Maandiko Matakatifu
Utangulizi


Utangulizi

Mafundisho na Maagano ni mkusanyiko wa mafunuo matakatifu na maazimio ya kuongozwa na Mungu yaliyotolewa kwa ajili ya kuanzisha na kusimamia ufalme wa Mungu hapa duniani katika siku hizi za mwisho. Ingawa kwa sehemu kubwa yamelengwa kwa waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, ujumbe, maonyo, na ushawishi ni kwa faida ya wanadamu wote na hufanya mwaliko kwa wanadamu wote kila mahali kuisikiliza sauti ya Bwana Yesu Kristo, ikisema nao kwa ajili ya ustawi wao wa kimwili na wokovu wao usio na mwisho.

Sehemu kubwa ya mafunuo katika mkusanyiko huu yalipokelewa kupitia Joseph Smith Mdogo, nabii wa kwanza, na rais wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Mengine yalitolewa kupitia baadhi ya warithi wake katika Urais (ona vichwa vya habari vya M&M 135, 136, na 138, na Matamko Rasmi 1 na 2).

Kitabu cha Mafundisho na Maagano ni moja ya Vitabu Vitakatifu vya Kanisa kwa pamoja na Biblia Takatifu, Kitabu cha Mormoni, na Lulu ya Thamani Kuu. Hata hivyo, Mafundisho na Maagano ni cha kipekee kwa sababu siyo tafsiri ya waraka wa kale, bali ni cha asili ya kisasa na kimetolewa na Mungu kupitia manabii Wake watende kwa ajili ya urejesho wa kazi Yake takatifu na kwa uanzishaji wa ufalme wa Mungu humu duniani katika siku hizi. Katika mafunuo, mtu husikia sauti ya upole lakini iliyo imara ya Bwana Yesu Kristo; akisema upya katika kipindi cha utimilifu wa nyakati; na kazi ambayo imeanzishwa ndani yake ni matayarisho kwa Ujio Wake wa pili, katika utimilifu na ulinganifu wa maneno ya manabii wote watakatifu tokea mwanzo wa ulimwengu.

Joseph Smith Mdogo alizaliwa 23 Desemba 1805, huko Sharon, Wilaya ya Windsor, Vermont. Wakati wa maisha yake ya mwanzoni, yeye pamoja na familia yake walihamia Manchester, magharibi ya New York kama ijulikanavyo hii leo. Ilikuwa wakati alipokuwa akiishi huko katika majira ya kuchipua ya mwaka 1820, alipokuwa na umri wa miaka kumi na minne, kwamba alipata ono lake la kwanza, katika ono hilo alitembelewa na Mungu, Baba wa Milele, na Mwanawe Yesu Kristo. Alielezwa katika ono hili kwamba Kanisa la kweli la Yesu Kristo ambalo lilianzishwa nyakati za Agano Jipya, na ambalo lilifundisha utimilifu wa injili, halikuwepo tena duniani. Maono mengine matakatifu yalifuata ambamo malaika wengi walimfundisha; ilioneshwa kwake kwamba Mungu alikuwa na kazi muhimu ya yeye kuifanya hapa duniani, na kwamba kupitia yeye Kanisa la Yesu Kristo litarejeshwa duniani.

Baada ya muda, Joseph Smith aliwezeshwa kwa msaada mtakatifu kutafsiri na kuchapisha Kitabu cha Mormoni. Wakati huu yeye na Oliver Cowdery walitawazwa katika Ukuhani wa Haruni na Yohana Mbatizaji mnamo Mei 1829 (ona M&M 13), na muda mfupi baadaye pia walitawazwa kwenye Ukuhani wa Melkizedeki na Mitume wa zamani Petro, Yakobo, na Yohana (ona M&M 27:12). Kutawazwa kwingine kulifuatia ambako funguo za ukuhani zilitolewa na Musa, Eliya, Elia, na manabii wengi wa kale (ona M&M 110; 128:18, 21). Kutawazwa huku kulikuwa, kwa kweli, ni urejesho wa mamlaka takatifu kwa mwanadamu duniani. Mnamo 6 Aprili 1830, chini ya maelekezo ya mbingu, Nabii Joseph Smith alilianzisha Kanisa, na hivyo Kanisa la kweli la Yesu Kristo kwa mara nyingine tena likifanya kazi kama taasisi miongoni mwa wanadamu, likiwa na mamlaka ya kufundisha injili na kutoa ibada za wokovu. (Ona M&M 20 na Lulu ya Thamani Kuu, Joseph Smith—Historia ya 1.)

