Sehemu ya 133
Ufunuo uliotolewa kupitia Joseph Smith Nabii, huko Hiram, Ohio, 3 Novemba 1831. Akiandika dibaji ya ufunuo huu Historia ya Joseph Smith inasema, “Kwa wakati huu palikuwa na mambo mengi ambayo Wazee walitaka kujua kuhusiana na kuhubiriwa kwa Injili kwa wakazi wa dunia, na juu ya kukusanyika; na ili kuenenda katika nuru ya kweli, na kufundishwa kutoka juu, mnamo 3 Novemba 1831, mimi nilimwomba Bwana na kupokea ufunuo muhimu ufuatao.” Sehemu hii kwanza iliongezwa kwenye kitabu cha Mafundisho na Maagano kama kiambatisho, na mwishowe ikapewa namba kama sehemu.
1–6, Watakatifu wanaamriwa kujitayarisha kwa ajili ya Ujio wa Pili; 7–16, Watu wote wanaamriwa kuikimbia Babilonia, na kuja Sayuni, na kujiandaa kwa ajili ya siku ile iliyo kuu ya Bwana; 17–35, Yeye atasimama juu ya Mlima Sayuni, mabara yatakuwa nchi moja, na makabila yaliyopotea ya Israeli yatarudi; 36–40, Injili ilirejeshwa kupitia Joseph Smith ili kuhubiriwa katika ulimwengu wote; 41–51, Bwana atashuka kulipiza kisasi kwa waovu; 52–56, Utakuwa mwaka wa wakombolewa Wake; 57–74, Injili itapelekwa ili kuwaokoa Watakatifu na kwa ajili ya angamizo la waovu.
1 Sikilizeni, Enyi watu wa kanisa langu, asema Bwana Mungu wenu, na sikieni neno la Bwana juu yenu—
2 Bwana ambaye atakuja ghafla katika hekalu lake; Bwana ambaye atashuka juu ya ulimwengu wa laana ili kuhukumu; ndiyo, juu ya mataifa yote yenye kumsahau Mungu, na juu ya wote wasio cha Mungu walio miongoni mwenu.
3 Kwani atauweka wazi mkono wake mtakatifu machoni pa mataifa yote, na miisho yote ya dunia yatauona wokovu wa Mungu wao.
4 Kwa hiyo jitengenezeeni, jitengenezeeni, Enyi watu wangu; jitakaseni ninyi wenyewe; kusanyikeni pamoja, Enyi watu wa kanisa langu, juu ya nchi ya Sayuni, ninyi nyote ambao hamkuamriwa kukaa.
5 Tokeni katika Babilonia. Kuweni safi ninyi mnaochukua vyombo vya Bwana.
6 Kuweni na makusanyiko yenu ya kiroho, na msemezane ninyi kwa ninyi mara kwa mara. Na acheni kila mtu alilingane jina la Bwana.
7 Ndiyo, amini ninawaambia tena, wakati umewadia ambapo sauti ya Bwana ipo kwenu ninyi: Tokeni Babilonia; jikusanyeni kutoka miongoni mwa mataifa, kutoka pepo nne, kutoka kona moja ya mbingu hadi nyingine.
8 Wapelekeni wazee wa kanisa langu kwa mataifa yaliyo mbali; kwenye visiwa vya bahari; wapelekeni kwenye nchi za kigeni; yasihini mataifa yote, kwanza juu ya Wayunani, na halafu juu ya Wayahudi.
9 Na tazama, na lo, hiki kitakuwa kilio chao, na sauti ya Bwana kwa watu wote: Enendeni nchi ya Sayuni, ili mipaka ya watu wangu ipate kupanuka, na ili vigingi vyake vipate kuimarishwa, na ili Sayuni ipate kuenea hata maeneo yaliyo karibu.
10 Ndiyo, acheni kilio kiendelee miongoni mwa watu wote: Amkeni na simameni na kwenda kumlaki Bwana harusi; tazama na lo, Bwana harusi yu aja; tokeni mwende kumlaki. Jiwekeni tayari kwa ajili ya siku ile iliyo kuu ya Bwana.
