Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 98


Sehemu ya 98

Ufunuo uliotolewa kupitia Joseph Smith Nabii, huko Kirtland, Ohio, 6 Agosti 1833. Ufunuo huu ulikuja kufuatia mateso waliyoyapata Watakatifu katika Missouri. Kuongezeka kwa makazi ya waumini wa Kanisa huko Missouri kuliwasumbua baadhi ya wahamiaji wengine, ambao walihisi ni kutishika kwa idadi ya Watakatifu, kwa nguvu ya kisiasa na kiuchumi, na kwa tofauti za kiutamaduni na kidini. Mnamo Julai 1833, kikundi cha wahuni kiliharibu mali za Kanisa, na kuwapaka lami na kuwabandika manyoya waumini wawili wa Kanisa, na kudai kwamba Watakatifu waondoke Wilaya ya Jackson. Ingawa taarifa fulani ya matatizo katika Missouri bila shaka zilikuwa zimemfikia Nabii huko Kirtland (umbali wa maili mia tisa), uzito wa hali hiyo ungeliweza kujulikana tu kwake kwa wakati huu kwa njia ya ufunuo.

1–3, Mateso ya Watakatifu yatakuwa ni kwa faida yao; 4–8, Watakatifu wajenge urafiki na sheria ya kikatiba ya nchi; 9–10, Waaminifu, wenye hekima, na watu wema yapaswa kuungwa mkono katika serikali ya nchi; 11–15, Wale wautoao uhai wao katika kazi ya Bwana watapata uzima wa milele; 16–18, Ikataeni vita na tangazeni amani; 19–22, Watakatifu katika Kirtland wanakemewa na kuamriwa kutubu; 23–32, Bwana anafunua sheria Zake zinazotawala usumbufu na mateso yaliyowekwa juu ya watu Wake; 33–38, Vita inakubalika tu ikiwa Bwana ameamuru; 39–48, Watakatifu watasamehe maadui zao, ambao, kama wakitubu, pia wataepuka kisasi cha Bwana.

1 Amini ninawaambia marafiki zangu, msiogope, mioyo yenu na ifarijike; ndiyo, furahini siku zote, na toeni shukrani katika kila kitu;

2 Mkimngoja Bwana kwa subira, kwani sala zenu zimeingia masikioni mwa Bwana wa Sabato, na zimeandikwa kwa muhuri na ushuhuda huu—Bwana ameapa na kutangaza kuwa atatoa.

3 Kwa hiyo, yeye hutoa ahadi hii kwenu, kwa ahadi isiyobadilika kwamba zitatimizwa; na mambo yote ambayo kwayo mmeteswa yatafanya kazi kwa pamoja kwa faida yenu, na kwa utukufu wa jina langu, asema Bwana.

4 Na sasa, amini ninawaambia juu ya sheria za nchi, ni mapenzi yangu kuwa watu wangu wakumbuke kufanya mambo yote ninayowaamuru wao.

5 Na sheria hii ya nchi ambayo ni ya kikatiba, inasaidia ile kanuni kwa kulinda haki na heshima, kwa ajili ya watu wote, na inakubalika mbele zangu.

6 Kwa hiyo, Mimi, Bwana, ninawakubali ninyi, na ndugu zenu wa kanisa langu, kwa kuikubali ile sheria ambayo ni sheria ya nchi kikatiba;

7 Na kuhusiana na sheria ya binadamu, chochote kilicho zaidi au pungufu ya hii, hutoka kwa yule mwovu.

8 Mimi, Bwana Mungu, nawafanya muwe huru, kwa hiyo hakika ninyi ni huru; na sheria pia huwafanya ninyi kuwa huru.

9 Hata hivyo, wakati mwovu atawalapo watu huomboleza.

10 Kwa hiyo, watu waaminifu na wenye hekima yapaswa watafutwe kwa bidii, na watu wema na wenye hekima ni lazima mzingatie kuwaunga mkono; vinginevyo chochote kilicho pungufu ya haya chatoka kwa yule mwovu.

11 Na ninawapa ninyi kwenu amri, ya kuwa muache uovu wote na mshikilie wema wote, ili mpate kuishi kwa kila neno litokalo kinywani mwa Mungu.

12 Kwani yeye atampa aliye mwaminifu amri juu ya amri, kanuni juu ya kanuni; nami nitawajaribu na kuwapima kwa njia hii.

13 Na yeyote autoaye uhai wake katika kazi yangu, kwa ajili ya jina langu, atauona tena, hata uzima wa milele.

14 Kwa hiyo, msiwaogope adui zenu, kwani nimeazimia moyoni mwangu, asema Bwana, kwamba nitawajaribu ninyi katika mambo yote, ikiwa mtakaa katika agano langu, hata mpaka kifo, ili muweze kuwa wenye kustahili.

15 Kwani kama hamtakaa katika agano langu hamnistahili.

16 Kwa hiyo, ikataeni vita na tangazeni amani, na tafuteni kwa bidii kuigeuza mioyo ya watoto kuwaelekea baba zao, na mioyo ya baba iwaelekee watoto wao;

17 Na tena, mioyo ya Wayahudi kwa manabii, na manabii kwa Wayahudi; ili nisije nikaipiga dunia kwa laana, na wenye mwili wote wakateketea mbele zangu.

18 Msifadhaike mioyoni mwenu; kwani nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi, na nimeandaa mahali kwa ajili yenu: na mahali alipo Baba na Mimi, hapo ndipo mtakuwepo pia.

19 Tazama, Mimi, Bwana, sijapendezwa na wengi walioko katika kanisa huko Kirtland;

20 Kwa kuwa hawajaacha dhambi zao, na njia zao za uovu, kiburi cha mioyo yao, na tamaa zao, na mambo yao yote ya machukizo, na kuyashika maneno ya hekima na ya uzima wa milele ambayo nimewapa.

