Sehemu ya 109
Sala iliyotolewa wakati wa kuwekwa wakfu kwa hekalu huko Kirtland, Ohio, 27Â Machi 1836. Kulingana na maelezo yaliyoandikwa na Nabii, sala hii ilitolewa kwake kwa ufunuo.
1–5, Hekalu la Kirtland lilijengwa kama mahali ambapo Mwana wa Mtu atatembelea; 6–21, Itakuwa ni nyumba ya sala, kufunga, imani, kujifunza, utukufu, na utaratibu, na nyumba ya Mungu; 22–33, Na wasiotubu na ambao huwapiga watu wa Bwana nawashindwe; 34–42, Na Watakatifu waendelee katika uwezo kuwakusanya wenye haki katika Sayuni; 43–53, Na Watakatifu waokolewe kutokana na mambo mabaya yatakayomiminwa juu ya waovu katika siku za mwisho; 54–58, Na mataifa na watu na makanisa yatayarishwe kwa ajili ya injili; 59–67, Na Wayahudi, na Walamani, na Waisraeli wote wakombolewe; 68–80, Na Watakatifu wavikwe taji la utukufu na heshima, na wapate wokovu wa milele.
1 Shukrani ziwe kwa jina lako, Ee Bwana Mungu wa Israeli, mwenye kuyashika maagano na kuonyesha rehema kwa watumishi wako watembeao wima mbele zako, kwa moyo wao wote—
2 Wewe uliyewaamuru watumishi wako kuijenga nyumba kwa jina lako katika mahali hapa [Kirtland].
3 Na sasa nawe waona, Ee Bwana, kwamba watumishi wako wamefanya kulingana na amri yako.
4 Na sasa twakuomba, Baba Mtakatifu, katika jina la Yesu Kristo, Mwana aliye kifuani mwako, ambaye katika jina lake pekee wokovu waweza kuhudumiwa kwa wanadamu, twakuomba, Ee Bwana, uikubali nyumba hii, kazi ya ustadi wa mikono yetu sisi, watumishi wako, ambao ulituamuru kuijenga.
5 Kwani wewe wajua kwamba tumeifanya kazi hii katika taabu kuu; na kutoka katika ufukara wetu tumetoa tulichokuwa nacho ili kuijenga nyumba kwa jina lako, ili Mwana wa Mtu apate mahali pa kujionyesha mwenyewe kwa watu wake.
6 Na kama ulivyosema katika ufunuo, uliotolewa kwetu sisi, ukituita marafiki zako, ukisema—Fanyeni kusanyiko lenu la kiroho, kama nilivyowaamuru;
7 Na kwa vile wote hawana imani, tafuteni kwa bidii na kufundishana maneno ya hekima; ndiyo, tafuteni kutoka kwenye vitabu vizuri maneno ya hekima, tafuteni maarifa hata kwa kujifunza na pia kwa imani;
8 Jipangeni wenyewe; tayarisheni kila kitu kilicho muhimu, na jengeni nyumba, hata nyumba ya sala, nyumba ya mfungo, nyumba ya imani, nyumba ya mafundisho, nyumba ya utukufu, nyumba ya utaratibu, nyumba ya Mungu;
9 Kwamba kuingia kwenu kupate kuwa katika jina la Bwana, kwamba kutoka kwenu kupate kuwa katika jina la Bwana, kwamba maamkizi yenu yote yapate kuwa katika jina la Bwana, mkiinua mikono kwake yeye Aliye Juu Sana—
10 Na sasa, Baba Mtakatifu, twakuomba utusaidie sisi, watu wako, kwa neema yako, kwa kuita kusanyiko letu la kiroho, ili lipate kufanyika kwa heshima yako na ukubali wako mtakatifu;
11 Na katika namna ambayo tutaweza kuonekana wenye kustahili, machoni mwako, ili tupate utimilifu wa ahadi ambazo umezifanya kwetu sisi, watu wako, katika mafunuo uliyotupatia;
12 Ili utukufu wako upate kutua juu ya watu wako, na juu ya nyumba yako hii, ambayo sasa tunakutunukia wewe, ili ipate kutakaswa na kuwekwa wakfu kuwa takatifu, na ili uwepo wako mtakatifu, upate daima kuwa ndani ya nyumba hii;
13 Na kwamba watu wote watakaoingia mlangoni mwa nyumba ya Bwana wapate kuhisi uwezo wako, na walazimike kutambua kwamba wewe umeitakasa, na kwamba ni nyumba yako, mahali pa utakatifu wako.
