Mkutano Mkuu
Acheni Mungu Ashinde
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2020


Acheni Mungu Ashinde

Je, wewe uko radhi kuacha Mungu ashinde katika maisha yako? Je, wewe uko radhi kuacha Mungu awe ushawishi muhimu zaidi katika maisha yako?

Wapendwa kaka zangu na dada zangu, nina shukrani iliyoje kwa jumbe nzuri za mkutano huu na kwa fursa yangu ya kunena nanyi.

Kwa zaidi ya miaka 36 niliyokuwa Mtume, mafundisho ya kukusanywa kwa Israeli yameivutia akili yangu.1 Kila kitu kuhusu jambo hili kinanivutia, ikijumuisha huduma na majina2 ya Ibrahimu, Isaka, na Yakobo; maisha yao na wake zao; agano ambalo Mungu alifanya nao na kuliendeleza katika ukoo wao wote;3 kutawanywa kwa makabila kumi na mawili; na unabii usio na idadi kuhusu kukusanywa kwao katika siku yetu.

Nimejifunza kuhusu kukusanya, nimeomba juu yake, nimesherehekea juu ya kila andiko linalohusiana, na kumwomba Bwana aongeze uelewa wangu.

Hivyo fikiria furaha yangu wakati nilipoongozwa hivi karibuni kwenye utambuzi huu mpya. Kwa msaada wa wasomi wawili wa Kiebrania, nimejifunza kwamba moja ya maana ya Kiebrania ya neno Israeli ni “acha Mungu ashinde.”4 Kwa hivyo jina la Israeli linamaanisha mtu ambaye yuko radhi kuacha Mungu ashinde katika maisha yake. Dhana hiyo inasisimua nafsi yangu!

Neno radhi ni muhimu kwa tafsiri hii ya Israeli.5 Sisi sote tunayo haki ya kujiamulia. Tunaweza kuchagua kuwa wa Israeli, au la. Tunaweza kuchagua kuacha Mungu ashinde katika maisha yetu, au la. Tunaweza kuchagua kuacha Mungu awe nguvu kubwa ya ushawishi katika maisha yetu, au la.

Kwa sekunde chache, acha tukumbuke mahali muhimu palipogeuza maisha ya Yakobo, mjukuu wa Ibrahimu. Mahali Yakobo alipopaita Penueli (maana yake “uso wa Mungu”),6 Yakobo alipigana mweleka na changamoto kubwa sana. Haki yake ya kujiamulia ilijaribiwa. Kupitia mweleka huu, Yakobo alithibitisha kile kilichokuwa muhimu zaidi kwake. Alionyesha kwamba yeye alikuwa radhi kuacha Mungu ashinde katika maisha yake. Katika kujibu, Mungu alibadilisha jina la Yakobo kuwa Israeli,7 maana yake “acha Mungu ashinde.” Kisha Mungu alimwahidi Israeli kwamba baraka zote ambazo zilikuwa zimetajwa juu ya kichwa cha Ibrahimu zitakuwa zake pia.8

Kwa huzuni, uzao wa Israeli ulivunja agano lao na Mungu. Waliwapiga kwa mawe manabii na hawakuwa radhi kumwacha Mungu ashinde katika maisha yao. Matokeo yake, Mungu aliwatawanya kwenye pembe nne za dunia.9 Kwa huruma, Yeye baadae aliahidi kuwakusanya, kama ilivyoarifiwa na Isaya: “Kwa kitambo kidogo nimekuacha [Israeli]; lakini kwa rehema nyingi nitakukusanya.”10

Pamoja na maana ya Kiebrania ya neno Israeli akilini, tunagundua kwamba kukusanywa kwa Israeli kunachukua maana iliyoongezeka. Bwana anawakusanya wale ambao wako radhi kuacha Mungu ashinde katika maisha yao. Mungu anawakusanya wale ambao watachagua kuacha Mungu awe ushawishi muhimu katika maisha yao.

Kwa karne nyingi, manabii wamekuwa wakitabiri kukusanywa huku,11 na kunafanyika hivi sasa! Kama utangulizi muhimu kwa Ujio wa Pili wa Bwana, hii ni kazi muhimu zaidi kufanyika ulimwenguni!