Mafunuo haya matakatifu yalikuwa yakipokelewa kama majibu ya sala, wakati wa shida, na zilijitokeza katika hali halisi za maisha zikiwahusisha watu halisi. Nabii na washirika wake walitafuta mwongozo mtakatifu, na funuo hizi zilithibitisha kwamba walipokea. Katika mafunuo, mtu huona urejesho na kufichuliwa kwa injili ya Yesu Kristo na kuingia kwa kipindi cha utimilifu wa nyakati. Kuhama kwa Kanisa kutoka New York na Pennsylvania kwenda Ohio, kwenda Missouri, kwenda Illinois, na hatimaye Bonde Kuu la Marekani ya magharibi na jitihada kubwa za Watakatifu katika kujaribu kujenga Sayuni hapa duniani katika nyakati za kisasa pia hujitokeza katika mafunuo haya.

Sehemu kadhaa za mwanzo zinahusiana na mambo yanayohusu tafsiri na uchapishaji wa Kitabu cha Mormoni (ona sehemu ya 3, 5, 10, 17, na 19). Baadhi ya sehemu za mwishoni zinaonyesha kazi ya Nabii Joseph Smith katika kufanya tafsiri ya Biblia, kipindi ambacho sehemu za mafundisho muhimu zilipokelewa (ona, kwa mfano, sehemu ya 37, 45, 73, 76, 77, 86, 91, na 132, ambazo kila moja ina uhusiano wa moja kwa moja na tafsiri ya Biblia).

Katika mafunuo, mafundisho ya injili yanatangazwa pamoja na maelezo juu ya mambo muhimu kama vile asili ya Uungu, mwanzo wa mwanadamu, ukweli juu ya kuwepo kwa Shetani, madhumuni ya kuishi hapa duniani, umuhimu wa utii, haja ya toba, utendaji kazi wa Roho Mtakatifu, ibada na matendo yanayohusiana na wokovu, hatima ya dunia, hali ya baadaye ya mwanadamu baada ya Ufufuko na Hukumu, umilele wa uhusiano wa ndoa, na asili ya milele ya familia. Vivyo hivyo, kufunuliwa pole pole kwa muundo wa usimamizi wa Kanisa unaonyeshwa kwa njia ya kuitwa kwa maaskofu, Urais wa Kwanza, Baraza la Mitume Kumi na Wawili, na Sabini, na kuanzishwa kwa ofisi simamizi zingine za uongozi na akidi. Mwishoni, ushuhuda ambao unatolewa juu ya Yesu Kristo—uungu Wake, utukufu Wake, ukamilifu Wake, upendo Wake, na uwezo Wake wa kukomboa—hufanya kitabu hiki kuwa cha thamani kubwa kwa familia ya mwanadamu na kuwa cha “thamani kwa Kanisa kuliko utajiri wa dunia yote” (ona kichwa cha habari kwa M&M 70).