11 Kesheni, kwa sababu hamjui siku wala saa.
12 Kwa hiyo, waacheni wao, walio miongoni mwa Wayunani wakimbilie Sayuni.
13 Na acha walio wa Yuda wakimbilie Yerusalemu, katika milima ya nyumba ya Bwana.
14 Tokeni miongoni mwa mataifa, hata kutoka Babilonia, kutoka katikati ya uovu, ambao ni Babeli ya kiroho.
15 Lakini amini, hivyo ndivyo asemavyo Bwana, acheni kukimbia kwenu kusiwe katika haraka, bali mambo yote yatengenezwe mbele yenu; na yule aendaye, na asiangalie nyuma lisije angamizo la ghafla likaja juu yake.
16 Sikilizeni na msikie, Enyi wakazi wa dunia. Sikieni kwa pamoja, ninyi wazee wa kanisa langu, na msikie sauti ya Bwana; kwani awaita watu wote, naye huwaamuru watu wote kila mahali kutubu.
17 Kwani tazama, Bwana Mungu amemtuma malaika akilia katikati ya mbingu, akisema: Itengenezeni njia ya Bwana, na yanyoosheni mapito yake, kwani saa ya kuja kwake imekaribia—
18 Wakati Mwanakondoo atakaposimama juu ya Mlima Sayuni, na pamoja naye watu mia arobaini na nne elfu, wenye jina la Baba yake limeandikwa katika vipaji vya nyuso zao.
19 Kwa hiyo, jitayarisheni kwa ajili ya ujio wa Bwana harusi; nendeni, nendeni nje kumlaki.
20 Kwani tazama, atasimama juu ya mlima wa Mizeituni, na juu ya bahari kuu, hata vilindi vikuu, na juu ya visiwa vya bahari, na juu ya nchi ya Sayuni.
21 Naye atatoa sauti yake toka Sayuni, naye atasema kutoka Yerusalemu, na sauti yake itasikika miongoni mwa watu wote;
22 Na itakuwa kama sauti ya maji mengi, na kama sauti ya radi kuu, ambayo itaivunja milima, na mabonde hayataonekana.
23 Ataviamuru vilindi vikuu, navyo vitasukumwa kurudi katika nchi za kaskazini, na visiwa vitakuwa nchi moja;
24 Na nchi ya Yerusalemu na nchi ya Sayuni zitarudishwa katika mahali pao, na dunia itakuwa kama ilivyokuwa katika siku zile kabla ya kugawanyika.
25 Na Bwana, hata Mwokozi, atasimama katikati ya watu wake, naye atatawala juu ya wote wenye mwili.
26 Nao walioko katika nchi za kaskazini watakumbukwa mbele za Bwana; na manabii wao wataisikia sauti yake, nao hawataweza tena kujizuia; nao wataipiga miamba, na barafu itatiririka mbele ya uwepo wao.
27 Na njia kuu itainuliwa katikati ya vilindi vikuu.
28 Maadui zao watakuwa mawindo kwao,
29 Na katika jangwa kame yatajitokeza mabwawa ya maji ya uzima; na ardhi kavu haitakuwa tena nchi yenye kiu.
30 Nao wataleta hazina za utajiri wao kwa watoto wa Efraimu, mtumishi wangu.
31 Na mipaka ya vilima isiyo na mwisho itatetemeka mbele ya uwepo wao.
32 Na hapo wataanguka chini na kuvikwa taji la utukufu, hata katika Sayuni, kwa mikono ya watumishi wa Bwana, hata watoto wa Efraimu.
33 Nao watajawa na nyimbo za shangwe isiyo na mwisho.
34 Tazama, hii ndiyo baraka ya Mungu asiye na mwisho juu ya makabila ya Israeli, na baraka iliyo kuu juu ya kichwa cha Efraimu na wenzake.