Kukusanywa huku kunakotangulia milenia ni jambo la hekima binafsi ya kupanua imani na ujasiri wa kiroho kwa mamilioni ya watu. Na kama waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, au “Israeli ya agano la siku za mwisho,”12 tumeamriwa kumsaidia Bwana kwenye kazi yake hii yenye maana kubwa.13

Tunapoongelea kukusanywa kwa Israeli kutoka pande zote mbili za pazia, tunamaanisha, ndiyo, kazi ya umisionari, hekaluni, na historia ya familia. Pia tunamaanisha kujenga imani na ushuhuda katika mioyo ya wale tunaoishi nao, kufanya nao kazi, na kuhudumu pamoja nao. Wakati wowote tunapofanya lolote ambalo linamsaidia mtu yeyote—upande wowote wa pazia—ili kufanya na kushika maagano yao na Mungu, tunasaidia kukusanya Israeli.

Siyo zamani sana, mke wa mmoja wa wajukuu zetu alikuwa akihangaika kiroho. Nitamwita “Jill.” Pamoja na kufunga, kuomba, na baraka za ukuhani, baba yake alikuwa anakufa. Aligubikwa na hofu kwamba atampoteza baba yake na ushuhuda wake.

Baadae jioni moja, mke wangu, Dada Wendy Nelson, aliniambia hali ya Jill. Asubuhi iliyofuata Wendy alihisi msukumo kushiriki na Jill kwamba jibu langu kwa mweleka wake wa kiroho lilikuwa neno moja! Neno hilo lilikuwa mayopia.

Jill baadae alikiri kwa Wendy kwamba mwanzoni alikasirishwa na jibu langu. Alisema, “Nilitumaini Babu angeniahidi muujiza kwa ajili ya baba yangu. Nilibaki nikijiuliza kwa nini neno mayopia ndilo neno alilolazimika kulisema.”

Baada ya baba wa Jilll kufariki dunia, neno mayopia liliendelea kuja akili mwake. Alifungua moyo wake ili kuelewa kwa kina zaidi kwamba mayopia lilimaanisha “kuona karibu.” Na kufikiri kwake kukaanza kubadilika. Jill kisha alisema, “Mayopia lilinisababisha kusimama, kufikiri, na kupona. Neno hilo sasa linanijaza amani. Linanikumbusha mimi kupanua mtazamo wangu na kutafuta umilele. Linanikumbusha kwamba kuna mpango mtakatifu na kwamba baba yangu bado anaishi na ananipenda na ananitazama. Mayopia limeniongoza kwa Mungu.”

Ninaona fahari kubwa kwa mjukuu-mkwe wetu wa thamani. Katika wakati huu wa kuvunjika moyo kwenye maisha yake, mpendwa Jill anajifunza kuyakumbatia mapenzi ya Mungu kwa baba yake, pamoja na mtazamo wa milele kwa ajili ya maisha yake mwenyewe. Kwa kuchagua kuacha Mungu ashinde, yeye anapata amani.

Kama tutaruhusu, kuna njia nyingi tafsiri hii ya Kiebrania ya Israeli inaweza kutusaidia. Fikiria jinsi maombi yetu kwa wamisionari wetu—na jitihada zetu wenyewe za kukusanya Israeli—zingeweza kubadilika kwa kuwa na dhana hii akilini. Mara kwa mara tunaomba kwamba sisi na wamisionari tuongozwe kwa wale waliotayarishwa kupokea ukweli wa injili iliyorejeshwa ya Yesu Kristo. Ninajiuliza, tutaongozwa kwa nani wakati tunapoomba kuwapata wale ambao wako radhi kumwacha Mungu ashinde katika maisha yao?

