Maandiko Matakatifu
Musa 1


Teuzi kutoka
Kitabu cha Musa

Kiziduo kutoka tafsiri ya Biblia kama kilivyofunuliwa kwa Joseph Smith Nabii, Juni 1830–Februari 1831.

Mlango wa 1

(Juni 1830)

Mungu Anajionyesha mwenyewe kwa Musa—Musa anageuzwa sura—Anakabiliana ana kwa ana na Shetani—Musa anaona dunia nyingi zenye kukaliwa na watu—Dunia zisizo na idadi ziliumbwa na Mwana—Kazi na utukufu wa Mungu ni kuleta maisha katika mwili usio kufa na uzima wa milele wa mwanadamu.

1 Maneno ya Mungu, ambayo aliyaongea kwa Musa wakati Musa alipokuwa amenyakuliwa juu katika Mlima mrefu sana,

2 Naye akamwona Mungu uso kwa uso, na akaongea naye, na utukufu wa Mungu ukawa juu ya Musa; kwa hiyo Musa aliweza kustahimili uwepo wake.

3 Na Mungu akamwambia Musa, akisema: Tazama, Mimi ndimi Bwana Mungu Mwenyezi, na Bila Mwisho ndilo jina langu; kwa maana Mimi sina mwanzo wa siku wala mwisho wa miaka; je, na hii siyo bila mwisho?

4 Na, tazama, wewe u mwanangu; kwa sababu hiyo angalia, nami nitakuonyesha wewe kazi za mikono yangu; lakini siyo zote, kwa maana kazi zangu hazina mwisho, na pia maneno yangu, kwa maana hayakomi.

5 Kwa sababu hiyo, hakuna mwanadamu awezaye kuziona kazi zangu zote, isipokuwa ameuona utukufu wangu wote; na hakuna mtu awezaye kuuona utukufu wangu wote, na baadaye akabaki katika mwili duniani;

6 Na ninayo kazi kwa ajili yako, Musa, mwanangu; nawe u mfano wa Mwanangu wa Pekee; na Mwanangu wa Pekee ni Mwokozi, na atakuwa Mwokozi, kwa maana yeye amejaa neema na kweli; lakini hakuna Mungu zaidi yangu, na vitu vyote viko mbele zangu, kwani ninavijua vyote.

7 Na sasa, tazama, jambo hili moja ninalionyesha kwako, Musa, mwanangu, kwa maana wewe uko ulimwenguni, na sasa ninalionyesha kwako.

8 Na ikawa kwamba Musa akaangalia, na akauona ulimwengu ambao juu yake aliumbwa; na Musa akauona ulimwengu na miisho yake, na wanadamu wote waliopo, na ambao waliumbwa; alishangaa na kustajaabu mno juu ya hayo.

9 Na uwepo wa Mungu ukatoweka mbele ya Musa, na kwamba utukufu wake haukuwa juu ya Musa; na Musa akaachwa pekee yake. Na vile alivyoachwa pekee yake, akaanguka chini.

10 Na ikawa kwamba masaa mengi yalipita kabla ya Musa kurudiwa tena na nguvu zake za kiasili kama mwanadamu; naye alijisemea: Sasa, kwa jinsi hii ninajua kwamba mwanadamu si kitu, kitu ambacho sikukidhania.

11 Lakini sasa macho yangu yenyewe yamemwona Mungu; lakini siyo kwa macho yangu ya asili, bali kwa macho yangu ya kiroho, kwa maana macho yangu ya asili hayangeweza kumwona; kwani ningelinyauka na kufa mbele zake; lakini utukufu wake ulikuwa juu yangu; nami nikauona uso wake, kwa kuwa nilibadilishwa mbele zake.

12 Na ikawa kwamba wakati Musa aliposema maneno haya, tazama, Shetani akaja kumjaribu, akisema: Musa, mwana wa mtu, niabudu mimi.

13 Na ikawa kwamba Musa akamtazama Shetani na akasema: Wewe ni nani? Kwa maana tazama, mimi ni mwana wa Mungu, katika mfano wa Mwanawe wa Pekee; na u wapi utukufu wako, hata nipate kukuabudu?

14 Kwani tazama, sikuweza kumwangalia Mungu, isipokuwa utukufu wake ulipokuwa juu yangu, nami nikabadilishwa mbele zake. Lakini ninaweza kukuangalia wewe katika hali ya kiasili ya mwanadamu. Je, hakika si ndivyo ilivyo?

15 Na libarikiwe jina la Mungu wangu, kwa maana Roho wake hajajiondoa kwangu moja kwa moja, au vinginevyo utukufu wako u wapi, kwa maana ni giza kwangu? Nami ninaweza kuwatofautisha kati yako wewe na Mungu; kwa maana Mungu aliniambia: Mwabudu Mungu, kwa maana ni yeye pekee utakayemtumikia.

16 Nenda zako, Shetani; usinidanganye; kwa maana Mungu aliniambia: Wewe ni mfano wa Mwanangu wa Pekee.

17 Naye pia alinipa amri wakati aliponiita kutoka kichaka kilichokuwa kinaungua, akisema: Mlingane Mungu katika jina la Mwanangu wa Pekee, na kuniabudu Mimi.

18 Na tena Musa akasema: Sitaacha kumlingia Mungu, ninayo mambo mengine ya kumwuliza: kwa maana utukufu wake ulikuwa juu yangu, kwa sababu hiyo ninaweza kuwatofautisha kati yake yeye na wewe. Ondoka hapa, Shetani.

19 Na sasa, Musa alipokwisha kusema maneno haya, Shetani akalia kwa sauti kubwa, na kujitapa juu ya nchi, na kuamuru, akisema: Mimi ndiye Mwana wa Pekee, niabudu mimi.