21 Amini ninawaambia, kwamba Mimi, Bwana, nitawarudi na nitawafanya lolote nitakalo, kama hawatatubu na kuyashika mambo yote niliyowaambia.

22 Na tena ninawaambia, kama mtayashika na kufanya yale yote ninayowaamuru, Mimi, Bwana, nitageuza ghadhabu na uchungu wangu kwenu, na milango ya jehanamu haitawashinda.

23 Sasa, ninasema nanyi kuhusu familia zenu—kama watu watawapiga ninyi, au familia zenu, mara moja, nanyi mkavumilia na msitukane dhidi yao, wala msitake kulipa kisasi, ninyi mtapata thawabu;

24 Lakini kama hamkuvumilia, itahesabiwa kwenu kuwa ndicho kipimo cha haki.

25 Na tena, ikiwa adui yenu atawapiga kwa mara ya pili, na hamumtukani adui yenu, na kuvumilia kwa upole, thawabu yenu itakuwa mara-mia.

26 Na tena, ikiwa adui yenu atawapiga kwa mara ya tatu, nanyi mkavumilia kwa upole, thawabu yenu itaongezeka mara-nne;

27 Na shuhuda hizi tatu zitasimama dhidi ya adui yenu kama hatatubu, na hazitafutwa.

28 Na sasa, amini ninawaambia, kama adui yule ataepuka kisasi changu, ili asiweze kuletwa katika hukumu mbele zangu, ndipo ninyi mtaangalia kwamba mnamwonya huyo katika jina langu, ili asije tena juu yenu, wala juu ya familia yenu, hata watoto wa watoto wenu hadi kizazi cha tatu na cha nne.

29 Na halafu, kama atakuja juu yenu au watoto wenu, au watoto wa watoto wenu hadi wa kizazi cha tatu na cha nne, nimemtoa huyo adui yenu mikononi mwenu;

30 Na halafu kama wewe wataka kumwachia, utapewa thawabu kwa ajili ya uadilifu wako; na pia watoto wako na watoto wa watoto wako hata kizazi cha tatu na cha nne.

31 Hata hivyo, adui yako yu mikononi mwako; na kama wewe utamlipa kulingana na matendo yake utahesabiwa haki; kama amekuwa akitafuta uhai wako, naye anahatarisha maisha yako, adui yako huyo yu mikononi mwako nawe utahesabiwa haki.

32 Tazama, hii ndiyo sheria niliyoitoa kwa mtumishi wangu Nefi, na baba zenu, Yusufu, na Yakobo, na Isaka, na Ibrahimu, na manabii na mitume wangu wote wa kale.

33 Na tena, hii ndiyo sheria ambayo niliwapa watu wangu wa kale, kwamba wasiingie katika mapambano dhidi ya taifa lolote, kabila, lugha, au watu, isipokuwa Mimi, Bwana, nimewaamuru.

34 Na kama taifa lolote, ndimi au watu watatangaza vita dhidi yao, kwanza yawapasa kuinyanyua bendera ya amani kwa watu hao, taifa, au ndimi;

35 Na kama watu hao hawatakubali toleo la amani, au la pili wala la mara ya tatu, walete shuhuda hizi mbele za Bwana;

36 Ndipo Mimi, Bwana, nitawapa amri, na kuwahesabia wao haki katika kwenda vitani dhidi ya taifa, ndimi, au watu.

37 Na Mimi, Bwana, nitapigana vita vyao, na vita vya watoto wao, na watoto wa watoto wao, hadi wamelipa kisasi juu ya adui zao wote, kwenye kizazi cha tatu na cha nne;

38 Tazama, huu ni utaratibu kwa watu wote, asema Bwana Mungu wenu, ili kuhesabiwa haki mbele zangu.

39 Na tena, amini ninawaambia, ikiwa baada ya adui yenu kuja juu yenu mara ya kwanza, akatubu na kuja kwenu kuwaomba msamaha, nanyi mtamsamehe, na msitumie tena ushuhuda dhidi ya adui yenu—

40 Na kuendelea mara ya pili na ya tatu; na kila wakati adui yenu akitubu makosa ambayo amewakosea, ninyi msameheni, hata sabini mara saba.

41 Na kama akikukosea na hakutubu mara ya kwanza, hata hivyo wewe utamsamehe.

42 Na kama atakukosea tena mara ya pili, na hakutubu, hata hivyo wewe utamsamehe.

43 Na akikukosea tena mara ya tatu, na hakutubu, wewe umsamehe pia.

44 Lakini akikukosea tena mara ya nne wewe usimsamehe, bali utazileta shuhuda hizi mbele ya Bwana; na hazitafutwa hadi atakapotubu na kukulipa wewe mara nne katika mambo yote ambayo amekosa dhidi yako.

45 Na kama atafanya hivi, wewe utamsamehe kwa moyo wako wote; na kama hakufanya hivi, Mimi, Bwana, nitalipa kisasi kwa adui yako mara mia zaidi;

46 Na juu ya watoto wake, na juu ya watoto wa watoto wake wote wanaonichukia, hadi kizazi cha tatu na cha nne.

47 Lakini ikiwa watoto watatubu, au watoto wa watoto wake, na kumgeukia Bwana Mungu wao, kwa moyo wao wote na kwa uwezo, akili, na nguvu zao zote, na kurejesha mara-nne makosa yao yote waliyokukosea, au ambayo baba zao wamekukosea, au baba za baba zao, ndipo uchungu wa hasira yako utakoma;

48 Na kisasi hakitakuja tena juu yao, asema Bwana Mungu wako, na makosa yao hayataletwa tena kama ushuhuda dhidi yao mbele ya Bwana. Amina.