35 Na wao pia wa kabila la Yuda, baada ya machungu yao watatakaswa katika utakatifu mbele za Bwana, ili kukaa mbele za uwepo wake mchana na usiku, milele na milele.
36 Na sasa, amini hivi ndivyo asema Bwana, ili mambo haya yapate kujulikana miongoni mwenu, Enyi wakazi wa dunia, nimemtuma malaika wangu akiruka katikati ya mbingu, mwenye injili isiyo na mwisho, ambaye amewatokea baadhi na kuikabidhi kwa mwanadamu, ambaye ataonekana kwa wengi wale wakaao duniani.
37 Na injili hii itahubiriwa kwa kila taifa, na kabila, na lugha, na watu.
38 Na watumishi wa Mungu watakwenda, wakisema kwa sauti kubwa: Mcheni Mungu na mtukuzeni yeye, kwa maana saa ya hukumu yake imefika;
39 Na mwabuduni yeye aliyezifanya mbingu, na dunia, na bahari, na chemi chemi za maji—
40 Mkililingana jina la Bwana mchana na usiku, mkisema: Ee laiti ungepasua mbingu, ili ushuke ili milima ipate kutiririka mbele zako.
41 Na itajibiwa juu ya vichwa vyao; kwa maana uwepo wa Bwana utakuwa kama moto wenye kuyeyuka unaowaka uunguzao, na kama moto ufanyao maji kuchemka.
42 Ee Bwana, utashuka chini ili kuwajulisha adui zako jina lako, na mataifa yote yatatetemeke mbele zako—
43 Unapofanya mambo ya kutisha, mambo wasiyoyatazamia;
44 Ndiyo, ushukapo, na milima kutiririka mbele zako, wewe wamlaki yeye afurahiaye yaliyo ya haki na kuyatenda, wale wakukumbukao katika njia zako.
45 Maana tangu mwanzo wa ulimwengu watu hawakusikia wala kufahamu kwa masikio, wala jicho lolote halikuona, Ee Mungu, zaidi yako wewe, ni mambo gani makuu uliyoyaandaa kwa ajili yake yeye akungojae wewe.
46 Na itasemwa: Ni nani yule ashukaye kutoka kwa Mungu mbinguni mwenye mavazi yaliyotiwa rangi; ndiyo, kutoka sehemu zisizojulikana, aliyevikwa katika mavazi yake matukufu, akitembea katika ukuu wa nguvu zake?
47 Naye atasema: Mimi ndiye niliyenena katika haki, mwenye nguvu ya kuokoa.
48 Naye Bwana atakuwa mwekundu katika mavazi yake, na nguo zake kama za yule akanyagaye katika pipa la mvinyo.
49 Na uwepo wake utakuwa na utukufu mkubwa kiasi kwamba jua litauficha uso wake kwa aibu, na mwezi itaizuia nuru yake, nazo nyota zitaondoshwa kutoka mahali pake.
50 Na sauti yake itasikika: Nalikanyaga shinikizo la mvinyo pekee yangu, na nimeileta hukumu juu ya watu wote; na hakuna hata mmoja aliyekuwa pamoja nami;
51 Na nimewavyoga katika ghadhabu yangu, na nikawakanyaga katika hasira yangu, na damu yao nikainyunyizia kwenye mavazi yangu, nayo imeharibu vazi langu lote; kwani hii ilikuwa siku ya kulipa kisasi kilichokuwa moyoni mwangu.
52 Na sasa mwaka wa waliokombolewa wangu umefika; nao watataja ukarimu wa Bwana wao, na yote ambayo ameyaweka juu yao kulingana na wema wake, na kulingana na ukarimu wake, milele na milele.
