Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 87


Sehemu ya 87

Ufunuo na unabii juu ya vita, uliotolewa kupitia Joseph Smith Nabii huko, au jirani na Kirtland, Ohio, 25 Desemba 1832. Wakati huu migogoro katika Marekani juu ya utumwa na Carolina ya Kusini kufuta kodi ya serikali kuu ilikuwa imeenea. Historia ya Joseph Smith inaeleza kwamba “mwonekano wa matatizo miongoni mwa mataifa” ilikuwa wazi zaidi kwa Nabii “kuliko hapo awali ilivyokuwa tangu Kanisa lianze safari yake kutoka nyikani.”

1–4, Vita vyatabiriwa kati ya Majimbo ya Kaskazini na Majimbo ya Kusini; 5–8, Majanga makubwa yatawaangukia wakazi wote wa dunia.

1 Amini, hivyo ndivyo asemavyo Bwana kuhusu vita ambavyo karibu vitatokea, kuanzia kwenye uasi wa Carolina ya Kusini, ambao hatimaye utaishia katika vifo na huzuni kwa watu wengi;

2 Na wakati utakuja ambao vita vitamwagika juu ya mataifa yote, kuanzia mahali hapa.

3 Kwani tazama, Majimbo ya Kusini yatagawanyika dhidi ya Majimbo ya Kaskazini, na Majimbo ya Kusini yatayaita mataifa mengine, hata taifa la Uingereza, kama linavyoitwa, na pia watayaita mataifa mengine, ili kujilinda wenyewe dhidi ya mataifa mengine; na ndipo vita vitamwagwa juu ya mataifa yote.

4 Na itakuwa, baada ya siku nyingi, watumwa watainuka dhidi ya mabwana wao, ambao wataandaliwa na kufundishwa kwa ajili ya vita.

5 Na itakuwa pia mabaki ya waliosalia katika nchi watajipanga wenyewe, na watakuwa wakali kupita kiasi, na watawaudhi Wayunani kwa maudhi makali.

6 Na hivyo, kwa upanga na kwa umwagaji damu wakazi wa dunia wataomboleza; na kwa njaa, na magonjwa, na matetemeko, na kwa ngurumo ya mbinguni, na radi kali ingʼarayo pia, wakazi wa dunia watafanywa waisikie ghadhabu, na uchungu wa hasira, na mkono wa adhabu wa Mwenyezi Mungu, hadi kuangamizwa kuliko kusudiwa kumeyakomesha mataifa yote;

7 Kwamba kilio cha watakatifu, na cha damu ya watakatifu, kitakoma kuja katika masikio ya Bwana wa Sabato, kutoka duniani, kulipiza kisasi kwa adui zao.

8 Kwa hiyo, simameni katika mahali pa takatifu, na wala msiondoshwe, hadi siku ya Bwana itapofika; kwani tazama, yaja haraka, asema Bwana. Amina.