Mafunuo haya awali yaliandikwa na waandishi wa Joseph Smith, na waumini wa Kanisa kwa shauku walishirikiana nakala za kuandikwa kwa mkono. Ili kutengeneza kumbukumbu ya kudumu, waandishi mara moja wakanakili mafunuo haya katika mswada kama kitabu cha kumbukumbu, ambacho viongozi wa Kanisa walikitumia katika kuyatayarisha mafunuo haya ili yapigwe chapa. Joseph Smith na watakatifu wa mwanzoni waliyaangalia mafunuo haya kama vile walivyokuwa wakiliangalia Kanisa: yenye uhai, yenye nguvu, na yanayoweza kuboreshwa kwa nyongeza ya ufunuo. Pia walitambua kwamba makosa yasiyo kusudiwa yawezekana kuwa yametokea katika mchakato wa kunakili mafunuo na kuyatayarishwa kwa uchapishaji. Kwa sababu hiyo, mkutano wa Kanisa ulimwomba Joseph Smith katika mwaka 1831 “kusahihisha upotofu au makosa hayo ambayo yawezekana akayagundua kwa njia ya Roho Mtakatifu”.

Baada ya mafunuo haya kufanyiwa marejeo na kusahihishwa, waumini wa Kanisa katika Missouri wakaanza kupiga chapa kitabu kilichoitwa A Book of Commandments for the Government of the Church of Christ (Kitabu cha Amri kwa ajili ya Kuongoza Kanisa la Kristo), ambacho kilikuwa na mafunuo mengi ya awali ya Nabii. Hata hivyo, jaribio hili la kwanza la kuchapisha mafunuo lilikwama, wakati kikundi cha wahuni kilipoharibu ofisi ya Watakatifu ya kupiga chapa huko Wilaya ya Jackson mnamo 20 Julai 1833.

Baada ya kusikia juu ya uharibifu wa ofisi ya kupiga chapa huko Missouri, Joseph Smith na viongozi wengine wa Kanisa wakaanza maandalizi ya kuchapisha mafunuo haya huko Kirtland, Ohio. Ili tena kusahihisha makosa, na ufafanuzi wa maneno, na kwa kutambua maendeleo katika Kanisa mafundisho na muundo, Joseph Smith alisimamia kazi ya kuhariri maneno ya baadhi ya mafunuo ili kuyaandaa kwa ajili ya uchapaji katika mwaka wa 1835 kama Doctrine and Covenants of the Church of the Latter Day Saints (Mafundisho na Maagano ya Kanisa la Watakatifu wa Siku za Mwisho). Joseph Smith aliidhinisha toleo jingine la Mafundisho na Maagano, ambalo lilichapishwa miezi michache tu baada ya kifo cha kishahidi cha Nabii mwaka 1844.

Watakatifu wa Siku za Mwisho wa mwanzoni kabisa waliyathamini mafunuo haya na kuyatazama kama vile ni ujumbe kutoka kwa Mungu. Katika tukio moja mwishoni mwa mwaka 1831, wazee kadhaa wa Kanisa walitoa ushuhuda wa dhati kwamba Bwana amezishuhudia nafsi zao juu ya ukweli wa mafunuo hayo. Ushuhuda huu ulichapishwa katika toleo la mwaka 1835 la Mafundisho na Maagano kama ushuhuda wa kimaandishi wa Mitume Kumi na Wawili:

Ushuhuda wa
Mitume Kumi na Wawili Juu ya Ukweli
wa Kitabu cha Mafundisho na Maagano

Ushuhuda wa Mashahidi juu ya Kitabu cha Amri za Bwana, amri ambazo alizitoa kwa Kanisa lake kupitia Joseph Smith, Mdogo, ambaye aliteuliwa kwa sauti ya Kanisa kwa dhumuni hili:

Kwa hiyo, sisi, tupo radhi kutoa ushuhuda kwa ulimwengu wa wanadamu wote, kwa kila kiumbe kilicho juu ya uso wa dunia, kwamba Bwana ametushuhudia nafsini mwetu, kupitia Roho Mtakatifu aliyemwagwa juu yetu, kwamba amri hizi zilitolewa kwa maongozi ya Mungu, na ni kwa manufaa ya watu wote na amini ni za kweli.

