Sehemu ya 112
Ufunuo uliotolewa kupitia Joseph Smith Nabii kwa Thomas B. Marsh, huko Kirtland, Ohio, 23 Julai 1837. Ufunuo huu unalo neno la Bwana kwa Thomas B. Marsh juu ya Mitume Kumi na Wawili wa Mwanakondoo. Ufunuo huu ulipokelewa siku ile Wazee Heber C. Kimball na Orson Hyde walipohubiri injili kwa mara ya kwanza huko Uingereza. Thomas B. Marsh kwa wakati huu alikuwa Rais wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili.
1–10, Mitume Kumi na Wawili wataipeleka injili na kupaza sauti ya onyo kwa mataifa yote na watu wote; 11–15, Wao wataubeba msalaba wao, kumfuata Yesu, na kulisha kondoo Wake; 16–20, Wale waupokeao Urais wa Kwanza wampokea Bwana; 21–29, Giza limeifunika dunia, na ni wale tu waaminio na kubatizwa wataokolewa; 30–34, Urais wa kwanza na Mitume Kumi na Wawili wanashikilia funguo za kipindi cha utimilifu.
1 Amini hivyo ndivyo asemavyo Bwana kwako wewe mtumishi wangu Thomas: Nimesikia sala zako; na sadaka zako zimefika juu kama ukumbusho mbele zangu, kwa niaba ya wale, ndugu zako, ambao walichaguliwa kutoa ushuhuda wa jina langu na kuupeleka ulimwenguni kote miongoni mwa mataifa yote, makabila, lugha, na watu, na kutawazwa kwa njia ya watumishi wangu.
2 Amini ninakuambia, pamekuwepo na baadhi ya mambo machache moyoni mwako na pamoja nawe ambayo Mimi, Bwana, sikupendezwa nayo.
3 Hata hivyo, kwa vile wewe umejidhili mwenyewe nawe utakwezwa; kwa hiyo, dhambi zako zote zimesamehewa.
4 Acha moyo wako na ufurahi mbele ya uso wangu; nawe utalishuhudia jina langu, siyo tu kwa Wayunani, bali pia kwa Wayahudi; nawe utalipeleka neno langu hata miisho ya dunia.
5 Jitahidi, kwa hiyo, asubuhi hadi asubuhi; na siku hadi siku na acha sauti yako ya kuonya isikike; na usiku uingiapo usiache wakazi wa dunia walale, kwa sababu ya maneno yako.
6 Acha makazi yako yafahamike katika Sayuni, na usiiondoe nyumba yako; kwa kuwa Mimi, Bwana, ninayo kazi kubwa ya kufanywa na wewe, kazi ya kulitangaza jina langu miongoni mwa wanadamu.
7 Kwa hiyo, funga viuno vyako kwa ajili ya kazi hii. Na acha miguu yako ifungiwe pia, kwani wewe umechaguliwa, na njia zako zitakuwa miongoni mwa milima, na miongoni mwa mataifa mengi.
8 Na kwa neno lako wengi walio juu watashushwa chini, na kwa neno lako wengi walio chini watakwezwa.
9 Acha sauti yako iwe karipio kwa wavunja sheria; na kwa kukaripia kwako ulimi wa mzushi na ukome uovu wake.
10 Jinyenyekeze; na Bwana Mungu wako atakuongoza kwa mkono, na kukupa jibu la sala zako.
11 Mimi naujua moyo wako, na nimesikia sala zako juu ya ndugu zako. Usiwe na upendo zaidi kwao kuliko watu wengine wengi, bali acha upendo wako kwao uwe kama ujipendavyo wewe mwenyewe; na acha upendo wako ubaki kwa watu wote, na kwa wote walipendao jina langu.
12 Na uwaombee ndugu zako Kumi na Wawili. Waonye kwa nguvu kwa ajili ya jina langu, na acha waonywe kwa ajili ya dhambi zao zote, na uwe mwaminifu mbele zangu kwa jina langu.
13 Na baada ya majaribu yao, na taabu nyingi, tazama, Mimi, Bwana, nitawatafuta, na kama hawakuishupaza mioyo yao, na kuzikaza shingo zao dhidi yangu, wataongolewa, nami nitawaponya.
14 Sasa, ninakuambia, na hilo nikuambialo, nawaambia wote Kumi na Wawili: Inukeni na vifungeni viuno vyenu, chukua msalaba wako, ukanifuate, na kuwalisha kondoo zangu.
