Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 11


Sehemu ya 11

Ufunuo uliotolewa kupitia Joseph Smith Nabii kwa kaka yake Hyrum Smith, huko Harmony, Pennsylvania, Mei 1829. Ufunuo huu ulipokelewa kupitia Urimu na Thumimu katika jibu kwa maombi na maulizo ya Joseph Smith. Historia ya Joseph Smith inapendekeza kwamba ufunuo huu ulipokelewa baada ya urejesho wa Ukuhani wa Haruni.

1–6, Watenda kazi katika shamba la mizabibu watapata wokovu; 7–14, Tafuta hekima, hubiri toba, amini katika Roho; 15–22, Shika amri, na jifunze neno la Bwana; 23–27, Usikatae roho wa ufunuo na wa unabii; 28–30, Wale ambao wanampokea Kristo huwa wana wa Mungu.

1 Kazi kubwa na ya ajabu i karibu kuja miongoni mwa wanadamu.

2 Tazama, Mimi ndimi Mungu; tiini neno langu, lililo hai na lenye nguvu, kali kuliko upanga wenye makali pande mbili, kwa kugawanya viungo na mafuta yaliyo ndani yake; hivyo basi, litiini neno langu.

3 Tazama, shamba ni jeupe tayari kwa mavuno; kwa hivyo, yeyote atakaye kuvuna na aingize mundu yake kwa nguvu zake, na kuvuna wakati siku ingali, ili aweze kujiwekea hazina ya wokovu usio na mwisho kwa ajili ya nafsi yake katika ufalme wa Mungu.

4 Ndiyo, yeyote yule atakayeingiza mundu yake na kuvuna, yeye huyo ameitwa na Mungu.

5 Kwa hivyo, kama wewe utaniomba Mimi utapata, kama utabisha utafunguliwa.

6 Sasa, kama ulivyoomba, tazama, ninakuambia, shika amri zangu, na tafuta kuanzisha na kustawisha kusudi la Sayuni.

7 Usitafute utajiri bali hekima; na, tazama, siri za Mungu zitafichuliwa kwako, na ndipo wewe utafanywa tajiri. Tazama, yule aliye na uzima wa milele ndiye tajiri.

8 Amini, amini, ninakuambia, kama vile unavyotaka kutoka kwangu na hivyo ndivyo itakavyokuwa kwako; na, kama unataka, utakuwa chanzo cha kufanya mema mengi katika kizazi hiki.

9 Usiseme lolote bali toba kwa kizazi hiki. Shika amri zangu, na saidia kuitenda kazi yangu, kulingana na amri zangu, nawe utabarikiwa.

10 Tazama, wewe unacho kipawa, au wewe waweza kuwa na kipawa kama utataka kutoka kwangu kwa imani, pamoja na moyo mwaminifu, ukiamini katika uwezo wa Yesu Kristo, au uwezo wangu mimi niongeaye nawe;

11 Kwani, tazama, ni Mimi niongeaye; tazama, Mimi ndimi nuru ingʼarayo gizani, na kwa uwezo wangu nitatoa maneno haya kwako wewe.

12 Na sasa, amini, amini, ninakuambia wewe, weka imani yako katika Roho yule ambaye huongoza kufanya mema—ndiyo, kufanya haki, kutembea kwa unyenyekevu, kuhukumu kwa haki; na huyu ndiyo Roho wangu.

13 Amini, amini ninakuambia, nitakupa Roho wangu, ambaye ataiangaza akili yako, ambayo itaijaza nafsi yako kwa shangwe;

14 Na ndipo utajua, au kwa haya utajua, mambo yote ambayo unahitaji kutoka kwangu, ambayo yanahusika na mambo ya haki, katika imani ukiamini katika mimi kwamba utapokea.

15 Tazama, ninakuamuru kwamba hauhitaji kudhani kwamba wewe umeitwa kuhubiri mpaka utakapoitwa.

16 Subiri kidogo, mpaka utakapopata neno langu, mwamba wangu, kanisa langu, na injili yangu, kwamba uweze kujua uhakika wa mafundisho yangu.

17 Na tena, tazama, kulingana na matakwa yako, ndiyo, hata kulingana na imani yako itafanyika kwako.

18 Zishike amri zangu; kaa kimya; omba kwa Roho wangu;

19 Ndiyo, ambatana nami kwa moyo wako wote, ili uweze kusaidia kuleta kwenye nuru mambo yale ambayo yamesemwa—ndiyo, tafsiri ya kazi yangu; uwe mvumilivu mpaka utakapoikamilisha.

20 Tazama, hii ndiyo kazi yako, kuzishika amri zangu, ndiyo, kwa nguvu zako zote, akili na uwezo.

21 Usitafute kulitangaza neno langu, bali kwanza tafuta kulipata neno langu, na kisha ulimi wako utalegezwa; halafu, kama unataka, utapata Roho wangu na neno langu, ndiyo, nguvu ya Mungu kwa kuwashawishi wanadamu.

22 Lakini sasa kaa kimya; jifunze neno langu ambalo limeanza miongoni mwa wanadamu, na pia jifunze neno langu ambalo litakuja miongoni mwa wanadamu, au lile ambalo sasa linatafsiriwa, ndiyo, mpaka utakapopata yote ambayo nitawapa wanadamu katika kizazi hiki, na kisha mambo yote yataongezwa juu ya hayo.

23 Tazama wewe ni Hyrum, mwanangu; tafuta ufalme wa Mungu, na mambo yote yataongezwa kulingana na kile kilicho cha haki.

24 Jenga juu ya mwamba wangu, ambao ni injili yangu;

25 Usikatae roho ya ufunuo, wala roho ya unabii, kwani ole wake yule ambaye huyakataa mambo haya;

26 Kwa hivyo, yatunze katika hazina ya moyo wako mpaka wakati ambao ni hekima kwangu mimi kwamba uenende mbele.

27 Tazama, ninasema kwa wale wote walio na matakwa yaliyo mema, na wameingiza mundu zao kuvuna.

28 Tazama, Mimi ndimi Yesu Kristo, Mwana wa Mungu. Mimi ni uzima na nuru ya ulimwengu.

29 Mimi ndimi yule yule niliyekuja kwa walio wangu na walio wangu hawakunipokea;

30 Lakini amini, amini ninawaambia ninyi, kwamba kadiri wengi wanavyonipokea Mimi, wao nitawapa uwezo wa kuwa wana wa Mungu, hata kwa wale ambao wataamini juu ya jina langu. Amina.