Tunaweza kuongozwa kwa baadhi ya wale ambao kamwe hawakuwahi kuamini katika Mungu au Yesu Kristo lakini ambao sasa wana hamu ya kujifunza kuhusu Wao na mpango Wao wa furaha. Wengine wanaweza kuwa “wamezaliwa ndani ya agano”14 lakini ni kitambo sasa wamepotoka mbali na njia ya agano. Yawezekana sasa wakawa tayari kutubu, kurudi na kuacha Mungu ashinde. Tunaweza kusaidia kwa kuwakaribisha kwa mikono na mioyo iliyo wazi. Na baadhi ya wale tunaoweza kuongozwa kwao yawezekana daima wamekuwa wakihisi kuna kitu fulani kinapungua katika maisha yao. Wao pia wanatamani utimilifu na shangwe ambayo huja kwa wale walio radhi kuacha Mungu ashinde katika maisha yao.

Nyavu ya injili ya kuikusanya Israeli iliyotawanyika ni pana. Kuna nafasi kwa ajili ya kila mtu ambaye ataikumbatia kwa ukamilifu injili ya Yesu Kristo. Kila mwongofu anakuwa mmoja wa watoto wa Mungu wa agano,15 iwe kwa kuzaliwa au kwa kuasiliwa. Kila mmoja anakuwa mrithi kamili wa vyote ambavyo Mungu amewaahidi watoto waaminifu wa Israeli!16

Kila mmoja wetu anao uwezekano wa kiungu kwa sababu kila mmoja ni mtoto wa Mungu. Kila mmoja ni sawa machoni Pake. Maana za ukweli huu ni nyingi sana. Akina kaka na akina dada, tafadhali sikilizeni kwa makini kwa yale ninayotaka kusema. Mungu haipendi jamii ya rangi moja kuliko nyingine. Mafundisho Yake katika jambo hili yako wazi. Anatualika sote tuje Kwake, “weusi na weupe, wafungwa na walio huru, wake na waume.”17

Ninawahakikishia kwamba kukubalika kwako mbele za Mungu hakuamuliwi na rangi ya ngozi yako. Kupendelewa au kutopendelewa na Mungu kunategemea kujitoa kwako kwa moyo kwa Mungu na amri Zake na si rangi ya ngozi yako.

Ninahuzunika kwamba kaka zetu na dada zetu weusi ulimwenguni kote wanavumilia machungu ya ubaguzi wa rangi na chuki. Leo ninatoa wito kwa waumini wetu kila mahali kuwa mfano katika kuacha mitazamo na matendo ya chuki. Ninawasihi mkuze heshima kwa watoto wote wa Mungu.

Swali kwa kila mmoja wetu, pasipo kujali rangi, ni moja. Je, wewe uko radhi kuacha Mungu ashinde katika maisha yako? Je, wewe uko radhi kuacha Mungu awe ushawishi muhimu zaidi katika maisha yako? Je, utaruhusu neno Lake, amri Zake, na maagano Yake, yashawishi kile unachofanya kila siku? Je, utaruhusu sauti Yake ichukue kipaumbele cha juu zaidi ya sauti zingine zote? Je, wewe uko radhi kuruhusu chochote Yeye anachohitaji wewe ufanye kiwe cha kwanza juu ya lengo lingine lolote? Je, wewe uko radhi kuruhusu mapenzi yako yamezwe katika Yake?18

Zingatia jinsi utayari huo unavyoweza kukubariki wewe. Kama hujaoa au kuolewa na unatafuta mwenzi wa milele, matamanio yako ya kuwa “wa Israeli” yatakusaidia kuamua nani wa kwenda naye miadi na jinsi gani ya kufanya hilo.

Ikiwa umeoa au umeolewa na mwenzi ambaye amevunja maagano yake, utayari wako wa kuacha Mungu ashinde katika maisha yako utaruhusu maagano yako na Mungu yabaki bila kuvunjwa. Mwokozi ataponya moyo wako uliovunjika. Mbingu zitafunguka unapotafuta kujua namna ya kusonga mbele. Hauna haja ya kukanganyikiwa au kutangatanga.

Ikiwa unayo maswali ya dhati kuhusu injili au Kanisa, kadiri unavyochagua kuacha Mungu ashinde, utaongozwa kupata na kuelewa ukweli mkamilifu, wa milele ambao utayaongoza maisha yako na kukusaidia kubaki imara kwenye njia ya agano.

