Mkutano Mkuu
Kujaribiwa, Kuthibitishwa, na Kung’arishwa
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2020


Kujaribiwa, Kuthibitishwa, na Kung’arishwa

Baraka kubwa itakayokuja tutakapo jithibitisha wenyewe kuwa waaminifu kwenye maagano yetu wakati wa majaribu yetu itakuwa ni mabadiliko katika asili zetu.

Wapendwa akina kaka na dada zangu, ninashukuru kuzungumza nanyi leo. Tumaini langu ni kuwapeni moyo pale maisha yanapoonekana kuwa magumu na yasiyo na uhakika. Kwa baadhi yenu, wakati huo ni sasa. Ikiwa sivyo, wakati huo utakuja.

Huo siyo mtazamo wenye giza. Ni uhalisia—na bado wa matumaini—kwa sababu ya lengo la Mungu katika Uumbaji wa ulimwengu huu. Lengo hilo lilikuwa ni kuwapa watoto Wake nafasi ya kujithibitisha wenyewe kuwa wanaweza na wako radhi kuchagua mema wakati inapokuwa vigumu kufanya hivyo. Kwa kufanya hivyo, asili zao zingebadilika na wangeweza kuwa zaidi kama Yeye. Yeye alijua hilo lingehitaji imani imara Kwake.

Mengi ninayoyafahamu yalitoka kwenye familia yangu. Wakati nilipokuwa na takriban umri wa miaka minane, mama yangu mwenye hekima alituomba mimi na kaka yangu kusaidiana nae kuondoa magugu kwenye bustani iliyokuwa nyuma ya nyumba ya familia yetu. Sasa, hiyo ilionekana kazi nyepesi, lakini tuliishi New Jersey. Mvua ilinyesha mara kwa mara. Udongo ulikuwa mfinyanzi mzito. Magugu yalikua haraka kuliko mboga mboga.

Nakumbuka kukasirika kwangu wakati magugu yalipokatikia mikononi mwangu, mizizi yake iliganda kwa nguvu katika matope mazito. Mama na kaka yangu walikuwa mbali kidogo katika safu zao. Kadiri nilivyojitahidi kwa nguvu, ndivyo zaidi nilivyobaki nyuma.

“Hii ni ngumu sana” Nililia.

Badala ya kunihurumia, mama yangu alitabasamu na kusema, “Oh, Hal, ndiyo, ni ngumu. Inapaswa kuwa hivyo. Maisha ni mtihani.”

Katika wasaa ule, nilijua maneno yake yalikuwa ya kweli na yangeendelea kuwa kweli katika nyakati zangu zijazo.

Sababu ya tabasamu la upendo la Mama yangu iliweza kuwa wazi kwangu miaka kadhaa baadaye niliposoma juu ya Baba wa Mbinguni na Mwanae Mpendwa wakizungumzia lengo Lao katika kuumba ulimwengu huu na kuwapatia watoto wa kiroho fursa ya maisha ya duniani:

“Nasi tutawajaribu kwa njia hii, ili kuona kama wao watafanya mambo yote yale ambayo Bwana Mungu wao atawaamuru;

“Na wao ambao watatunza hali yao ya kwanza wataongezewa; na wao ambao hawatatunza hali yao ya kwanza hawatapata utukufu katika ufalme ule ule pamoja na wale walioitunza hali yao ya kwanza; nao wale watakaoitunza hali yao ya pili watapata kuongezewa utukufu juu ya vichwa vyao kwa milele na milele.”1

Mimi na wewe tulikubali mwaliko huo wa kujaribiwa na kuthibitisha kuwa tutachagua kushika amri za Mungu pale ambapo tutakuwa mbali na uwepo wa Baba yetu wa Mbinguni.

Hata pamoja na mwaliko huo wa upendo kutoka kwa Baba yetu wa Mbinguni, Lusiferi aliwashawishi theluthi moja ya watoto wa kiroho kumfuata na kukataa mpango wa Baba kwa ajili ya ukuaji wetu na furaha ya milele. Kwa uasi huo wa Shetani, alitupwa nje na wafuasi wake. Sasa anajaribu kusababisha wengi kadiri anavyoweza wageuke mbali na Mungu katika kipindi hiki cha maisha ya duniani.

Wale kati yetu tulioukubali mpango huu tulifanya hivyo kwa sababu ya imani yetu katika Yesu Kristo, aliyejitolea kuwa Mwokozi na Mkombozi wetu. Ni lazima tulikuwa tumeamini wakati huo kwamba udhaifu wowote wa mwili wenye kufa ambao tungekuwa nao na nguvu zozote za uovu ambazo zingekuwa dhidi yetu, nguvu za wema zingekuwa ni kubwa kupindukia.

Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo wanakujua na wanakupenda. Wanakutaka urudi Kwao na uwe kama Wao. Mafanikio yako ni mafanikio Yao. Umehisi upendo huo ukithibitishwa kwako na Roho Mtakatifu wakati uliposoma au kusikia maneno haya: “Na tazama, hii ni kazi yangu na utukufu wangu—kuleta kutokufa na uzima wa milele wa mwanadamu.”2

Mungu anao uwezo wa kuzifanya njia zetu kuwa rahisi. Aliwalisha mana watoto wa Israel katika kutangatanga kwao kuelekea nchi ya ahadi. Bwana katika huduma Yake duniani aliponya wagonjwa, alifufua wafu, na kutuliza bahari. Baada ya Ufufuko Wake, Alifungua “kifungo kwa wale waliofungwa.”3

Na bado Nabii Joseph Smith, mmoja wa manabii Wake wakuu, aliteseka gerezani na alifundishwa somo ambalo sote tunanufaika nalo na tunalihitaji katika majaribu yetu yanayojirudia ya imani: “Na kama utatupwa ndani ya shimo, au katika mikono ya wauaji, na hukumu ya kifo ikapitishwa juu yako; kama utatupwa kilindini; kama mawimbi makali yatakula njama dhidi yako; kama upepo mkali utakuja kuwa adui yako; kama mbingu zitakusanya giza, na vitu vyote vya asili vikiungana ili kuzingira njia yako; na juu ya yote, kama mataya yale ya jahanamu yataachama kinywa wazi kwa ajili yako, fahamu wewe, mwanangu, kwamba mambo haya yote yatakupa wewe uzoefu, na yatakuwa kwa faida yako.”4

Unaweza kwa kutafakari kujiuliza kwa nini Mungu mwenye upendo na nguvu-zote anaruhusu majaribu yetu ya duniani kuwa magumu. Ni kwa sababu Yeye anajua kwamba tunapaswa kukua katika usafi wa kiroho na kimo ili kuweza kuishi katika uwepo Wake katika familia milele. Ili kufanya hilo liwezekane, Baba wa Mbinguni alitupatia Mwokozi na uwezo wa kuchagua wenyewe kwa imani kutii amri zake na kutubu na hivyo kuja Kwake.

Mpango wa Baba wa furaha umebeba katika kiini chake sisi kuwa kama Mwanawe Mpendwa, Yesu Kristo. Katika mambo yote, mfano wa Mwokozi ndio mwongozo wetu bora. Yeye hakusamehewa kutokana na hitaji la kujithibitisha Mwenyewe. Alivumilia kwa ajili ya watoto wote wa Baba wa Mbinguni, akilipa gharama kwa ajili ya dhambi zetu zote. Aliyasikia maumivu ya wote ambao waliwahi kuwepo na watakaokuja katika dunia.

Unapojiuliza ni maumivu kiasi gani unaweza kuvumilia, mkumbuke Yeye. Aliteseka yale unayoteseka ili aweze kujua namna ya kukunyanyua. Anaweza asiondoe mzigo, lakini atakupa nguvu, faraja, na tumaini. Yeye anaijua njia. Alikunywa kikombe kichungu. Alivumilia mateso ya wote.

Unatunzwa na kufarijiwa na Mwokozi mwenye upendo, anayejua jinsi ya kukusaidia katika hali yoyote ya majaribu unayoyakabili. Alma alifundisha:

“Na atakwenda, na kuteseka maumivu na masumbuko na majaribio ya kila aina; na hii kwamba neno litimizwe ambalo linasema atabeba maumivu na magonjwa ya watu wake.

“Na atajichukulia kifo, ili afungue kamba za kifo ambazo zinafunga watu wake; na atajichukulia unyonge wao, ili moyo wake ujae rehema, kulingana na mwili, ili ajue kulingana na mwili jinsi ya kuwasaidia watu wake kulingana na unyonge wao.”5

Njia moja Atakayokusaidia wewe itakuwa kukualika wewe daima kumkumbuka Yeye na kuja Kwake. Ametuhimiza.

“Njooni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.

“Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo: nanyi mtapata raha nafsini mwenu.”6

Njia ya kuja Kwake ni kusherehekea neno Lake, kuonyesha imani katika toba, kuchagua kubatizwa na kuthibitishwa na watumishi Wake wenye mamlaka, na kisha kutunza maagano yako na Mungu. Yeye humtuma Roho Mtakatifu kuwa mwenzi wako, mfariji, na mwongozaji.

Utakapoishi kwa ustahili wa kipawa cha Roho Mtakatifu, Bwana anaweza kukuongoza kwenye usalama hata wakati ambapo huwezi kuona njia. Kwangu mimi, Amekuwa mara kwa mara akinionyesha hatua moja au mbili zinazofuata za kuchukua. Mara chache Amenipa mimi mtazamo mrefu wa siku zijazo, lakini hata hiyo mitazamo isiyo ya mara kwa mara huongoza kwenye kile ambacho mimi huchagua kufanya katika maisha yangu ya kila siku.

Bwana alifafanua:

“Hamuwezi kuona kwa macho yenu ya asili, kwa wakati huu, mipango ya Mungu wenu juu ya mambo yale ambayo yatakuja hapo baadaye, na utukufu utakaofuata … baada ya taabu kubwa.

