Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 121


Sehemu ya 121

Sala na unabii ulioandikwa na Joseph Smith Nabii katika waraka wake kwa Kanisa wakati akiwa mfungwa gerezani la Liberty, Missouri, ulioandikwa 20 Machi 1839. Nabii na wenzake kwa miezi kadhaa walikuwa wako gerezani. Msaada wa maombi na rufaa zao zilielekezwa kwa maofisa watendaji na mahakama vilishindwa kuwaletea msaada wowote.

1–6, Nabii amwomba Bwana kwa ajili ya Watakatifu wanaoteseka; 7–10, Bwana amwambia amani; 11–17, Laana i juu ya wale wote waletao vilio vya uongo vya uvunjaji wa sheria dhidi ya watu wa Bwana; 18–25, Hawatakuwa na haki ya kupata ukuhani na watahukumiwa; 26–32, Mafunuo matukufu yameahidiwa kwa wale wastahimilio kwa ujasiri; 33–40, Kwa nini wengi huitwa na wachache huteuliwa; 41–46, Ukuhani unapaswa kutumika tu katika haki.

1 Ee Mungu, uko wapi? Na ni wapi lilipo hema lifichalo mahali pako pa kujificha?

2 Ni kwa muda gani mkono wako utazuiliwa, na jicho lako, ndiyo, jicho lako lililo safi, litatazama kutoka katika mbingu za milele maovu ya watu wako na ya watumishi wako, na sikio lako kupenywa kwa vilio vyao?

3 Ndiyo, Ee Bwana, ni kwa muda gani watateseka kwa maovu haya na dhuluma zisizo za kisheria, kabla moyo wako haujalainika kwa ajili yao, na matumbo yako kusikia huruma kwa ajili yao?

4 Ee Bwana Mungu Mwenyezi, muumba wa mbingu, dunia, na bahari, na wa vitu vyote vilivyomo ndani yake, na umtawalaye na kumtiisha ibilisi, na utawala wa giza na usiofahamika wa Sheoli—nyoosha mkono wako; jicho lako na lipenye; hema lako na linyakuliwe; mahali pako pa kujificha na pasifunikwe; sikio lako na litegwe, moyo wako na ulainike, na moyo wako utuonee huruma.

5 Hasira yako na iwake dhidi ya adui zetu; na, katika ghadhabu ya moyo wako, kwa upanga wako tulipie kisasi kwa mabaya tuliyotendewa.

6 Wakumbuke watakatifu wako wanaoteseka, Ee Mungu wetu; na watumishi wako watafurahi katika jina lako milele.

7 Mwanangu, amani iwe katika nafsi yako; taabu yako na mateso yako yatakuwa kwa muda mfupi;

8 Na halafu, kama utastahimili vyema, Mungu atakuinua juu; nawe utawashinda maadui zako wote.

9 Marafiki zako watakuwa waaminifu kwako, nao watakushangilia tena kwa moyo wa upendo na mikono ya urafiki.

10 Wewe bado hujawa kama Ayubu; marafiki zako hawashindani nawe, wala hawatakushtaki kwa uvunjaji wa sheria, kama walivyomfanya Ayubu.

11 Nao wenye kukushtaki kwa uvunjaji wa sheria, matumaini yao yataharibika, na matarajio yao yatayeyukia mbali kama umande uyeyukavyo mbele ya miale iunguzayo ya jua linalochomoza;

12 Na pia kwamba Mungu amepeleka mkono wake na kutia muhuri kubadilisha nyakati na majira, na kupofusha akili zao, ili wasipate kufahamu matendo yake ya ajabu; ili apate kuwajaribu wao pia na kuwachukua wakiwa katika mitego yao wenyewe;

13 Pia kwa sababu mioyo yao imeharibiwa; na mambo ambayo wako tayari kuwaletea wengine, na kupenda kuwaona wengine wakiteseka, na yaje juu yao wenyewe kwa kiwango cha juu kabisa;

14 Ili nao wapate kukatishwa tamaa pia, na matumaini yao yapate kuvunjiliwa mbali;

15 Na siyo miaka mingi kutoka sasa, ili wao na wazao wao wafagiliwe kutoka chini ya mbingu, asema Mungu, ili hata mmoja wao asiachwe hai.

16 Walaaniwe wale wote watakaoinua visigino dhidi ya wapakwa mafuta wangu, asema Bwana, na kulia wametenda dhambi wakati hawajatenda dhambi mbele yangu, asema Bwana, bali wametenda yale yaliyofaa machoni pangu, na yale ambayo niliwaamuru.

17 Lakini wale waliao kuwa uvunjaji wa sheria umetendeka, ndiyo wafanyao kwa sababu wao ni watumwa wa dhambi, nao wenyewe ni wana wa uasi.

18 Na wale waapao kwa uongo dhidi ya watumishi wangu, ili wapate kuwaleta katika utumwa na mauti—

19 Ole wao; kwa sababu wamewakosea wadogo zangu hao watatengwa kwenye ibada za nyumba yangu.

20 Kapu lao halitajaa, nyumba zao na vihenga vyao vitaangamia, na wao wenyewe watadharauliwa na wale walio walaghai.

21 Hawatakuwa na haki ya ukuhani, wala wazao wao baada yao kutoka kizazi hadi kizazi.

22 Ingelikuwa bora kwao kwamba wangefungiwa shingoni jiwe la kusagia, na kutoswa katika kilindi cha bahari.

23 Ole wao wale wote wawasumbuao watu wangu, na kuwafukuza, na kuwaua, na kushuhudia dhidi yao, asema Bwana wa Majeshi; kizazi cha nyoka hakitaepuka hukumu ya jehanamu.