53 Katika mateso yao yote yeye aliteswa. Na malaika wa uwepo wake akawaokoa; na katika upendo wake, na katika huruma yake, akawakomboa, na aliwasaidia, na kuwabeba siku zote za kale;
54 Ndiyo, na Henoko pia, na wale waliokuwa pamoja naye; manabii waliokuwa kabla yake; na Nuhu pia, na wale waliokuwa kabla yake; na Musa pia, na wale waliokuwa kabla yake;
55 Na tangu Musa hadi Eliya, na tangu Eliya hadi Yohana, waliokuwa pamoja na Kristo katika ufufuko wake, na mitume watakatifu, pamoja na Ibrahimu, Isaka, na Yakobo, watakuwa katika uwepo wa Mwanakondoo.
56 Na makaburi ya watakatifu yatafunguliwa; nao wataamka na kusimama mkono wa kuume wa Mwanakondoo, wakati atakaposimama juu ya Mlima Sayuni, na juu ya mji mtakatifu, Yerusalemu Mpya; nao wataimba wimbo wa Mwanakondoo, mchana na usiku milele na milele.
57 Na kwa sababu hii, ili wanadamu wapate kufanywa washiriki wa utukufu ambao utafunuliwa, Bwana aliupeleka utimilifu wa injili yake, agano lake lisilo na mwisho, wakisemezana kwa uwazi na urahisi—
58 Kuwaandaa walio dhaifu kwa ajili ya mambo yale yajayo duniani, na kwa ajili ya kazi ya Bwana katika siku ile walio wapumbavu watakapo washinda wenye hekima, na mnyonge atakapokuwa taifa hodari, na wawili watawafanya makumi elfu wao kuwakimbia.
59 Na kwa walio wadhaifu wa dunia Bwana atayapura mataifa kwa uwezo wa Roho wake.
60 Na ni kwa ajili hii amri hizi zilitolewa; ziliamriwa kuzuiliwa kuja ulimwenguni katika siku ile zilipotolewa, lakini sasa ziende kwa wote wenye mwili—
61 Na hii ni kulingana na nia na mapenzi ya Bwana, atawalaye juu ya wenye mwili wote.
62 Na kwake yeye atubuye na kujitakasa mwenyewe mbele za Bwana atapewa uzima wa milele.
63 Na juu yao wale wasiosikiliza sauti ya Bwana litatimizwa lile lililoandikwa na nabii Musa, kwamba watakatiliwa mbali kutoka miongoni mwa watu.
64 Na pia lile lililoandikwa na nabii Malaki: Kwa maana, tazameni, siku ile inakuja itakayowaka kama tanuri, na wote wenye kiburi, ndiyo, nao wote watendao uovu, watakuwa makapi; na siku ile inayokuja itawateketeza, asema Bwana wa majeshi, hata haitawaachia mzizi wala tawi.
65 Kwa hiyo, hili ndilo litakuwa jibu la Bwana kwao:
66 Katika siku ile nilipokuja kwa walio wangu, hakuna mtu miongoni mwenu aliyenipokea, nanyi mlifukuzwa.
67 Nilipoita tena hapakuwa na yeyote kati yenu wa kunijibu; lakini mkono wangu haukuwa mfupi kwa namna yoyote kwamba nisiweze kukomboa, wala uwezo wangu wa kukomboa.
68 Tazama, kwa kemeo langu ninaikausha bahari. Naifanya mito kuwa jangwa; samaki wao kunuka, na kufa kwa kiu.
69 Nazivika mbingu kwa weusi, nafanya nguo ya gunia kuwa mavazi yake.
70 Na hili mtalipata kutoka mikononi mwangu—mtalala chini kwa huzuni.
71 Tazama, na lo, hakuna wa kuwakomboa ninyi; kwa kuwa hamkutii sauti yangu wakati nilipokuiteni kutoka mbinguni; hamkuwaamini watumishi wangu, na walipoletwa kwenu hamkuwapokea.
72 Kwa hiyo, waliutia muhuri ushuhuda na kuifunga sheria, nanyi mkaachwa gizani.
73 Hawa watakwenda katika giza la nje, ambako kuna kilio, na kuomboleza, na kusaga meno.
74 Tazama Bwana Mungu wenu amenena hilo. Amina.