20 Na ikawa kwamba Musa akaanza kuogopa kupita kiasi; na mara alipoanza kuogopa, akaona machungu ya jehanamu. Hata hivyo, akamlingana Mungu, naye akapokea nguvu, naye akaamuru, akisema: Ondoka kwangu, Shetani, kwa maana ni Mungu huyu mmoja tu nitakayemwabudu, ambaye ndiye Mungu wa utukufu.

21 Na sasa Shetani akaanza kutetemeka, na nchi kutingishika; na Musa akapata nguvu, na kulilingania jina la Mungu, akisema: Katika jina la Mwana wa Pekee, ondoka, Shetani.

22 Na ikawa kwamba Shetani akalia kwa sauti kubwa, kwa kuomboleza, na huzuni, na kusaga meno; na akaondoka mahali hapo, hata kutoka uwepo wa Musa, kwamba hakumwona.

23 Na sasa juu ya jambo hili Musa analishuhudia; lakini kwa sababu ya uovu halijakuwepo miongoni mwa wanadamu.

24 Na ikawa kwamba Shetani alipokuwa ameondoka katika uwepo wa Musa, kwamba Musa aliinua macho yake mbinguni, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, ambaye huwashuhudia Baba na Mwana;

25 Na akalilingania jina la Mungu, akauona utukufu wake tena, kwa maana ulikuwa juu yake; na akasikia sauti, ikisema: Heri wewe, Musa, kwa maana Mimi, Mwenyezi, nimekuchagua wewe, nawe utafanywa kuwa mwenye nguvu kushinda maji mengi; kwa maana yatatii amri yako kama vile, wewe ndiye Mungu.

26 Na lo, Mimi nipo pamoja nawe, hata mwisho wa siku zako; kwa maana wewe utawakomboa watu wangu kutoka utumwani, hata Israeli mteule wangu.

27 Na ikawa kwamba, wakati sauti ikiwa bado inaongea, Musa alitupa macho yake na akaiona dunia, ndiyo, hata dunia yote; na hakuna sehemu yake yoyote ambayo hakuiona, akiitambua kwa uwezo wa Roho wa Mungu.

28 Naye pia aliwaona wakazi wake, na hapakuwa na nafasi ambayo hakuiona; na alizitambua kwa uwezo wa Roho wa Mungu; na idadi yao ilikuwa kubwa, hata isiyohesabika kama vile mchanga juu ya pwani ya bahari.

29 Naye aliona nchi nyingi; na kila nchi iliitwa dunia, nako kulikuwapo na wakazi juu ya uso wake.

30 Na ikawa kwamba Musa akamlingana Mungu, akisema: Niambie, nakuomba, kwa nini mambo haya yako hivi, na kwa njia gani wewe uliyatengeneza?

31 Na tazama, utukufu wa Bwana ulikuwa juu ya Musa, na hivyo Musa alisimama katika uwepo wa Mungu, na kuzungumza naye uso kwa uso. Na Bwana Mungu akamwambia Musa: Kwa madhumuni yangu Mimi mwenyewe nimeyatengeneza mambo haya. Hii ndiyo hekima nayo yabaki kwangu.

32 Na kwa neno la uwezo wangu, nimeviumba, ambaye ndiye Mwanangu wa Pekee, aliyejaa neema na kweli.

33 Na dunia zisizo na idadi nimeziumba; na pia nimeziumba kwa madhumuni yangu mwenyewe; na kwa njia ya Mwana nimeziumba, ambaye ndiye Mwanangu wa Pekee.

34 Na mwanadamu wa kwanza kwa wanadamu wote nikamwita Adamu, ambalo ni wengi.

35 Lakini ni maelezo ya dunia hii tu, na wakazi wake, ndiyo nikupayo. Kwa maana tazama, ziko dunia nyingi ambazo zimepita kwa neno la uwezo wangu. Na ziko nyingi ambazo sasa zinasimama, na kwa mwanadamu hazihesabiki; lakini vitu vyote vinahesabika kwangu, kwa kuwa ni vyangu nami navijua.

36 Na ikawa kwamba Musa akamwambia Bwana, akisema: Umrehemu mtumishi wako, Ee Mungu, na uniambie juu ya dunia hii, na wakazi wake, na pia mbingu, na ndipo mtumishi wako ataridhika.

37 Na Bwana Mungu akasema kwa Musa, akisema: Mbingu hizi, ziko nyingi, nazo haziwezi kuhesabika kwa mwanadamu; lakini zinahesabika kwangu, kwa kuwa ni zangu.

38 Na kama vile dunia moja itakavyopita, na mbingu zake na hivyo nyingine zitakuja; na hakuna mwisho wa kazi zangu, wala wa maneno yangu.

39 Kwa maana tazama, hii ndiyo kazi yangu na utukufu wangu—kuleta kutokufa na uzima wa milele wa mwanadamu.

40 Na sasa, Musa, mwanangu, nitakuambia juu ya dunia hii ambayo juu yake wewe umesimama; nawe utaandika mambo ambayo nitayasema.

41 Na katika siku ambayo wanadamu watakapoyachukulia maneno yangu kuwa kazi bure na kuyaondoa mengi kutoka kwenye kitabu ambacho utakiandika, tazama, nitamwinua mwingine kama wewe; nayo yatasikika tena miongoni mwa wanadamu—miongoni mwa wengi kadiri watakavyoamini.

42 (Maneno haya yalinenwa kwa Musa mlimani, mlima ambao jina lake halitajulikana miongoni mwa wanadamu. Na sasa yananenwa kwako. Usiyaonyeshe kwa yeyote isipokuwa wao waaminio. Hivyo ndivyo. Amina.)