Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 27


Sehemu ya 27

Ufunuo uliotolewa kwa Joseph Smith, Nabii, huko Harmony, Pennsylvania, Agosti 1830. Katika maandalizi ya ibada ambapo sakramenti ya mkate na divai ilikuwa itolewe, Joseph alikuwa akienda kununua divai. Alikutana na mjumbe kutoka mbinguni na akapokea ufunuo huu, ambao sehemu yake iliandikwa wakati huo, na iliyosalia iliandikwa mwezi uliofuata wa Septemba. Maji sasa yanatumika badala ya divai katika ibada ya sakramenti ya Kanisa.

1–4, Ishara zitakazotumika kupokea sakramenti zinaelezwa; 5–14, Kristo na watumishi Wake kutoka nyakati zote wanapokea Sakramenti; 15–18, Vaeni silaha za Mungu.

1 Sikilizeni sauti ya Yesu Kristo, Bwana wenu, Mungu wenu, na Mkombozi wenu, ambaye neno lake ni la haraka na lenye nguvu.

2 Kwani, tazama, ninawaambia, kwamba si muhimu ni nini utakachokunywa au utakachokula wakati unapopokea sakramenti, ili mradi kwamba unafanya hayo kwa jicho likiwa kwenye utukufu wangu pekee—mkikumbuka kwa Baba mwili wangu uliotolewa kwa ajili yenu, na damu yangu iliyomwangwa kwa ondolea la dhambi zenu.

3 Kwa hiyo, amri ninakupa, kwamba usinunue divai wala kinywaji kikali cha adui zako;

4 Kwa hiyo, msipokee chochote isipokuwa kimetengenezwa upya miongoni mwenu; ndiyo, katika huu ufalme wa Baba yangu ambao utajengwa hapa duniani.

5 Tazama, hii ni hekima kwangu; kwa hiyo, usistaajabie, kwani saa yaja ambayo nitakunywa matunda ya mvinyo pamoja nanyi duniani, na pamoja na Moroni, ambaye nilimtuma kwako kufichua Kitabu cha Mormoni, chenye utimilifu wa injili yangu isiyo na mwisho, ambaye nimemkabidhi funguo za kumbukumbu ya fimbo ya Efraimu;

6 Na pia Elia, ambaye nimemkabidhi funguo za kukamilisha urejesho wa mambo yote yaliyonenwa kwa vinywa vya manabii watakatifu tangu mwanzo wa ulimwengu, kuhusu siku za mwisho;

7 Na pia Yohana mwana wa Zakaria, Zakaria ambaye yeye (Elia) alimtembelea na kumpa ahadi kwamba atapata mwana, na jina lake litakuwa Yohana, na yeye atakuwa amejazwa na roho ya Elia;

8 Yohana ambaye nimekwisha mtuma kwenu ninyi, watumishi wangu Joseph Smith, Mdogo, na Oliver Cowdery, kuwatawaza ninyi katika ukuhani wa kwanza ambao mmeupokea, ili kwamba muwe mmeitwa na kutawazwa kama ilivyokuwa hata kama Haruni.

9 Na pia Eliya, ambaye kwake nimemkabidhi funguo za uwezo wa kuigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto, na mioyo ya watoto kwa baba, ili kwamba dunia yote isiweze kupigwa kwa laana.

10 Na pia pamoja na Yusufu na Yakobo, na Isaka, na Ibrahimu, baba zako, ambao hao ahadi zinabakia;

11 Na pia Mikaeli, au Adamu, baba wa wote, mtawala wa wote, mzee wa siku;

12 Na pia pamoja na Petro, na Yakobo, na Yohana, ambao niliwatuma kwako, kwa wao nimekutawazeni ninyi na kuwathibitisha kuwa mitume, na mashahidi maalumu wa jina langu, na kuchukua funguo za huduma yenu, na mambo yale yale niliyowafunulia wao;

13 Kwako wewe nimekukabidhi funguo za ufalme wangu, na kipindi cha injili kwa nyakati za mwisho; na kwa utimilifu wa nyakati, ambao ndani yake nitayakusanya pamoja mambo yote, yaliyoko mbinguni na yaliyoko duniani;

14 Na pia wale wote ambao Baba yangu amenipa mimi nje ya ulimwengu.

15 Kwa hiyo, inua moyo wako na ufurahie, na funga viuno vyako, na jitwalie deraya zangu zote, upate kushindana siku ya uovu, na ukiisha kuyatimiza yote, uweze kusimama.

16 Kwa hiyo, simama, ukiwa umejifunga na ukweli kiunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani, na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa injili ya amani, ambayo nimemtuma malaika wangu kuikabidhi kwako;

17 Mkitwaa ngao ya imani ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya adui;

18 Na chukueni helmeti ya wokovu, na upanga wa Roho yangu, ambayo nitaimwaga juu yenu, na neno langu ambalo ninalifunua kwenu, na mpatane kuhusiana na jambo lolote mtakaloniomba Mimi, na kuweni waaminifu mpaka nijapo Mimi, na ninyi mtanyakuliwa, ili nilipo Mimi nanyi muwepo pia. Amina.