Misaada ya Kujifunza
24. Kapernaumu


24. Kapernaumu

Picha
picha 24

Kapernaumu, iliyo katika pwani ya Bahari ya Galilaya, kilikuwa ndiyo kituo cha huduma ya Yesu katika Galilaya (Mt. 9:1–2; Mk. 2:1–5). Kituo muhimu na chenye mafanikio kiuvuvi na kibiashara, ilikuwa ni makao kwa Wayunani na vile vile kwa Wayahudi. Idadi ya watu katika karne ya kwanza huenda haikuzidi watu 1,000. Kapernaumu ilikuwa katika njia panda ya njia muhimu za kibiashara, pamoja na ardhi yenye rutuba iliyoizunguka. Askari wa Kirumi walijenga majumba ya kuogea na maghala ya hifadhi hapa, Licha ya miujiza mingi iliyofanyika hapa, watu hawa kwa ujumla walikataa hudumu ya Mwokozi. Yesu kwa hivyo aliulaani mji huu (Mt. 11:20, 23–24). Baada ya muda, Kapernaumu ikaangukia katika magofu na kubaki bila wakazi.

Matukio Muhimu: Kapernaumu ilijulikana kama “mji wake Mwokozi” (Mt. 9:1–2; Mk. 2:1–5). Alitenda miujiza mingi katika eneo hili. Kwa mfano, aliwaponya watu wengi (Mk. 1:32–34), ikiwa ni pamoja na mtumishi wa akida (Lk. 7:1–10), mama mkwe wa Petro (Mk. 1:21, 29–31), mtu aliyepooza ambaye kitanda chake kilishushwa kupitia juu ya paa (Mk. 2:1–12), na mtu aliyekuwa na mkono ulionyauka (Mt. 12:9–13). Hapa Yesu pia aliwatoa pepo wengi wachafu (Mk. 1:21–28, 32–34), alimfufua binti wa Yairo kutoka kwa wafu (Mt. 9:18–19, 23–26; Mk. 5:22–24, 35–43), na akatoa mahubiri ya mkate wa uzima katika sinagogi huko Kapernaumu (Yn. 6:24–59). Mwokozi alimwelekeza Petro kuvua samaki kutoka katika Bahari ya Galilaya, akamfunua kinywa chake yule samaki, na kukuta sarafu ambayo kwayo alilipa kodi (Mt. 17:24–27).