Mlango wa 6
(Novemba–Desemba 1830)
Uzao wa Adamu watunza kitabu cha ukumbusho—Uzao wake wenye haki wahubiri toba—Mungu Anajionyesha mwenyewe kwa Henoko—Henoko anahubiri injili—Mpango wa wokovu ulifunuliwa kwa Adamu—Alipokea ubatizo na ukuhani.
1 Na Adamu alisikiliza sauti ya Bwana Mungu, naye akawasihi wanawe kutubu.
2 Naye Adamu akamjua mke wake tena, naye akamzaa mwana, na akamwita jina lake Sethi. Na Adamu akalitukuza jina la Mungu; kwa maana yeye alisema: Mungu ameniwekea uzao mwingine, mahali pa Habili, ambaye Kaini alimwua.
3 Na Mungu akajidhihirisha mwenyewe kwa Sethi, naye hakuasi, bali akamtolea dhabihu ya kukubalika, kama ile ya ndugu yake Habili. Na kwake pia alizaliwa mwana wa kiume, naye akamwita jina lake Enoshi.
4 Na halafu watu hawa wakaanza kulilingana jina la Bwana, na Bwana akawabariki;
5 Na kitabu cha ukumbusho kikaandikwa, ambamo ndani yake kuliandikwa, katika lugha ya Adamu, kwa maana ilitolewa kwa wengi kwa kadiri walivyomlingana Mungu kuandika kwa roho wa mwongozo;
6 Na kupitia wao watoto wao walifundishwa kusoma na kuandika, wakiwa na lugha iliyokuwa safi na isiyochafuliwa.
7 Sasa Ukuhani huu huu, ambao ulikuwepo mwanzoni, utakuwepo mwisho wa ulimwengu pia.
8 Sasa unabii huu Adamu aliusema, kama alivyoongozwa na Roho Mtakatifu, na historia ya nasaba ya watoto wa Mungu iliandikwa. Na hiki kilikuwa kitabu cha vizazi vya Adamu, kikisema: Katika siku ile ambayo Mungu alipoumba mtu, kwa mfano wa Mungu alimuumba;
9 Katika mfano wa mwili wake yeye mwenyewe, aliwaumba mwanaume na mwanamke, na akawabariki, na kuwaita majina yao Adamu, katika siku ile waliyoumbwa na kuwa nafsi hai katika nchi iliyo mahali pa Mungu pa kuwekea miguu.
10 Na Adamu aliishi miaka mia moja na thelathini, na akamzaa mwana kwa sura yake, kwa mfano wake, akamwita jina lake Sethi.
11 Na siku za Adamu, baada ya kumzaa Sethi, zilikuwa miaka mia nane, na akazaa wana na mabinti wengi;
12 Na siku zote za Adamu alizoishi zilikuwa miaka mia tisa na thelathini, naye akafa.
13 Sethi akaishi miaka mia na mitano, naye akamzaa Enoshi, naye akatoa unabii katika siku zake zote, na kumfundisha mwanawe Enoshi njia za Mungu; kwa sababu hiyo Enoshi pia naye alitoa unabii.
14 Na Sethi aliishi, baada ya kumzaa Enoshi, miaka mia nane na saba, naye akazaa wana na mabinti wengi.
15 Na wanadamu wakawa wengi juu ya uso wa nchi. Na katika siku hizo Shetani alikuwa na utawala mkubwa miongoni mwa watu, na alighadhibika mioyoni mwao; na kutoka hapo vikazuka vita na umwagaji wa damu; na mkono wa mtu ukawa dhidi ya ndugu yake mwenyewe, katika kumletea mauti, kwa sababu ya matendo ya siri, wakitafuta mamlaka.
16 Siku zote za Sethi zilikuwa miaka mia tisa kumi na miwili, naye akafa.
17 Na Enoshi aliishi miaka tisini, na akamzaa Kanaani. Na Enoshi na mabaki ya watu wa Mungu wakatoka katika nchi hiyo, iliyoitwa Shuloni, nao wakaishi katika nchi ya ahadi, ambayo aliiita kwa jina la mwanawe mwenyewe, ambaye alimwita Kanaani.
18 Na Enoshi aliishi, baada ya kumzaa Kanaani, miaka mia nane na kumi na mitano, na akazaa wana na mabinti wengi. Na siku zote za Enoshi zilikuwa miaka mia tisa na mitano, naye akafa.
