Mkutano Mkuu
Saburi Na Iwe na Kazi Kamilifu, na Hesabuni Ya Kuwa ni Shangwe Tupu!
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2020


Saburi Na Iwe na Kazi Kamilifu, na Hesabuni Ya Kuwa ni Shangwe Tupu!

Tunapoonyesha subira, imani yetu huongezeka. Imani yetu inapoongezeka, ndivyo itakavyokuwa na shangwe yetu.

Miaka miwili iliyopita, kaka yangu mdogo, Chad, alivuka upande wa pili wa pazia. Kuvuka kwake upande wa pili kumeacha pengo katika moyo wa shemeji yangu, Stephania; watoto wao wadogo wawili, Braden na Bella, vile vile familia yote iliyosalia. Tulipata faraja katika maneno ya Mzee Neil L. Andersen katika mkutano mkuu wiki moja kabla ya Chad kufariki: “Katika ukali wa majaribu ya kidunia, kwa saburi songa mbele, na nguvu ya uponyaji ya Mwokozi itakuletea nuru, uelewa, amani, na tumaini” (“Aliyejeruhiwa,Liahona, Nov. 2018, 85).

Picha
Chad Jaggi na familia

Tunayo imani katika Yesu Kristo; tunajua tutaungana na Chad tena, lakini kupoteza uwepo wake wa Kimwili kunaumiza! Wengi wamepoteza wapendwa wao. Ni vigumu kuwa wavumilivu na kusubiria wakati ule tutakapoungana nao.

Mwaka ule alipofariki, tulihisi kama wingu jeusi limetufunika. Tulitafuta kimbilio katika kusoma maandiko yetu, kuomba kwa dhati zaidi, na kuhudhuria hekaluni mara nyingi zaidi. Mistari kutoka kwenye wimbo huu iliteka hisia zetu kwa wakati ule: “Kunakucha, ulimwengu unaamka, mawingu ya giza yanatoweka” (“The Day Dawn Is Breaking,” Nyimbo za Kanisa, na. 52).

Familia yetu iliazimia kwamba 2020 ungekuwa mwaka wa kuleta nguvu mpya! Tulikuwa tunasoma masomo yetu ya Njoo, Unifuate katika Agano Jipya kitabu cha Yakobo mwishoni mwa Novemba 2019 wakati dhima ilipojifunua yenyewe kwetu. Yakobo, Sura ya 1, mstari wa 2 unasomeka, “Ndugu zangu hesabuni ya kuwa ni shangwe tupu, mkiangukia katika mateso mengi” (Tafsiri ya Joseph Smith, Yakobo 1:2 [katika Yakobo 1:2, tanbihi a]). Katika hamu yetu ya kufungua mwaka mpya, muongo mpya, kwa shangwe, tuliamua kwamba mwaka 2020 “tutahesabu ya kuwa shangwe tupu.” Tulipata hisia za nguvu kabisa kuhusu hilo kiasi kwamba Krismasi iliyopita tuliwapa zawadi ya T–sheti ndugu zetu ambazo zilisomeka katika maandishi mazito, “Hesabuni Kuwa ni Shangwe Tupu” Mwaka wa 2020 ungekuwa hakika mwaka wa shangwe na kushangilia.

Ndiyo, tuko hapa—2020 badala yake umeleta COVID-19 janga la ulimwengu, machafuko ya raia, na changamoto za kiuchumi. Baba yetu wa mbinguni anaweza kuwa anatupatia sisi muda wa kutafakari na kuzingatia uelewa wetu juu ya uvumilivu na uamuzi wa makusudi wa kuchagua shangwe.

Kitabu cha Yakobo tangu hapo kimechukua maana mpya kwetu sisi. Yakobo, mlango wa1, mstari wa 3 na 4 unaendelea:

“Mkifahamu ya kwamba kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi.

“Saburi na iwe na kazi kamilifu, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu, bila kupungukiwa na neno.”

Katika jitihada zetu za kutafuta shangwe katikati ya majaribu yetu, tulisahau kwamba kuwa na saburi ndio ufunguo wa kuacha majaribu hayo yote yafanye kazi kwa faida yetu.

Mfalme Benjamin alitufundisha kumvua mtu wa asili na kuwa “mtakatifu kupitia upatanisho wa Kristo Bwana, na [kuwa] kama mtoto, mtiifu, mpole, mnyenyekevu, mwenye subira, aliyejaa upendo, aliye tayari kutii mambo yote” (Mosia 3:19).

