Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 57


Sehemu ya 57

Ufunuo uliotolewa kupitia Joseph Smith Nabii, huko Sayuni, katika Wilaya ya Jackson, Missouri, 20 Julai 1831. Katika kutii amri za Bwana ya kusafiri kwenda Missouri, mahali ambapo atafunua “ardhi ya urithi wenu” (sehemu ya 52), wazee walisafiri kutoka Kirtland hadi mpaka wa upande wa magharibi wa Missouri. Joseph Smith alitafakari juu ya hali ya Walamani na akishangaa: “Ni lini nyika itachanua kama waridi? Ni lini Sayuni itajengwa katika utukufu wake, na ni wapi hekalu Lako litasimama, ambako mataifa yote yatakuja katika siku za mwisho?” Baada ya hayo alipokea ufunuo huu.

1–3, Independence, Missouri, ndiyo mahali pa Jiji la Sayuni na pa hekalu; 4–7, Watakatifu watanunua ardhi na kupokea urithi katika eneo lile; 8–16, Sidney Gilbert ataanzisha stoo, William W. Phelps atakuwa mchapaji, na Oliver Cowdery atakariri maandiko kwa ajili ya uchapaji.

1 Sikilizeni, Enyi wazee wa kanisa langu, asema Bwana Mungu wenu, ninyi mliojikusanya pamoja, kulingana na amri zangu, katika nchi hii, ambayo ni nchi ya Missouri, nchi ambayo nimeiteua na kuiweka wakfu kwa ajili ya kukusanyika watakatifu.

2 Kwa hiyo, hii ni nchi ya ahadi, na mahali pa mji wa Sayuni.

3 Na hivyo ndivyo asemavyo Bwana Mungu wenu, kama mnataka hekima hapa ndipo penye hekima. Tazama, mahali ambapo sasa panaitwa Independence ni katikati, na eneo kwa ajili ya hekalu linalala upande wa magharibi, kwenye kiwanja ambacho hakiko mbali na nyumba ya mahakama.

4 Kwa hiyo, ni hekima ardhi hiyo inunuliwe na watakatifu, na kila ardhi iliyoko upande wa magharibi, hadi kwenye mpaka kati ya Myahudi na Myunani;

5 Na pia kila ardhi inayopakana na mbuga pana, kadiri wanafunzi wangu watakavyowezeshwa kununua ardhi. Tazama, hii ni hekima, kwamba waweze kuipata kwa ajili ya urithi usio na mwisho.

6 Na mtumishi wangu Sidney Gilbert asimame katika ofisi ambayo nilimteua, kupokea fedha, kuwa wakala kwa kanisa, kwa kununua ardhi katika maeneo yote ya karibu, kadiri itakavyoweza kufanyika katika haki, na kama hekima itakavyoelekeza.

7 Na mtumishi wangu Edward Partridge asimame katika ofisi ambayo nimemteua, na agawe kwa watakatifu urithi wao, kama vile nilivyoamuru; na pia wale aliowateua kumsaidia.

8 Na tena, amini ninawaambia, na mtumishi wangu Sidney Gilbert ajipandikize mwenyewe katika mahali hapa, na kuanzisha duka, ili aweze kuuza mali kwa uaminifu, ili aweze kupata fedha za kununua ardhi kwa ajili ya watakatifu, na ili aweze kupata vitu vingine ambavyo wanafunzi watahitaji kupanda katika urithi wao.

9 Na pia mtumishi wangu Sidney Gilbert apate leseni—tazama hapa ndipo penye hekima, na yeyote asomaye na afahamu—ili aweze kutuma mali pia kwa watu, hata kwa amtakaye kumwajiri kama karani katika huduma yake;

10 Na hivyo kuwahudumia watakatifu wangu, ili injili yangu iweze kuhubiriwa kwa wale wakaao gizani na katika maeneo ya uvuli wa mauti.

11 Na tena, amini ninawaambia, na mtumishi wangu William W. Phelps awekwe katika mahali hapa, na afanywe kuwa mchapaji wa kanisa.

12 Na lo, kama ulimwengu utayapokea maandiko yake—tazama hii ndiyo hekima—na apate kila awezacho kupata katika haki, kwa faida ya watakatifu.

13 Na mtumishi wangu Oliver Cowdery amsaidie, hata kama vile nilivyo waamuru, katika mahali popote nitakapopateua kwa ajili yake, kunakili, na kusahihisha, na kuchagua, ili mambo yote yaweze kuwa sahihi mbele zangu, kulingana na Roho atakavyoidhinisha kupitia yeye.

14 Na hivyo basi wale ambao nimewazungumza na wawekwe katika nchi hii ya Sayuni, kwa haraka iwezekanavyo, pamoja na familia zao, kufanya mambo yale kama nilivyoyanena.

15 Na sasa juu ya kukusanyika—Askofu na wakala wafanye matayarisho kwa ajili ya familia zilizoamriwa kuja katika nchi hii, upesi iwezekanavyo, na kuwaweka katika urithi wao.

16 Na kwa mabaki ya wote wazee na waumini maelekezo zaidi yatatolewa hapo baadaye. Hivyo ndivyo. Amina.