19 Naye Kanaani aliishi miaka sabini, na akamzaa Mahalaleli; na Kanaani aliishi baada ya kumzaa Mahalaleli miaka mia nane na arobaini, na akazaa wana na mabinti. Na siku zote za Kanaani zilikuwa miaka mia tisa na kumi, naye akafa.
20 Na Mahalaleli aliishi miaka sitini na mitano, naye akamzaa Yaredi; na Mahalaleli aliishi, baada ya kumzaa Yaredi, miaka mia nane na thelathini, na akazaa wana na mabinti. Na siku zote za Mahalaleli zilikuwa mia nane na tisini na tano, naye akafa.
21 Na Yaredi aliishi miaka mia na sitini na miwili, naye akamzaa Henoko; na Yaredi aliishi, baada ya kumzaa Henoko, miaka mia nane, na akazaa wana na mabinti. Na Yaredi alimfundisha Henoko katika njia zote za Mungu.
22 Na hii ni nasaba ya wana wa Adamu, aliyekuwa mwana wa Mungu, ambaye Mungu, mwenyewe, alizungumza naye.
23 Nao walikuwa wahubiri wa haki, na walinena na kutoa unabii, na wakiwaitia watu wote, kila mahali, kutubu; na imani ilifundishwa kwa wanadamu.
24 Na ikawa kwamba siku zote za Yaredi zilikuwa mia tisa na sitini na miwili, naye akafa.
25 Na Henoko aliishi miaka sitini na mitano, na akamzaa Methusela.
26 Na ikawa kwamba Henoko alisafiri katika nchi, miongoni mwa watu; na alipokuwa akisafiri, Roho wa Mungu akamshukia kutoka mbinguni, na kukaa juu yake.
27 Naye akasikia sauti kutoka mbinguni, ikisema: Henoko, mwanangu, toa unabii kwa watu hawa, na uwaambie—Tubuni, na hivyo ndivyo asemavyo Bwana: Nimekasirishwa na watu hawa, na hasira yangu kali inawaka dhidi yao; kwa kuwa mioyo yao imekuwa migumu, na masikio yao hayasikii vyema, na macho yao hayawezi kuona mbali;
28 Na kwa vizazi hivi vingi, hata tangu siku ile ambayo niliwaumba, wamepotoka, nao wamenikana Mimi, nao wamefuata ushauri wao wa gizani; na katika machukizo yao wenyewe wamebuni mauaji, na hawakuzishika amri, ambazo nilimpa baba yao, Adamu.
29 Kwa sababu hiyo, wamejiapia wenyewe, na kwa viapo vyao, wamejiletea mauti juu yao wenyewe; na jehanamu nimeitengeneza kwa ajili yao, kama hawatatubu;
30 Na hili ni tangazo, ambalo nimelitangaza katika mwanzo wa ulimwengu, kutoka kinywani mwangu mwenyewe, kutoka kuwekwa msingi wake, na kwa vinywa vya watumishi wangu, baba zenu, nimelitangaza hilo, hata kama litakavyopelekwa ulimwenguni, hadi miisho yake.
31 Na Henoko alipoyasikia maneno haya, akapiga magoti chini ya nchi, mbele za Bwana, na kunena mbele za Bwana, akisema: Kwa nini nimepata upendeleo mbele za uso wako, nami ni kijana mdogo, na watu wote wanichukia; kwa maana mimi si mwepesi wa kusema; kwani mimi ni mtumishi wako?
32 Naye Bwana akamwambia Henoko: Enenda zako na ukafanye kama nilivyokuamuru wewe, na hakuna mtu atakayekurarua wewe. Fumbua kinywa chako, nacho kitajazwa, nami nitakupa maneno, kwa maana wenye mwili wote wako mikononi mwangu, nami nitafanya kama nionavyo kuwa vyema.
33 Uwaambie watu hawa: Chagueni leo hii, kumtumikia Bwana Mungu aliyewaumba ninyi.
34 Tazama Roho yangu i juu yako, kwa sababu hiyo maneno yako yote nitayahesabia kuwa haki; na milima itakukimbia mbele yako, na mito itageuka kutoka uelekeo wake; nawe utakaa ndani yangu, nami ndani yako; kwa hiyo tembea pamoja nami.
35 Naye Bwana akamwambia Henoko, akisema: Jipake udongo macho yako, na uyaoshe, nawe utaona. Naye alifanya hivyo.
36 Naye akaona roho zile ambazo Mungu aliziumba; na akaona pia vitu ambavyo havikuonekana kwa macho ya asili; na kutoka hapo ukaja usemi nao ukaenea katika nchi: Bwana amemwinua mwonaji kwa watu wake.