14 Na uwajalie, Baba Mtakatifu, kwamba wale wote watakaoabudu katika nyumba hii wapate kufundishwa maneno ya hekima kutoka katika vitabu vilivyo bora, na kwamba wapate kutafuta maarifa hata kwa kujifunza, na pia kwa imani, kama wewe ulivyotuambia;
15 Na kwamba waweze kukua ndani yako, na kuupokea utimilifu wa Roho Mtakatifu, na kusimamiwa kulingana na sheria zako, na kujitayarisha kupokea kila jambo linalohitajika;
16 Na kwamba nyumba hii iwe nyumba ya sala, nyumba ya mfungo, nyumba ya imani, nyumba ya utukufu na ya Mungu, hata nyumba yako;
17 Kwamba kuingia kote kwa watu wako, ndani ya nyumba hii, kupate kuwa katika jina la Bwana;
18 Kwamba kutoka kwao ndani ya nyumba hii kupate kuwa katika jina la Bwana;
19 Na kwamba maamkizi yao yote yapate kuwa katika jina la Bwana, kwa mikono iliyotakata, iliyoinuliwa kwa Aliye Juu Sana;
20 Na kwamba hakuna kitu kilicho kichafu kitakacho ruhusiwa kuja ndani ya nyumba yako ili kuichafua;
21 Na ikiwa watu wako watavunja sheria, yeyote miongoni mwao, atubu haraka na kurejea kwako, na kuona fadhili machoni pako, na kurejeshwa kwenye baraka ambazo wewe umeziweka ili kuzimwaga juu ya wale watakaokuabudu wewe katika nyumba yako.
22 Na tunakuomba wewe, Baba Mtakatifu, kwamba watumishi wako wapate kwenda katika nyumba hii wakiwa wamevikwa uwezo wako, na kwamba jina lako liweze kuwa juu yao, na utukufu wako uwazingire pande zote, na malaika zako wawalinde;
23 Na kutoka mahali hapa wao wapate kushuhudia habari hizi zilizo kuu na tukufu kupita kiasi, katika ukweli, hadi miisho ya dunia, ili wao wapate kujua kwamba hii ni kazi yako, na kwamba wewe umeunyoosha mkono wako, kutimiza lile ambalo ulilinena kwa vinywa vya manabii, juu ya siku za mwisho.
24 Tunakuomba, Baba Mtakatifu, kuwastawisha watu ambao watakuabudu, na watakuwa na jina na heshima katika hii nyumba yako, kwa vizazi vyote na yote;
25 Kwamba kila silaha itakayofanyika juu yao isifanikiwe; kwamba achimbaye shimo kwa ajili yao atumbukie mwenyewe;
26 Kwamba hakuna kundi la uovu litakalo kuwa na uwezo wa kuinuka na kuwashinda watu wako ambao juu yao jina lako litawekwa katika nyumba hii;
27 Na kama watu wowote watainuka dhidi ya watu hawa, kwamba hasira yako na iwake dhidi yao;
28 Na kama watawapiga watu hawa na wewe utawapiga; wewe utapigana kwa ajili ya watu wako kama ulivyofanya katika siku ya vita, ili wapate kukombolewa kutoka mikononi mwa adui zao wote.
29 Tunakuomba, Baba Mtakatifu, kuwafadhaisha, na kuwashangaza, na kuwatia aibu na kiwewe, wale wote walioeneza taarifa za uongo kote, ulimwenguni, dhidi ya mtumishi au watumishi wako, kama hawatatubu, wakati injili isiyo na mwisho itakapotangazwa masikioni mwao;
30 Na kwamba kazi zao zote ziwe si kitu, na kufagiliwa mbali kwa mvua ya mawe, na kwa hukumu ambazo utazileta juu yao katika hasira yako, ili uweze kuwa mwisho wa uongo na kashfa dhidi ya watu wako.