Wakati unapokabiliwa na majaribu—hata kama majaribu yanakuja wakati ukiwa umechoka au unahisi mpweke au kutoeleweka—fikiria ujasiri unaoweza kujipatia kwa kujipa moyo wakati unapochagua kuacha Mungu ashinde katika maisha yako na unapomwomba Yeye akuimarishe.

Wakati hamu yako kuu inapokuwa kumwacha Mungu ashinde, kuwa sehemu ya Israeli, maamuzi mengi yanakuwa rahisi. Matatizo mengi yanakuwa si matatizo tena! Unajua namna bora ya kujiandaa mwenyewe! Unajua nini cha kuangalia na kusoma, wapi pa kutumia muda wako, na nani wa kushirikiana naye. Unajua kile unachotaka kutimiza. Unajua ni aina gani ya mtu unataka kuwa.

Sasa, wapendwa kaka zangu na dada zangu, inahitaji vyote imani na ujasiri ili kuacha Mungu ashinde. Inahitaji kazi ya kiroho iliyo endelevu, na ya ukakamavu ili kutubu na kumvua mwanadamu wa tabia ya asili kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo.19 Inahitaji msimamo, juhudi ya kila siku ili kukuza tabia binafsi ya kujifunza injili, kujifunza zaidi kuhusu Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo, na kutafuta na kuitikia ufunuo binafsi.

Wakati wa nyakati hizi za hatari ambazo Mtume Paulo alizitolea unabii,20 Shetani wala hajaribu tena kuficha mashambulizi yake juu ya mpango wa Mungu. Uovu wenye kushawishi umetapakaa. Kwa hiyo, njia pekee ya kunusurika kiroho ni kuwa na msimamo wa kuacha Mungu ashinde katika maisha yetu, kujifunza kuisikia sauti Yake, na kutumia nguvu zetu kusaidia kuikusanya Israeli.

Sasa, Bwana anajisikiaje kuhusu watu ambao wataacha Mungu ashinde? Nefi alifupisha hilo vizuri sana: “[Bwana] anawapenda wale ambao watataka yeye awe Mungu wao. Tazama, aliwapenda baba zetu, na akaagana nao, ndiyo, hata Ibrahimu, Isaka na Yakobo; na [anakumbuka] maagano ambayo [yeye] amefanya.”21

Na ni kitu gani Bwana yuko radhi kufanya kwa ajili ya Israeli? Bwana ametoa ahadi kwamba Yeye “atapigana vita [vyetu], na vita vya watoto [wetu], na [vita] vya watoto wa watoto wetu, hadi kizazi cha tatu na cha nne …”!22

Unapojifunza maandiko yako miezi sita inayokuja, ninakuhimiza kuandika orodha ya yale yote Bwana aliyoahidi atayafanya kwa Israeli ya agano. Ninafikiri utashangazwa! Tafakari ahadi hizi. Zungumza kuhusu ahadi hizo na familia yako na marafiki. Kisha ishi na uziangalie ahadi hizi zikitimia katika maisha yako mwenyewe.

Wapendwa kaka zangu na dada zangu, mnapochagua kuacha Mungu ashinde katika maisha yenu, mtajionea wenyewe kwamba Mungu wetu ni “Mungu wa miujiza.”23 Kama watu, sisi ni watoto Wake wa agano, nasi tutaitwa kwa jina Lake. Juu ya hili ninashuhudia katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Nimezungumza juu ya Israeli angalau mara 378 kwenye zaidi ya jumbe 800 nilizotoa katika miaka yangu 36 kama Mtume.

  2. Katika Kiebrania, Abramu ni jina maarufu likimaanisha “baba aliyeinuliwa.” Lakini Mungu alipolibadilisha jina lile na kuwa Ibrahimu, jina lilichukua umuhimu mkuu zaidi, likimaanisha “baba wa wengi.” Ndiyo, Ibrahimu ilikuwa awe “baba wa mataifa mengi” (Ona Mwanzo 17:5; Nehemia 9:7.)

  3. Bwana Mungu Yehova alifanya agano na Ibrahimu kwamba Mwokozi wa ulimwengu angezaliwa kupitia uzao wa Ibrahimu, nchi kadhaa zingerithiwa, na mataifa yote yatabarikiwa kupitia ukoo wa Ibrahimu (ona Bible Dictionary, “Abraham, covenant of”).

