Sehemu ya 100
Ufunuo uliotolewa kwa Joseph Smith Nabii na Sidney Rigdon, huko Perrysburg, New York, tarehe 12Â Oktoba 1833. Ndugu hawa wawili, wakiwa mbali na familia zao kwa siku kadhaa, walipatwa na wasi wasi juu yao.
1–4, Joseph na Sidney watahubiri injili kwa ajili ya wokovu wa wanadamu; 5–8, Watapewa saa ile watakayosema; 9–12, Sidney atakuwa msemaji na Joseph atakuwa mfunuzi na mwenye nguvu katika ushuhuda; 13–17, Bwana atawainua watu safi, na watiifu wataokolewa.
1 Amini, hivyo ndivyo asemavyo Bwana kwenu, marafiki zangu Sidney na Joseph, familia zenu ni njema; wako mikononi mwangu, na nitawafanyia nionavyo kuwa ni vyema; kwani ndani yangu kuna uwezo wote.
2 Kwa hiyo, nifuateni, na sikilizeni ushauri nitakaowapa.
3 Tazama, na lo, ninao watu wengi katika eneo hili, katika maeneo ya jirani; na mlango wenye kuleta matokeo yanayotakiwa wakufaa utafunguliwa katika maeneo ya jirani katika nchi za mashariki.
4 Kwa hiyo, Mimi, Bwana, nimewaruhusu ninyi kuja mahali hapa; hivyo niliona ni muhimu kwa wokovu wa wanadamu.
5 Kwa hiyo, amini ninawaambia, pazeni sauti zenu kwa watu hawa; yasemeni mawazo nitakayoyaweka mioyoni mwenu, na ninyi hamtashindwa mbele za watu;
6 Kwani mtapewa katika saa ile ile, ndiyo, katika wakati ule ule, kile mtakachosema.
7 Lakini amri ninaitoa kwenu, kwamba mtakitangaza kitu chochote mtakachotangaza kwa jina langu, kwa taadhima moyoni, kwa roho ya unyenyekevu, katika mambo yote.
8 Na ninatoa ahadi hii kwenu, ya kuwa ilimradi mtayatenda haya Roho Mtakatifu atamwagwa katika kutoa ushuhuda kwa mambo yote mtakayosema ninyi.
9 Na ni muhimu kwangu kwamba wewe, mtumishi wangu Sidney, uwe msemaji kwa watu hawa; ndiyo, amini, nitakutawaza kwa wito huu, hata kuwa msemaji kwa mtumishi wangu Joseph.
10 Nami nitampa yeye uwezo wa kuwa mwenye nguvu katika ushuhuda.
11 Na nitakupa wewe uwezo wa kuwa mwenye nguvu katika kuyaelezea maandiko yote, ili wewe uwe msemaji kwake, naye atakuwa mfunuzi kwako, ili uweze kujua uhakika wa mambo yote yahusuyo mambo ya ufalme hapa duniani.
12 Kwa hiyo, endeleeni na safari yenu na mioyo yenu ifurahi; kwani tazameni, na lo, Mimi nipo pamoja nanyi hadi mwisho.
13 Na sasa ninawapa neno juu ya Sayuni. Sayuni itakombolewa, ingawa yeye anatiwa adabu kwa kipindi kifupi.
14 Ndugu zenu, watumishi wangu Orson Hyde na John Gould, wako mikononi mwangu; na ilimradi wao wanazishika amri zangu wataokolewa.
15 Kwa hiyo, mioyo yenu na ifarijike; kwani mambo yote yatafanya kazi kwa pamoja kwa manufaa yao wale watembeao wima, na kwa utakaso wa kanisa
16 Kwani nitajiinulia watu safi, ambao watanitumikia katika haki.
17 Na wale wote walilingao jina la Bwana, na kuzishika amri zake, wataokolewa. Hivyo ndivyo. Amina.