31 Kwa kuwa wewe unajua, Ee Bwana, kwamba watumishi wako wamekuwa hawana hatia mbele zako katika kulishuhudia jina lako, kwa sababu hiyo wameteseka mateso haya.
32 Kwa hiyo tunaomba mbele zako ukombozi kamili na mtimilifu kutoka chini ya kongwa hili;
33 Livunje, Ee Bwana; livunje kutoka shingoni mwa watumishi wako, kwa uwezo wako, ili tuweze kuinuka katikati ya kizazi hiki na kufanya kazi yako.
34 Ee Yehova, uwarehemu watu hawa, na kama vile watu wote hutenda dhambi, samehe uvunjaji sheria wa watu wako, na wafutiwe milele.
35 Na mpako wa mafuta wa wahudumu wako na ufungwe juu yao kwa uwezo kutoka juu.
36 Na itimizwe juu yao, kama vile juu ya wale wa siku ya Pentekoste; na vipawa vya ndimi vimwagwe juu ya watu wako, hata ndimi zilizogawanyika kama ndimi za moto, na tafsiri yake.
37 Na nyumba yako na ijazwe, kama kwa uvumi wa upepo wa nguvu uendao kasi, kwa utukufu wako.
38 Weka juu ya watumishi wako ushuhuda wa agano, ili wakati wakienda nje na kutangaza neno lako wapate kuzifunga sheria, na kuitayarisha mioyo ya watakatifu wako kwa ajili ya hukumu zile zote ambazo u karibu kuzileta, katika ghadhabu yako, juu ya wakazi wa dunia, kwa sababu ya uvunjaji wao wa sheria, ili watu wako wasikate tamaa katika siku ya dhiki.
39 Na katika mji wowote watumishi wako watakaoingia, na watu wa mji huo wakaupokea ushuhuda wao, na amani yako na wokovu wako uwe juu ya mji huo; ili wapate kuwakusanya kutoka mji huo wenye haki, ili waweze kuja Sayuni, au katika vigingi vyake, mahali pa uteuzi wako, kwa nyimbo za shangwe isiyo na mwisho;
40 Na hadi hili litimizwe, usiache hukumu yako ianguke juu ya mji ule.
41 Na mji wowote watumishi wako watakaoingia, na watu wa mji huo wasiupokee ushuhuda wa watumishi wako, na watumishi wako wakawaonya wajiokoe kutoka kizazi hiki chenye ukaidi, na iwe juu ya mji huo kulingana na yale uliyoyanena kwa vinywa vya manabii wako.
42 Lakini waokoe wewe, Ee Yehova, tunakuomba, watumishi wako kutoka mikononi mwao, na kuwaosha kutokana na damu yao.
43 Ee Bwana, hatufurahii katika maangamizo ya wanadamu wenzetu; nafsi zao ni za thamani kubwa mbele zako;
44 Lakini neno lako lazima litimizwe. Wasaidie watumishi wako kusema, wakisaidiwa na neema yako: Mapenzi yako yatimizwe, Ee Bwana, na wala si yetu.
45 Sisi tunajua kwamba umenena kwa vinywa vya manabii wako mambo ya kutisha juu ya waovu, katika siku za mwisho—kwamba utamwaga hukumu zako, pasipo kipimo;
46 Kwa hiyo, Ee Bwana, waokoe watu wako kutokana na majanga ya waovu; wawezeshe watumishi wako kuitia muhuri sheria, na kuufunga ushuhuda, ili waweze kutayarishwa dhidi ya siku ya mchomo.
47 Tunakuomba, Baba Mtakatifu, kuwakumbuka wale waliofukuzwa na wakazi wa wilaya ya Jackson, Missouri, kutoka viwanja vya urithi wao, na livunje, Ee Bwana, kongwa hili la mateso ambalo limewekwa juu yao.
