Sehemu ya 95
Ufunuo uliotolewa kupitia Joseph Smith Nabii, huko Kirtland, Ohio, 1 Juni 1833. Ufunuo huu ni mfululizo wa maelekezo matakatifu ya kujenga nyumba kwa ajili ya kuabudu na mafundisho nyumba ya Bwana (ona sehemu ya 88:119–136).
1–6, Watakatifu wanakemewa kwa kushindwa kwao kujenga nyumba ya Bwana; 7–10, Bwana anataka kuitumia nyumba Yake kwa kuwapa endaomenti watu Wake kwa uwezo utokao juu; 11–17, Nyumba hiyo iwekwe wakfu kama mahali pa kuabudu na kwa ajili ya shule ya Mitume.
1 Amini, hivyo ndivyo asemavyo Bwana kwenu ninyi ambao ninawapenda, na wale niwapendao pia huwarudi ili dhambi zao ziweze kusamehewa, kwani pamoja na kuwarudi ninawatayarishia njia kwa ajili ya ukombozi wao katika mambo yote yatokanayo na majaribu, na nimewapenda ninyi—
2 Kwa hiyo, ninyi yafaa kuwarudi na kukemewa mbele ya uso wangu;
3 Kwani ninyi mmenitendea dhambi kubwa, kwa sababu hamkuipa umuhimu amri ile iliyo kuu katika mambo yote, ambayo nimeitoa kwenu juu ya ujenzi wa nyumba yangu;
4 Kwa ajili ya matayarisho ambayo ninapanga kuwatayarisha mitume wangu kwa ajili ya kupogoa shamba langu la mizabibu kwa mara ya mwisho, ili nipate kulitimiza tendo langu la ajabu, ili niweze kumwaga Roho yangu juu ya watu wote—
5 Lakini tazama, amini ninawaambia, kwamba wako wengi waliotawazwa miongoni mwenu, ambao nimewaita lakini ni wachache kati yao walioteuliwa.
6 Wale ambao hawajateuliwa wametenda dhambi mbaya sana, kwa sababu wanatembea gizani saa sita mchana.
7 Na kwa sababu hii niliwapa ninyi amri ya kwamba yawapasa kuitisha kusanyiko lenu la kiroho, ili kufunga kwenu na kuomboleza kwenu kuweze kupaa juu masikioni mwa Bwana wa Sabato, ambaye kwa tafsiri, ni muumba wa siku ya kwanza, mwanzo na mwisho.
8 Ndiyo, amini ninawaambia, niliwapa amri ya kwamba mjenge nyumba, ambamo ndani ya nyumba hiyo ninapanga kuwapa endaomenti wale ambao nimewateua kwa uwezo utokao juu;
9 Kwani hii ndiyo ahadi ya Baba kwenu ninyi; kwa hiyo ninawaamuru ninyi kaeni humu, hata kama wale mitume wangu wa Yerusalemu.
10 Hata hivyo, watumishi wangu walitenda dhambi kubwa sana; na ushindani ulianza katika shule ya manabii; ambao yalikuwa ya kuhuzunisha kwangu, asema Bwana; kwa sababu hiyo, niliwatoa ili kuwarudi.
11 Amini ninawaambia, ni mapenzi yangu kuwa mjenge nyumba. Kama mtazishika amri zangu mtapata uwezo wa kuijenga.
12 Kama hamtazishika amri zangu, upendo wa Baba hautakuwamo ndani yenu, kwa hiyo mtatembea gizani.
13 Sasa hapa ndipo ilipo hekima, na mapenzi ya Bwana—nyumba na ijengwe, siyo kwa jinsi ya ulimwengu, kwani siwaruhusu ninyi kuishi kwa jinsi ya ulimwengu;
14 Kwa hiyo, na ijengwe kwa jinsi ambayo nitaionyesha kwa watatu kati yenu, ambao mtawachagua na kuwaweka katika mamlaka haya.
15 Na ukubwa wake utakuwa futi hamsini na tano katika upana, na iwe futi sitini na tano katika urefu, katika ukumbi wake wa ndani.
16 Na sehemu ya chini ya ukumbi wa ndani uwekwe wakfu kwangu kwa ajili ya sakramenti na matoleo, na kwa ajili ya kuhubiri kwenu, na kufunga kwenu, na kuomba kwenu, na kwa kunitolea matakwa yenu yaliyo matakatifu sana, asema Bwana wenu.
17 Na sehemu ya juu ya ukumbi wa ndani iwekwe wakfu kwangu kwa ajili ya shule ya mitume wangu, asema Mwana Amani; au, kwa maneno mengine, Alfa, au, kwa maneno mengine, Omega; hata Yesu Kristo Bwana wenu. Amina.