Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 7


Sehemu ya 7

Ufunuo uliotolewa kwa Joseph Smith Nabii na Oliver Cowdery, huko Harmony, Pennsylvania, Aprili 1829, wakati walipoulizia kupitia Urimu na Thumimu kama ikiwa Yohana, mwanafunzi kipenzi, alikuwa bado yu hai au amekufa. Ufunuo huu ni tafsiri ya masimulizi ya kumbukumbu iliyoandikwa na Yohana kwenye karatasi ya ngozi na kufichwa na yeye mwenyewe.

1–3, Yohana Kipenzi ataishi mpaka Bwana atakapokuja; 4–8, Petro, Yakobo na Yohana wanashikilia funguo za injili.

1 Na Bwana akaniambia: Yohana mpendwa wangu, wataka nini wewe? Kwani ukiomba kile utakachotaka, utapewa.

2 Na mimi nikamwambia: Bwana, nipe uwezo wa kushinda mauti, ili niweze kuishi na kuzileta nafsi nyingi kwako.

3 Na Bwana akaniambia: Amini, amini, ninakuambia, kwa sababu wewe umetaka hili na wewe utaishi mpaka nitakapokuja katika utukufu wangu, na utatoa unabii kwa mataifa, makabila, lugha na watu.

4 Na kwa sababu hii Bwana akamwambia Petro: Kama ninataka kwamba aishi mpaka nitakapokuja, hii ni nini kwako? Kwani anataka kwangu kwamba aweze kuzileta roho nyingi kwangu, lakini wewe watamani uje haraka katika ufalme wangu.

5 Ninakuambia wewe, Petro, hii ilikuwa ni tamaa iliyo njema; lakini mpendwa wangu ametamani kwamba aweze kufanya zaidi, au kazi kubwa zaidi miongoni mwa wanadamu kuliko alivyofanya awali.

6 Ndiyo, amekubali kazi kubwa zaidi; hivyo basi nitamfanya yeye kuwa kama moto unaowaka na malaika mhudumu; atawahudumia wale watakaokuwa warithi wa wokovu waishio duniani.

7 Na nitakufanya wewe kuwa mhudumu wake na kwa ndugu yako Yakobo; na kwenu ninyi watatu nitawapa mamlaka haya na funguo za huduma hii mpaka nitakapokuja.

8 Amini ninawaambia ninyi, mtapata kila mtu kulingana na matakwa yenu, kwani ninyi nyote mnajawa shangwe katika yale mnayoyataka.