48 Wewe wajua Ee Bwana, kwamba wameonewa na kuteswa sana na watu waovu; na mioyo yetu imetiririka kwa huzuni kwa sababu ya masumbuko yao makali.
49 Ee Bwana, hata lini utawaacha watu hawa kuteseka mateso haya, na vilio vya wasio na hatia kupanda juu masikioni mwako, na damu yao kuja kwako kwa ushuhuda mbele zako, na wala usionyeshe ushuhuda wako kwa niaba yao?
50 Uwe na huruma, Ee Bwana, juu ya kundi la wahuni waovu, ambao wamewafukuza watu wako, ili wapate kukoma kuharibu, ili waweze kutubu dhambi zao kama toba itaonekana;
51 Lakini ikiwa hawatafanya hivi, uweke wazi mkono wako, Ee Bwana, na ukomboe kile ambacho ulikiteua kuwa Sayuni kwa ajili ya watu wako.
52 Na kama haiwezekani kuwa vinginevyo, ili kazi ya watu wako isipate kushindwa mbele zako hasira yako na iwake, na uchungu wa hasira yako uanguke juu yao, ili waharibiwe mbali, vyote shina na tawi, kutoka chini ya mbingu;
53 Lakini kadiri watakavyotubu, wewe ni mwenye neema na huruma, nawe utaigeuza ghadhabu yako wakati uangaliapo juu ya sura ya Mpakwa mafuta wako.
54 Uwe na huruma, Ee Bwana, juu ya mataifa yote ya dunia; uwe na huruma juu ya watawala wa nchi yetu; na kanuni zile ambazo kwa heshima na taadhima zililindwa na mababu zetu, ambazo ndiyo Katiba ya nchi yetu, na idumu milele.
55 Wakumbuke wafalme, watawala, watu mashuhuri, na wakuu wa duniani, na watu wote, na makanisa, maskini wote, na wenye shida, na wanaoteseka duniani;
56 Ili mioyo yao ipate kulainishwa wakati watumishi wako watakapo waendea kutoka nyumbani mwako, Ee Yehova, kulishuhudia jina lako; ili chuki zao zipate kutoa njia mbele ya ukweli, na watu wako wapate kukubalika machoni pa wote;
57 Ili miisho yote ya dunia ipate kujua kwamba sisi, watumishi wako, tumeisikia sauti yako, na kwamba wewe umetutuma sisi;
58 Ili kutoka miongoni mwao wote hawa, watumishi wako, wana wa Yakobo, waweze wawakusanye wenye haki kuujenga mji mtakatifu kwa jina lako, kama wewe ulivyowaamuru.
59 Tunakuomba kuichagulia Sayuni vigingi vingine licha ya hiki ambacho umekiteua, ili kukusanyika kwa watu wako kupate kuendelea katika uwezo mkuu na utukufu, ili kazi yako ipate kufupishwa kwa haki.
60 Sasa maneno haya, Ee Bwana, tumeyanena mbele zako, juu ya mafunuo na amri ambazo umezitoa kwetu sisi, ambao tunashirikishwa na Wayunani.
61 Lakini wewe unajua kwamba unayo mapenzi makubwa kwa watoto wa Yakobo, ambao wametawanywa juu ya milima kwa muda mrefu, katika siku ya mawingu na giza.
62 Sisi kwa hiyo tunakuomba uwe na huruma juu ya watoto wa Yakobo, ili Yerusalemu, kutoka saa hii, iweze kuanza kukombolewa;
63 Na kongwa la utumwa lianze kuvunjwa kutoka nyumba ya Daudi;
64 Na watoto wa Yuda waanze kurejea kwenye viwanja ambavyo wewe ulivitoa kwa Ibrahimu, baba yao.
65 Na fanya kuwa mabaki ya Yakobo, ambao wamelaaniwa na kupigwa kwa sababu ya uvunjaji wao wa sheria, waongolewe kutoka katika hali yao ya unyama na ukatili kuja katika utimilifu wa injili isiyo na mwisho;
66 Ili wapate kuziweka chini silaha zao za umwagaji damu, na kuacha uasi wao.
67 Na mabaki ya Israeli wote waliotawanywa, ambao wamefukuzwa hadi miisho ya dunia, waje katika ufahamu wa ukweli, wamwamini Masiya, na wakombolewe kutokana na kuonewa, na wafurahi mbele zako.