24 Tazama, macho yangu yanaona na kujua matendo yao yote, na nimeiweka tayari hukumu ya haraka katika majira yake, kwa ajili yao wote;

25 Kwani kuna wakati uliopangwa kwa kila mwanadamu, kulingana na matendo yake yatakavyokuwa.

26 Mungu atakupa maarifa kwa njia ya Roho wake Mtakatifu, ndiyo, kwa kipawa chake kisichosemeka cha Roho Mtakatifu, maarifa ambayo hayajafunuliwa tangu ulimwengu kuwepo hadi sasa;

27 Ambayo babu zetu wamekuwa wakiyasubiri kwa shauku kubwa yafunuliwe katika nyakati za mwisho, mababu ambao akili zao zilielekezwa huko na malaika, kama yalivyozuiliwa kwa ajili ya utimilifu wa utukufu wao;

28 Wakati ujao ambamo hakuna kitakachozuiliwa, iwe kuna Mungu mmoja au miungu wengi, watajulikana.

29 Enzi zote na tawala, himaya na nguvu, vitafunuliwa na kuwekwa juu ya wote ambao wamestahimili kwa ujasiri mkubwa kwa ajili ya injili ya Yesu Kristo.

30 Na pia, kama kuna mipaka iliyowekwa kwa mbingu au bahari, au kwa nchi kavu, au kwa jua, mwezi, au nyota—

31 Nyakati za mzunguko wao wote, siku zilizoteuliwa zote, miezi, na miaka, na siku zote za siku zao, miezi, na miaka, na utukufu wao wote, sheria, na nyakati zilizowekwa, zitafunuliwa katika siku za kipindi cha utimilifu wa nyakati—

32 Kulingana na kile ambacho kilitawazwa katikati ya Baraza la Mungu wa Milele, Mungu wa miungu wengine wote kabla ya ulimwengu huu kuwepo, kile ambacho kilipaswa kuhifadhiwa hadi kumalizika na mwisho wake, wakati kila mtu atakapoingia katika uwepo wake wa milele na katika pumziko lake katika mwili usiokufa.

33 Ni kwa muda gani maji yatembeayo yatabaki kuwa machafu? Ni nguvu gani zitazizuia mbingu? Kama vile mwanadamu asivyoweza kunyoosha mkono wake dhaifu kuusimamisha mto Missouri katika mkondo wake uliokusudiwa, au kuugeuza mtiririko wake kwenda juu, vivyo hivyo hawezi kumzuia Mwenyezi kumwaga chini maarifa kutoka mbinguni juu ya vichwa vya Watakatifu wa Siku za Mwisho.

34 Tazama, wengi huitwa, lakini wachache huteuliwa. Na ni kwa nini hawakuteuliwa?

35 Kwa sababu mioyo yao imekuwa juu ya mambo ya ulimwengu huu, na kutafuta kupata heshima kutoka kwa wanadamu, kwamba hawajifunzi somo hili moja—

36 Kwamba haki za ukuhani zimeungana na hazitenganishwi na nguvu za mbinguni, na kwamba nguvu za mbinguni haziwezi kudhibitiwa wala kutawaliwa isipokuwa tu kwa kanuni za haki.

37 Ni kweli, kwamba zinaweza kutunukiwa juu yetu; lakini tutakapojaribu kuficha dhambi zetu, au kuridhisha kiburi chetu, tamaa yetu ya makuu, au kutumia katika udhibiti au utawala au ulazimishaji juu ya nafsi za wanadamu, katika kiwango chochote kisicho cha haki, tazama, mbingu hujitoa zenyewe; Roho wa Bwana husikitika; na mara akijitoa, Amina kwa ukuhani au mamlaka ya mtu yule.

38 Tazama, kabla hajatambua, ameachwa peke yake, kuupiga mateke miiba, kuwatesa watakatifu, na kupigana na Mungu.

39 Tumejifunza kwa uzoefu wa kuhuzunisha kwamba ni kawaida na ni tabia ya karibu wanadamu wote, kwamba mara wapatapo mamlaka kidogo, kama wanavyodhani, huanza mara moja kuyatumia mamlaka hayo bila haki.

40 Kwa sababu hiyo wengi huitwa, lakini wachache huteuliwa.

41 Hakuna nguvu au uwezo unaoweza au upaswao kudumishwa kwa njia ya ukuhani, isipokuwa tu kwa njia ya ushawishi, kwa uvumilivu, kwa upole na unyenyekevu, na kwa upendo usio unafiki;

42 Kwa wema, na maarifa safi, ambayo yataikuza sana nafsi isiyo na unafiki, na isiyo na hila

43 Kukemea kwa ukali kwa wakati wake, utakapokuwa umeongozwa na Roho Mtakatifu; na halafu baadaye kuonyesha ongezeko la upendo kwa yule uliyemkemea, asije akakudhania wewe kuwa ni adui yake;

44 Ili apate kujua kwamba uaminifu wako ni imara zaidi kuliko kamba za mauti.

45 Na moyo wako pia uwe umejaa hisani kwa wanadamu wote, na kwa jamaa ya waaminio, na wema uyapambe mawazo yako bila kukoma; ndipo kujiamini kwako kutakuwa imara katika uwepo wa Mungu; na mafundisho ya ukuhani yatatonatona juu ya roho yako kama umande utokao mbinguni.

46 Roho Mtakatifu atakuwa mwenzi wako daima, na fimbo yako ya kifalme fimbo isiyobadilika ya haki na ukweli; na utawala wako utakuwa utawala usio na mwisho, na usio wa njia ya kulazimisha utatiririka kwako milele na milele.