Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 35


Sehemu ya 35

Ufunuo uliotolewa kwa Joseph Smith Nabii na Sidney Rigdon, huko au karibu na Fayette, New York, 7 Desemba 1830. Kwa wakati huu, Nabii alikuwa akijishughulisha karibu kila siku na kufanya tafsiri ya Biblia. Tafsiri hiyo ilianza mapema Juni 1830, na wote Oliver Cowdery na John Whitmer walikuwa wametumika kama waandishi. Kwa vile wote sasa walikuwa wameitwa kwenye majukumu mengine, Sidney Rigdon aliitwa kwa uteuzi ulio mtakatifu kuwa kama mwandishi wa Nabii katika kazi hii (ona aya ya 20). Kama utangulizi katika kumbukumbu yake ya ufunuo huu, Historia ya Joseph Smith inaeleza: “Mnamo Desemba Sidney Rigdon alikuja [kutoka Ohio] ili kumwomba Bwana, na pamoja naye alikuja pia Edward Partridge. … Muda mfupi baada ya kuwasili kwao ndugu hawa wawili, na hivi ndivyo alivyosema Bwana.”

1–2, Ni kwa namna gani watu wanaweza kufanyika wana wa Mungu; 3–7, Sidney Rigdon ameitwa kubatiza na kutoa Roho Mtakatifu; 8–12, Ishara na miujiza hufanyika kwa imani; 13–16, Watumishi wa Bwana watawapura mataifa kwa uwezo wa Roho; 17–19, Joseph Smith anashikilia funguo za siri; 20–21, Wateule watastahimili siku ya ujio wa Bwana; 22–27, Israeli ataokolewa.

1 Sikilizeni sauti ya Bwana Mungu wenu, hata Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, ambaye uelekeo wake ni imara milele, yeye yule leo kama jana, na hata milele.

2 Mimi ndimi Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, aliyesulubiwa kwa ajili ya dhambi za ulimwengu, hata wale wote watakaoliamini jina langu, kwamba waweze kuwa wana wa Mungu, hata wamoja ndani yangu kama Mimi tulivyo wamoja na Baba, vile Baba yu ndani yangu ili tuweze kuwa wamoja.

3 Tazama, amini, amini, ninasema mtumishi wangu Sidney, nimekuangalia wewe na kazi zako. Nimezisikia sala zako, na nimekutayarisha kwa kazi iliyo kuu.

4 Umebarikiwa wewe, kwani utafanya mambo makubwa. Tazama wewe umetumwa, kama vile Yohana, kuitengeneza njia mbele yangu, na mbele ya Eliya ambaye atakuja, na wewe hujui.

5 Na wewe umebatiza kwa maji kwa ajili ya toba, lakini hawakumpokea Roho Mtakatifu;

6 Lakini sasa ninakupa wewe amri, kwamba utawabatiza kwa maji, na watampokea Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono, kama vile mitume wa kale.

7 Na itakuwa kwamba kutakuwa na kazi kubwa katika nchi, hata miongoni mwa Wayunani, kwani upumbavu wao na machukizo yao yatakuwa dhahiri machoni pa watu wote.

8 Kwani Mimi ni Mungu, na mkono wangu haujafupishwa; na nitaonyesha miujiza, ishara, na maajabu, kwa wale wote waaminio katika jina langu.

9 Na yeyote atakayeomba kwa imani katika jina langu, watawatoa pepo wabaya, watawaponya wagonjwa; watawafanya vipofu kuona, na viziwi kusikia, na mabubu kusema, na viwete kutembea.

10 Na saa yaja haraka ambapo mambo makuu yataonyeshwa kwa wanadamu;

11 Lakini pasipo imani hakuna kitu chochote kitakachoonyeshwa isipokuwa ukiwa juu ya Babilonia, ule ule ambao ulifanya mataifa yote kunywa mvinyo wa ghadhabu ya uasherati wake.

12 Na hakuna yeyote afanyaye yaliyo mema isipokuwa wale walio tayari kupokea utimilifu wa injili yangu, ambayo nimeitoa kwa kizazi hiki.

13 Kwa hiyo, nimewachagua walio wadhaifu wa ulimwengu, wale ambao hawakusoma na waliodharauliwa, ili kuyapura mataifa kwa uwezo wa Roho wangu;

14 Na mkono wao utakuwa mkono wangu, na nitakuwa ngao yao na kigao chao; na nitafunga viuno vyao, watapigana kiume kwa ajili yangu; na maadui zao watakuwa chini ya miguu yao; na Mimi nitaushusha upanga kwa niaba yao, na kwa moto wa hasira yangu nitawalinda.

15 Na maskini na wanyenyekevu watahubiriwa injili, nao watautazamia wakati wa ujio wangu, kwani u karibu

16 Nao watajifunza mfano wa mtini, kwani hata sasa wakati wa mavuno tayari u karibu.

17 Na nimepeleka utimilifu wa injili yangu kwa mkono wa mtumishi wangu Joseph; na katika unyonge nimembariki;

18 Na nimempa funguo za siri ya mambo yaliyofungwa, hata mambo yaliyokuwepo tangu misingi ya ulimwengu, na mambo yatakayokuja, tangu wakati huu hadi wakati wa ujio wangu, kama atakaa ndani yangu, na kama siyo, mwingine nitampanda mahali pake.

19 Kwa hiyo, utamwangalia yeye kwamba imani yake isitindike, na itatolewa na Mfariji, Roho Mtakatifu, ajuaye mambo yote.

20 Na amri ninakupa wewe—kwamba utaandika kwa ajili yake; na maandiko yatatolewa, kama vile yalivyo moyoni mwangu, kwa wokovu wa wateule wangu;

21 Kwani wataisikia sauti yangu, na kuniona Mimi, na wala hawatakuwa wamelala, nao watakaa siku ya ujio wangu; kwani watatakaswa, kama vile mimi nilivyotakasika.

22 Na sasa ninakuambia, kaa pamoja naye, naye atasafiri pamoja na wewe; wala usimwache, na hakika mambo haya yatatimia.

23 Na kwa kuwa huandiki, tazama, itatolewa kwake yeye kutoa unabii; nawe utahubiri injili yangu na kuwataja manabii watakatifu ili kuthibitisha maneno yake, kama yatakavyotolewa naye.

24 Shika amri na maagano yote ambayo kwayo mmefungwa; na Mimi nitazifanya mbingu zitikisike kwa ajili yenu, na Shetani atatetemeka, na Sayuni itafurahi juu ya milima na kustawi;

25 Na Israeli ataokolewa katika wakati wangu mwenyewe utakapofika; na kwa funguo nilizompa wataongozwa, na wala hawatachanganyika tena kamwe.

26 Inueni mioyo yenu na furahini, ukombozi wenu u karibu.

27 Msiogope, enyi kundi dogo, ufalme ni wenu hadi nitakapokuja. Tazama, naja haraka. Hivyo ndivyo. Amina.