37 Na ikawa kwamba Henoko akaenda katika nchi, miongoni mwa watu, akisimama juu ya vilima na mahali palipoinuka, na akalia kwa sauti kubwa, akiwashuhudia dhidi ya matendo yao; na watu wote wakaudhika kwa sababu yake.
38 Nao wakaja kumsikiliza, juu ya mahali palipoinuka, wakiwaambia walinda mahema: Kaeni hapa na myalinde mahema, wakati sisi tukienda huko kumwona mwonaji, kwani yeye hutoa unabii, na kuna jambo geni katika nchi; mtu wa mwituni amekuja miongoni mwetu.
39 Na ikawa wakati walipomsikia, hakuna mtu aliyeweka mkono wake juu yake; kwa maana woga uliwajia juu yao wote wale waliomsikia; kwa maana yeye alitembea pamoja na Mungu.
40 Na hapo akamjia mtu, ambaye jina lake lilikuwa Mahija, naye akamwambia: Tuambie wazi wazi wewe ni nani, na umetoka wapi?
41 Naye akawaambia: Nimetoka nchi ya Kanaani, nchi ya baba zangu, nchi ya haki hadi siku hii ya leo. Na baba yangu alinifundisha katika njia zote za Mungu.
42 Na ikawa, wakati nikisafiri kutoka nchi ya Kanaani, kwa bahari ya mashariki, nikaona ono; na lo, nikaona mbingu, na Bwana akanena nami, na akanipa amri; kwa hiyo, kwa ajili ya amri hii, ya kushika amri, ninayanena maneno haya.
43 Naye Henoko aliendeleza hotuba yake, akisema: Bwana aliyesema nami, huyo ndiyo Mungu wa mbinguni, naye ni Mungu wangu, na Mungu wenu, nanyi ni ndugu zangu, na kwa nini mnajishauri wenyewe, na kumkana Mungu wa mbinguni?
44 Mbingu hizo alizifanya; na dunia ni mahali pake pa kuwekea miguu; na msingi wake ni wake. Tazama, yeye aliuweka, na jeshi la watu amelileta juu ya uso wake.
45 Na mauti yamekuja juu ya baba zetu; hata hivyo tunawajua, na hatuwezi kuwakana, na wote hata wa kwanza wao wote tunamjua, hata Adamu.
46 Kwa maana kitabu cha ukumbusho tumekiandika miongoni mwetu, kulingana na utaratibu uliotolewa kwa kidole cha Mungu; nacho kinatolewa katika lugha yetu wenyewe.
47 Na wakati Henoko alipokuwa akinena maneno ya Mungu, watu wakatetemeka, na hawakuweza kusimama mbele yake.
48 Naye akawaambia: Kwa sababu Adamu alianguka, sisi tupo; na kwa kuanguka kwake mauti yakaja; nasi tumefanywa washiriki wa dhiki na huzuni.
49 Tazama Shetani amekuja miongoni mwa wanadamu, naye huwajaribu ili wamwabudu yeye; na watu wamekuwa wenye tamaa, anasa, na uibilisi, nao wamefungiwa nje ya uwepo wa Mungu.
50 Lakini Mungu alifanya ijulikane kwa baba zetu kwamba watu wote lazima watubu.
51 Naye akamwitia baba yetu Adamu kwa sauti yake yeye mwenyewe, akisema: Mimi ndimi Mungu; niliyeufanya ulimwengu, na watu kabla hawajawa katika mwili.
52 Naye pia akamwambia: Kama utanigeukia, na kuisikiliza sauti yangu, na kuamini, na kutubu uvunjaji sheria wako wote, na kubatizwa, hata katika maji, katika jina la Mwanangu wa Pekee, aliyejaa neema na kweli, ambaye ndiye Yesu Kristo, jina pekee litakalotolewa chini ya mbingu, ambalo kwalo wokovu waweza kuja kwa wanadamu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu, mkiomba mambo yote katika jina lake, na lolote mtakaloliomba, mtapewa.
53 Naye baba yetu Adamu akamwambia Bwana, na akasema: Ni kwa nini watu lazima watubu na kubatizwa katika maji? Na Bwana akamwambia Adamu: Tazama mimi nimekusamehe uvunjaji wako wa sheria katika Bustani ya Edeni.