Kwani baada ya taabu kubwa huja baraka.”7

Baraka kubwa itakayokuja tutakapo jithibitisha wenyewe kuwa waaminifu kwenye maagano yetu wakati wa majaribu yetu itakuwa ni mabadiliko katika asili zetu. Kwa kuchagua kwetu kutunza maagano, nguvu za Yesu Kristo na baraka za Upatanisho Wake vinaweza kufanya kazi kwetu. Mioyo yetu inaweza kulainishwa ili kupenda, kusamehe, na kuwaalika wengine kuja kwa Mwokozi. Kujiamini kwetu katika Bwana kunaongezeka. Woga wetu unapungua.

Sasa, pamoja na baraka hizi zilizoahidiwa kupitia mateso, hatutafuti mateso. Katika uzoefu wa duniani, tutakuwa na fursa za kutosha za kujithibitisha wenyewe, kushinda majaribu magumu zaidi ili kuwa zaidi kama Mwokozi na Baba yetu wa Mbinguni.

Zaidi, lazima tutambue mateso ya wengine na tujaribu kusaidia. Hii itakuwa ngumu hasa pale tunapokuwa tunapitia majaribu makali sisi wenyewe. Ila tutagundua pale tunapobeba mizigo ya wengine, hata kidogo tu, kwamba migongo yetu inaimarishwa na tunahisi nuru katika giza.

Katika hili, Bwana ni Mfano wetu. Juu ya msalaba wa Golgotha, akiwa tayari ameteseka maumivu makali kwamba Angeweza kufa kama asingekuwa Mwana Mpendwa wa Mungu, Aliwatazama watesi wake na kusema kwa Baba Yake, “Wasamehe; kwani hawajui watendalo.”8 Wakati akiteseka kwa ajili ya wote ambao wangeishi, Alimtazama kutoka msalabani, Yohana na mama Yake aliyekuwa akihuzunika na akamhudumia katika jaribu lake:

“Basi Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake, Mama, tazama, mwanao!

“Kisha akamwambia yule mwanafunzi, Tazama, mama yako! Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake.”9

Kwa matendo Yake katika siku ile takatifu sana, kwa hiari Alitoa maisha Yake kwa ajili ya kila mmoja wetu, akijitolea si tu kutusaidia katika maisha haya bali uzima wa milele katika wakati ujao.

Nimeona watu wakiinuka kufikia viwango vya juu kupitia kuthibitisha uaminifu katika majaribu ya kutisha. Kanisani kote leo kuna mifano. Dhiki inawapeleka watu kwenye kupiga magoti. Kwa uvumilivu wao wa uminifu na juhudi, wanakuwa zaidi kama Mwokozi na Baba yetu wa Mbinguni.

Nilijifunza somo lingine kutoka kwa mama yangu. Kama msichana, alikuwa na ugonjwa wa diptheria na karibu afe. Baadae alikuwa na homa ya uti wa mgongo. Baba yake alifariki akiwa kijana, na hivyo mama yangu na kaka zake walimsaidia mama yao.

Maisha yake yote, alihisi matokeo ya majaribu ya ugonjwa. Katika miaka yake 10 ya mwisho wa maisha yake, alihitajika kufanyiwa upasuaji mara kadhaa. lakini katika yote, alithibitisha uaminifu kwa Bwana, na hata alipokuwa amelazwa kitandani. Picha pekee katika ukuta wa chumba chake ilikuwa ya Mwokozi. Maneno yake ya mwisho kwangu kwenye kitanda chake akikaribia kufa yalikuwa haya: “Hal, sauti yako iko kama unataka kupata mafua. Unapaswa kujilinda.”

Kwenye mazishi yake mzungumzaji wa mwisho alikuwa Mzee Spencer W. Kimball. Baada ya kusema jambo kuhusu majaribu yake na uaminifu wake, alisema hili kwa umuhimu: “Baadhi yenu mnaweza kujiuliza kwa nini Mildred alipaswa kuteseka sana na kwa muda mrefu. Nitawaambia kwa nini. Ilikuwa ni kwa sababu Bwana alitaka kumng’arisha zaidi.”

Ninaelezea shukurani zangu kwa waumini wengi waaminifu wa Kanisa la Yesu Kristo wanaobeba mizigo wakiwa na imani thabiti na wanaowasaidia wengine kubeba yao kadiri Bwana anavyotafuta kuwang’arisha zaidi. Ninaelezea pia upendo na matamanio yangu kwa watoa huduma na viongozi ulimwenguni kote wanaowahudumia wengine wakati wao na familia zao wakivumilia ung’arishwaji huo.

Ninashuhudia kwamba sisi tu watoto wa Baba wa Mbinguni, anayetupenda. Ninahisi upendo wa Rais Russell M. Nelson kwa wote. Yeye ni nabii wa Bwana ulimwenguni leo. Ninashuhudia hivyo katika jina takatifu la Bwana Yesu Kristo, amina.