Mlango wa 6 wa Preach My Gospel unafundisha sifa muhimu za Kristo ambazo tunaweza kuziiga: “ Subira ni uwezo wa kuvumilia kuchelewa, matatizo, upinzani, au mateso bila kuwa na hasira, mwenye kuchanganyikiwa, au wasiwasi. Ni uwezo wa kufanya mapenzi ya Mungu na kuukubali wakati Wake. Unapokuwa mwenye subira, unakuwa mtulivu kwenye shinikizo na unaweza kukabiliana na dhiki pasipo ghasia na kwa matumaini” (Preach My Gospel: A Guide to Missionary Service, rev. ed. [2019], 126).

Kazi kamilifu ya saburi inaweza pia kuelezwa katika maisha ya mmoja wa wafuasi wa awali wa Kristo, Simoni Mkanaani. Wazelote walikuwa kikundi cha watu wa taifa la Wayahudi ambao kwa nguvu walikuwa wakipinga utawala wa Warumi. Harakati za Wazelote ziliangazia fujo dhidi ya Warumi, washirika wao wa Kiyahudi, na Masadukayo kwa kushambulia ili kupora vyakula na kufanya shughuli nyingine ili kusaidia kusudi lao (ona Encyclopedia Britannica, “Zealot,” britannica.com. Simoni Mkanaani alikuwa Mzelote (ona Luka 6:15). Fikiria Simoni akijaribu kumshawishi Mwokozi ashike silaha, aongoze kundi la mgambo, au kufanya fujo Yerusalemu. Yesu alifundisha:

“Heri wenye upole; Maana hao watairithi nchi. …

“Heri wenye rehema; Maana hao watapata rehema. …

“Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu” (Mathayo 5:5, 7, 9).

Simoni yawezekana aliikumbatia na kuitetea falsafa yake kwa shauku na hamu kubwa, lakini maandiko yanapendekeza kwamba kupitia ushawishi na mfano wa Mwokozi, fokasi yake ilibadilika. Ufuasi wake kwa Kristo ukawa ndio kitovu cha jitihada za maisha yake.

Tunapofanya na kushika maagano yetu na Mungu, Mwokozi anaweza kutusaidia sisi “kuzaliwa mara ya pili; ndiyo, kuzaliwa na Mungu, kubadilishwa kutoka hali zetu za kimwili na ya kuanguka, kwa hali ya haki, na kukombolewa na Mungu, na kuwa wana na mabinti zake” (Mosia 27:25).

Kati ya jitihada zote za kazi za kijamii, kidini, na kisiasa za siku yetu, acha ufuasi wetu kwa Yesu Kristo uwe ushirika maarufu na wenye kukubalika. “Kwa kuwa hazina yako ilipo , ndipo utakapokuwapo na moyo wako” (Mathayo 6:21). Na tusisahau kwamba hata baada ya wafuasi waaminifu kuwa “wamekwisha kuyafanya mapenzi ya Mungu,” nao “[walikuwa] na hitaji la saburi” (Waebrania 10:36).

Kama vile tu kujaribiwa kwa imani yetu kunaleta saburi ndani yetu, tunapoonyesha subira, imani yetu huongezeka. Imani yetu inapoongezeka, ndivyo itakavyokuwa na shangwe yetu.

Machi hii iliyopita, binti yetu wa pili, Emma, kama wamisionari wengi katika Kanisa, alikwenda kukaa katika upweke wa lazima. Wamisionari wengi walikuja nyumbani. Wamisionari wengi walisubiri kupangiwa upya. Wengi waliondoka pasipo kupokea baraka zao za hekaluni kabla ya kuondoka kuingia kwenye eneo lao la kazi. Asanteni sana, wazee na akina dada. Tunawapenda.

Emma na mwenzi wake huko Netherlands walitumika kupita kiasi katika zile wiki kadhaa za mwanzoni—walitumika hadi machozi kuwatoka katika matukio mengi. Wakiwa na fursa za muda mfupi za kuonana na mtu uso kwa uso na kutoka nje ya makazi mara chache, mategemeo ya Emma kwa Mungu yaliongezeka. Tuliomba naye kwa njia ya mtandao na kumwuliza jinsi gani tungeweza kusaidia. Alituomba tujiunganishe na marafiki ambao alikuwa akiwafundisha kwa njia ya Mtandao!