  4. Ona Kamusi ya Biblia, “Israeli.”

  5. Neno Israeli ninaonekana zaidi ya mara elfu moja katika maandiko. Linaweza kutumika kwa familia ya Yakobo (Israeli) ya wana kumi na wawili, jumlisha mabinti zake (ona Mwanzo 35:23–26; 46:7). Leo linaweza kutumika kijiografia kama sehemu juu ya sayari Dunia. Lakini matumizi yake kimaandiko yanatumika kwa watu ambao wako radhi kuacha Mungu ashinde katika maisha yao.

  6. Ona Mwanzo 32:30; pia imeandikwa kama Penueli katika Mwanzo 32:31.

  7. Ona Mwanzo 32:28.

  8. Ona Mwanzo 35:11–12.

  9. Kwa kujifunza zaidi, ona Mwongozo wa Mada, “Israeli, Kutawanywa kwa.”

  10. Isaya 54:7.

  11. Ona Isaya 11:11–12; 2 Nefi 21:11–12; Mosia 15:11.

  12. Ona Encyclopedia of Mormonism (1992), “Covenant Israel, Latter-Day,” 1:330–31.

  13. Tunaposhiriki katika kukusanya Israeli, Bwana anayo njia ya kushangaza ya kuelezea wale wanaokusanywa. Yeye anatuelezea sisi kwa pamoja kama “hazina Yake ya kipekee,” (Kutoka 19:5; Zaburi 135:4), kama “hazina” Yake (Malaki 3:17; Mafundisho na Maagano 101:3), na kama “taifa takatifu” (Kutoka 19:6; ona pia Kumbukumbu la Torati14:2; 26:18).

  14. Maneno haya yanamaanisha agano lile hasa Mungu alilofanya na Ibrahimu, akisema, “Katika uzao wako watoto wote wa dunia watabarikiwa” (3 Nefi 20:27). “Kuzaliwa katika agano” inamaanisha kwamba kabla mtu hajazaliwa, mama na baba wa mtu huyo walikuwa wameunganishwa hekaluni.

  15. Ahadi ya jinsi hiyo ilifundishwa na Mungu kwa Ibrahimu: “Kadiri wengi wanavyoipokea injili hii wataitwa kwa jina lako, na watahesabiwa uzao wako nao watainuka na kukubariki wewe, kama baba yao” (Ibrahimu 2:10; ona pia Warumi 8:14–17; Wagalatia 3:26–29).

  16. Kila muumini mwaminifu anaweza kuomba baraka ya patriaki. Kupitia mwongozo wa kiungu wa Roho Mtakatifu, patriaki anatamka nasaba ya mtu huyo katika nyumba ya Israeli. Tamko hilo siyo lazima liwe tamko la rangi yake, utaifa wake, au nasaba zake. Badala yake, nasaba iliyotamkwa inatambulisha kabila la Israeli ambalo kupitia kwalo mtu huyo atapokea baraka zake.

  17. 2 Nefi 26:33.

  18. Ona Mosia 15:7. Kuwa wa Israeli siyo kwa ajili ya kufa moyo. Ili kupokea baraka zote ambazo Mungu anazo ghalani kwa ajili ya uzao wa Ibrahimu, sisi sote tunaweza kutegemea kupata jaribu letu wenyewe la kipekee “jaribu la Ibrahimu.” Mungu atatujaribu sisi, kama Nabii Joseph Smith alivyofundisha, kwa kuvunja mishipa ya mioyo yetu hasa. (Ona kumbukumbu ya John Taylor katika Teachings of Presidents of the Church: Joseph Smith [2007], 231.)

  19. Ona Mosia 3:19.

  20. Ona 2 Timotheo 3:1–13.

  21. 1 Nefi 17:40; msisitizo umeongezwa.

  22. Mafundisho na Maagano 98:37; ona pia Zaburi 31:23; Isaya 49:25; Mafundisho na Maagano 105:14.

  23. Mormoni 9:11.