15 Msijikweze wenyewe; msimuasi mtumishi wangu Joseph; kwani amini ninawaambia, Mimi nipo pamoja naye, na mkono wangu utakuwa juu yake; na funguo nilizompa yeye, na pia ninyi, hazitachukuliwa kutoka kwake hadi nitakapokuja.
16 Amini ninakuambia, mtumishi wangu Thomas, wewe ni mtu ambaye nimekuchagua kuzishika funguo za ufalme wangu, zinazowahusu Kumi na Wawili, popote miongoni mwa mataifa yote—
17 Ili upate kuwa mtumishi wangu kwa kufungua mlango wa ufalme mahali pote ambapo mtumishi wangu Joseph, na mtumishi wangu Sidney, na mtumishi wangu Hyrum, hawawezi kufika.
18 Kwani juu yao nimeweka mzigo wa makanisa yote kwa kipindi kifupi.
19 Kwa sababu hiyo, kokote watakakowatuma, nendeni, nami nitakuwa pamoja nanyi; na mahali popote mtakapotangaza jina langu mlango wa matokeo ya kufaa utafunguliwa kwenu, ili wapate kulipokea neno langu.
20 Yeyote alipokeaye neno langu anipokea Mimi, na yeyote anipokeaye Mimi, huwapokea wale, Urais wa Kwanza, ambao nimewatuma, ambao nimewafanya kuwa washauri kwa ajili ya jina langu kwenu.
21 Na tena, ninawaambia, kwamba yeyote mtakayemtuma katika jina langu, kwa sauti ya ndugu zenu, hawa Kumi na Wawili, akiwa amependekezwa na kupewa mamlaka kisheria na ninyi, atakuwa na uwezo wa kufungua mlango wa ufalme wangu kwa taifa lolote ambako ninyi mtawatuma—
22 Ilimradi kama watajinyenyekeza wenyewe mbele zangu, na kukaa katika neno langu, na kuisikia sauti ya Roho wangu.
23 Amini, amini, ninawaambia, giza hufunika dunia, na giza kuu huzifunika akili za watu, na wenye mwili wote wameharibika mbele za uso wangu.
24 Tazama, kisasi chaja haraka juu ya wakazi wa dunia, siku ya ghadhabu, siku ya kuteketezwa kwa moto, siku ya ukiwa, ya kulia, ya kilio, na ya maombolezo; na kama tufani itakuja juu ya uso wote wa dunia, asema Bwana.
25 Na juu ya nyumba yangu itaanzia, na kutoka nyumbani mwangu itaenea, asema Bwana;
26 Kwanza miongoni mwa wale walio miongoni mwenu, asema Bwana, ambao wamedai kulijua jina langu na hawakunijua Mimi, nao wamenitukana katikati ya nyumba yangu, asema Bwana.
27 Kwa hiyo, angalieni msijisumbue kuhusu mambo ya kanisa langu mahali hapa, asema Bwana.
28 Bali itakaseni mioyo yenu mbele zangu, na ndipo mwende ulimwenguni kote, na kuihubiri injili yangu kwa kila kiumbe ambacho bado hakijaipokea;
29 Na yule aaminiye na kubatizwa ataokolewa, na yule asiyeamini, na hakubatizwa, atalaaniwa.
30 Kwani kwenu, Kumi na Wawili, na wale, Urais wa Kwanza wa Kwanza, ambao wameteuliwa na ninyi kuwa washauri wenu na viongozi wenu, ndiyo uwezo huu wa ukuhani umetolewa, kwa ajili ya siku za mwisho na kwa mara ya mwisho, ambacho ndicho kipindi cha utimilifu wa nyakati.
31 Uwezo ambao ninyi mnaushikilia, kwa pamoja na wale wote waliopokea kipindi kwa wakati wowote kutoka mwanzo wa uumbaji;
32 Kwani amini ninawaambia, funguo za kipindi, ambazo ninyi mmezipokea, zimekuja chini kutoka kwa mababu, na mwisho wa yote, zimeshushwa kwenu kutoka mbinguni.
33 Amini ninawaambia, tazama wito wenu ni mkubwa kiasi gani. Isafisheni mioyo yenu na mavazi yenu, isije damu ya kizazi hiki ikadaiwa mikononi mwenu.
34 Kuweni waaminifu hadi nijapo, kwani naja upesi; na ujira wangu u pamoja nami kumlipa kila mtu kulingana na kazi yake itakavyokuwa. Mimi ni Alfa na Omega. Amina.