni mwake, na kupaza sauti ya kuonya kwa wakazi wa dunia; na kutangaza kwa maneno na kwa kukimbia kwamba ukiwa utawapata waovu.

38 Kwa hiyo, na wanafunzi wangu katika Kirtland wapange mambo yao ya maisha, wale waishio kwenye shamba hili.

39 Na mtumishi wangu Titus Billings, ambaye ni msimamizi wake, aitoe ardhi, ili aweze kujiandaa katika majira ya kuchipua yajayo kwa kuanza safari yake kuja katika nchi ya Sayuni, pamoja na wale wakaao hapo, isipokuwa wale nitakaowabakisha kwa makusudi yangu, ambao hawatakwenda hadi nitakapowaamuru.

40 Na fedha zote zinazoweza kutunzwa, wala sitajali kama zitakuwa nyingi au kidogo zipelekwe katika nchi ya Sayuni, kwao wale niliowateua kuzipokea.

41 Tazama, Mimi, Bwana, nitatoa kwa mtumishi wangu Joseph Smith, Mdogo, uwezo ambao utamwezesha kutambua kwa uwezo wa Roho wale watakaokwenda katika nchi ya Sayuni, na wale wanafunzi wangu ambao watabaki.

42 Na mtumishi wangu Newel K. Knight abaki na stoo yake, au kwa maneno mengine, duka, kwa muda mfupi ujao.

43 Hata hivyo, naye atoe fedha zote ambazo anaweza kutoa, ili zipelekwe katika nchi ya Sayuni.

44 Tazama, mambo haya yapo mikononi mwake mwenyewe, na afanye kulingana na hekima.

45 Amini ninawaambia, na atawazwe kama wakala kwa wanafunzi wangu wale watakaobaki na atawazwe katika uwezo huu;

46 Na sasa upesi ukayatembelee makanisa, ukayaelezea mambo haya kwao, pamoja na mtumishi wangu Oliver Cowdery. Tazama, hilo ndilo penzi langu, kupata fedha hata kama vile nilivyoelezea.

47 Yule aliye mwaminifu na mwenye kustahimili ataushinda ulimwengu.

48 Yule ambaye hupeleka hazina katika nchi ya Sayuni atapokea urithi katika ulimwengu huu, na matendo yake yatamfuata, na pia thawabu katika ulimwengu ujao.

49 Ndiyo, na heri wafu wafao katika Bwana, tangu sasa, wakati Bwana atakapokuja, na mambo ya zamani yatapita, na mambo yote yamekuwa mapya, watafufuka kutoka kwa wafu na hawatakufa tena, na watapokea urithi mbele za Bwana, katika mji mtakatifu.

50 Na yule atakayekuwa hai wakati Bwana atakapokuja, na akiwa ameishika imani, amebarikiwa; hata hivyo, imepangwa kwake kufa katika umri wa mwanadamu.

51 Kwa hiyo, watoto watakua hadi wamekuwa wazee; na wazee watakufa, bali hawatalala katika mavumbi, bali watageuzwa katika muda wa kufumba na kufumbua jicho.

52 Kwa hiyo, kwa sababu hii mitume walihubiri kwa walimwengu juu ya ufufuko wa wafu.

53 Mambo hayo ni mambo ambayo ni lazima myatazamie; na, nikisema kulingana na njia ya Bwana, sasa yapo karibu, na katika wakati ujao, hata katika siku ya kuja kwa Mwana wa Mtu.

54 Na hadi saa hiyo patakuwa na wanawali wajinga miongoni mwa wenye hekima; na katika saa hiyo waja utengano mkamilifu wa wenye haki na waovu; na katika siku hiyo nitawatuma malaika wangu kuwaondoa waovu na kuwatupa katika moto usiozimika.

55 Na sasa tazama, amini ninawaambia, Mimi, Bwana, sijapendezwa na mtumishi wangu Sidney Rigdon; amejiinua mwenyewe moyoni mwake, na hakupokea ushauri, bali amemhuzunisha Roho;

56 Kwa hiyo maandishi yake hayakubaliki kwa Bwana, na atafanya mengine; na ikiwa Bwana hatayapokea, tazama yeye hatasimama katika ofisi ambayo nimemteua.

57 Na tena, amini ninawaambia, wale watamanio katika mioyo yao, kwa unyenyekevu, kuwaonya wenye dhambi ili watubu, na watawazwe katika uwezo huo.

58 Kwani hii ni siku ya kuonya, na siyo siku ya maneno mengi. Kwani Mimi, Bwana siyo wa kudhihakiwa katika siku ya mwisho.

59 Tazama, Mimi ni wa juu, na uwezo wangu uko hata chini yake. Mimi ni juu ya vyote, na katika yote, na ndani ya yote na yatafuteni mambo yote, na siku yaja ambayo mambo yote yatafanywa kuwa chini yangu.

60 Tazama, Mimi ni Alfa na Omega, hata Yesu Kristo.

61 Kwa hiyo, na watu wote wajihadhari namna walichukuavyo jina langu katika midomo yao—

62 Kwani tazama, amini ninasema, kuwa wapo wengi chini ya hatia hii, ambao hulitaja jina la Bwana, na hulitaja bure, bila mamlaka.

63 Kwa hiyo, na kanisa litubu dhambi zake, na Mimi, Bwana, nitawamiliki; vinginevyo, watakatiliwa mbali.

64 Kumbukeni kwamba kile ambacho huja kutoka juu ni kitakatifu, na ni lazima kitamkwe kwa uangalifu, na kwa ridhaa ya Roho; na katika hili hakuna hatia, nanyi mnampokea Roho kwa njia ya sala; kwa hiyo, bila hivyo hubakia hatia.

65 Na watumishi wangu, Joseph Smith, Mdogo, na Sidney Rigdon, wajitafutie nyumba, kama watakavyofundishwa na Roho kwa njia ya sala.

66 Mambo haya mtayashinda kwa njia ya uvumilivu, ili watakaoshinda waweze kupokea utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi sana, vinginevyo, hukumu kuu. Amina.