Familia yetu ilianza kujiunganisha kwenye mtandao, mmoja baada ya mwingine, pamoja na marafiki wa Emma huko Netherlands. Tuliwaalika kujiunga nasi katika familia yetu kubwa, ya mtandaoni, kila wiki, katika masomo ya Njoo, Unifuate. Floor, Laura, Renske, Freek, Benjamin, Stal na Muhammad wote wamekuwa marafiki zetu. Baadhi ya marafiki zetu kutoka Uholanzi wameingia “ kwenye mlango mwembamba” (3 Nefi 14:13). Wengine wanaonyeshwa “unyofu wa njia, na wembamba wa mlango, ambamo wataingilia” (2 Nefi 31:9). Wao ni kaka na dada zetu katika Kristo. Kila wiki sisi “tunahesabu kuwa ni shangwe tupu” tunapofanya kazi pamoja katika kuendelea kwenye njia ya agano.

Tunaacha “Saburi na iwe na kazi kamilifu” (Yakobo 1:4) katika kutoweza kwetu kukutana uso kwa uso kama familia za kata kwa muda. Lakini tuhesabu kuwa ni shangwe kwani imani ya familia zetu inakua kwa njia ya kuunganishwa kwa teknolojia mpya na masomo ya Njoo, Unifuate ya Kitabu cha Mormoni.

Rais Russell M. Nelson aliahidi, “Juhudi zako zisizokoma katika swala hili—hata katika nyakati hizo ambapo unaweza kuhisi kwamba haufanikiwi—zitabadili maisha yako, yale ya familia yako, na ya ulimwengu” (“Go Forward in Faith,” Liahona, May 2020, 114).

Sehemu tunapofanyia maagano matakatifu na Mungu—hekaluni—kumefungwa kwa muda. Sehemu tunayotunzia maagano na Mungu—nyumbani—kuko wazi! Tunayo fursa nyumbani ya kujifunza na kutafakari juu ya uzuri wa kipekee wa maagano ya hekaluni. Hata bila kuingia ndani ya ile sehemu takatifu, mioyo “yetu … itafurahia kwa furaha kuu kwa matokeo ya baraka zitakazomwagwa” (Mafundisho na Maagano 110:9).

Wengi wamepoteza kazi, wengine wamepoteza fursa. Tunashangilia, hata hivyo, pamoja na Rais Nelson, ambaye hivi karibuni alieleza: “Matoleo ya mfungo ya hiari kutoka kwa waumini wetu kwa kweli yameongezeka, vile vile michango ya hiari kwenye mfuko wetu wa misaada ya kibinadamu. … Pamoja tutaushinda wakati huu mgumu. Bwana atakubariki unapoendelea kuwabariki wengine” (ukurasa wa facebook wa Russell M. Nelson, alioweka kutoka Aug. 16, 2020, facebook.com/russell.m.nelson).

“Jipeni moyo” ni amri kutoka kwa Bwana, siyo jipeni uwoga mwema (Mathayo 14:27).

Wakati mwingine tunakosa uvumilivu tunapofikiria kuwa “tunafanya vitu vyote sawa” na bado hatupokei baraka tunazotamani. Henoko alitembea na Mungu kwa miaka 365 kabla ya yeye na watu wake kupalizwa mbinguni. Miaka mia tatu na sitini na tano ya kujitahidi kufanya kila kitu sawa na kisha ikatokea! (Ona Mafundisho na Maagano 107:49.)

Kifo cha kaka yangu Chad kilikuja miezi michache tu baada ya kupumzishwa kuongoza Misheni ya Ogden Utah. Ilikuwa ni muujiza kwamba japo tuliishi California Kusini, kati ya misheni zote 417 ambazo tungeweza kupangiwa katika mwaka 2015, tulipangiwa Utah kaskazini. Nyumba ya misheni ilikuwa mwendo wa dakika 30 kwa gari hadi nyumbani kwa Chad. Saratani ya Chad iligundulika baada ya sisi kupokea wito wa misheni yetu. Hata katika hali ya kujaribiwa sana, tulijua kwamba Baba wa Mbinguni alikuwa anatujua na anatusaidia kupata shangwe.

Ninashuhudia juu ya nguvu za ukombozi, kutakasa, kunyenyekeza, na shangwe ya Mwokozi Yesu Kristo. Ninashuhudia kwamba tunapoomba kwa Baba wa Mbinguni katika jina la Yesu Kristo, Yeye atatujibu. Ninashuhudia kwamba tunapomsikia, tunapomsikiliza, na kutii sauti ya Bwana na nabii Wake aliye hai, Rais Russell M. Nelson, tunaweza kuacha “saburi iwe na kazi kamilifu” na “kuhesabu kuwa shangwe tupu” Katika jina la Yesu Kristo, amina.