54 Kuanzia hapa ukaenea msemo miongoni mwa watu, kwamba Mwana wa Mungu amefanya upatanisho kwa ajili ya hatia ya asili, ambayo dhambi za wazazi haziwezi kujibiwa juu ya vichwa vya watoto, kwa maana wao ni safi tangu kuwekwa kwa msingi wa ulimwengu.
55 Na Bwana akamwambia Adamu, akisema: Kadiri watoto wako watakavyotungwa mimba katika dhambi, vivyo hivyo wakati watakapoanza kukua, dhambi hutunga katika mioyo yao, nao huonja uchungu, ili wapate kujua kutunza chema.
56 Na imetolewa kwao kujua mema na maovu; kwa sababu hiyo wao wanajiamulia wenyewe, na nimekupa sheria na amri nyingine.
57 Kwa hiyo wafundishe watoto wako, kwamba watu wote, kila mahali, lazima watubu, au vinginevyo hawataweza kuurithi ufalme wa Mungu, kwa maana hakuna kitu kilicho kichafu kinachoweza kukaa huko, au kukaa mbele zake; kwani, katika lugha ya Adamu, Mtu wa Utakatifu ndilo jina lake, na jina la Mwanawe wa Pekee ni Mwana wa Mtu, hata Yesu Kristo, Mwamuzi wa haki, ambaye atakuja wakati wa meridiani.
58 Kwa hiyo ninakupeni amri, kuyafundisha mambo haya kwa uhuru kwa watoto wenu, mkisema:
59 Kwamba kwa sababu ya uvunjaji wa sheria limekuja anguko, ambalo laleta mauti, na kadiri ninyi mlivyozaliwa katika ulimwengu kwa maji, na damu, na roho, ambavyo nilivifanya, na hivyo kuwa vumbi la nafsi iliyo hai, hata hivyo lazima mzaliwe tena katika ufalme wa mbinguni, kwa maji, na kwa Roho, na kuoshwa kwa damu, hata damu ya Mwanangu wa Pekee; ili mpate kutakaswa kutokana na dhambi zote, na kufurahia maneno ya uzima wa milele katika ulimwengu huu, na uzima wa milele katika ulimwengu ujao, hata utukufu katika mwili usiokufa;
60 Kwa maana kwa maji mnazishika amri; na kwa Roho mnahesabiwa haki, na kwa damu ninyi mnatakaswa;
61 Kwa hiyo imetolewa kukaa ndani yenu; ushuhuda wa mbinguni; yule Mfariji; mambo ya amani ya utukufu usiokufa; ukweli wa mambo yote; kile ambacho huhuisha vitu vyote, kile ambacho hufanya vitu vyote kuwa hai; kile kinachojua vitu vyote, na chenye uwezo wote kulingana na hekima, huruma, ukweli, haki, na hukumu.
62 Na sasa, tazama, ninawaambia: Huu ndiyo mpango wa wokovu kwa watu wote, kupitia damu ya Mwanangu wa Pekee, ambaye atakuja wakati wa meridiani.
63 Na tazama, vitu vyote vina mfano wake, na vitu vyote vimeumbwa na vimefanywa ili kunishuhudia Mimi, vitu vyote vilivyo vya kimwili, na vile vya kiroho; vitu vilivyoko mbinguni juu, na vitu vilivyo juu ya nchi, na vitu vilivyo ndani ya nchi, na vitu vilivyo chini ya nchi, vyote juu na chini: vitu vyote vinanishuhudia Mimi.
64 Na ikawa kwamba, Bwana aliposema na Adamu, baba yetu, kwamba Adamu alilia kwa Bwana, naye akanyakuliwa na Roho wa Bwana, naye akachukuliwa ndani ya maji, na kulazwa chini majini, na kutolewa kutoka majini.
65 Na hivyo akawa amebatizwa, na Roho wa Mungu akamshukia juu yake, na hivyo akawa amezaliwa kwa Roho, na akawa amehuishwa katika utu wa ndani.
66 Naye akasikia sauti kutoka mbinguni, ikisema: Wewe umebatizwa kwa moto, na kwa Roho Mtakatifu. Huu ndiyo ushuhuda wa Baba, na Mwana, na kutoka sasa na hata milele;
67 Na wewe ni kwa mfano wake yeye ambaye hana mwanzo wa siku au mwisho wa miaka, kutoka milele yote hadi milele yote.
68 Tazama, wewe u mmoja ndani yangu, mwana wa Mungu; na hivyo wote wapate kuwa wana wangu. Amina.