Sehemu ya 28
Ufunuo uliotolewa kupitia Joseph Smith Nabii kwa Oliver Cowdery, huko Fayette, New York, Septemba 1830. Hiram Page, muumini wa Kanisa, alikuwa na jiwe fulani na kudai kuwa kunapokea mafunuo kwa msaada wa jiwe hilo kuhusiana na ujenzi wa Sayuni na taratibu za Kanisa. Waumini kadhaa walikuwa wamedanganyika kwa madai haya, na hata Oliver Cowdery alishawishika vibaya kwa hilo. Muda mfupi kabla ya mkutano, Nabii alimwuliza Bwana kwa bidii kuhusiana na jambo hili, na ufunuo huu ulifuata.
1–7, Joseph Smith hushikilia funguo za siri, na ndiye pekee mwenye kupokea ufunuo kwa Kanisa; 8–10, Oliver Cowdery anapaswa kwenda kuwafundisha Walamani; 11–16, Shetani alimdanganya Hiram Page na kumpa mafunuo ya uongo.
1 Tazama, ninakuambia wewe, Oliver, kwamba itatolewa kwako kwamba utasikilizwa na kanisa katika mambo yote ambayo wewe utawafundisha kwa uwezo wa Mfariji, kuhusu mafunuo na amri ambazo nimezitoa.
2 Lakini tazama, amini, amini, ninakuambia, hakuna mtu atakayeteuliwa kupokea amri na mafunuo katika kanisa hili isipokuwa mtumishi wangu Joseph Smith, Mdogo, kwani yeye huzipokea kama vile Musa.
3 Na wewe uwe mtiifu kwa mambo ambayo nitampa yeye, kama vile Haruni, kuzitangaza kiuaminifu amri hizi na mafunuo, kwa nguvu na mamlaka kwenyea kanisa.
4 Na endapo wewe utaongozwa kwa wakati wowote na Mfariji kuzungumza au kufundisha, au kwa nyakati zote kwa njia ya amri kwa kanisa, waweza kufanya hivyo.
5 Lakini usiliandike kwa njia ya amri, bali kwa hekima;
6 Na wewe usimwamuru yeyote aliye juu yako, na juu ya kanisa;
7 Kwani Mimi nimempa yeye kuzungumza funguo za siri, na mafunuo ambayo yamefungwa, hadi hapo nitakapomteua mwingine kwa ajili yao badala yake.
8 Na sasa, tazama, ninakuambia kwamba utakwenda kwa Walamani na kuhubiri injili yangu kwao; na kadiri wao watakavyopokea mafundisho yako na wewe utalifanya kanisa langu kuanzishwa miongoni mwao; na wewe utapata mafunuo, walakini usiyaandike kwa njia ya amri.
9 Na sasa, tazama, ninakuambia kwamba haijafunuliwa bado, na hakuna mtu ajuaye mahali mji wa Sayuni utakapojengwa, lakini itatolewa hapo baadaye. Tazama, ninakuambia kwamba itakuwa mipakani mwa Walamani.
10 Na wewe usiondoke mahali hapa mpaka baada ya mkutano, na mtumishi wangu Joseph Smith atateuliwa kuongoza mkutano huo kwa sauti ya mkutano na atakalolisema kwako na wewe utalisema.
11 Na tena, wewe utamchukua ndugu yako Hiram Page, kati yake na wewe peke yenu, na umwambie kwamba yale mambo aliyoyaandika kutoka kwenye jiwe lile siyo yangu na kwamba Shetani anamdanganya;
12 Kwani, tazama, mambo haya hayakuchaguliwa kwake, wala hakuna lolote lililoteuliwa kwa yeyote katika kanisa hili kinyume na maagano ya kanisa.
13 Kwani mambo yote, lazima yafanyike katika utaratibu, na kwa ridhaa ya wengi katika kanisa, na kwa sala ya imani.
14 Na wewe utasaidia kurekebisha mambo haya yote, kulingana na maagano ya kanisa, kabla ya kufanya safari yako miongoni mwa Walamani.
15 Na itatolewa kwako tangu wakati utakapoondoka, hadi wakati utakaporejea, juu ya nini utakachofanya.
16 Na wewe utafumbua kinywa chako nyakati zote, ukitangaza injili yangu kwa sauti ya kufurahi. Amina.