68 Ee Bwana, umkumbuke mtumishi wako, Joseph Smith, Mdogo, na dhiki na mateso yake yote—jinsi alivyoagana na Yehova, na alivyoweka nadhiri kwako, Ewe Mwenyezi Mungu wa Yakobo—na amri ambazo umezitoa kwake, na kwamba kwa moyo wote amejitahidi kuyafanya mapenzi yako.
69 Uwe na huruma, Ee Bwana, juu ya mke na watoto wake, ili wapate kutukuzwa katika uwepo wako, na watunzwe kwa mkono wako wenye kulea.
70 Uwe na huruma juu ya jamaa zao wa karibu, ili chuki zao zipate kuvunjwa na kufagiliwa mbali kama kwa gharika; ili waweze kuongolewa na kukombolewa pamoja na Israeli, na wajue kuwa wewe ndiye Mungu.
71 Wakumbuke, Ee Bwana, marais, hata marais wote wa kanisa lako, ili mkono wako wa kuume upate kuwainua, pamoja na familia zao zote, na jamaa zao wa karibu, ili majina yao yaweze kudumishwa na kuwa katika ukumbusho usiyo na mwisho kutoka kizazi hadi kizazi.
72 Ulikumbuke kanisa lako lote, Ee Bwana, pamoja na familia zao zote, na jamaa zao wote wa karibu, pamoja na wagonjwa na wenye kuteseka wao wote, pamoja na maskini na wanyonge wa dunia wote; ili ufalme, ambao umeuanzisha pasipo mikono, uweze kuwa mlima mkuu na kuijaza dunia yote;
73 Ili kanisa lako liweze kujitokeza kutoka nyika zenye giza, na kuangaza vizuri kama mwezi, safi kama jua, wakutisha kama jeshi lenye bendera;
74 Na kurembeshwa kama bibi harusi kwa siku ile utakapozifunua mbingu, na kuifanya milima ishushwe mbele ya uwepo wako, na mabonde yainuliwe, mahali palipoparuzwa patalainishwa; ili utukufu wako upate kuijaza nchi;
75 Ili wakati baragumu litakapolia kwa ajili ya wafu, tunyakuliwe mawinguni kukulaki wewe, ili daima tuwe pamoja na Bwana;
76 Ili mavazi yetu yapate kuwa safi, ili tuweze kuvikwa majoho ya haki, tukiwa na matawi ya miti mikononi mwetu, na mataji ya utukufu juu ya vichwa vyetu, na kuvuna shangwe ya milele kwa mateso yetu yote.
77 Ee Bwana Mungu Mwenyezi, utusikilize sisi katika maombi yetu haya, na utujibu kutoka mbinguni, makao yako matakatifu, mahali wewe uketipo katika kiti cha enzi, kwa utukufu, heshima, uwezo, fahari, nguvu, utawala, kweli, haki, hukumu, neema, na utimilifu usio na mwisho, tangu milele hata milele.
78 Ee tusikie, Ee tusikie, Ee tusikie sisi, Ee Bwana! Na ujibu maombi haya, na upokee kuwekwa wakfu kwa nyumba hii kwako, kazi ya mikono yetu, ambayo tumeijenga kwa ajili ya jina lako;
79 Na pia kanisa hili, kuwekwa juu yake jina lako. Na utusaidie sisi kwa uwezo wa Roho wako, ili tuweze kuchanganya sauti zetu pamoja na wale maserafi wazuri na wenye kungʼara kuzunguka kiti chako cha enzi, kwa shangwe za kusifu, tukiimba Hosana kwa Mungu na kwa Mwanakondoo!
80 Na hawa, wapakwa mafuta wako, na wavikwe wokovu, na watakatifu wako wapige kelele kwa sauti kwa ajili ya shangwe. Amina, na Amina.