Sisi tunatoa ushuhuda huu kwa ulimwengu, Bwana akiwa msaidizi wetu; na ni kwa neema za Mungu Baba, na Mwana Wake, Yesu Kristo, kwamba sisi tumeruhusiwa kupata nafasi hii ya kutoa ushuhuda huu kwa ulimwengu, nafasi ambayo tunaifurahia kupita kiasi, tukimwomba Bwana daima kwamba kwa hicho wanadamu waweze kufaidika.

Majina ya Mitume Kumi na Wawili yalikuwa:

 • Thomas B. Marsh

 • David W. Patten

 • Brigham Young

 • Heber C. Kimball

 • Orson Hyde

 • William E. McLellin

 • Parley P. Pratt

 • Luke S. Johnson

 • William Smith

 • Orson Pratt

 • John F. Boynton

 • Lyman E. Johnson

Katika mfululizo wa matoleo ya Mafundisho na Maagano, mafunuo ya nyongeza au mambo mengine muhimu yameongezwa, kama yalivyopokelewa, na kama yalivyo kubaliwa na mikusanyiko au mikutano yenye mamlaka ya Kanisa. Toleo la 1876, lililo tayarishwa na Mzee Orson Pratt chini ya maelekezo ya Bringham Young, akiyapanga mafunuo katika utaratibu wa wendo na kuyapa upya vichwa vya habari pamoja na utangulizi wa kihistoria.

Kuanzia toleo la mwaka 1835, mfululizo wa masomo saba ya teolojia pia yaliingizwa ndani; haya yalipewa jina la Lectures on Faith (Mihadhara juu ya Imani). Haya yalikuwa yametayarishwa kwa matumizi katika Shule ya Manabii huko Kirtland, Ohio, kutoka mwaka 1834 hadi 1835. Ingawa ni ya manufaa kwa ajili ya mafundisho na maelekezo, mihadhara hii imeondolewa kutoka kwenye Mafundisho na Maagano tangu toleo la mwaka 1921 kwa sababu hayakuwa yametolewa kama mafunuo kwa Kanisa zima.

Katika toleo la mwaka wa 1981 la Kiingereza la Mafundisho na Maagano, nyaraka tatu ziliingizwa kwa mara ya kwanza. Hizi ni sehemu ya sehemu ya 137 na 138, zikiweka misingi ya wokovu kwa ajili ya wafu; na Tamko Rasmi 2, linalotangaza kwamba waumini wa Kanisa wanaume wote wenye kustahili wanaweza kutawazwa kwenye ukuhani bila kujali asili au rangi.

Kila toleo jipya la Mafundisho na Maagano limesahihisha makosa yaliyopita na kuongeza taarifa mpya, hususani katika eneo la vichwa vya habari vya sehemu. Toleo la sasa linaboresha zaidi tarehe na majina ya mahali na kufanya masahihisho mengine. Mabadiliko haya yamefanyika ili kuleta taarifa hizi katika ulinganifu na taarifa za kihistoria zilizo sahihi zaidi. Sehemu nyingine muhimu za toleo hili la mwisho ni pamoja na ramani zilizo sahihishwa zikionyesha maeneo muhimu kijiografia ambako mafunuo haya yalipokelewa, pamoja na picha iliyoboreshwa ya picha iliyoboreshwa ya maeneo ya kihistoria katika Kanisa, marejeo, vichwa vya habari vya sehemu, na ufupisho wa mada, yote yakiwa yameundwa ili kumsaidia msomajikuelewa na kufurahia katika ujumbe wa Bwana kama ulivyotolewa katika Mafundisho na Maagano. Taarifa kwa ajili ya vichwa vya habari vya sehemu zimechukuliwa kutoka kwenye Muswada wa Historia ya Kanisa na History of the Church (Historia ya Kanisa) iliyochapishwa (kwa pamoja zimeitwa katika vichwa vya habari kama historia ya Joseph Smith) na Joseph Smith Papers (Karatasi za Joseph Smith).